USAWIRI WA MCHAKATO WA KUJIUA KATIKA RIWAYA ...
-
Upload
khangminh22 -
Category
Documents
-
view
35 -
download
0
Transcript of USAWIRI WA MCHAKATO WA KUJIUA KATIKA RIWAYA ...
USAWIRI WA MCHAKATO WA KUJIUA KATIKA
RIWAYA TEULE ZA EUPHRASE KEZILAHABI: NI
MWANGWI WA MTANZIKO WA KIJAMII?
ADRIA FULUGE
SHAHADA YA UZAMIVU KATIKA KISWAHILI
CHUO KIKUU CHA DODOMA
JULAI, 2021
USAWIRI WA MCHAKATO WA KUJIUA KATIKA RIWAYA
TEULE ZA EUPHRASE KEZILAHABI: NI MWANGWI WA
MTANZIKO WA KIJAMII?
NA
ADRIA FULUGE
TASINIFU HII IMEWASILISHWA KWA AJILI YA KUTUNUKIWA
SHAHADA YA UZAMIVU KATIKA KISWAHILI CHUO KIKUU
CHA DODOMA
CHUO KIKUU CHA DODOMA
JULAI, 2021
i
IKIRARI NA HAKIMILIKI
Mimi, Adria Fuluge, ninathibitisha kwamba tasinifu hii ni kazi yangu halisi, na
kwamba haijawahi kuwasilishwa na wala haitawasilishwa katika Chuo Kikuu
kingine chochote kwa ajili ya mahitaji ya kutunukiwa Shahada kama hii au Shahada
nyingine yoyote ile.
Saini:
Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi kuiga, kuzalisha, kutoa kopi, kunakili, ama
kusambaza sehemu yoyote ya tasinifu hii kwa namna yoyote bila kibali cha
maandishi kutoka kwa mwandishi au Chuo Kikuu cha Dodoma.
ii
ITHIBATI YA WASIMAMIZI
Waliotia saini hapa chini wanathibitisha kuwa wameisoma tasinifu hii inayoitwa
“Usawiri wa Mchakato wa Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase
Kezilahabi: Ni Mwangwi wa Mtanziko wa Kijamii?” na wanapendekeza kwamba
itahiniwe na kukubaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ajili ya kukamilisha
masharti ya kutunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Kiswahili ya Chuo Kikuu cha
Dodoma.
Prof. Joshua Samuel Madumulla
Saini Tarehe:
(Msimamizi)
Dkt. Zuhura Abdallah Badru
Saini Tarehe:
(Msimamizi)
iii
SHUKRANI
Ninatambua kuwa hakuna mwingine zaidi anayestahili kupewa sifa, heshima na
utukufu wote, bali ni Mungu baba wa Mbinguni. Hii ni kwa sababu ndiye aliyenijalia
uhai na nguvu hadi kufikia hatua hii. Si kwa uweza wangu, na wala sikustahili
heshima kubwa kiasi hiki, bali ni kwa neema tu, kwani kwa uweza wake, nilijaliwa
nguvu na welewa wa kufanya utafiti huu. Basi, atukuzwe Yeye awezaye kufanya
mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu
itendayo kazi ndani yetu (Efe 3:20).
Aidha, kukamilika kwa kazi hii kulitokana na michango ya watu mbalimbali.
Ninatambua na kuuthamini sana mchango wao wa hali na mali. Hivyo basi, sina budi
kutoa shukrani zangu za dhati kwao. Hata hivyo, kwa kuwa si rahisi kuwataja wote
hapa, itanilazimu kuwataja wachache wafuatao:
Kwanza kabisa, ninapenda kutoa shukrani kwa wasimamizi wangu, Prof. Joshua
Samuel Madumulla na Dkt. Zuhura Abdallah Badru, ambao wamekuwa nami bega
kwa bega na kuhakikisha kuwa kazi hii inakuwa katika kiwango hiki. Licha ya
majukumu mengi waliyo nayo, hawakusita kunishauri na kunipa miongozo bora na
imara iliyowezesha kazi hii kufikia katika kiwango hiki. Asanteni sana.
Pili, ninakishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa kunipa ufadhili wa masomo yangu na
kuniwezesha kukamilisha Shahada yangu ya Uzamivu bila usumbufu wowote.
Vilevile, nawashukuru wana-Idara wenzangu, hususani Mudiri wa Idara ya Lugha na
Stadi za Mawasiliano, Dkt. Maria Mkunde Kanigi, kwa kunihamasisha. Mungu
awajalie thawabu maridhawa.
Tatu, shukrani zangu za dhati na za upendo zimwendee Dkt. Athumani Salum Ponera
wa Chuo Kikuu cha Dodoma, na baadaye Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere kwa ushauri na miongozo ya mara kwa mara aliyonipa kila nilipohitaji. Pia,
ninawashukuru sana Bw. Selestino Helman Msigala wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Bi. Martina Duwe wa Chuo Kikuu Mzumbe, na Bw. Hassan Hassan wa
Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, kwa kukubali kupitia na kutoa maoni na
ushauri ulioiboresha zaidi rasimu ya tasinifu hii. Vilevile, ninawashukuru wanafunzi
wenzangu wa Shahada ya Uzamivu Bw. Gervas Kasiga, Bi. Getrude Shima, Bi.
Johari Hakimu, Bi. Martina Duwe, na Bi. Tatu Khamis, kwa ushirikiano mzuri na
iv
kutiana moyo, hasa pale mambo yalipokatisha tamaa kutokana na ugumu wa safari
hii ya uzamivu. Mungu awalinde daima. Wengine wanaopaswa kushukuriwa ni
Regina Tanu wa Mwanza na Rozina Mugabe Bununja wa Ukerewe, kwa
makaribisho mazuri, kuniongoza na kunisaidia kuwapata kwa urahisi watafitiwa
wengine huko Namagondo na Murutunguru, Wilayani Ukerewe.
Tano, ninatoa shukrani zangu za upendo kwa mke wangu mpenzi, Mary Michael
Makongwa, pamoja na familia yangu kwa jumla. Kipekee hawa walionesha
uvumilivu na walinitia moyo, hasa pale nilipotaka kukata tamaa. Pia, walinisaidia
sana katika kipindi chote cha kufanyika kwa utafiti huu. Bila ya nguzo imara ya
familia yangu, huenda kazi hii isingeweza kuwa katika mwonekano huu, ikiwa ni
pamoja na kukamilika kwa wakati.
v
TABARUKU
Tasinifu hii naitabaruku kwa marehemu baba yangu mpenzi, Mzee Nanisa Benedikto
Fuluge. Baba, ninatamani sana leo hii ungekuwepo na kujionea kwa macho yako,
mbegu ya mafanikio uliyoipanda, ambayo sasa matunda yake ni bayana, kwani
yamekomaa na kuiva vilivyo. Mwenyezi Mungu, kwa mapenzi yake, aliutwaa uhai
wako kabla hata ya kushuhudia mafanikio haya. Baba, uangaziwe mwanga wa milele
na upumzike kwa amani. Amina.
Kwa mama yangu mpenzi, Betina Solomon se-Kalenga wa Iringa (Mapanda),
ulinizaa, ulinilea na kunifunza maadili mema ya utu, heshima, utii na uvumilivu.
Sina cha kukulipa zaidi ya kukupa hidaya hii na kukuombea fanaka katika maisha
yako. Unastahili heshima tele. Mungu akupe maisha marefu ya amani na furaha na
akujalie kila thawabu.
Kwa mke wangu mpenzi, Mary Michael Makongwa, pamoja na watoto wetu
wapenzi, Grace, Erick, Agnes na Brightness. Pokeeni zawadi ya upendo na ya
uvumilivu wenu kwangu.
vi
IKISIRI
Tasinifu hii ni matokeo ya utafiti wenye mada inayoitwa ―Usawiri wa Matukio ya
Mchakato wa Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase Kezilahabi: Ni Mwangwi wa
Mtanziko wa Kijamii?‖ Lengo kuu lilikuwa kuchunguza usawiri wa matukio ya
kujiua katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi kama ni mwangwi wa mtanziko
wa kijamii, au la. Malengo mahususi yaliyoshughulikiwa ni matatu: Mosi,
kubainisha usawiri wa matukio yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya teule
za Euphrase Kezilahabi; pili, kubainisha sababu za mitanziko ya wahusika
zinazosawiriwa katika riwaya teule; na tatu, kutathmini uhusiano baina ya usawiri wa
matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya
kujiua katika jamii. Ili kuyafikia malengo hayo, mbinu za aina mbili zilitumika
katika mchakato wa ukusanyaji wa data. Mbinu ya kwanza ilikuwa ni ukusanyaji wa
data za maktabani kwa kusoma na kuchambua kwa makini matini teule na magazeti
mbalimbali yenye taarifa zinazohusiana na mada ya utafiti. Pili, ilikuwa ni mbinu ya
mahojiano na watafitiwa iliyotumika kukusanya data za uwandani. Kimsingi,
shughuli nzima ya ukusanyaji wa data, uchanganuzi wake, na suala la kutafsiri
matokeo ya utafiti ilikitwa katika mkabala wa kitaamuli. Data hizo zilihakikiwa,
kuchanganuliwa na kupangwa katika mada ndogondogo kulingana na namna
zinavyooana kimaudhui. Nadharia za Udhanaishi na Sosholojia ya Kifasihi ndizo
zilizomwongoza mtafiti katika mchakato wa uchambuzi wa data zake.
Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba, matukio yanayosawiriwa katika riwaya
teule ndiyo yaliyounda mchakato wa kujiua kwa wahusika. Katika riwaya ya Rosa
Mistika matukio hayo yanamhusu Rosa Mistika; nayo ni: kupigwa na baba yake,
kuwachongea wasichana wenzake, kuota ndoto, kusimamishwa shule, kufumaniwa
na kufukuzwa chuo. Mengine ni kutoa mimba, kujitenga na kutengwa na jamii yake,
na kuachwa na mchumba wake. Kwa upande wa riwaya ya Kichwamaji matukio
hayo yanayohusu kujiua kwa Kazimoto ni: kunyimwa kazi, Rukia kutiwa mimba,
vifo vya Rukia na mama yake, na kifo cha Kalia. Matukio mengine ni kifo cha mtoto
wake, kuugua ugonjwa wa ajabu, na kujitenga kijamii. Matukio mengine ya kujiua
yanasawiriwa katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo na yanamhusu Tumaini,
yaani matukio ya aibu na fedheha, na tukio la Tumaini kumuua Mkuu wa Wilaya.
Pia, sababu mbalimbali za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, na kifalsafa, zimebainika
kuwa chanzo cha mtu kupata mitanziko ya kimaisha. Mitanziko hiyo husababisha
mtu huyo kuwa katika mkinzano wa mawazo, ambayo humpa wakati mgumu wa
kuamua la kufanya, kwa kuwa uamuzi wowote kwake huwa na madhara. Aidha,
utafiti umebaini kuwa kuna uhusiano mkubwa baina ya matukio ya mchakato wa
kujiua yaliyomo katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii
vii
kwa jumla. Uhusiano huo umebainishwa na kuwekwa katika makundi mawili. Mosi,
uhusiano wa sababu za matukio ya kujiua, ambazo ni kujiua kunakosababishwa na
athari za mahusiano ya kimapenzi, kujiua kunakosababishwa na athari katika malezi
na migogoro ya kifamilia, na kujiua kunakosababishwa na athari za magonjwa. Pili,
uhusiano wa njia zinazotumika katika kujiua. Njia hizo ni kujiua kwa kujinyonga,
kujipiga risasi, kujichoma kisu, na kwa kutumia sumu.
Mchango mpya wa utafiti huu ni pamoja na: Mosi, kubainishwa kwamba kujiua ni
mchakato na siyo tukio la ghafla kama ilivyofahamika awali kupitia tafiti
zilizotangulia miongoni mwa wanajamii. Pili, kuleta mtagusano wa kitaaluma kwa
kuzishikamanisha nyuga mbalimbali, zikiwamo Afya, Saikolojia, Sosholojia, na
Fasihi. Tatu, kinadharia na kiuchambuzi ambapo licha ya kuendeleza nadharia ya
Udhanaishi iliyozoeleka katika uchambuzi wa riwaya teule, nadharia ya Sosholojia
ya Kifasihi pia imetumika. Nne, kwa watunga sera na wakuza mitalaa kuweza
kuchukua hatua madhubuti na za pamoja katika kulishughulikia tatizo la watu kujiua
ili lisiendelee kuzikumba na kuziathiri jamii zetu.
viii
YALIYOMO
IKIRARI NA HAKIMILIKI ......................................................................................... i
ITHIBATI YA WASIMAMIZI ................................................................................... ii
SHUKRANI ................................................................................................................ iii
TABARUKU................................................................................................................ v
IKISIRI ........................................................................................................................ vi
YALIYOMO ............................................................................................................. viii
UFAFANUZI WA VIFUPISHO VILIVYOTUMIKA .............................................. xii
SURA YA KWANZA ................................................................................................. 1
UTANGULIZI WA JUMLA ..................................................................................... 1
1.1 Utangulizi ............................................................................................................... 1
1.2 Ufafanuzi wa Dhana Muhimu ................................................................................ 1
1.2.1 Mchakato ............................................................................................................. 1
1.2.2 Kujiua .................................................................................................................. 1
1.2.3 Riwaya................................................................................................................. 1
1.2.4 Mwangwi............................................................................................................. 3
1.2.5 Mtanziko ............................................................................................................. 3
1.3 Usuli wa Tatizo la Utafiti ....................................................................................... 4
1.4 Tamko la Tatizo la Utafiti ...................................................................................... 8
1.5 Malengo ya Utafiti ................................................................................................. 9
1.5.1 Lengo Kuu ........................................................................................................... 9
1.5.2 Malengo Mahususi ............................................................................................ 10
1.6 Maswali ya Utafiti ................................................................................................ 10
1.7 Manufaa ya Matokeo ya Utafiti ........................................................................... 10
1.8 Mawanda ya Utafiti .............................................................................................. 11
1.9 Muhtasari wa Sura ya Kwanza ............................................................................. 12
SURA YA PILI ......................................................................................................... 13
MAPITIO YA MAANDIKO NA KIUNZI CHA NADHARIA ........................... 13
2.1 Utangulizi ............................................................................................................. 13
2.2 Mapitio ya Maandiko ........................................................................................... 13
2.2.1 Mapitio Kuhusu Kazi za Kezilahabi kwa Jumla ............................................... 13
ix
2.2.2 Mapitio Kuhusu Mchakato wa Kujiua katika Riwaya za Kezilahabi ............... 18
2.2.3 Mapitio Kuhusu Dhana ya Kujiua kwa Mitazamo ya Nje ya Fasihi................. 22
2.2.4 Mwanya Uliotakiwa Kuzibwa na Utafiti .......................................................... 24
2.3 Viunzi vya Nadharia ............................................................................................ 24
2.3.1 Nadharia ya Udhanaishi .................................................................................... 25
2.3.1.1 Misingi ya Nadharia ya Udhanaishi ............................................................... 25
2.3.1.2 Nadharia ya Udhanaishi Ilivyotumika ........................................................... 26
2.3.2 Nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi ................................................................... 26
2.3.2.1 Misingi ya Nadharia ya Kisosholojia ............................................................. 28
2.3.2.2 Nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi Ilivyotumika .......................................... 28
2.4 Muhtasari wa Sura ya Pili .................................................................................... 29
SURA YA TATU ...................................................................................................... 30
METHODOLOJIA YA UTAFITI .......................................................................... 30
3.1 Utangulizi ............................................................................................................. 30
3.2 Usanifu wa Utafiti ................................................................................................ 30
3.3 Mkabala wa Utafiti ............................................................................................... 31
3.4 Eneo la Utafiti ...................................................................................................... 32
3.5 Walengwa wa Utafiti............................................................................................ 34
3.5.1 Wango la Utafiti ................................................................................................ 34
3.5.1.1 Usampulishaji ................................................................................................. 35
3.5.1.2 Sampuli ya Utafiti .......................................................................................... 36
3.6 Ukusanyaji wa Data ............................................................................................. 38
3.6.1 Njia za Ukusanyaji wa Data .............................................................................. 39
3.6.1.1 Usomaji na Uchambuzi Makini wa Matini .................................................... 39
3.6.1.2 Mahojiano ...................................................................................................... 39
3.6.2 Mchakato wa Ukusanyaji Data ......................................................................... 40
3.7 Mbinu za Uchambuzi wa Data ............................................................................. 41
3.8 Itikeli za Utafiti .................................................................................................... 42
3.9 Uhalali na Uthabiti wa Matokeo ya Utafiti .......................................................... 43
3.10 Muhtasari wa Sura ya Tatu ................................................................................ 43
x
SURA YA NNE ......................................................................................................... 44
UWASILISHAJI WA DATA NA MJADALA WA MATOKEO YA UTAFITI 44
4.1 Utangulizi ............................................................................................................. 44
4.2 Matukio ya Mchakato wa Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase
Kezilahabi ....................................................................................................... 44
4.2.1 Muhtasari wa Riwaya ya Rosa Mistika ............................................................. 45
4.2.1.1 Kupigwa na Baba yake................................................................................... 47
4.2.1.2 Kuwachongea Wasichana Wenzake .............................................................. 50
4.2.1.3 Kuota Ndoto ................................................................................................... 52
4.2.1.4 Kusimamishwa Shule, Kufumaniwa na Kufukuzwa Chuo ............................ 55
4.2.1.5 Kutoa Mimba ................................................................................................. 58
4.2.1.6 Kujitenga na Kutengwa na Jamii yake ........................................................... 59
4.2.1.7 Kuachwa na Mchumba Wake ........................................................................ 61
4.2.2 Muhtasari wa Riwaya ya Kichwamaji............................................................... 68
4.2.2.1 Tukio la Kunyimwa Kazi ............................................................................... 69
4.2.2.2 Rukia Kutiwa Mimba ..................................................................................... 72
4.2.2.3 Vifo vya Rukia na Mama Yake ...................................................................... 75
4.2.2.4 Kifo cha Kalia ................................................................................................ 78
4.2.2.5 Kifo cha Mtoto Wake ..................................................................................... 81
4.2.2.6 Kazimoto Kuugua Ugonjwa wa Ajabu .......................................................... 83
4.2.2.7 Kujitenga Kijamii ........................................................................................... 85
4.2.3 Muhtasari wa Riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo ............................................ 88
4.2.3.1 Matukio ya Aibu na Fedheha ......................................................................... 89
4.2.3.2 Tukio la Tumaini Kumuua Mkuu wa Wilaya ................................................ 92
4.3 Sababu za Mitanziko ya Wahusika katika Riwaya Teule za Euphrase
Kezilahabi ....................................................................................................... 96
4.3.1 Sababu za Kijamii ............................................................................................. 96
4.3.1.1 Mahusiano ya Kimapenzi ............................................................................... 96
4.3.1.2 Mfumo wa Malezi ........................................................................................ 111
4.3.2 Sababu za Kiutamaduni................................................................................... 123
4.3.2.1 Suala la Mila na Desturi ............................................................................... 124
4.3.2.2 Suala la Dini ................................................................................................. 135
4.3.2.3 Tatizo la Ndoa na Uzazi ............................................................................... 138
xi
4.3.3 Sababu za Kiuchumi ....................................................................................... 147
4.3.4 Sababu za Kifalsafa ......................................................................................... 155
4.3.4.1 Dhana ya Maisha .......................................................................................... 155
4.3.4.2 Dhana ya Kifo .............................................................................................. 160
4.3.4.3 Dhana Kuhusu Mungu ................................................................................. 166
4.4 Uhusiano wa Mchakato wa Kujiua katika Fasihi na Uhalisi katika Jamii ......... 175
4.4.1 Uhusiano wa Sababu za Matukio ya Kujiua ................................................... 176
4.4.1.1 Kujiua Kunakosababishwa na Athari za Mahusiano ya Kimapenzi ............ 178
4.4.1.2 Kujiua Kunakosababishwa na Athari katika Malezi na Migogoro ya
Kifamilia ....................................................................................................... 181
4.4.1.3 Kujiua Kunakosababishwa na Athari za Magonjwa .................................... 185
4.4.2 Uhusiano wa Njia Zinazotumika katika Kujiua .............................................. 187
4.4.2.1 Kujiua kwa Kujinyonga ............................................................................... 188
4.4.2.2 Kujiua kwa Kujipiga Risasi ......................................................................... 194
4.4.2.3 Kujiua kwa Kujichoma Kisu ........................................................................ 198
4.4.2.4 Kujiua kwa Kutumia Sumu .......................................................................... 199
4.5 Muhtasari wa Sura ya Nne ................................................................................. 202
SURA YA TANO.................................................................................................... 204
MUHTASARI, HITIMISHO NA MAPENDEKEZO ......................................... 204
5.1 Utangulizi ........................................................................................................... 204
5.2 Muhtasari wa Tasinifu Hii ................................................................................. 204
5.3 Hitimisho la Tasinifu Hii ................................................................................... 207
5.3.1 Utoshelevu wa Nadharia Zilizotumika............................................................ 207
5.3.2 Mchango Mpya wa Matokeo ya Utafiti Huu .................................................. 208
5.3.3 Mapendekezo Kuhusu Tafiti Zijazo ................................................................ 209
MAREJELEO ........................................................................................................ 211
VIAMBATISHO .................................................................................................... 223
xii
UFAFANUZI WA VIFUPISHO VILIVYOTUMIKA
BAKITA Baraza la Kiswahili la Tanzania
BAKIZA Baraza la Kiswahili la Zanzibar
Bi. Bibi
Bw. Bwana
Co. Company
Dkt. Daktari
DSM Dar es Salaam
DUP Dar es Salaam University Press
EALB East African Literature Bureau
EAPH East African Publishing House
Http Hyper Text Transfer Protocal
IFAMU Idara ya Fasihi, Mawasiliano na Uchapishaji
Juz. Juzuu
Kur. Kurasa
Ltd Limited
M.A Master of Arts
MUM Muslim University of Morogoro
Na. Namba
No. Number
Ph.D Doctor of Philosophy
Prof. Profesa
TATAKI Taasisi ya Taaluma za Kiswahili
Tol. Toleo
TPH Tanzania Printing House
TUKI Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili
UDOM University of Dodoma
UDSM University of Dar es Salaam
Uk Ukurasa
Vol. Volume
1
SURA YA KWANZA
UTANGULIZI WA JUMLA
1.1 Utangulizi
Sura hii inayojenga msingi wa tasinifu ina sehemu saba. Imeanza kwa kufafanua
dhana za msingi zilizotumika katika utafiti huu kwa lengo la kuweka msingi wa
uelewekaji wake kwa wasomaji. Sehemu nyingine ni usuli wa tatizo la utafiti, tamko
la tatizo utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, manufaa tarajiwa, pamoja na
mawanda ya utafiti.
1.2 Ufafanuzi wa Dhana Muhimu
Sehemu hii inafafanua dhana muhimu zilizotumika katika tasinifu hii. Ufafanuzi huo
umetolewa kwa kuzingatia mitazamo na maoni ya wataalamu mbalimbali, na
baadaye, mtafiti kutoa maana ya jumla kulingana na namna alivyokusudia kuzitumia
katika kazi yake. Dhana zilizotolewa ufafanuzi ni hizi zifuatazo:
1.2.1 Mchakato
TUKI (2014) inafafanua kuwa mchakato ni nomino inayomaanisha mfululizo wa
shughuli unaosababisha kitu fulani kufanyika au lengo fulani kufikiwa. Hii ina
maana kuwa mchakato ni kitendo cha kufanya jambo au kitu fulani hatua kwa hatua,
kwa lengo la kusababisha kitu kingine kitokee, kikiwa na hali au umbo jipya tofauti
na lile lililokuwapo awali. Katika tasinifu hii, dhana hii imetumika kumaanisha jumla
ya matukio, mitanziko na miktadha inayohusiana na maisha ya mtu hadi kuchukua
maamuzi ya kujiua.
1.2.2 Kujiua
BAKIZA (2010) linaeleza kuwa dhana ya ‗kujiua‘ inatokana na kitenzi ‗ua‘ chenye
maana ya kutoa roho ya mja au kufisha. Kulingana na utafiti huu, kujiua ni kitendo
cha mtu kuiangamiza roho kwa kupoteza uhai wake (kufa). Hivyo, dhana ya kujiua
imechunguzwa kwa kuzingatia matukio mbalimbali aliyopitia mhusika hadi kufikia
maamuzi ya kujiua.
1.2.3 Riwaya
Dhana ya riwaya ni tata, kwani hakuna namna moja ya kuielezea. Hii inatokana na
ukweli kwamba pamekuwa na mgogoro wa fikra miongoni mwa wataalamu wa uga
huu kuhusiana na maana halisi ya riwaya. Aidha, wataalamu hao bado
2
hawajakubaliana kuhusu namna ya kuzigawa au kuziainisha riwaya kitanzu. Baadhi
ya wataalamu waliofasili dhana hii ni Mphahlele (1976), Muhando na Balisidya
(1976), Njogu na Chimerah (2008) na Madumulla (2009). Kwa mfano, Mphahlele
(1976) anaeleza kuwa, riwaya ni utanzu wenye maneno kati ya 35,000 na 75,000 au
zaidi. Anaona kuwa, kazi yoyote yenye maneno pungufu ya idadi hiyo haifai kuitwa
riwaya. Maelezo haya hayatofautiani sana na yale ya Muhando na Balisidya (1976)
wanaofafanua kuwa:
… Riwaya yaweza kuanzia maneno 35,000 hivi na kuendelea,
lakini tukisema juu ya urefu na tukaishia hapo tu, jambo hili
halitakuwa na maana. Maana mtu yeyote aweza kuweka habari
yoyote ile katika wingi wa maneno kama hayo. Jambo
muhimu hapa ni kuwa riwaya huwa na mchangamano wa
matukio, ujenzi wa wahusika na dhamira, muundo wake na
hata mtindo (mitindo inayotumiwa) maalumu… Si ajabu kuwa
utunzi wa riwaya wategemea sana jamii yenye ujuzi wa
kuandika kama zana bora ya kuhifadhi (uk. 63).
Ufafanuzi wa Muhando na Balisidya una uzito zaidi ya ule wa Mphahlele, kwa
sababu wao wanaenda hatua kadhaa mbele. Wanaeleza kwamba kinachotakiwa
kuzingatiwa si urefu au wingi wa maneno pekee, bali mchangamano wa matukio,
ujenzi wa wahusika na dhamira, muundo wake, pamoja na mtindo maalumu.
Kwa upande wake, Madumulla (2009) anaeleza kuwa dhana ya riwaya ni telezi
kuifafanua, kwa sababu hubadilika kulingana na mabadiliko ya jamii. Anabainisha
kuwa kuna namna mbili ya kufafanua maana ya riwaya. Namna ya kwanza, ni
ufafanuzi wa riwaya kwa kujikita katika kamusi. Kimsingi, ufafanuzi huu huhitaji
maelezo mafupi ya kiufafanuzi. Namna ya pili ni ufafanuzi unaojikita katika sifa
bainifu zinazoupambanua utanzu huo. Anataja baadhi ya sifa zinazoitambulisha
riwaya kuwa ni matumizi ya lugha ya kinathari, kutofungwa na sheria, urefu na
upana, pamoja na kuwa karibu na uhalisi wa maisha ya jamii.
Kwa jumla, ufafanuzi wa riwaya kulingana na wataalamu hao unadhihirisha kuwa,
riwaya ni andiko ambalo huwa na sifa zifuatazo: masimulizi ya kubuni (ubunifu),
hadithi au simulio la kinathari (usimulizi) na mpangilio au msuko fulani wa matukio
(ploti). Sifa nyingine ni ufungamano na wakati (visa hutendeka katika wakati fulani),
urefu, mawanda mapana (mada zinazozungumziwa, ya wakati, na mahali pa matukio
hayo), na uchangamano (wa visa, dhamira, na wahusika). Katika tasinifu hii, riwaya
3
imerejelewa kuwa ni kazi ya kisanaa inayoandikwa kwa kutumia lugha ya kibunifu.
Kazi hiyo huwa na mawanda mapana katika kuelezea mambo kwa kina. Aidha, ina
uchangamani wa visa na matukio, wahusika, na mandhari, ambayo husawiri maisha
ya watu kulingana na mazingira yao.
1.2.4 Mwangwi
Ni sauti inayorudi baada ya mawimbi ya sauti kugonga mahali na kumrudia
mzungumzaji ambayo, aghalabu, hutokea pangoni, msituni, au kwenye jengo kubwa
na tupu (BAKITA, 2017). Pia, sauti hiyo huweza kusambaa au kutawanyika kwenda
umbali fulani kulingana na ukubwa wa chanzo chake. Katika tasinifu hii, dhana hii
imetumika katika kuchunguza iwapo matukio mbalimbali yanayotokea katika jamii
ni sababu ya watu kuchukua uamuzi wa kujiua au la.
1.2.5 Mtanziko
BAKITA (2017) linaeleza kuwa mtanziko ni dhana inayotokana na kitenzi ‗tanza‘,
ikiwa na maana ya kutatanisha au kushindwa kueleweka vizuri kwa ujumbe uliomo
katika jambo au tukio. Kwa maneno mengine, mtanziko ni hali ya kutatiza,
kukanganya, au kuhangaisha. Dhana hii ambayo katika lugha ya Kiingereza huitwa
―dilemma‖ katika Fasihi iliasisiwa na Sletteboe (1997). Mtaalamu huyu anaielezea
dhana hii kuwa ni hali ya mhusika kuwa katika mkinzano wa mawazo, ambayo
humpa wakati mgumu wa kuchagua la kufanya, kwa sababu uamuzi wowote
anaoamua kuuchukua huwa na madhara kwake. Anaongeza kuwa kuna namna tatu
za mtu mwenye mtanziko, ambazo ni: Mosi, kuwa katika hali kuu mbili au zaidi za
kufanyia uamuzi au uchaguzi. Hoja hii inaungwa mkono na Madumulla (2009)
anayeeleza kuwa, mtu akiwa katika mtanziko mara nyingi, husukumwa katika
ukingo wa kuamua kati ya kufa na kuyaepuka matatizo, au kuishi ili kuendelea na
maisha kwa uvumilivu, yaani hulazimika kufanya uchaguzi kati ya mambo mawili
magumu (dilemma). Kwa mfano, kutosikiliza wosia wa wazazi na kufanya jambo
ambalo jamii inakataza. Pili, uamuzi ambao mhusika hajui matokeo yake
yatakuwaje. Tatu, uamuzi ambao mhusika hajui jambo au uamuzi sahihi ni upi.
Sletteboe anafafanua zaidi kuwa, ili kuufikia uamuzi huo, mhusika hujiuliza maswali
kama vile: kwanza, nataka kufanya au kuchukua uamuzi gani? Na pili, kitu gani ni
sahihi kinachotakiwa kufanyika? Kwa hiyo, kutanzika ni kuwa katika hali ya
4
kushindwa kuamua juu ya jambo fulani, yaani kuwa katika mkinzano wa mawazo
katika kufanya uamuzi wa jambo.
Kwa muktadha wa utafiti huu, dhana hii imetumika kumaanisha athari za matukio
mabaya au ya hatari, ambayo huleta masikitiko, majonzi, huzuni au msiba katika
jamii. Athari hizo huweza kusababisha mtu kuwa katika hali ya kushindwa kuamua
(mtanziko) juu ya jambo fulani.
1.3 Usuli wa Tatizo la Utafiti
Fasihi husawiri ulimwengu kulingana na jadi pamoja na hali ya maendeleo ya jamii,
na hivyo kuzifanya kazi za fasihi kufungamana na muktadha uliozizaa. Mtunzi
huumba kazi yake ya kifasihi kwa kuzingatia mambo yanayoihusu jamii kwa kuwa
fasihi haiwezi kukwepa kaida za jamii husika. Hii inayakinisha hoja kuwa, fasihi ni
zao la jamii. Kwa mantiki hiyo, maisha halisi ndio msingi na mzazi wa fasihi. Dhima
ya jumla ya fasihi ni kusawiri kisanaa hali ya mwanadamu, mazingira yake, uhusiano
wake na mazingira hayo, mahusiano yake ya kijamii, hisia na mawazo yake, kwa
lengo la kuonesha hali ilivyo, kuelewesha, na hata kuleta mabadiliko (Mulokozi,
2017). Ufafanuzi huu unalenga kutoa dira kuwa dhima ya fasihi inatakiwa
kusawiriwa kwa kigezo cha jamii mahususi. Hoja hii haitofautiani na mawazo ya
Selden na wenzake (2005) wanaoeleza kuwa usawiri huo haupaswi kuwa wa tukio
mojamoja, bali kama mchakato mzima wa maisha ya jamii. Wanaongeza kuwa,
msomaji hutakiwa kuchukua tahadhari kutokana na ukweli kuwa kazi ya sanaa siyo
huo ukweli, bali ni njia ya kuakisi ukweli.
Watafiti mbalimbali kama vile Wellek na Warren (1949) na Escarpit (1974)
wanabainisha kuwapo kwa uhusiano baina ya fasihi na jamii. Wanaeleza kuwa
uhusiano huo unatokana na ukweli kwamba, pindi maisha ya jamii yabadilikapo,
mielekeo, tamaduni, pamoja na maadili ya jamii nayo hubadilika. Kwa kuwa fasihi ni
kielelezo cha maisha ya jamii, ni muhimu kuichukulia sanaa hiyo kama zao la jamii,
ambalo pia huweza kuathiri na kuathiriwa na jamii husika. Hoja hii inaungwa mkono
na Vasquez (1973) anaposema kuwa:
… kazi ya fasihi huathiri watu na inachangia katika kuhimiza
au kupuuza dhana zao, maazimio yao, hata maadili yao – ina
msukumo wa kijamii ambao huathiri watu kwa nguvu zake za
5
kihisia na kiitikadi. Ama kwa hakika, hakuna anayebaki kama
alivyokuwa baada ya ‗kuguswa‘ na kazi halisi ya fasihi.
Ni wazi kwamba uwezo wa Fasihi katika kusawiri mambo mbalimbali kama vile
mazingira, uchumi, siasa, mila na desturi, maadili, na saikolojia huweza kuiteka
hadhira na hata kuisababisha ibadili mienendo yake ya maisha. Kwa hali hiyo,
mtunzi anapotunga kazi yake huunganisha vipengele mbalimbali vya uhalisi
kulingana na uwezo alio nao katika kuwasilisha uhalisi huo, hata kama asili hiyo
haikusawiriwa kwa ukamilifu. Hivi ndivyo anavyofanya Euphrase Kezilahabi katika
utunzi wa kazi zake za mwanzo ambazo ni: Rosa Mistika (1971), Kichwamaji
(1974), na Dunia Uwanja wa Fujo (1975). Katika riwaya hizo anasawiri hali ya
mazingira ya jamii yake, kwa kutuibulia matukio ya kujiua.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (2018) na gazeti la Habari Leo la Novemba 5
(2018), kujiua ni janga linalotokea kila siku duniani kote na linawaathiri watu wa
mataifa, tamaduni, jinsi, dini, na matabaka yote. Janga hili linapotokea husababisha
huzuni, majonzi, na matatizo makubwa kwa jamii, hususani katika familia ya
mhusika. Kutokana na hilo, mara nyingi watu hujiuliza maswali mengi wanaposikia
kuwa mtu fulani amejiua. Hujiuliza maswali hayo kwa sababu suala la kujiua ni
gumu, linatisha, na linaogofya. Hii inatokana na namna kila binadamu
anavyoyatazama na kuyapa thamani maisha na mchakato mzima wa kuishi kwake.
Katika hali ya kawaida, kujiua huchukuliwa kama kitendo cha ghafla kinaposikika
masikioni mwa watu. Hata hivyo, kwa maoni yetu, tunaona kuwa kitendo hiki huwa
ni mchakato kwa anayejiua, kwa sababu kabla ya kuchukua uamuzi huo, mhusika
hupitia matukio, mitanziko na miktadha mbalimbali ya kimaisha. Maoni haya
yanaendana na yale ya Muller (1964) na Freeman (1971) wanaoeleza kuwa
mwanadamu huendelea kufa polepole tangu anapozaliwa. Hii inatokana na ukweli
kwamba maisha ya binadamu ni sawa na kitendawili kigumu ambacho jibu lake si
rahisi kulipata. Kutokana na hilo, siku zote binadamu huyo huwa katika mchakato
wa kutaka kutatua kitendawili hicho. Hii ni kwa sababu maisha kwake ni fumbo.
Hali hiyo ya maisha ya binadamu kuwa fumbo ndiyo inayosababisha pia asawiriwe
kwa namna mbalimbali. Kwa mfano, Wamitila (2002) anamsawiri binadamu kama
kiumbe anayeteseka na anayeishi katika ulimwengu usiomjali, aliyezungukwa na
mateso na ubwege, na anayeshindwa kukabiliana au kupatana vyema na uhalisi huo.
6
Hali hiyo ya kuzungukwa na mateso na ubwege huenda ndicho kichocheo cha
kuamua hata kujiua.
Tafiti mbalimbali zinabainisha kuwa kujiua ni tatizo la kisaikolojia linalohusishwa
na michakato kadhaa ya kiafya ambayo hushambulia mfumo wa akili (Freud, 1900;
Ndosi na wenzake, 2004; Glucksman & Kramer, 2017). Zinafafanua zaidi kuwa
msongo wa mawazo, ambao ni tatizo la kisaikolojia, ni chanzo kimojawapo
kinachosababisha mtu kujiua. Hii ni kwa sababu humweka mtu huyo katika hali ya
hofu au wasiwasi kutokana na kuzidiwa na mawazo kwa kukosa jibu la kitu
kilichoko mbele yake au kichwani mwake. Freud (1900) anaeleza kuwa binadamu
huwa na sehemu inayofahamika kama ‗ung‘amuzibwete‘ wa kibinafsi, ambapo fikra
nyingi na mawazo mengi hasi hubuniwa na kuhifadhiwa. Mtaalaamu huyo
anafafanua zaidi kuwa sehemu ya akili ya binadamu huhodhi fikra, mawazo, hofu na
mitazamo hasi, ambayo haiwezi kukubalika katika jamii. Anahusisha masuala ya
saikolojia na ndoto. Anaona kuwa, ndoto huhusisha matukio yaliyotendeka zamani
yanayosheheni maana na ukweli kuhusu maisha. Anaongeza kuwa, kupitia ndoto,
mtu anaweza kukiuka miiko aliyowekewa na kujikamilishia utashi pasipo kukatizwa
wala kukatazwa na wanajamii wengine. Hii ni kwa sababu mwota ndoto, wakati
mwingine, huamini kwamba anayoyaota ni kweli. Hali hiyo huweza kumsababishia
mhusika kuchukua uamuzi autakao, ikiwamo kujiua.
Aidha, wataalamu mbalimbali wamelishughulikia zaidi suala la kujiua kwa jicho la
kisosholojia, kisaikolojia na kiafya (Durkheim, 1979; Practorius, 2006; Tiwari &
Ruhela, 2012; Glucksman & Kramer, 2017; na Shirika la Afya Duniani, 2018).
Baadhi yao kama vile Williams (1970), Friedman (1973), Durkheim (1979),
Neubeck (1986), na Stack (1987) wanabainisha kuwa watu wengi hujiua kutokana na
hali ya kukata tamaa, pamoja na matatizo ya kiakili. Wengine kama vile Glucksman
& Kramer (2017) wanabainisha kuwa kujiua huchochewa na sababu mbalimbali,
zikiwamo za kitabia, kijamii, kibaiolojia, na kiutamaduni; na kwamba, ni vigumu
kumbainisha na kumtambua mtu anayepanga kujiua. Wanataja baadhi ya sababu za
mtu kujiua kuwa ni sonona, maradhi ya hisia mseto, sikizofrenia, matumizi ya dawa
za kulevya, na matumizi mabaya ya pombe na vilevi vingine. Hata hivyo,
wanatahadharisha kuwa, siyo mara zote kujiua ni ishara ya maradhi ya akili.
7
Pia, siyo mara zote maradhi ya akili huweza kusababisha mtu kujiua. Wanabainisha
kuwa kila mtu anayeamua kujiua huwa na sababu zake binafsi zinazomsukuma
kuchukua uamuzi huo. Wanaongeza kuwa, mtu huyo anapobaini kuwa ametengwa
kutokana na mabadiliko ya ghafla ama ya kijamii, kihisia, au kiuchumi,
huchanganyikiwa na huweza kuamua kujiua (Durkheim, 1979). Licha ya tafiti hizo
kufanyika kulingana na malengo yaliyomsukuma kila mhusika, hakuna utafiti
unaoelezea kwa uwazi, matukio yanayounda mchakato wa kujiua na namna
yanavyosawiriwa katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi. Pia, hapajawa na
utafiti wa wazi unaobainisha kama kujiua ni mwangwi wa mtanziko wa kijamii, au
la.
Kimsingi, mchakato wa kujiua unatakiwa pia kushughulikiwa kwa kina katika fasihi,
ikiwamo riwaya, kutokana na ukubwa wa tatizo lenyewe. Tafiti mbalimbali
zinabainisha kuwa kujiua ni tatizo kubwa na linaendelea kukua duniani kote.
Zinafafanua zaidi kwamba lisipofanyiwa kazi kwa kina, litaendelea kuziathiri jamii
nyingi duniani kote, ikiwa ni pamoja na kupoteza nguvu-kazi katika jamii zetu. Kwa
mujibu wa Shirika la Afya Duniani (2018), watu laki nane (800,000) hadi milioni
moja (1,000,000) kila mwaka hujiua duniani kote, huku wengine wengi wakifanya
majaribio ya kujiua. Utafiti huo unaitaja nchi ya Sri Lanka kuwa kinara kwa watu
wake kujiua ikiwa na asilimia 35.3, ikifuatiwa na Lithuania yenye asilimia 32.7, na
Guyana asilimia 29. Kwa upande wa Afrika nchi inayoongoza ni Angola yenye
asilimia 20.5, ikifuatiwa na Afrika ya Kati asilimia 17.5, na Eswatin (zamani ilikuwa
inaitwa Swaziland) yenye asilimia 14.7. Katika Afrika Mashariki, Rwanda inaongoza
kwa kuwa na asilimia 8.5, ikifuatiwa na Burundi asilimia 8, Uganda asilimia 7.2, na
Tanzania asilimia 7. Aidha, ripoti hiyo inabainisha kuwa kitendo hiki cha watu
kujiua kinajitokeza katika marika yote, ingawa kundi linaloongoza ni la vijana wenye
umri kati ya miaka kumi na mitano na ishirini na tisa (15 - 29). Mtafiti anatambua
kuwa ripoti hiyo ni ya kisosholojia, lakini kwa kuwa inazihusu jamii zetu,
alilazimika kulichunguza jambo hilo kwa mwegamo wa kifasihi pia. Hii inatokana na
ukweli kuwa Fasihi ni sanaa ya lugha yenye ubunifu inayojaribu kusawiri vipengele
vya maisha, mahusiano, mazingira na hisia za watu katika muktadha fulani
(Mulokozi, 2017).
8
Kama ilivyobainishwa katika ripoti ya Shirika la Afya Duniani hapo juu, nchi ya
Tanzania pia inakumbwa na tatizo la watu kujiua na linazidi kukua na kuongezeka
mwaka hadi mwaka. Katika kuthibitisha ukubwa wa tatizo hilo, gazeti la Habari Leo
(2018) linaeleza kwamba watu wanaojiua hapa nchini idadi yao ni kubwa na
linatisha. Taarifa hiyo inazidi kubainisha kuwa idadi ya watu waliojiua kwa
kujinyonga kuanzia mwaka 2016 hadi Juni mwaka 2018 ni mia tatu thelathini na tatu
(333). Inazidi kubainisha kuwa idadi ya watu waliojiua mwaka 2016 ni 131. Uwiano
wa kijinsi ni kama ifuatavyo: Mwaka 2016 wanaume walikuwa 106 na wanawake
25. Mwaka 2017 wanaume 81 na wanawake 7, na mwaka 2018 kuanzia mwezi
Januari hadi Juni, matukio ya kujiua yaliongezeka hadi kufikia 113. Taarifa hiyo
inaitaja Mikoa iliyoongoza kwa watu kujiua kwa kujinyonga kuwa ni Mwanza
matukio 29, Mbeya matukio 18, Dodoma matukio 11, Tabora matukio 11, na
Shinyanga matukio 8. Ikumbukwe kuwa matukio haya ni yale tu yaliyoweza
kuripotiwa na kumbukumbu zake kuhifadhiwa, kwani inawezekana kabisa kuwa
yako mengine ambayo hayakuripotiwa.
Kushamiri kwa tatizo hilo duniani kote, ikiwamo Tanzania, kulileta hamasa na
msukumo wa kufanyika kwa utafiti huu. Msukumo huu ulitokana na ukweli kwamba,
licha ya tatizo hili kushughulikiwa zaidi katika nyuga za Afya, Saikolojia na
Sosholojia, bado linaendelea kushamiri siku hadi siku. Aidha, tafiti za Fasihi ya
Kiswahili zilikuwa hazijabainisha kwa uwazi matukio ya mchakato wa kujiua
pamoja na sababu za mitanziko ya wahusika katika riwaya teule. Pia, uhusiano wa
matukio ya mchakato wa kujiua yanayosawiriwa katika riwaya teule na vichocheo
vya matukio ya kujiua katika jamii haukutathminiwa. Kutokana na hilo, mtafiti
alipata hamasa ya kulishughulikia suala hili kwa mwegamo wa kifasihi kama njia
mojawapo ya kutoa mchango wa uga huu wa Fasihi katika jitihada za kulipatia
suluhisho tatizo hili. Kwa hiyo, utafiti huu ulikusudia kuchunguza usawiri wa
mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi, ili kubaini kama
kujiua huko ni mwangwi wa mtanziko wa kijamii, au la.
1.4 Tamko la Tatizo la Utafiti
Tafiti mbalimbali za kisosholojia, kisaikolojia na kiafya zimefanyika kuhusu tatizo
la kujiua (Durkheim, 1979; Practorius, 2006; Tiwari & Ruhela, 2012; Glucksman &
Kramer, 2017; na WHO, 2018). Miongoni mwa hizo zililenga kuchunguza ukubwa
9
wa tatizo la watu kujiua, sababu za jumla za kujiua, pamoja na athari zitokanazo na
mtu kujiua. Katika Fasihi ya Kiswahili, tatizo hili la kujiua halijashughulikiwa kwa
kina. Mathalani, tafiti chache zimefanyika kuhusiana na dhana ya maisha kwa jumla
ikihusishwa na nadharia ya udhanaishi. Baadhi ya wataalamu waliolishughulikia
suala hili katika Fasihi ya Kiswahili ni Mulokozi (1983 & 2010), Musau (1985),
Mlacha (1985), Madumulla (1993), Mbatiah (1998), Wamitila (2003), Senkoro
(2007), na Fuluge (2013).
Licha ya tafiti hizo kufanyika na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike, bado lipo
tatizo la watu kujiua kama ilivyofafanuliwa kwenye ripoti ya utafiti uliofanywa na
Shirika la Afya Duniani (2018) na Habari Leo (2018), kama ilivyokwishaelezwa
katika usuli wa tasinifu hii. Kutokana na hali hiyo, zinahitajika jitihada za pamoja
katika kukabiliana nalo, kwani kama halitashughulikiwa kwa kina, litaendelea
kuziathiri jamii zetu, hususani vijana ambao ni nguvu-kazi ya taifa. Pamoja na kuwa
dhima mojawapo ya Fasihi ni kusawiri kisanaa hali ya mwanadamu, mazingira yake,
uhusiano wake na mazingira hayo na hata kuleta mabadiliko bado katika Fasihi ya
Kiswahili hapajawa na utafiti wa kina uliofanyika kwa lengo la kulisawiri tatizo la
kujiua kwa umahsusi wake na kutoa elimu ya namna ya kukabiliana nalo kwa jamii.
Aidha, matukio ya mchakato wa kujiua na sababu za mitanziko ya wahusika
zinazosawiriwa katika kazi za Fasihi hazijabainishwa wazi. Pia, hakuna utafiti
uliofanyika kwa lengo la kutathmini uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya
mchakato wa kujiua katika kazi za fasihi na vichocheo vya matukio ya kujiua katika
jamii. Hivyo, utafiti huu ulilenga kuchunguza usawiri wa matukio ya mchakato wa
kujiua katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi ili kubaini kama kujiua huko ni
mwangwi wa mtanziko wa kijamii au la.
1.5 Malengo ya Utafiti
Tasinifu hii iliongozwa na lengo kuu na malengo mahususi.
1.5.1 Lengo Kuu
Lengo kuu la tasinifu hii lilikuwa kuchunguza usawiri wa mchakato wa kujiua katika
riwaya teule za Euphrase Kezilahabi kama ni mwangwi wa mtanziko wa kijamii, au
la.
10
1.5.2 Malengo Mahususi
a) Kubainisha namna matukio yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya
teule za Euphrase Kezilahabi yanavyosawiriwa;
b) Kubainisha sababu za mitanziko ya wahusika zinazosawiriwa katika riwaya
teule za Euphrase Kezilahabi;
c) Kutathmini uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua
katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii.
1.6 Maswali ya Utafiti
Maswali yaliyoongoza utafiti huu na kuwezesha kufikiwa kwa malengo mahususi
yaliyokusudiwa ni haya yafuatayo:
a) Matukio yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase
Kezilahabi yanasawiriwa namna gani?
b) Sababu za mitanziko ya wahusika zinazosawiriwa katika riwaya teule za
Euphrase Kezilahabi ni zipi?
c) Kuna uhusiano gani baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua
katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii?
1.7 Manufaa ya Matokeo ya Utafiti
Matokeo ya utafiti uliofanyika yatakuwa na manufaa makubwa katika uga wa Fasihi
na jamii kwa jumla. Manufaa hayo ni pamoja na:
Mosi, kusaidia jamii kufahamu matukio ya mchakato wa kujiua, sababu za mitanziko
ya wahusika kujiua katika jamii, pamoja na athari za miktadha mbalimbali ya maisha
ya jamii anayopitia mhusika katika maisha yake, ambayo huweza kusababisha
mhusika kufikia maamuzi ya kujiua. Kufahamika kwa matukio, sababu na athari za
miktadha hiyo kutawezesha jamii kupata elimu juu ya masuala ya kujiua, na hivyo
kupunguza tatizo hilo.
Pili, kwa kuwa uchambuzi ambao umefanyika umeonesha mtagusano wa kitaaluma
kwa kuzishikamanisha nyuga za Afya, Saikolojia, Sosholojia, na Fasihi, mwingiliano
huo wa kitaaluma utaongeza ufahamu zaidi kwa watafiti wengine kutambua kuwa
matatizo ya kisosholojia, kama lilivyo la kujiua, yanaweza pia kushughulikiwa katika
11
uga wa Fasihi na nyuga nyinginezo za kitaaluma, na hivyo kupatiwa masuluhisho
kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Tatu, inatarajiwa kuwa tasinifu hii italeta manufaa kinadharia na kiuhakiki. Kwa
upande wa nadharia, licha ya kuendeleza nadharia ya kidhanaishi ambayo
imezoeleka katika uhakiki na uchambuzi wa kazi za Euphrase Kezilahabi, pia utafiti
huu umetumia nadharia nyingine, ambayo ni Sosholojia ya Kifasihi. Kabla ya
kufanyika kwa utafiti huu, kulingana na upeo wa mtafiti, nadharia hii ilikuwa
haijawahi kutumika katika uhakiki wa riwaya teule za Euphrase Kezilahabi. Aidha,
tasinifu hii imependekeza nadharia nyingine zinazofaa katika uhakiki wa kazi zenye
mwelekeo wa kidhanaishi. Nadharia hizo ni pamoja na: nadharia ya korasi, nadharia
ya usimulizi, nadharia ya simiotiki, nadharia ya uhalisia, na nadharia ya Saikolojia
changanuzi. Kutumiwa kwa nadharia hizo katika uhakiki wa kazi za Euphrase
Kezilahabi, kutasaidia kubainisha mambo mengine yanayosawiriwa katika kazi hizo
katika kuihakiki jamii.
Nne, matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kuwa na faida kwa watafiti wengine, kwani
yataongeza hamasa ya kufanyika kwa tafiti nyingine zenye mwelekeo wa kuzihakiki
jamii katika nyanja mbalimbali. Kichocheo cha kufanyika kwa tafiti hizo ni pamoja
na mapendekezo yaliyotolewa katika tasinifu hii.
Tano, matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kuwa chanzo kimojawapo cha taarifa kwa
watafiti na wasomaji wengine wanaochunguza na kutafiti kazi mbalimbali za Fasihi
kwa kutumia nadharia ya Kisosholojia na nadharia ya Kidhanaishi kwa kuhusianisha
na jamii za Kitanzania. Aidha, watafiti na wasomaji hao wataweza kupata maarifa
yanayohusiana na taaluma nyingine kama vile Saikolojia, Sosholojia, Afya, pamoja
na Sayansi za Jamii kwa jumla.
1.8 Mawanda ya Utafiti
Utafiti huu ulihusu usawiri wa mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase
Kezilahabi tu, ambazo ni Rosa Mistika, Kichwamaji, na Dunia Uwanja wa Fujo na
kama ni mwangwi wa mtanziko wa kijamii au la. Tunatambua kuwa ni vigumu
kuchunguza dhana hii ya kujiua katika riwaya zote za Kiswahili au jamii nzima ya
Watanzania kutokana na suala la muda na rasilimali. Hata hivyo, tunaamini kuwa
matokeo ya utafiti huu yameweza kuakisi matukio ya mchakato wa kujiua
12
yanayosawiriwa katika kazi za Fasihi kwa jumla. Hii ni kwa sababu: Mosi, kazi zote
za fasihi zinachota malighafi kutoka katika jamii; hivyo, yaliyomo katika riwaya
teule yametosha kuwakilisha yale yaliyomo katika riwaya nyingine, ambazo
hazikushughulikiwa na utafiti huu. Pili, jamii ya mwandishi wa riwaya teule inafaa
kuwakilisha jamii nyingine za Tanzania kwa kuhusianisha matukio na miktadha ya
kijamii inayopatikana katika jamii hiyo. Tatu, kwa kuwa data zilizotumika katika
utafiti huu zilipatikana kutoka katika makundi mbalimbali ya watafitiwa, tunaamini
kuwa makundi hayo yalisaidia katika upatikanaji wa data wakilishi kwa jamii pana
ya Watanzania. Hii inatokana na ukweli kwamba matukio ya watu kujiua
yanajitokeza pia katika jamii nyingine za Watanzania.
Hivyo, katika kuchambua usawiri wa mchakato wa kujiua katika riwaya teule za
Euphrase Kezilahabi tulichunguza kama kujiua huko ni mwangwi wa mtanziko wa
kijamii au la. Hata hivyo, pale ambapo mifano mingine nje ya kazi hizo teule
imetumika, mifano hiyo isichukuliwe kama data za msingi, bali kutumika kwake
kulilenga kujenga na kuthibitisha au kuwezesha hoja mbalimbali kuwa madhubuti na
kueleweka zaidi.
1.9 Muhtasari wa Sura ya Kwanza
Sura hii ya kwanza imeweka msingi wa utafiti huu kwa kujadili vipengele vya
utangulizi kuhusu lengo la utafiti wetu. Vipengele muhimu vilivyoshughulikiwa ni
ufafanuzi wa dhana muhimu, usuli wa tatizo la utafiti, tamko la utafiti, na malengo
ya utafiti. Vipengele vingine ni maswali ya utafiti, manufaa ya matokeo ya utafiti, na
mipaka ya utafiti. Vipengele hivi vilimpa mtafiti mwanga na mwelekeo wa kufanya
utafiti ili kubaini ni nini hasa alikusudia kufanya, na ni nini matokeo ya utafiti wake.
Kupitia vipengele hivi, mtafiti alibaini kuwa tatizo la watu kujiua ni kubwa katika
jamii zetu na linaendelea kuziathiri jamii zote duniani. Kutokana na hilo, alibainisha
kwa ufupi umuhimu wa kufanyika kwa utafiti huu kwa kueleza kuwa jamii inatakiwa
kushirikiana na kuchukua jitihada za pamoja ili kulishughulikia kwa kina tatizo hili.
Sura inayofuata inahusu mapitio ya maandiko mbalimbali yaliyowezesha mwanya
wa utafiti huu kubainishwa. Aidha, inajadili viunzi vya nadharia zilizomwongoza
mtafiti na kuwezesha matokeo ya utafiti huu kupatikana.
13
SURA YA PILI
MAPITIO YA MAANDIKO NA KIUNZI CHA NADHARIA
2.1 Utangulizi
Sura hii inahusu mambo makuu mawili. Jambo la kwanza, ni mapitio ya maandiko
mbalimbali kuhusiana na mada yetu. Jambo la pili, ni ufafanuzi wa viunzi vya
nadharia zilizotumika katika mchakato mzima wa ukusanyaji na uchambuzi wa data.
2.2 Mapitio ya Maandiko
Katika sehemu hii, tumepitia maandiko mbalimbali yanayohusiana na mada yetu.
Mapitio hayo yamegawanywa katika sehemu tatu, ambazo ni: mapitio ya maandiko
kuhusu kazi za Kezilahabi kwa jumla, mapitio kuhusu mchakato wa kujiua katika
riwaya teule za Kezilahabi, na mapitio kuhusu dhana ya kujiua kwa mitazamo ya nje
ya Fasihi. Sehemu hii inahitimishwa kwa kufafanua mwanya uliokusudiwa kuzibwa
kupitia tasinifu hii.
2.2.1 Mapitio Kuhusu Kazi za Kezilahabi kwa Jumla
Ziko tafiti na tahakiki mbalimbali kuhusu kazi za Kezilahabi, hususani riwaya,
ambapo kila mtafiti na mhakiki amefanya utafiti wake kulingana na malengo
yaliyomsukuma kufanya hivyo. Miongoni mwa wataalamu waliohakiki kazi za
Kezilahabi ni Mulokozi (1983, 2010); Senkoro (1982, 2007 & 2011), Musau (1985),
Mlacha (1985), Madumulla (1993), na Mbatiah (1998).
Mulokozi (1983) anaeleza dhamira ya uhusiano wa mtu binafsi na jamii. Pia,
anafafanua tatizo la mtu kutengwa au kubaguliwa na jamii yake. Anaeleza kuwa,
ingawa mtu binafsi ana hiari ya kufanya fujo zake, lakini hana nguvu mbele ya jamii,
na kwamba anapogombana nayo, yeye ndiye atakayeumia, kwani fujo ya mtu binafsi
huhanikizwa na fujo ya jamii au taifa. Anaendelea kueleza kuwa katika riwaya ya
Dunia Uwanja wa Fujo, kuna wahusika waliotengwa na jamii kutokana na matendo
yao. Kwa mfano, Mugala kutokana na uchawi1, Makoroboi kwa sababu ya wizi,
vijana wazinzi kwa sababu ya kuzini hadharani na kuvunja miiko ya jamii, Dennis
1 Ufundi wa kutumia dawa au vitabu maalumu vya uganga ili kuleta madhara kwa
viumbe (TUKI, 2014).
14
kwa sababu ya usomi, utajiri wake, na kazi ya upelelezi, na Tumaini kwa sababu ya
uzinzi, kazi ya upelelezi, na hatimaye ubepari wake. Anaeleza zaidi kuwa Tumaini,
ambaye ni mhusika mkuu alichukiwa na kijiji kizima kwa kuharibu mabinti za watu,
kwa kuwatia mimba, pamoja na fedheha ya wazazi wake kutokana na tabia za
uchawi. Kutokana na hilo, aliamua kuhama pale kijijini na kukimbilia mjini, kwani
aliona hawezi kushinda vita vyake dhidi ya kijiji. Hata hivyo, pamoja na kwamba
andiko hilo halielezi moja kwa moja kuhusu usawiri wa mchakato wa kujiua kama ni
mwangwi wa mtanziko wa kijamii au la, bado lilikuwa muhimu katika utafiti huu.
Hii ni kwa sababu linabainisha baadhi ya mambo na matukio kama vile mtu
kujitenga kijamii au kutengwa na jamii ambayo humletea mtu upweke na msongo wa
mawazo, hatimaye, huweza kusababisha mtu huyo kujiua.
Naye Musau (1985), kupitia riwaya za Rosa Mistika, Kichwamaji, na Dunia Uwanja
wa Fujo, alishughulikia suala la maana ya maisha. Anamwona Kezilahabi kama mtu
aliyekata tamaa. Anafafanua kuwa dunia ni uwanja wa fujo na mahala pasipo na
furaha. Utafiti huo wa Musau ulikuwa na umuhimu mkubwa sana katika utafiti huu.
Hii ni kwa sababu umesaidia na kumpa mwanga mtafiti wa kuyafahamu masuala ya
furaha, sababu za kukata tamaa ya maisha, na namna yanavyowaathiri wahusika
katika kazi hizi. Hata hivyo, utafiti huo bado hauelezi lolote kuhusu usawiri wa
mchakato wa kujiua katika kazi hizo, na kama ni mwangwi wa mtanziko wa kijamii
au la. Tasinifu hii ilipata nafasi ya kulishughulikia suala hilo kwa kina.
Mbatiah (1998) anaeleza kuwa kazi za Euphrase Kezilahabi zinaweza kugawanywa
katika vipindi viwili: yaani, kipindi cha kwanza zilipoandikwa riwaya za awali
ambazo ni: Rosa Mistika, Kichwamaji, Dunia Uwanja wa Fujo, na Gamba la Nyoka.
Anaeleza kuwa katika riwaya hizi zote kuna sifa nyingi za kimaudhui na kimtindo
zinazolingana. Anaongeza kuwa riwaya hizo ni za kiuhalisia kwa sababu zinaelezea
maisha halisi ya Watanzania baada ya uhuru na Azimio la Arusha. Katika uchambuzi
wake, anaegemea kwenye nadharia ya Udhanaishi na anaeleza kuwa Rosa Mistika
aliathiriwa na mazingira yaliyomlea. Anaichambua zaidi riwaya ya Rosa Mistika na
anaona kuwa imetawaliwa na hisia ya kicheko cha uchungu, kwa sababu mwandishi
anaicheka jamii yake kwa kushindwa kuwalea watoto wake wa kike. Aidha, katika
Kichwamaji, mwandishi anajadili masuala kama vile kifo, furaha, maisha na uwepo
wa Mungu. Kutokana na hilo, tunapata falsafa kuhusu dhana ya ‗kichwamaji‘ kuwa
15
ni ishara ya ukosefu wa mawazo mwafaka katika muktadha wa jamii, ambayo ni
alama ya mkengeuko. Katika Dunia Uwanja wa Fujo tunapata mwendelezo wa
mjadala kuhusu tatizo la maisha kama lilivyoanza kujadiliwa katika Kichwamaji.
Hapa tunaelezwa kuwa maisha ya mwanadamu ni vurumai ambayo huletwa
ulimwenguni na watu fulani katika nyakati mbalimbali za kihistoria. Andiko hili
lilikuwa muhimu kwa utafiti wetu kwa sababu lilitupa taswira ya wahusika
wanaochunguzwa katika utafiti huu. Pia, lilimpa mtafiti welewa zaidi kuhusu
nadharia ya Udhanaishi, ambayo ni mojawapo ya nadharia alizozitumia katika utafiti
wake.
Katika kipindi cha pili, Mbatiah anaziangalia riwaya za Euphrase Kezilahabi ambazo
ni Nagona na Mzingile. Katika uchunguzi wake, anadai kuwa riwaya hizi si za
kiuhalisia, kwani zimejikita katika udhanaishi na zinaelezea kitendawili kuhusu
maisha ya mwanadamu na nafasi yake ulimwenguni. Anafafanua zaidi kuwa riwaya
hizi zinamtoa msomaji katika mazingira halisi ya kiulimwengu aliyoyazoea na
kumpeleka kwenye ulimwengu wa kindoto baina ya kifo na uhai, baina ya kuwa
macho na kuwa na usingizi, na msomaji anasafiri kifikra kwa kuutalii ulimwengu ili
kujua ukweli wake. Anaendelea kueleza kuwa mwanadamu hawezi kupata fanaka na
furaha maishani mwake kwa sababu ulimwengu ni mbovu na haumjali; na kwamba,
juhudi anazofanya ili kujiendeleza apate furaha daima ni za kumletea maangamizi.
Andiko hili la Mbatiah limekuwa na umuhimu mkubwa katika tasinifu hii kwa
sababu linadokeza baadhi ya mihimili ya nadharia ya Udhanaishi, ambayo ni
mojawapo ya nadharia zilizozitumia katika utafiti wetu. Mihimili hiyo ni pamoja na
kutafuta uhuru binafsi, uwezo wa mtu wa kujifikiria na kujiamulia mambo yake,
pamoja na wajibu wake katika ulimwengu. Msingi mwingine ni kukengeuka kwa
misingi ya jamii husika, kukata tamaa na mauti. Mihimili hii ni muhimu katika utafiti
wetu kwani ndiyo iliyoitumika katika kubaini matukio ya wahusika kujiua na sababu
za mitanziko yao. Pia, andiko hilo linaeleza kuhusu falsafa ya maana ya maisha na
mitazamo ya jamii katika kazi teule, na hivyo kubainisha chanzo cha baadhi ya
wahusika kujiua, ambacho ni kipengele cha msingi kilichokusudiwa kushughulikiwa
katika utafiti huu.
Nao Wamitila (1999) na Senkoro (2006) walihakiki na kutoa maana za majina katika
riwaya za Kezilahabi. Wamitila anaona kuwa majina mengi aliyoyatumia
16
yanaendana na mazingira ya Ukerewe, mahali alikokulia Kezilahabi. Anafafanua
zaidi kwamba, wakati mwingine, majina huweza kutumika kama ploti na motifu.
Katika Rosa Mistika jina la Rosa Mistika lenye maana ya ‗waridi lenye fumbo‘
linamfanya msomaji ajiulize maswali yanayoibua ploti. Wamitila anaendelea
kufafanua kuwa jina lenyewe ni rahisi kueleweka, lakini linamwachia msomaji
taharuki. Anakwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa Kezilahabi ametumia kejeli
katika baadhi ya majina ya wahusika, kama vile, Deogratias katika Rosa Mistika
linalotokana na neno la Kigriki lenye maana ya ‗Asante Mungu‘, lakini tabia za
mhusika haziendani kabisa na jina hilo kutokana na kukosa maadili. Andiko hilo
limekuwa na umuhimu, kwa kuwa lilimhamasisha kufahamu taharuki inayoibuliwa
na msomaji kutokana na jina la mhusika Rosa, ambaye baadaye aliamua kujiua. Hata
hivyo, andiko hilo halikuwa na lengo tulilolishughulikia katika tasinifu yetu. Hivyo,
kutupatia mwanya wa kulishughulikia kwa kina katika utafiti uliofanyika.
Kwa upande wake, Senkoro (2006) alitafiti masuala ya Fasihi ya Kiswahili ya
Majaribio kama makutano ya Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi katika riwaya ya
Rosa Mistika. Anabainisha kuwa, mara kwa mara, wahusika katika Fasihi simulizi
huwakilisha pande kuu mbili: wa wema au haki na wa ubaya au uonevu. Anaendelea
kueleza kuwa, katika riwaya hii, kuna majina ya wahusika ambao tabia zao
hazibadiliki tangu mwanzo hadi mwisho wa riwaya. Akitolea mfano wa jina la Rosa
Mistika, anaeleza kuwa hili ni jina jingine la Bikira Maria likiwakilisha ua waridi
lenye fumbo. Anaona kuwa jina hili ni lile la ua moja wakati Flora (ambalo ni jina la
mdogo wake Rosa Mistika) maana yake ya asili ni mimea, na hivyo hili si la ua moja
wala mmea mmoja tu, bali mimea yote. Anadai kwamba, bila shaka, mwandishi
alitutaka tumwone Rosa Mistika kuwa yu dhaifu sana kama ua moja tu
alinganishwapo na Flora, ambaye anawakilisha mimea yote. Maelezo haya
yanatupatia picha kuwa, inawezekana ndiyo maana hata baada ya vifo vya wazazi
wake, pamoja na kile cha Rosa, Flora aliweza kustahimili kwa kuwalea wadogo
zake, wakati Rosa alichukua maamuzi ya kujiua. Hivyo, kwa kuwa utafiti huo
unadokeza juu ya maisha ya Rosa Mistika ambaye ni mhusika aliyejiua, uliacha
mwanya wa kuyafuatilia maisha yake kwa undani kwa lengo la kubaini mchakato wa
matukio ya kujiua kwake na sababu za mitanziko yake.
17
Aidha, Diegner (2002) alichunguza riwaya za Kezilahabi kwa kujikita katika
kipengele cha sitiari kama inavyoelezwa katika taaluma ya Fasihi. Anaeleza kwamba
riwaya hizi zimebeba falsafa ya udhanaishi na zina mfuatano wa maudhui ambayo ni
ya kihalisi kulingana na mazingira, ikiwa ni pamoja na yale yanayoelezwa ndani
yake. Anaongeza kuwa tunaweza kuzigawa kazi za Euphrase Kezilahabi katika
vipindi viwili: kipindi cha kwanza ambapo mwandishi alishughulikia masuala mazito
ya kijamii kwa kutumia mtindo wa lugha nyepesi kwa wasomaji wake. Anaongeza
kuwa kipindi hiki ni cha Rosa Mistika, Kichwamaji, Dunia Uwanja wa Fujo, na
Gamba la Nyoka. Anabainisha kwamba mandhari aliyotumia mwandishi ni ya
Ukerewe, Mkoani Mwanza, ambapo hata uumbaji wa wahusika wake unafanana.
Mtafiti huyu anaeleza kuwa Kezilahabi anashughulishwa sana na suala la maana ya
maisha na kumtafuta Mungu. Anafafanua zaidi kuwa yote haya yanajitokeza kwa
njia ya istiara. Kipindi cha pili ni wakati zilipoandikwa Nagona na Mzingile. Riwaya
hizi ni tofauti na zile za mwanzo kutokana na kutumia lugha ya kiishara na kitaswira,
na hivyo kutoeleweka kwa urahisi. Hata hivyo, pamoja na ufafanuzi mzuri
uliofanywa na mtafiti huyo, bado suala la kujiua halikushughulikiwa kwa undani
katika utafiti wake, bali limedokezwa tu. Hii ni kwa sababu utafiti huo umezibainisha
riwaya hizo kuwa ni za kidhanaishi tu, pasipo kuelezea kwa kina suala la kujiua.
Hivyo, utafiti huo uliacha mwanya uliouzibwa katika utafiti wetu.
Flavian (2012) alichunguza suala la usimulizi katika riwaya ya Dunia Uwanja wa
Fujo. Anafafanua kuwa tahakiki zilizofanywa kuhusiana na kazi za Kezilahabi
zinajaribu kueleza masuala mbalimbali ya kijamii kama vile falsafa, dhamira, istiara,
na motifu. Anaona kuwa kazi hizi zinaonekana kukamilika kutokana na mbinu za
usimulizi ambazo wahakiki wengine hawakuzishughulikia kwa undani. Pia, anaeleza
namna mwandishi anavyoyasuka matukio, na kumfanya msomaji asafiri na
mwandishi, huku akiwafuatilia wahusika na maudhui wanayoyabeba. Anatolea
ufafanuzi wa Wamitila (1997) anayeeleza kwa ufupi tu kuwa, usimulizi wa riwaya ya
Dunia Uwanja wa Fujo, una athari kubwa kama zilivyo taswira na ishara. Ijapokuwa
utafiti huo haubainishi wala kudokeza lolote juu ya masuala ya usawiri wa mchakato
wa kujiua, bado mawazo yake yametumika kama kianzio cha kuchunguza maisha ya
baadhi ya wahusika na maudhui wanayobeba, ikiwa ni pamoja na hatima zao. Haya
yote yamechangia katika ukamilifu wa tasinifu hii.
18
Naye Ponera (2014) alichunguza jinsi ufutuhi unavyojitokeza katika nathari za
Kiswahili, hususani katika nathari za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi.
Anaona kuwa nathari hizo zimeundwa kwa kutumia ufutuhi kama mbinu mojawapo
ya kibunilizi. Akifafanua kipengele kimojawapo cha ufutuhi ambacho ni furaha,
anaeleza kuwa furaha ni kionjo cha kisaikolojia ambacho huhusu hali ya ukunjufu
wa moyo na bashasha ambayo, aghalabu, hutokana na ridhiko la moyo au nafsi.
Utafiti huo umekuwa na mchango katika utafiti huu, kwa sababu suala la furaha na
uhusiano wake na matukio ya kujiua limeshughulikiwa kwa kina.
Kwa upande mwingine, Chuachua (2016) alichunguza namna maarifa ya Wabantu
yanavyojitokeza katika riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi. Katika
uchunguzi wake, alijikita katika vipengele kama vile, uchawi, tambiko, imani au
fikra kuhusu roho na kifo na moyo. Vipengele vingine ni Mungu, mwanya, uzazi,
utoaji majina, uganga na ardhi. Utafiti huo unahitimisha kuwa kazi hizo
zinawasilisha maarifa halisi ya Wabantu yakiegemea katika misingi ya kiontolojia2.
Ni wazi kwamba utafiti huo unataja baadhi ya vipengele ambavyo vimechunguzwa
katika utafiti huu. Vipengele hivyo ni pamoja na suala la kifo na majina ya wahusika.
Kwa jumla, katika utafiti huu andiko hilo lilimwongezea maarifa mtafiti, hususani
katika kuchunguza dhana ya kifo, na baadhi ya majina ya wahusika kwa lengo la
kubaini sifa na uhusika wao.
2.2.2 Mapitio Kuhusu Mchakato wa Kujiua katika Riwaya za Kezilahabi
Katika kupitia na kuchunguza maandiko kuhusiana na suala la wahusika kujiua,
hususani katika kazi za Kezilahabi, ni maandiko machache sana tuliyofanikiwa
kuyapata. Miongoni mwa maandiko hayo ni: Mulokozi (1983, 2010), Mlacha (1985),
Madumulla (1993), Senkoro (1996), Wamitila (2008), Sakkos (2008), na Fuluge
(2013). Kwa jumla, watafiti hao wanaeleza kuwa, kazi za Kezilahabi zimefungamana
na matukio ya kujiua.
2 Ni maarifa, mtazamo na imani ya jamii kuhusu maisha na kuwapo kwake, na kuhusu ulimwengu
kwa jumla. Ontolojia hujaribu kujibu maswali yafuatayo: Binadamu ni nani au ni nini? Asili ya
binadamu ni nini? Asili ya ulimwengu ni nini? Asili ya mwanamume/mwanamke ni nini? Lengo na
hatima ya maisha ni nini? Je, kuna mamlaka nje ya ulimwengu inayotawala maisha na jaala ya
mwanadamu? Binadamu anahusianaje na ulimwengu na vilivyomo? Wakati ni nini; binadamu
anahusianaje nao? Mauti ni nini? Je, kuna maisha baada ya kufa? (Mulokozi, 2017:343).
19
Mulokozi (1983, 2010) alitafiti maandiko ya Kezilahabi kwa kuangalia maudhui
katika Rosa Mistika, Kichwamaji na Dunia Uwanja wa Fujo. Katika Rosa Mistika,
anaonesha athari ya maisha ya Seminari ambayo mwandishi amekulia, pamoja na
uhasama dhidi ya malezi na maisha hayo. Anaona kuwa kuna dalili za mtazamo wa
kukata tamaa katika kutafakari maisha ambazo zinajitokeza katika riwaya hii. Katika
Kichwamaji, alishughulikia zaidi suala la falsafa na maana ya maisha, kuwapo au
kutokuwapo kwa Mungu na athari za wakoloni. Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa
Fujo, ameonesha dhamira mbalimbali zinazojitokeza ambazo ni pamoja na ndoa,
malezi, uchawi na mazingaombwe, kuwapo kwa maisha, maana yake na kiini cha
riwaya, na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi katika jamii. Anamchukua mtu katika
hatua zote za maisha yake: uzazi na ujana, malezi, ndoa, uzee hadi kifo.
Kwa jumla, Mulokozi anazichambua kazi za Kezilahabi kwa kuzihusisha kwa kiasi
kikubwa na udhanaishi, huku akiwaona wahusika waliojengwa katika kazi hizi kuwa
wamekata tamaa. Mulokozi anakwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa kujiua huko
kwa kukata tamaa pia ni njia ya kukimbia matatizo, njia ambayo haifai. Utafiti huo
umekuwa na umuhimu mkubwa sana katika utafiti wetu kwa sababu unadokeza suala
la maisha ya wahusika na makuzi yao, ambapo kwa upande wetu tumeyachunguza
kama sehemu ya michakato ya kijamii. Hata hivyo, utafiti huo unatofautiana na
utafiti wetu, kwani mtafiti huyo alichunguza maudhui katika riwaya hizo, huku
akihusisha na nadharia ya udhanaishi. Kwa upande wa utafiti wetu, tumeshughulikia
usawiri wa mchakato wa kujiua katika riwaya teule kwa kuuhusisha na mwangwi wa
mtanziko wa kijamii. Aidha, kwa upande wa nadharia, tumetumia nadharia ya
Udhanaishi na Sosholojia ya Kifasihi.
Mlacha (1985) aliangalia udhanaishi unaojitokeza katika nathari za Kezilahabi.
Alibainisha matukio kama vile ulevi, kujiua na kuua ambayo yanaashiria
kuchanganyikiwa kwa akili. Kulingana na mwelekeo wa malengo yake, andiko hili
halijatoa ufafanuzi wa kutosha kuhusu nini husababisha mtu kuchanganyikiwa, bali
linadokeza baadhi tu ya vipengele vya udhanaishi na kuishia kueleza kuwa matukio
hayo huashiria kuchanganyikiwa kwa akili. Hivyo, utafiti huo ulikuwa muhimu kwa
mtafiti katika kuchunguza usawiri wa vipengele vingine vya kidhanaishi na namna
vinavyohusiana na dhana ya kujiua katika riwaya teule za Kezilahabi. Aidha, utafiti
umechunguza matukio yanayounda mchakato wa kujiua, pamoja na namna athari za
20
miktadha ya maisha ya jamii inavyochangia katika kumwathiri mhusika kiasi cha
kufikia hatua ya kujiua kama ilivyowatokea wahusika katika riwaya teule.
Madumulla (1993) alitafiti namna wahusika katika nathari za Kezilahabi, kama vile
Rosa Mistika, Kichwamaji, Gamba la Nyoka, Cha Mnyonge Utakitapika Hadharani
na Mayai Waziri wa Maradhi, wanavyojiua. Katika utafiti wake, anaona kwamba
Kezilahabi ana upungufu wa kisanii katika kutafuta suluhu za matatizo yawapatayo
wahusika wake. Anabainisha upungufu wa mwandishi huyo kwamba unatokana na
namna anavyoumba wahusika wake wanaoamua kujiua kwa lengo la kuyakwepa
matatizo ya kijamii. Anaongeza kwamba kujiua hakumalizi tatizo la jamii, bali
pengine humaliza kwa kiasi fulani matatizo ya aliyejiua na kuyahamishia matatizo
hayo kwa wanaobaki hai. Mtafiti huyo amefanikiwa kubainisha aina ya wahusika
wanaopatikana katika kazi za Kezilahabi, huku akidokeza tu kuhusu udhaifu wa
mwandishi huyu. Hatimaye, anatoa hitimisho la jumla kuhusu mwandishi huyu
anavyowaumba wahusika hao wanaojiua pasipo kutoa suluhisho la nini kifanyike.
Hivyo, utafiti huo haujakidhi maswali yote kuhusu matukio ya wahusika kujiua na
mitanziko inayosababisha kujiua kwao. Kutokana na andiko hilo kushindwa
kubainisha matukio na sababu za mitanziko ya wahusika, utafiti huu umeshughulikia
masuala hayo kwa kina na kuziba mwanya uliokuwa umeachwa na andiko hilo.
Aidha, Senkoro (1996) amezichambua kazi za Kezilahabi kwa jicho la kidhanaishi
kwa kuchunguza maana ya maisha. Anasema kuwa uchotarishaji katika kazi za
mwandishi huyu ulianzia katika zile riwaya za mwanzo, yaani Rosa Mistika,
Kichwamaji, na Dunia Uwanja wa Fujo. Anaona kuwa kazi hizi zinajishughulisha
na suala la maana ya maisha kwa kutumia mazingira ya vijijini na miji ya Tanzania,
lakini kwa jicho la udhanaishi. Kimsingi, udhanaishi huyaona maisha kuwa ni kitu
kisichokuwa na maana. Hii ndiyo sababu wahusika wa Kezilahabi kama vile
Kazimoto wa Kichwamaji, Rosa Mistika na Charles wa Rosa Mistika, mwishoni
wanaamua kuwa maisha hayana maana; kwa hiyo, ama wanaamua kujiua (Kazimoto
na Rosa) au wanaamua kujitenga na uwongo wa maisha hayo kwa kugeuka kuwa
buruda (Charles). Makala yake hiyo imetalii kwa kiasi kikubwa udhanaishi
unaojitokeza katika kazi za Kezilahabi. Inaeleza kuwa Kezilahabi alifanya majaribio
na falsafa ya udhanaishi, akionesha kuwa maisha hayana maana, kwani mtu
anazaliwa ili afe. Kwa Kezilahabi, maisha ni fumbo sawa na Rosa alivyo ua waridi
21
lenye fumbo. Hata hivyo, pamoja na kutalii sana katika suala la udhanaishi, bado
uhakiki wake unaacha mwanya wa utafiti, kwa sababu hauelezi lolote kuhusu usawiri
wa mchakato wa kujiua katika riwaya hizo, na kama ni mwangwi wa mtanziko wa
kijamii, au la. Pia, haudokezi lolote kuhusu matukio ya mchakato wa kujiua na
namna yanavyosawiriwa katika riwaya hizo.
Sakkos (2008) alihakiki riwaya ya Kichwamaji kwa kutumia nadharia ya Udhanaishi
na ile ya Ufeministi ili kubaini nadharia inayofaa katika kuchambua riwaya hii.
Anaeleza habari za Kazimoto kwenda kuomba kazi kwa Mkuu wa Wilaya ambaye
pia ni rafiki yake wa utotoni. Baada ya kunyimwa kazi, anajiona kama mtu
aliyetengwa na kila mtu katika jamii yake. Inaelezwa mikasa aliyoipitia Kazimoto
baada ya kifo cha dada yake (Rukia), mama yake, na mkewe (Sabina) kumzalia
mtoto mwenye kichwa kikubwa. Kutokana na majanga yote hayo, Kazimoto alikosa
tumaini na kuamua kujiua. Kazi hii ni muhimu, kwa kuwa imempa mtafiti mwanga
wa kuyamulika kwa kina maisha ya Kazimoto na kubainisha sababu za za kujiua
kwake.
Kwa upande wake, Wamitila (2008) amehakiki riwaya ya Rosa Mistika, Kichwamaji,
Dunia Uwanja wa Fujo, na Gamba la Nyoka. Katika uhakiki wake, anaeleza kuwa
kazi hizi, zimefungamana na matukio ya vifo. Vilevile, anaeleza kuwa kazi hizi
zimeangalia maana ya maisha, nafasi ya Mungu katika ulimwengu, nafasi ya mtu
binafsi dhidi ya jamii, na dhana ya furaha na kifo. Anaona kuwa Kezilahabi
ameathiriwa na waandishi wa kidhanaishi kama vile Martin Heidegger (1889),
Friedrich Nietzche (1844), Samuel Beckett (1975), Albert Camus (1913) na
wengineo walioandika kazi zao zilizobobea katika falsafa hii. Ni wazi kuwa kazi
hiyo imekuwa mwanga katika utafiti huu, kwani inadokeza baadhi ya sifa za
udhanaishi, pamoja na sifa za mwandishi. Hata hivyo, kazi hiyo haielezi kwa kina
kuhusiana na matukio ya kujiua pamoja na athari za miktadha ya kijamii
inayosawiriwa katika mchakato wa mtu kujiua. Hivyo, utafiti huu ulikusudia
kuchunguza usawiri wa mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase
Kezilahabi kwa kuuhusisha na uhalisi katika jamii.
22
2.2.3 Mapitio Kuhusu Dhana ya Kujiua kwa Mitazamo ya Nje ya Fasihi
Kama ilivyoelezwa hapo awali, tatizo la kujiua, kwa kiasi kikubwa, limefanyiwa
utafiti katika nyanja za sosholojia, saikolojia na afya. Hapa chini tunadokeza kazi
chache zinazohusu suala hilo la kujiua.
Durkheim (1979) anahusisha tatizo la kujiua na suala la kujitenga kijamii.
Anafafanua kuwa suala la kujiua linatokana na kujitenga kijamii na linaonekana zaidi
vijijini, ikilinganishwa na mijini. Anaongeza kuwa mtu anayepanga kujiua
anapobaini kuwa ametengwa kutokana na mabadiliko ya kijamii, kihisia, au
kiuchumi, huchanganyikiwa na huweza kujiua. Licha ya kuwa kazi hiyo ni ya
kisosholojia, na kwamba inadokeza mojawapo ya sababu zinazoweza kusababisha
mtu kujiua, bado haielezi kwa kina kuhusu matukio ya mchakato wa kujiua na
sababu za mitanziko ya wahusika inayoweza kusababisha mtu kujiua. Hata hivyo,
kazi hiyo imekuwa na umuhimu katika utafiti wetu, kwani ilimpa mtafiti maarifa ya
awali katika kuchunguza na kubainisha matukio ya mchakato wa kujiua na sababu za
mitanziko ya wahusika zinazosababisha mtu kujiua.
Maltsberger (1993) katika utafiti wake anaona kuwa kujiua kuna uhusiano na
masuala ya ndoto. Anaeleza kwamba ndoto hutufundisha mambo yasiyo ya hiari
kuhusu suala la kujiua ambalo linahusishwa na dalili za mtu kukosa uvumilivu.
Anaongeza kwamba, mara nyingi, mgonjwa aotaye ndoto za kutaka kujiua huwa na
lengo la kutaka kulipa kisasi kwa yaliyompata. Pia, hukusudia kumwadhibu
aliyemsababishia matatizo, mfadhaiko na huzuni aliyo nayo, na/au kuanza maisha
mapya tofauti na yale anayopitia, ili kujitenga na dunia aliyopo. Maelezo haya
yanabainisha wazi kwamba suala la kujiua ni la kimchakato, na siyo la ghafla. Kazi
hiyo ilikuwa muhimu katika utafiti huu, kwani imemsaidia mtafiti kufahamu
mchakato wa matukio yanayohusiana na masuala ya kujiua na namna
yanavyosawiriwa katika riwaya teule.
Ndosi na wenzake (2004) wanabainisha kuwa kujiua ni chanzo cha pili au cha tatu
cha vifo vinavyowapata vijana baada ya vile vinavyotokana na ajali. Wanaongeza
kuwa, kwa kila jaribio moja la mtu kujiua, kuna majaribio mengine manane ya watu
kutaka kujiua. Baadhi ya sababu zinazobainishwa katika kazi hiyo ni matatizo ya
akili ambayo humsababishia mhusika kupata msongo wa mawazo, na kutumia
23
madawa ya kulevya na vilevi vingine. Sababu nyingine ni migogoro ya kijamii na
wahusika kuugua kwa muda mrefu. Kazi hii ni muhimu, kwani imempa mtafiti
mwanga wa kuyajua baadhi ya matukio ya kujiua, pamoja na sababu za mtu kujiua.
Hata hivyo, kwa kuwa haielezi kwa uwazi kuhusu matukio ya mchakato wa kujiua
na sababu za mitanziko ya wahusika, iliacha mwanya kwa utafiti kushughulikia
masuala hayo kwa kina.
Glucksman na Kramer (2017) wanabainisha kwamba kujiua kunatokana na sababu
mbalimbali, zikiwamo za kitabia, kijamii, kibaiolojia na kiutamaduni. Wanaendelea
kufafanua kuwa ni vigumu kubainisha wazi na kumtambua mtu anayepanga kujiua.
Watafiti hawa wanaona kwamba suala la ndoto na majaribio ya kutaka kujiua
kutokana na huzuni au mfadhaiko wa mawazo ni chanzo kimojawapo kikubwa
kinachoweza kusababisha mtu kujiua. Wanaelezea zaidi kwamba kuna tofauti kubwa
baina ya wagonjwa wenye mfadhaiko na dalili za kujiua, na wale walio na
mfadhaiko, lakini hawana dalili za kutaka kujiua. Glucksman na Kramer (2017:17)
wanayashadidia zaidi kwa kusema:
…the manifest dream content of depressed, non-suicidal patients
differs from that of depressed, suicidal patients. The dream
imagery of depressed, suicidal patients contains themes of death,
dying, violence, and depature. The dream imagery of depressed,
non-suicidal patients contains themes of rejection, helplessness,
hopelessness, humiliation, failure and loss.
…mambo yanayodhihirika kwenye ndoto za wagonjwa wenye
mfadhaiko wasiokusudia kujiua ni tofauti na yale ya wagonjwa
wa mfadhaiko wanaokusudia kujiua. Taswira ya ndoto kwa
wagonjwa wa mfadhaiko na wanaokusudia kujiua huwa na
mawazo ya kifo, kufa, vurugu, na kutoweka. Taswira ya ndoto
kwa wagonjwa wa mfadhaiko wasiokusudia kujiua hubeba
mawazo ya kukataliwa, kukosa msaada, kukosa tumaini
kutothaminiwa/kunyanyapaliwa, kushindwa na kuchanganyikiwa
(Tafsiri ya Mtafiti).
Utafiti wa wataalamu hawa umetupa picha kwamba kuna uhusiano baina ya ndoto na
kujiua, na kwamba anayepanga kujiua hupitia mchakato na mlolongo wa matatizo
ambayo, hatimaye, humsababisha kuwaza kuutoa uhai wake kwa kujiua. Hata hivyo,
licha ya kuwa utafiti huo hauelezi kwa kina kuhusu usawiri wa mchakato wa kujiua
kama ni mwangwi wa mtanziko wa kijamii, au la, umesaidia katika kubainisha
24
baadhi ya matukio anayopitia mhusika kabla ya kuchukua uamuzi wa kujiua katika
riwaya teule za Euphrase Kezilahabi.
2.2.4 Mwanya Uliotakiwa Kuzibwa na Utafiti
Baada ya kupitia maandiko mbalimbali kuhusiana na mada yetu, tulibaini mwanya
ambao ulileta msukumo wa kufanyika kwa utafiti huu. Mwanya huo unajitokeza kwa
nia kuu tatu ambazo ni:
Mosi, watafiti wengi katika mapitio ya Kiswahili hawakubainisha kwa kina matukio
ya mchakato wa kujiua, sababu za mitanziko ya wahusika, na miktadha ya maisha ya
jamii inayosawiriwa katika mchakato wa kujiua. Matukio ya kujiua katika tafiti hizo
yametazamwa kama kitendo tu cha kukata tamaa kwa wahusika; na kwamba, huo ni
udhaifu wa mwandishi katika kuumba wahusika wenye kukata tamaa.
Pili, watafiti mbalimbali wamechunguza tatizo la kujiua katika kazi za Kezilahabi
kwa jicho la kidhanaishi. Wamebainisha kuwa wahusika katika kazi hizo hujiua
kutokana na kukata tamaa. Hata hivyo, tafiti zao hazikuhusisha nadharia hiyo ya
Udhanaishi na ile ya Sosholojia ya Kifasihi ili kubaini namna mchakato wa kujiua
unavyohusiana na kuathiriwa na miktadha ya kijamii. Aidha, katika kazi za
mwandishi huyu, mchakato wa matukio ya kujiua, sababu za mitanziko ya wahusika,
pamoja na tathmini ya uhusiano wa matukio ya mchakato wa kujiua na vichocheo
vya matukio ya kujiua katika jamii, haikushughulikiwa kwa kina.
Tatu, matukio ya watu kujiua, kwa kiasi kikubwa, yamekuwa yakitazamwa kwa
jicho la kisosholojia, kisaikolojia na kiafya, pasipo kuhusishwa na Fasihi (Ndosi na
wenzake, 2004; Shirika la Afya Duniani, 2018; na Habari Leo, 2018). Katika
mapitio yetu, tulibaini kuwa tafiti nyingi za kifasihi zilizolishughulikia tatizo hili la
kujiua, zimejikita zaidi katika matini zenyewe pasipo kuchunguza hali halisi ya tatizo
hili katika jamii. Kutokana na hilo, palikuwa na haja ya kufanyika utafiti wenye
mwelekeo huo ili kulishughulikia kifasihi, huku tukihusisha na data halisi
zinazopatikana katika jamii mahususi.
2.3 Viunzi vya Nadharia
Utafiti huu uliongozwa na nadharia mbili, ambazo ni: Nadharia ya Udhanaishi na
Nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi. Misingi ya nadharia hizi ndiyo iliyomwongoza
25
mtafiti katika mchakato wote wa ukusanyaji wa data, uchambuzi na uwasilishaji
wake.
2.3.1 Nadharia ya Udhanaishi
Udhanaishi ni harakati au hali ya kukata tamaa inayoendana na kuyaona maisha
kuwa ni kitu kisichokuwa na maana. Hufungamana na kukata tamaa, ulevi, na hata
kujiua. Camus (1984) anauelezea udhanaishi kuwa ni falsafa inayoshughulikia
masuala mbalimbali kuhusu maisha. Anaugawa katika mitazamo miwili: mosi,
maisha kama ombwe, yaani mahali patupu, na kwamba maisha hayana faida yoyote.
Pili, kujiua kama suluhisho la matatizo anayopitia au anayokabiliana nayo binadamu
duniani kwa kuamini kwamba hakuna maisha baada ya kifo. Wamitila (2003)
anauelezea udhanaishi kuwa ni maono au mtazamo unaohusiana na hali na maisha ya
binadamu, nafasi na majukumu yake ulimwenguni na uhusiano wake na Mungu. Nao
Wafula na Njogu (2007) wanauelezea Udhanaishi kuwa ni falsafa inayotokana na
‗utamaushi‘, yaani kutokuwa na furaha, na kukosa tumaini katika maisha kulingana
na namna yalivyo.
Wataalamu wengi wanaamini kwamba falsafa ya udhanaishi inatokana na mawazo
ya mwanatheolojia Soren Kierkegaard (1813 - 1855) kutoka Denmark. Katika vitabu
vyake vya Fear and Trembling (1843), The Concept of Dread (1844), na Sickness
unto Death (1849), Kierkgaard anashikilia kwamba mtu ni kikaragosi cha nguvu
zilizomuumba na za kijamii. Kwa jumla, wadhanaishi huyaona maisha ya mtu kuwa
ni ya kitanzia na hayana maana, kwa kuwa mwisho wa mwanadamu ni kifo.
2.3.1.1 Misingi ya Nadharia ya Udhanaishi
Misingi ya nadharia hii ni pamoja na:
a) Kujadili matatizo halisi yanayomkumba binadamu na kukwepa imani ya
kinjozi juu ya maana ya maisha;
b) Kutoamini kuhusu uwepo wa Mungu anayedaiwa kwamba ndiye muumba wa
ulimwengu, ambao kimsingi, haumjali binadamu huyu;
c) Kutafuta uhuru binafsi, uwezo wa mtu wa kujifikiria na kujiamulia mambo
yake, pamoja na wajibu wake katika ulimwengu; na
d) Kukengeuka kwa misingi ya jamii husika, kukata tamaa na mauti. Aidha,
kukumbwa na fadhaa, mashaka, pekecho na uchovu.
26
2.3.1.2 Nadharia ya Udhanaishi Ilivyotumika
Nadharia hii ilikuwa mwongozo katika kufikiwa kwa lengo la kwanza, lililokusudia
kubainisha usawiri wa matukio yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya teule
za Euphrase Kezilahabi. Vilevile, ilimwongoza mtafiti katika kupatikana kwa
matokeo ya lengo la pili, lililohusiana na kuchunguza sababu za mitanziko ya
wahusika zinazosawiriwa katika riwaya teule. Pia, ilisaidiana na nadharia ya
Sosholojia ya Kifasihi katika kumwongoza mtafiti ili kupatikana kwa matokeo ya
lengo la tatu. Hii ilitokana na misingi ya nadharia ya Udhanaishi kushindwa
kutosheleza mahitaji ya malengo yote matatu ya utafiti huu. Lengo hilo lilikuwa ni
kutathmini uhusiano wa matukio ya mchakato wa kujiua yanayosawiriwa katika
riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii. Kwa jumla, misingi ya
nadharia hizi mbili ilikamilishana kwa sababu ilimwongoza mtafiti katika mchakato
wake wa kupata matokeo ya utafiti wake kwa lengo hilo la tatu.
2.3.2 Nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi
Nadharia nyingine iliyotumika katika utafiti huu ni ile ya Sosholojia ya Kifasihi.
Kwa mujibu wa Coser (1963), nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi iliasisiwa na
Charles Taylor (1822 - 1917) na George Lukacs (1885 - 1971). Katika ufafanuzi
wake, Lukacs anaona kuwa masuala mbalimbali ya kijamii yanayohusiana na
uumbaji wa kazi za Fasihi, kwa kiasi kikubwa, hutegemea jinsi mwandishi
anavyofungamana na maisha ya jamii husika. Anaongeza kuwa, badala ya
kumithilisha au kufananisha hali ya maisha, Fasihi na sanaa zinapaswa kuwa ‗picha
ya uhalisi,‘ ijapokuwa picha hiyo hukiuka misingi ya uigaji wa moja kwa moja wa
uhalisi. Hii ina maana kuwa ni vigumu kuitenga kazi ya Fasihi na jamii, ambayo
kwayo kazi hiyo imechipuzwa. Kwa msingi huo, ni wazi kwamba Nadharia ya
Sosholojia ya Kifasihi ni kitengo muhimu sana cha uchunguzi ambacho humulika
mahusiano yaliyopo baina ya kazi halisi ya sanaa, umma, muundo wa jamii, na
namna kazi hiyo inavyojitokeza na kutathminiwa kuhusiana na uzuri na udhaifu
wake. Vilevile, nadharia hii huelezea sababu za kuibuka kwa kazi fulani ya sanaa
yenye umbo fulani la kijamii, ikiwamo namna fikra za mwandishi zinavyoongozwa
na mila, desturi na maisha ya jamii yake. Kimsingi, nadharia hii huchunguza jinsi
mtunzi wa kazi fulani ya kifasihi anavyoathiriwa na tabaka lake, itikadi yake ya
kijamii, mazingira ya kiuchumi ya kazi yake, na hali ya jamii yake anayoilenga.
27
Coser (1963) anaeleza kuwa, Fasihi ni zao la jamii na hufungamana na maisha halisi
ya jamii husika katika kila nyanja. Kuhusiana na suala la utamaduni, anaeleza kuwa
dhana hii ni ngumu kuielezea kwa sababu ni dhana changamani sana. Hii inatokana
na kuhusisha ndani yake masuala ya imani, mila, desturi, itikadi, maadili, sheria,
elimu, pamoja na mazoea anayokuwa nayo mtu akiwa ni sehemu ya jamii. Kwa
msingi huo, ni wazi kwamba mawazo haya ya Coser yanadhihirisha kuwa Fasihi
hufungamana na historia, fikra, pamoja na mitazamo na imani ya jamii husika.
Vipengele hivi ni muhimu katika utafiti wetu, kwani kwa namna moja ama nyingine,
tumevishughulikia katika utafiti wetu tulipokuwa tunachunguza usawiri wa
mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi ili kubaini kama ni
mwangwi wa mtanziko wa kijamii au la.
Kwa upande wake, Mungah (1999) anaeleza kuwa mtu anayesifika kama mmoja wa
waasisi wa nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi ni Hippolyte Taine (1828 – 1893).
Anaeleza zaidi kuwa Taine katika kitabu chake cha History of English Literature
(1863), alichunguza kazi ya Kifasihi kama taswira ya kijiografia, kiutamaduni na
kimazingira inayochimbuka kutoka katika jamii husika. Anaongeza kuwa kazi ya
kifasihi inatakiwa kuchukuliwa kama taarifa ya kweli inayohusu maisha halisi ya
watu. Kimsingi, nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi huiweka kazi ya Fasihi katika
ulimwengu wa jamii na kuelezea uhusiano uliopo baina yake. Hutawaliwa na imani
kuwa kuna uhusiano baina ya Fasihi na jamii, ambapo, kutokana na uhusiano huo,
kazi hiyo huweza kuandikwa.
Vilevile, Mungah (k.h.j) anaelezea zaidi kuwa Taine anadai kwamba kazi yoyote ya
fasihi, kama vile riwaya, ni kioo ambacho husawiri vipengele vyote vya maisha ya
jamii husika. Anatilia mkazo kuwa, kwa hakika, fasihi haiwezi kutengwa na
miktadha ya maisha ya binadamu katika harakati zake za maisha. Kipengele hiki
kinachoihusu Fasihi na jamii, pamoja na maisha ya jamii kwa jumla kilikuwa
muhimu sana katika utafiti wetu. Hii ni kwa sababu kimeshughulikiwa tulipokuwa
tunatathmini uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika
riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii.
28
2.3.2.1 Misingi ya Nadharia ya Kisosholojia
Misingi ya nadharia hii imejengwa katika mawazo kwamba:
a) Binadamu ni uti wa mgongo wa ulimwengu pamoja na sanaa kwa jumla. Hivyo,
kazi yoyote ya Fasihi ni taswira ya kijiografia, kimazingira na kitamaduni,
ambamo kazi hiyo imezuka. Kwa msingi huo, kazi hiyo haipaswi kutenganishwa
na muktadha, kwa kuwa mara nyingi hufungamana na historia ya jamii;
b) Fasihi ni dhihirisho la ujumi na ubunifu wa jamii katika kupambana na mazingira
yake, na hivyo, haiwezi kutengwa na harakati za binadamu zinazoongoza maisha
yake;
c) Usuluhishi wa migororo unaosawiriwa ndani ya Fasihi, kama vile katika msuko
wa matukio, unaficha tu migongano anuwai ya kijamii ambayo haijasuluhishwa.
Hivyo, una dhima ya kiitikadi;
d) Mhakiki hawezi kuhakiki kazi yoyote ya Fasihi bila kuzingatia miktadha yake ya
mazingira na maisha ya mwandishi. Siyo kazi tu ya fasihi inayochunguzwa, bali
pia na vipengele vilivyo nje ya kazi hiyo.
2.3.2.2 Nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi Ilivyotumika
Nadharia hii imekuwa na umuhimu mkubwa katika utafiti huu, kwani imetuongoza
katika kufikiwa kwa lengo la tatu, lililolenga kutathmini uhusiano baina ya usawiri
wa matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya
kujiua katika jamii. Kulingana na Narizvi (1982) uhusiano baina ya Fasihi na jamii ni
suala muhimu sana katika uchunguzi unaohusu masuala ya binadamu. Anaongeza
kuwa uhusiano huo husawiriwa kwa kuchunguza namna kazi husika
inavyofungamana na jamii. Ili kudhihirisha kuwa Fasihi ni zao la jamii, Escarpit
(1971), kama alivyonukuliwa na Mungah (keshatajwa), anaeleza kwamba bila msingi
wa kijamii, ukweli wa Fasihi hubadilishwa sawa na wa ramani isiyo na vitu vya
kimaumbile. Maelezo haya ya Escarpit yanalandana na mhimili mmojawapo wa
nadharia hii unaodai kwamba Sosholojia ya Kifasihi pia hushughulikia mamlaka na
nguvu fulani za kijamii. Kwa muktadha wa utafiti huu, mamlaka ni uwezo wa
kuamua na kufuatilia mwenendo na tabia za watu wengine kulingana na matakwa ya
huyo mwenye mamlaka. Mamlaka hayo yanaweza kuwa ni ya kisheria, mila na
desturi, au mamlaka ya kihaiba. Kwa mantiki hiyo, uchunguzi kuhusu jamii ya
mwandishi, umetusaidia tulipokuwa tunafanya tathmini ya uhusiano baina ya
29
usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya
matukio ya kujiua katika jamii.
Kipengele kingine muhimu katika nadharia hii ambacho tumekitumia katika utafiti
wetu ni kile kinachosisitiza kwamba mhakiki hawezi kuhakiki kazi ya Fasihi pasipo
kuzingatia miktadha inayomhusu mwandishi. Hii ina maana kuwa kinachotakiwa
kuchunguzwa si kazi za mwandishi pekee, bali ni pamoja na vipengele vingine
ambavyo viko nje ya kazi. Pia, inatakiwa kuchunguza maisha ya jamii
yaliyosababisha kupatikana kwa kazi husika. Mazingira hayo ni kama vile ya kisiasa,
kiuchumi, kiutamaduni, na kijamii.
2.4 Muhtasari wa Sura ya Pili
Sura hii imebainisha mapitio mbalimbali yanayohusiana na mada ya utafiti wetu ili
kupata msingi wa hoja za utafiti wetu. Kilichobainika ni kwamba, kwa kiasi
kikubwa, wataalamu na wahakiki wengi wa kazi za Euphrase Kezilahabi
wamezichambua na kuzihakiki kazi hizo kwa jicho la kidhanaishi. Aidha, kwa upeo
wa mtafiti, hakuna utafiti uliofanyika kuhusiana na riwaya teule uliotumia nadharia
ya Sosholojia ya Kifasihi pamoja na ile ya Udhanaishi kwa pamoja. Zaidi mapitio ya
maandiko ya wataalamu mbalimbali yalibaini kuwa wahakiki na watafiti wengi wa
Fasihi ya Kiswahili hawajalishughulikia kwa kina tatizo la watu kujiua katika jamii.
Pia, sura hii imejadili nadharia zilizomwongoza mtafiti katika kujenga hoja na
kukamilisha utafiti wake. Nadharia hizo ni Udhanaishi na Sosholojia ya Kifasihi.
Imebainishwa kwamba, misingi ya nadharia hizi imekamilishana ili kuweza kufikiwa
na kupatikana kwa matokeo ya utafiti kulingana na malengo yaliyokusudiwa. Sura ya
Tatu inahusu methodolojia na njia za utafiti.
30
SURA YA TATU
METHODOLOJIA YA UTAFITI
3.1 Utangulizi
Sura hii inaeleza namna utafiti huu ulivyosanifiwa na kufanyika hadi kukamilika
kwake. Vipengele vilivyoshughulikiwa katika sehemu hii ni usanifu wa utafiti,
mkabala wa utafiti, eneo la utafiti, walengwa wa utafiti, na ukusanyaji wa data.
Vipengele vingine ni mchakato wa ukusanyaji data, mbinu za uchambuzi wa data,
maadili na itikeli za utafiti, pamoja na uhalali na uthabiti wa data.
3.2 Usanifu wa Utafiti
Kwa mujibu wa Kothari (2004), usanifu wa utafiti ni uamuzi kuhusu nini, wapi, lini,
kwa kiwango gani na namna gani utafiti utafanyika. Hii ina maana kuwa usanifu wa
utafiti ni mpangilio maalumu wa kanuni za kukusanya data na uchanganuzi wake ili
kufikia uyakinifu wa malengo ya utafiti kwa kuzingatia muda, mahali pa utafiti, na
hali ya uchumi uliopo katika kukamilisha mada ya utafiti. Usanifu wa utafiti wetu
ulikuwa ni wa kifenomenolojia. Fenomenolojia hujishughulisha na maisha ya
binadamu na namna ya kuufahamu ulimwengu kulingana na uzoefu wa maisha ya
watu hao kuhusiana na hali au jambo fulani linalofanyiwa utafiti (Brentano, 1995;
Schram, 2003; Van Manen, 2014). Usanifu wa kifenomenolojia hujikita katika
ufafanuzi wa taarifa ambazo, kimsingi, hukusanywa na kuchambuliwa kwa njia ya
maelezo yenye kuakisi mtazamo wa wahojiwa kuhusiana na jambo husika. Nguzo
kuu ya fenomenolojia ni uzoefu au tajiriba za maisha alizonazo mtu kuhusu hali au
jambo fulani katika maisha yake kulingana na mazingira aliyopo (Chuachua, 2016).
Data za kifenomenolojia hukusanywa kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na
mapitio ya maandiko, mahojiano, ushuhudiaji, pamoja na majadiliano katika vikundi.
Shabaha kubwa ya kutumia usanifu wa kifenomenolojia ilikuwa kupata maelezo ya
kina kutoka kwa watafitiwa kuhusu uzoefu na uelewa wao juu ya usawiri wa
mchakato wa kujiua katika jamii, hususani jamii ya mwandishi wa riwaya teule.
Aidha, kupitia usanifu huu, mtafiti aliweza kubainishiwa matukio yanayounda
mchakato wa kujiua, sababu za mitanziko ya kujiua kwa wahusika na kutathmini
uhusiano uliopo baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya
teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii. Vilevile, usanifu huu
31
ulimwongoza mtafiti katika kubainisha athari za miktadha ya jamii inavyomwathiri
mhusika hadi kufikia maamuzi ya kujiua kwake.
3.3 Mkabala wa Utafiti
Utafiti huu ulitumia mkabala wa kitaamuli katika ukusanyaji, uchanganuzi wa data,
pamoja na utoaji wa matokeo. Mkabala wa kitaamuli ni ule ambao data zake
hazielezwi na kufafanuliwa kwa kutumia namba (au takwimu). Hii haina maana
kuwa takwimu na namba hazitumiki kabisa, isipokuwa kinachosemwa hapa ni kuwa
hutumia maneno kuwasilisha na kujadili data za utafiti (Enon, 1998; Merriam &
Tisdell, 2016). Ponera (2016:116) anafafanua zaidi kwa kusema:
Utaamuli ni aina mojawapo ya mikabala ya kufanyia utafiti,
ambao hutumia zaidi tafakuri katika kuhusisha taarifa
mbalimbali za kitafiti. Kisha kutoa ufafanuzi kwa kuzingatia
misingi ya nadharia husika, pamoja na ithibati bayana,
zipatikanazo ama maskanini (uwandani) au katika matini.
Utafiti huu umetumia mkabala wa kitaamuli kwa sababu:
a) Mkabala wa kitaamuli una sifa ya kupokea fasili zinazotofautiana kwa tukio
lilelile moja, kwa sababu una sifa ya kuruhusu mitazamo mbalimbali ya watu
kulingana na uzoefu wao;
b) Mkabala huu una sifa ya kuruhusu sampuli ndogo kutumika kwa kuwa muda
mwingi hutumika katika kukusanya data za kimaelezo baina ya mtafiti na
watafitiwa;
c) Mbinu zilizotumika katika kukusanya data ni nusu funge. Hii ina maana
kuwa, pamoja na kuwapo kwa maswali mbalimbali yaliyokuwa
yameandaliwa ili kuongoza mahojiano, mtafiti alikuwa na uhuru wa kuuliza
maswali mengine ya nyongeza na fuatizi kwa watafitiwa wake. Aidha,
watafitiwa nao walikuwa na uhuru wa kujieleza kwa kina na kutoa maoni yao
kuhusu dhana na maswali yaliyoulizwa;
d) Malengo na maswali ya utafiti huu yalikusudia kuchunguza tabia, hali,
mitazamo na uzoefu wa watafitiwa kuhusu usawiri wa matukio ya mchakato
wa kujiua kwa kuhusisha na maisha yao halisi ya kila siku;
e) Utafiti huu ulihusisha uchambuzi wa data za maktabani kwa kujikita katika
riwaya teule na magazeti. Uchambuzi huo ulifafanuliwa kwa njia ya maelezo
na siyo namba au takwimu;
32
f) Utafiti ulijikita katika ufafanuzi wa matukio mbalimbali ya kujiua kwa
wahusika, sababu za mitanziko ya wahusika kama zinavyosawiriwa katika
riwaya teule, pamoja na tathmini ya uhusiano baina ya matukio ya mchakato
wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika
jamii.
Mkabala huu, basi, ulifaa kutumika katika utafiti huu kwa sababu data zilizopatikana
uwandani na maktabani zilihakikiwa, kuchanganuliwa na kufafanuliwa kwa njia ya
maelezo zaidi na siyo kwa njia ya takwimu. Lengo lake lilikuwa kupata matokeo ya
malengo mahususi kwa kuhusianisha na maswali ya utafiti yaliyokusudiwa kujibiwa.
Kimsingi, malengo ya utafiti huu hayakuhitaji data ama takwimu za kimahesabu.
Kwa maana hiyo, pale ambapo namba na idadi zilitumika, hazikutumika kama
mkabala wa kiidadi, bali kwa lengo la kutoa ufafanuzi tu.
3.4 Eneo la Utafiti
Utafiti huu ulifanyika maktabani na uwandani. Maeneo yaliyohusishwa katika
upatikanaji wa data ni Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam. Dodoma ni eneo ambalo
mtafiti alikusudia kupata nyaraka mbalimbali zinazohusiana na mada ya utafiti wake
yakiwamo magazeti, kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, pamoja na Maktaba ya Mkoa
huo. Nyaraka hizo zilikuwa mahususi kwa ajili ya kupata data za kimaktaba hususani
zile za magazetini ambazo zilihitajika zaidi kwa ajili ya lengo la tatu. Aidha,
alilitumia eneo hilo la Dodoma katika kufanya mahojiano na baadhi ya wataalamu
wa Fasihi, wataalamu wa Saikolojia, pamoja na wataalamu wa magonjwa ya akili ili
kupata data za uwandani ambazo zilikuwa mahususi kwa ajili ya lengo la tatu.
Mtafiti alikuwa na uhakika wa kuwapata watafitiwa hao kwa urahisi kutokana na
kuwapo kwa Chuo Kikuu cha Dodoma ambacho kina wataalamu wengi wa Fasihi na
Saikolojia. Vilevile, Mkoani Dodoma kuna hospitali maalumu ya magonjwa ya akili
iitwayo Mirembe na kuna madaktari bingwa wa magonjwa ya akili, ambapo mtafiti
aliweza kupata data za lengo la tatu zinazobainisha uhusiano wa magonjwa ya akili
na masuala ya kujiua.
Kwa upande wa Mkoa wa Mwanza, mtafiti alilitumia eneo hilo kwa lengo la kupata
data za uwandani kutoka katika jamii ya mwandishi. Data hizo ni zile zilizohusu
matukio ya mchakato wa kujiua kwa wahusika, pamoja na miktadha mbalimbali ya
33
kijamii juu ya usawiri wa mchakato wa kujiua. Mkoa wa Mwanza ulichaguliwa kama
mojawapo ya eneo la utafiti kwa sababu ndiko alikozaliwa mwandishi wa riwaya
teule. Aidha, riwaya hizo, kwa kiasi kikubwa, zinasawiri mandhari na matukio
yanayohusu mkoa huo. Kutokana na hilo, mtafiti alikuwa na uhakika wa kuwapata
kwa urahisi watafitiwa wake, hususani wale wa kabila la Wakerewe na Wakara
wanaopatikana katika kata ya Namagondo, kijiji cha Namagondo. Watafitiwa
wengine waliolengwa na utafiti huu kwa upande wa Mwanza ni viongozi wa dini,
viongozi wa serikali na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama. Kimsingi, data
zilizokusudiwa kupatikana katika Mkoa huo wa Mwanza, zilikuwa mahususi kwa
ajili ya lengo la tatu la utafiti wetu. Lengo hilo lilimtaka mtafiti kufanya tathmini ya
uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na
vichocheo vya mchakato wa kujiua katika jamii.
Vilevile, mtafiti alifanya utafiti katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa sababu ya
kuwapo kwa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iitwayo Maktaba ya Dkt.
Wilbert Chagula na Makavazi ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI). Lengo
la kuchagua eneo hili lilikuwa kufanya mapitio ya nyaraka na maandiko mbalimbali
kuhusiana na utafiti wake. Maktaba hiyo ilitumika kwa kuwa, ikilinganishwa na
maktaba nyingine, hii ni kongwe zaidi. Hivyo, mtafiti alikuwa na uhakika wa kupata
maandiko mengi kutokana na tafiti na tahakiki nyingi kufanyika katika Chuo hicho
kikongwe hapa nchini. Aidha, eneo hili lilitumika katika kuwapata wataalamu wa
Fasihi na wahakiki wa kazi za Fasihi zikiwamo za Euphrase Kezilahabi. Kwa kiasi
kikubwa, data zilizolengwa kupatikana katika Mkoa wa Dar es Salaam zilikuwa ni za
kimaktaba. Data nyingine zilizopatikana kutoka kwa watafitiwa zililenga kushadidia
na kujaliza data za msingi za kimaktaba.
Kwa jumla, maeneo hayo, mbali na kuteuliwa kutokana na sababu zilizoelezwa, kwa
upande mwingine, yaliteuliwa ili kuwakilisha maeneo mengine ya Tanzania yenye
matukio ya kujiua. Uwakilishi huo unatokana na kutumia watafitiwa kutoka maeneo
tofauti, wenye umri na tajiriba tofauti, ambao waliweza kutoa mawazo yao kuhusiana
na matukio ya mchakato wa kujiua.
34
3.5 Walengwa wa Utafiti
Hii ni jamii iliyokusudiwa kutafitiwa na mtafiti ili iweze kutoa taarifa mbalimbali
kuhusiana na malengo ya utafiti wake. Kwa msingi huo, walengwa wa utafiti huu
waligawanywa katika makundi mawili. Kundi la kwanza, ni wango la utafiti, kwa
maana ya jamii ya watafitiwa kwa jumla. Kundi la pili, ni sampuli iliyoshughulikiwa,
ikiwa ni pamoja na usampulishaji wake.
3.5.1 Wango la Utafiti
Wango la utafiti ni jumla ya watu, vitu au elementi zote ambazo mtafiti amekusudia
kuvitumia katika utafiti wake ili kupata sampuli inayohitajika kulingana na mahitaji
ya utafiti wake. Wango la utafiti huu lilijumuisha:
a) Riwaya zilizoandikwa na Euphrase Kezilahabi: Hizi zilisaidia kuyabainisha
matukio mbalimbali ya mchakato wa kujiua kwa wahusika. Aidha, zilisaidia
katika kubainisha sababu za mitanziko ya wahusika, pamoja na kutathmini
uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya
teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii;
b) Taarifa za matukio ya kujiua kutoka katika vyanzo mbalimbali vya habari
yakiwamo magazeti na televisheni: Hizi zilisaidia kupatikana kwa matukio
halisi yanayohusu kujiua yanayozikumba jamii zetu. Data hizi zilitusaidia
zaidi katika kufanya tathmini ya uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya
mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua
katika jamii;
c) Wataalamu na wahakiki mbalimbali waliozisoma au kuzihakiki kazi
mbalimbali za Fasihi ya Kiswahili: Kwa jumla, hawa walisaidia katika
upatikanaji wa taarifa za matukio ya kujiua katika riwaya za Kiswahili. Pia,
walitoa maoni na mitazamo yao kuhusu matukio hayo ya kujiua;
d) Jamii ya mwandishi wa riwaya teule: Hii ilisaidia kutoa taarifa kuhusu jamii
yao pamoja na matukio ya kujiua kwa wahusika. Taarifa hiyo ilikuwa
mahususi kwa ajili ya lengo la tatu;
e) Viongozi wa dini: Hawa walisaidia kutoa mtazamo wao kuhusu matukio ya
kujiua kwa misingi ya dini wanazoziongoza;
f) Viongozi wa serikali: Hawa walisaidia katika upatikanaji wa data za lengo la
tatu, ambapo walieleza jitihada zinazofanywa na serikali katika kutoa elimu
kuhusu matukio ya watu kujiua;
35
g) Wanasaikolojia: Walitoa sababu za kisaikolojia za watu kufikia maamuzi ya
kujiua; na
h) Wataalamu wa magonjwa ya akili: Kundi hili lilisaidia kutoa ufafanuzi
kuhusu matukio ya watu kujiua, pamoja na uhusiano uliopo baina ya
magonjwa ya akili na matukio ya kujiua.
Taarifa zilizopatikana kutoka katika makundi hayo zilisaidia kujibu maswali ya
utafiti wetu na kuwezesha upatikanaji na ukamilifu wa tasinifu hii.
3.5.1.1 Usampulishaji
Usampulishaji ni mchakato wa kupata sampuli kutoka kwenye wango la utafiti. Hii
ni mbinu ya uteuzi wa sampuli, yaani mwongozo unaotumika katika kuteua kundi
dogo kutoka katika sampuli kuu ili kuwa kiwakilishi cha sampuli hiyo katika kutoa
data zinazohitajika katika utafiti husika (Babbie, 1999). Ufafanuzi huu una maana
kuwa usampulishaji ni mbinu ya kiufundi anayoitumia mtafiti katika kuchagua
wawakilishi wake kutoka katika sampuli kubwa ili kuwakilisha wango lote. Utafiti
huu ulitumia usampulishaji lengwa ili kupata sampuli ya watafitiwa.
Enon (1995) na Newman (2007) wanaeleza kuwa usampulishaji lengwa ni mbinu ya
usampulishaji ambapo mtafiti huchagua sampuli anayoihitaji kutokana na sifa za
watafitiwa alizozikusudia kwa kuzingatia malengo mahususi ya utafiti wake. Mbinu
hii hujikita katika matarajio kwamba mtafiti anataka kugundua, kuelewa au kupata
ufafanuzi kuhusu jambo fulani kulingana na vigezo alivyojiwekea. Vigezo hivyo
huakisi moja kwa moja lengo kuu la utafiti na huongoza katika mchakato wa
upatikanaji wa data zinazohitajika. Hii ni pamoja na kueleza umuhimu wa vigezo
hivyo katika utafiti husika. Mbinu hii ya usampulishaji lengwa ilimsaidia mtafiti
kuwapata watafitiwa wenye sifa zilizolengwa katika utafiti wake na namna
walivyokidhi haja na malengo ya utafiti wake. Hivyo, utafiti huu ulitumia
usampulishaji lengwa wa aina tatu kama zilivyoainishwa na Meriam & Tisdell
(2016):
a) Usampulishaji lengwa wa kipekee: Aina hii ilichaguliwa kwa kuzingatia sifa
za kipekee za sampuli zilizokidhi malengo ya utafiti wetu;
b) Usampulishaji tajwa au wa kupokezana: Katika aina hii ya usampulishaji,
watafitiwa wachache mahususi walifanyiwa mahojiano kuhusu mchakato wa
36
kujiua, kisha nao waliweza kuwataja watafitiwa wengine wenye ufahamu
kuhusiana na matukio ya mchakato wa kujiua hususani katika riwaya za
Euphrase Kezilahabi;
c) Usampulishaji wa kutegemea fursa: Mtafiti aliitumia aina hii ya
usampulishaji kuwapata watafitiwa, ambao kimsingi walihitajika sana ili
kutoa taarifa kuhusu utafiti, lakini kutokana na majukumu yao ya kazi,
ilikuwa vigumu kuwapata kwa urahisi. Hali hiyo ilimlazimu mtafiti
kuwafanyia mahojiano mara tu ilipopatikana fursa ya kufanya hivyo, huku
akizingatia suala la gharama na mahali.
3.5.1.2 Sampuli ya Utafiti
Sampuli ni sehemu ndogo ya kundi lengwa iliyochaguliwa kushiriki katika kutoa
data za utafiti (Gay, 1987; Kothari, 2009). Kipengele hiki ni muhimu sana katika
suala la utafiti kwa sababu humsaidia na kumpa mtafiti mwelekeo katika kupanga
muda na gharama za utafiti wake. Cohen na Lawrence (2000) na Bryman (2004)
wanaeleza kuwa uteuzi wa sampuli ni mchakato muhimu ambao humsaidia mtafiti
katika kuchagua kikundi cha vitu au watu kwa lengo la kutumiwa katika utafiti wake.
Sampuli hiyo hutumika kama kiwakilisho cha kundi zima litakalotafitiwa kwa
sababu si rahisi kulifanyia utafiti kundi zima. Sampuli ya utafiti wetu iliteuliwa kwa
kuzingatia mada ya utafiti, malengo na maswali ya utafiti, na ukubwa wa jamii ya
watafitiwa. Kwa hiyo, katika utafiti wetu, sampuli lengwa iliyotumika ina jumla ya
watoa taarifa thelathini na sita (36) ambao wamegawanyika katika makundi
yafuatayo:
a) Riwaya teule tatu (3) za Euphrase Kezilahabi, ambazo ni: Rosa Mistika,
Kichwamaji, na Dunia Uwanja wa Fujo. Riwaya hizi ziliteuliwa kutokana na
uchunguzi wa awali uliofanywa na mtafiti kuonesha kuwa zina sifa za
kipekee zinazoendana na mada na malengo ya utafiti wake. Sifa hizo ni
pamoja na uwezo wa kutoa data za kutosheleza utafiti wake, kwa sababu ni
za kihalisia na zina matukio yanayohusu kujiua kwa baadhi ya wahusika
wake. Riwaya nyingine za mwandishi huyu kama vile Nagona (1990) na
Mzingile (2011) si za kiuhalisia na hazina matukio ya kujiua, bali zinaelezea
zaidi kuhusu falsafa ya maisha kwa namna ya kiuhalisiajabu;
37
b) Magazeti matano (5) ya matoleo mbalimbali yenye taarifa za matukio ya
kujiua kwa miaka minne mfululizo, yaani 2016 hadi 2019. Mtafiti aliamua
kufuatilia matukio ya kujiua kwa miaka minne mfululizo ili kupata uwiano
wa utokeaji wa matukio hayo. Magazeti yaliyochaguliwa ni Habari Leo,
Mtanzania, Mwananchi, Nipashe, na Tanzania Daima. Haya yalichaguliwa
miongoni mwa mengi kutokana na upekee wake, kwa sababu hutoa taarifa za
kiuchunguzi na huchapishwa kila siku. Pia, mtafiti alibaini kuwa yalikuwa na
data za matukio ya kujiua zilizokuwa zinahitajika katika utafiti wake.
Vyombo vingine vya habari vilivyotoa data ni vinne (4), yaani ―Global TV on
line‖, ―Azam TV‖, Televisheni ya Afrika Mashariki (EATV), na ―BBC
Swahili‖. Hivi vilichaguliwa kwa kutegemeana na fursa, kwani matukio ya
kujiua yalitangazwa mtafiti akiwa anafuatilia taarifa mbalimbali za habari;
c) Wataalamu na wahakiki saba (7) wa kazi za Fasihi: Kati ya hao wanne (4)
walipatikana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mmoja (1) Chuo Kikuu cha
Dodoma, na wawili (2) walipatikana Dar es Salaam na Dodoma kwa
kutegemeana na fursa. Upatikanaji wa wataalamu na wahakiki hawa
ulizingatia nafasi yao kitaaluma, ukongwe wao katika kufundisha somo la
Kiswahili, pamoja na kujihusisha kwao na masuala mbalimbali ya utafiti wa
Kiswahili. Idadi hiyo ya wataalamu ilifikiwa baada ya kupatikana kwa data
muhimu zilizokuwa zinahitajika kulingana na malengo ya utafiti huu.
Wataalamu hawa walisaidia kutoa data kuhusu mwandishi wa riwaya teule na
mtazamo wao juu ya matukio yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya
teule;
d) Watafitiwa kumi (10) (watu wazima kuanzia miaka arobaini na kuendelea na
vijana wenye umri kati ya miaka kumi na mitano hadi arobaini), kutoka
katika Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Ukerewe. Upatikanaji wa watafitiwa
hawa ulizingatia uzoefu wao wa kuishi katika eneo husika na namna
wanavyomfahamu Euphrase Kezilahabi, au kazi zake, au familia yake. Aidha,
mtafiti aliomba ridhaa kutoka mamlaka ya eneo husika ili iweze kumsaidia
kuwapata watafitiwa wenye sifa zinazohitajika. Mgawanyo wake ulikuwa
kama ifuatavyo: wanaume 2, wanawake 3, vijana wa kiume 2, na vijana wa
kike 3. Mgawanyo wa idadi unaozingatia uwakilishi wa kijinsia ulilenga
kupata ulinganifu wa mitazamo kutoka jinsi hizo kuhusu usawiri wa
38
mchakato wa kujiua, na fursa ya upatikanaji wao. Watafitiwa hawa
walichaguliwa kwa sababu wanaishi katika eneo ambalo mwandishi wa
riwaya teule alizaliwa, na pia kazi zake kwa kiasi kikubwa zinasawiri eneo
hilo. Hivyo, idadi hiyo ilitosha kutoa data wakilishi zinazohusu matukio ya
mchakato wa kujiua na athari za miktadha ya maisha ya jamii iliyomwibua
mwandishi wa riwaya teule kulingana na uzoefu wao;
e) Viongozi wawili (2) wa dini kutoka Mkoa wa Mwanza. Upatikanaji wa
viongozi hawa ulizingatia nafasi na majukumu yao ya uongozi katika
kuihudumia jamii. Viongozi wote wawili waliopatikana walitoka katika dini
ya Kikristo. Hatukufanikiwa kuwapata viongozi wa dini ya Kiislamu
kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu. Hata hivyo, data
zilizotolewa na viongozi wa dini ya Kikristo, zilitosheleza mahitaji ya data
zilizokuwa zinahitajika katika kukamilika kwa utafiti huu;
f) Watafitiwa wengine watano (5) walikuwa ni wataalamu wa masuala ya
Saikolojia na magonjwa ya akili kutoka katika Mkoa wa Dodoma.
Upatikanaji wa wataalamu hawa pia ulizingatia nafasi yao kitaaluma, na
ukongwe wao katika masuala ya kutoa nasaha na katika kuhudumia
wagonjwa wa akili. Hawa waligawanywa katika makundi kama ifuatavyo:
wataalamu wa Saikolojia wawili (2) - mwanaume mmoja (1) na mwanamke
mmoja (1); na wataalamu wa magonjwa ya akili watatu (3) - wanaume
wawili (2), na mwanamke mmoja (1). Mgawanyo wa idadi unaozingatia
uwakilishi huo kijinsia ulikusudia kupata ulinganifu wa mitazamo kutoka
jinsi hizo kuhusu usawiri wa mchakato wa kujiua. Kundi hili la wataalamu
wa Saikolojia na magonjwa ya akili lilichaguliwa ili kusaidia kufafanua
kitaalamu kuhusu, uhusiano wa masuala ya kiakili na kisaikolojia, namna
yanavyohusika katika mchakato mzima wa mtu kujiua. Pia, lilisaidia
kubainisha mazingira, dalili za mtu anayekusudia kujiua, na tahadhari
zinazotakiwa kuchukuliwa ili kumsaidia mtu mwenye dalili za kutaka kujiua.
3.6 Ukusanyaji wa Data
Ukusanyaji wa data katika utafiti wowote ule unahusu kukusanya taarifa mahususi,
zinazokusudiwa kutoa au kupinga uhalisi wa mambo fulani (Kombo na Tromp, 2006).
39
3.6.1 Njia za Ukusanyaji wa Data
Data za utafiti huu zilikusanywa kwa kutumia mbinu kuu mbili: usomaji na uchambuzi
makini wa matini teule (riwaya, magazeti na ufuatiliaji wa taarifa za habari), na
mahojiano.
3.6.1.1 Usomaji na Uchambuzi Makini wa Matini
Mtafiti alikwenda maktabani ambako alizisoma na kuzichambua kwa makini riwaya
teule (Rosa Mistika, Kichwamaji, na Dunia Uwanja wa Fujo), magazeti teule
(Habari Leo, Mtanzania, Mwananchi, Nipashe, na Tanzania Daima), na ufuatiliaji
wa taarifa mbalimbali za habari. Alifanya hivyo ili kupata data msingi, yaani data
halisi zilizokusanywa kwa mara ya kwanza na ambazo zilihitajika kulingana na
malengo ya utafiti wake. Katika hatua hiyo, aliweza kubainisha data za matukio ya
mchakato wa kujiua yanayosawiriwa katika riwaya teule, katika magazeti teule, na
taarifa mbalimbali za habari. Pia, alitumia mbinu hiyo katika kupata data kuhusu
sababu za mitanziko ya wahusika zinazosawiriwa katika riwaya teule. Vilevile,
mbinu hii ilimsaidia kupata data kuhusu matukio ya mchakato wa kujiua
yanayosawiriwa katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika
jamii.
Kwa msingi huo, data zilizopatikana kutokana na usomaji na uchambuzi makini wa
matini zilikuwa mahususi katika kupima malengo yote matatu ya utafiti huu.
Mwongozo wa usomaji na uchambuzi wa matini ulitumika katika kufanikisha mbinu
hii. Pia, vifaa kama vile kompyuta pakatwa, shajara, kinyonyi, simu ya mkononi, na
kalamu vilitumika katika kurekodi, kutunzia data na kuandikia taarifa zilizopatikana
maktabani.
3.6.1.2 Mahojiano
Drake na Linda (2011) wanaeleza kuwa mahojiano ni majibizano ya ana kwa ana
yanayohusisha watu wawili au zaidi, yenye lengo la kukusanya taarifa au maoni
yanayohusu mada fulani. Pia, mahojiano hayo yanaweza kuwa ya simu au barua
pepe. Utafiti huu ulitumia mbinu ya mahojiano nusu funge, kwa kuwa licha ya
kuwapo kwa maswali yaliyoongoza mahojiano baina ya mtafiti na watafitiwa, mtafiti
na watafitiwa wake hawakufungwa na mwongozo huo. Mbinu hii ilitumika ili kupata
data za moja kwa moja kutoka kwa watafitiwa. Mtafiti alikuwa huru kuuliza maswali
40
mengine fuatizi mbali na yale yaliyomo katika mwongozo wa mahojiano kulingana
na muktadha wa watafitiwa wake. Aidha, watafitiwa nao walikuwa huru kueleza
zaidi ya kile kilichoandaliwa katika mwongozo wa mahojiano.
Mbinu ya mahojiano ilitumika kukusanya data za uwandani katika maeneo matatu ya
watafitiwa, kama ifuatavyo: Mosi, wataalamu na wahakiki waliowahi kutafiti au
kufanyia tahakiki riwaya za Kiswahili, hususani riwaya teule. Kundi hili lilihojiwa ili
liweze kutoa taarifa juu ya mwandishi wa riwaya teule na namna linavyofahamu
matukio ya mchakato wa kujiua yanayosawiriwa katika riwaya hizo, sababu za
mitanziko ya wahusika, pamoja na kutoa tathmini ya uhusiano baina ya usawiri wa
matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya
kujiua katika jamii. Watafitiwa hao walipatikana Dodoma na Dar es Salaam. Pili,
wataalamu wa saikolojia na wale wa magonjwa ya akili waliopatikana katika Mkoa
wa Dodoma. Kundi hili lilihojiwa ili kutoa ufafanuzi wa kitaalamu kuhusu uhusiano
uliopo baina ya masuala ya magonjwa ya akili na saikolojia katika mchakato wa mtu
kujiua. Pia, lilisaidia kubainisha mazingira na dalili za mtu anayekusudia kujiua.
Tatu, watafitiwa kutoka Mkoani Mwanza. Hawa walihojiwa ili kutoa taarifa
zinazohusiana na mwandishi wa riwaya teule na uzoefu wa maisha ya jamii ya
mwandishi huyo. Mtafiti alirekodi majibu katika shajara na kwenye kinasa sauti kwa
ajili ya uchambuzi. Kwa kiasi kikubwa, mbinu hii ilisaidia kupatikana data
zilizokuwa mahususi kwa ajili ya lengo la tatu la utafiti huu. Zana iliyotumika
sambamba na njia hii ni mwongozo wa mahojiano. Pia, vifaa kama vile shajara,
kinasa sauti, kamera, simu ya mkononi, na kalamu vilitumika katika kurekodi na
kutunzia data zilizopatikana uwandani.
3.6.2 Mchakato wa Ukusanyaji Data
Mchakato wa kukusanya data ni suala muhimu sana linalopaswa kuzingatiwa na
mtafiti ili kuthibitisha au kupinga uhalisi wa mambo fulani. Katika utafiti huu, taarifa
mbalimbali zilikusanywa maktabani na uwandani kwa kutumia vifaa mbalimbali
vilivyoandaliwa na mtafiti. Mtafiti alianza na mbinu ya usomaji na uchambuzi
makini wa matini teule ili kupata data msingi kwa ajili ya malengo yote matatu. Kwa
kuwa usomaji na uchambuzi huo wa matini teule kwa kiasi kikubwa ulifanyikia Dar
es Salaam na Dodoma, mtafiti alitumia muda huo pia kuwatafuta watafitiwa
41
kulingana na sampuli yake kwa ajili ya kupata data za uwandani. Muda wa miezi
miwili ulitumika katika kukamilisha mchakato huo.
Baada ya kukamilika kwa data za maktabani na za uwandani katika Mkoa wa Dar es
Salaam na Dodoma, mtafiti alikwenda jijini Mwanza ili kupata data nyingine za
uwandani kama ilivyobainishwa katika sampuli yake ya utafiti. Akiwa katika Mkoa
wa Mwanza, alifanya mahojiano na jamii ya mwandishi wa riwaya teule pamoja na
viongozi wa dini kuhusiana na usawiri wa mchakato wa kujiua. Hata hivyo, kutokana
na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake, mtafiti hakufanikiwa kufanya mahojiano
na Mkuu wa Mkoa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, na
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ukerewe. Kutokana na hilo, mtafiti aliamua kutumia
data zilizopatikana katika vyanzo mbalimbali vya habari yakiwamo magazeti na
televisheni ili kupata matokeo thabiti kulingana na malengo yake. Muda uliotumika
katika kukusanya data za uwandani Mkoani Mwanza ulikuwa mwezi mmoja. Katika
mchakato mzima wa ukusanyaji wa data, mwongozo wa usomaji na uchambuzi
makini wa matini ndio uliotumika ili kupata data za maktabani na mwongozo wa
mahojiano kwa data za uwandani.
3.7 Mbinu za Uchambuzi wa Data
Baada ya kukamilika kwa mchakato wa ukusanyaji wa data za utafiti, mtafiti
alizichambua data zake kwa kutumia mkabala wa kitaamuli. Mbinu iliyotumika
katika uchambuzi wa data ilikitwa katika mwegamo wa kimaudhui. Sababu za
kutumia uchambuzi wa kimaudhui ilikuwa ni kumwezesha mtafiti kuunganisha,
kuainisha, kulinganisha na kufafanua data zilizopatikana maktabani na zile za
uwandani ili kupata matokeo bora. Kwa mujibu wa Patton na Michael (2002)
uchambuzi wa data kitaamuli kwa kutumia mbinu ya kimaudhui ni mchakato wa
kuzibadilisha na kuzichakata data zilizokusanywa kwa njia ya maandishi na sauti na
kuzichuja kwa kuchukua taarifa muhimu na kuzipanga kulingana na namna
zinavyowiana kimaudhui. Nao Kombo na Tromp (2006) wanaeleza kuwa
uchanganuzi wa kimaudhui ni mbinu ya uchambuzi ambayo huziweka mada
kulingana na namna zinavyofanana na kuhusiana.
Katika utafiti huu, mtafiti alizichambua na kuzipanga data katika makundi kulingana
na malengo na maswali ya utafiti wake kama ifuatavyo: Kundi la kwanza lilihusu
42
data zilizobainisha matukio ya mchakato wa kujiua na namna yanavyosawiriwa
katika riwaya teule. Kundi la pili lilihusu data zilizolenga kuchunguza sababu za
mitanziko ya wahusika zinazosawiriwa katika riwaya teule. Na, kundi la tatu lilikuwa
na data zilizolenga kutathmini uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya mchakato
wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii. Data
za malengo hayo zilipatikana kwa mbinu ya usomaji na uchambuzi makini wa matini
maktabani na mahojiano baina ya mtafiti na watafitiwa uwandani. Baada ya
kuzipanga data hizo katika makundi, hatua iliyofuata ilikuwa ni kuzifafanua kwa
kutumia maelezo kulingana na malengo ya utafiti na kwa kuzingatia mwoano wa
kimaudhui, huku mtafiti akiongozwa na nadharia ya Udhanaishi na ile ya Sosholojia
ya Kifasihi ili kujibu maswali ya utafiti wake.
3.8 Itikeli za Utafiti
Itikeli ni dhana inayotumika kumaanisha usahihi wa matendo katika mahusiano ya
watu wa jamii fulani yaliyokubaliwa na jamii hiyo kuwa ndiyo sahihi au si sahihi
kwa kuzingatia matakwa ya jamii hiyo (Faustine, 2017). Utafiti huu ulizingatia
taratibu zote muhimu kabla ya kuanza kufanyika na wakati wa ufanyikaji wake.
Mtafiti alilazimika kuzingatia itikeli za utafiti, kuanzia hatua ya ukusanyaji wa data,
uchanganuzi wake, pamoja na uandishi wa matokeo ya utafiti. Mambo muhimu
aliyoyazingatia ni:
a) Kanuni na taratibu zote za utafiti za Chuo Kikuu cha Dodoma, ikiwa ni
pamoja na kuomba barua ya utambulisho, na vibali mbalimbali vilivyompa
ruhusa ya kufanya utafiti katika maeneo yaliyobainishwa katika sampuli yake
ya utafiti. Barua na vibali hivyo, aliviwasilisha katika mamlaka za maeneo
aliyoomba kufanyia utafiti, ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, na Mwanza
ili mamlaka hizo nazo zimpe ridhaa hiyo;
b) Kuwaomba ridhaa watafitiwa wake ili aweze kutimiza jukumu la kuhojiana
nao. Aidha, aliwaeleza na kuomba ridhaa yao ili awarekodi na kunukuu
taarifa walizozitoa kwa ajili ya kuzitumia katika utafiti wake;
c) Kuwafafanulia watafitiwa wake malengo na umuhimu wa utafiti huo na
kuwaeleza kwamba taarifa walizotoa zitakuwa ni siri baina yake na wao, na
kwamba zitatumika kwa shughuli ya utafiti lengwa tu;
43
d) Maadili na itikeli za jamii ya watafitiwa, ikiwa ni pamoja na kuvaa mavazi ya
heshima, na kuzingatia mila na desturi zao;
e) Kuwafafanulia watafitiwa haki yao ya msingi wakati wote wa utafiti, ikiwa ni
pamoja na kusitisha mahojiano palipokuwa na haja ya kufanya hivyo,
kufichwa kwa majina yao walipotaka iwe hivyo, uhuru wa kutoa taarifa na
kuuliza maswali na mengine ya namna hiyo.
3.9 Uhalali na Uthabiti wa Matokeo ya Utafiti
Ponera (2014) anaeleza kuwa uhalali wa utafiti maana yake ni hali ya utafiti kuwa na
uwezo wa kupima jambo au mambo yaliyotakiwa kupimwa au kutafitiwa tu. Kuhusu
uthabiti wa utafiti, anaeleza kuwa ni hali ya utafiti kutoa matokeo yanayowiana ikiwa
utafiti utafanyika katika wakati mwingine, mahali pengine, au na mtu mwingine. Hii
ina maana kuwa matokeo ya utafiti yanatakiwa kuthibitisha kile ambacho mtafiti
alikusudia kukipima kulingana na malengo na mipaka ya utafiti wake bila kuathiriwa
na mambo yaliyo nje ya malengo ya utafiti. Kwa mantiki hiyo, ili kuhakikisha kuwa
utafiti huu unakuwa na uhalali na thabiti, mtafiti alikwenda katika maeneo halisi ili
kupata data za uwandani, alitumia matini sahihi kulingana na sampuli ya utafiti
wake, alipata data kutoka katika vyanzo sahihi, pamoja na kutumia njia na mbinu
sahihi katika ukusanyaji na uchanganuzi wa data.
Kwa jumla, uhalali na uthabiti wa utafiti huu ulitokana na namna mtafiti
alivyohusisha mbinu, pamoja na utoshelevu wa njia za kukusanyia data za utafiti
wake. Pia, misingi ya nadharia zilizotumika ilimwongoza katika kuchanganua na
kufasiri data kulingana na malengo mahususi.
3.10 Muhtasari wa Sura ya Tatu
Sura hii imeshughulikia mbinu mbalimbali zilizomwongoza mtafiti katika mchakato
mzima wa ukusanyaji wa data na uchambuzi wake. Vipengele vilivyoshughulikiwa
ni usanifu wa utafiti, mkabala wa utafiti, eneo la utafiti, na walengwa wa utafiti.
Vipengele vingine ni mchakato wa ukusanyaji wa data, mbinu za uchambuzi wa
data, maadili na itikeli za utafiti, pamoja na uhalali na uthabiti wa data. Mbinu hizi
zilisaidia kupata matokeo ya utafiti ili kukamilisha uandishi wa tasinifu yetu. Sura
inayofuata inahusu uwasilishaji wa data na mjadala wa matokeo ya utafiti wetu.
44
SURA YA NNE
UWASILISHAJI WA DATA NA MJADALA WA MATOKEO YA UTAFITI
4.1 Utangulizi
Sura hii inawasilisha data na kujadili matokeo kulingana na malengo yaliyoongoza
utafiti wetu. Mjadala huo umegawanywa katika sehemu kuu tano. Sehemu ya
kwanza ni utangulizi wa jumla. Sehemu ya pili imebainisha na kujadili matukio
mbalimbali ya mchakato wa kujiua yanayosawiriwa katika riwaya teule za Euphrase
Kezilahabi. Sehemu ya tatu imechunguza sababu za mitanziko ya wahusika
zinazosawiriwa katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi. Sababu hizo zimewekwa
katika makundi manne, yaani sababu za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kifalsafa.
Sehemu ya nne imetathmini uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa
kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii. Sehemu
ya tano inahitimisha kwa kutoa muhtasari wa jumla kuhusiana na mambo
yaliyojadiliwa katika sura nzima.
4.2 Matukio ya Mchakato wa Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase
Kezilahabi
Sehemu hii inawasilisha data na matokeo yanayohusiana na swali la kwanza la
utafiti lisemalo ‗Matukio yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya teule za
Euphrase Kezilahabi yana usawiri gani?‘ Sehemu yenyewe imegawanyika katika
vijisehemu sita. Mosi, muhtasari wa riwaya ya Rosa Mistika. Pili, matukio ya
mchakato wa kujiua katika riwaya ya Rosa Mistika. Tatu, muhtasari wa riwaya ya
Kichwamaji. Nne, matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya ya Kichwamaji.
Tano, muhtasari wa riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo. Sita, ni matukio ya mchakato
wa kujiua katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo. Kufahamika kwa matukio hayo
kunaweka bayana sababu za wahusika hao kujiua, mapito yao katika kupambana na
maisha, na mitazamo yao kuhusu dhana ya maisha.
Kwa jumla, matukio ya kujiua yanaweza kuwekwa katika makundi mawili, yaani,
kujiua kimwili na kujiua kiroho. Kujiua kimwili ni kitendo cha mhusika
kutenganisha mwili wake na roho na kuwa ndiyo hatima ya maisha yake hapa
duniani (Kubler-Ross, 1991). Kwa upande mwingine, kujiua kiroho ni kitendo cha
mtu kujitenga na Mungu kutokana na kutenda dhambi na hivyo kuyakosa maisha ya
milele (ufalme wa Mungu) (Luka 23:46; Rumi 6:23 katika Biblia Takatifu, 1997).
45
Mtazamo huu unahusiana zaidi na masuala ya kiimani (kidini). Kimsingi, katika
tamaduni nyingi duniani, hususani za Kiafrika, kujiua ni kitendo kisichokubalika
kijamii na kiimani. Utafiti huu umejikita zaidi katika kuchunguza matukio ya kujiua
kwa wahusika kimwili kwa kubainisha matukio hayo katika riwaya za Rosa Mistika,
Kichwamaji, na Dunia Uwanja wa Fujo.
4.2.1 Muhtasari wa Riwaya ya Rosa Mistika
Rosa Mistika (1971) ni riwaya ya kwanza kuandikwa miongoni mwa riwaya za
Euphrase Kezilahabi. Inajadili dhana ya maisha. Jambo hili linamshughulisha sana
mwandishi huyu katika takribani kazi zake zote. Alianza kuiandika alipokuwa
anasoma katika Seminari ya Mtakatifu Maria huko Nyegezi, Mwanza na
kuikamilisha akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mulokozi, 1983). Ilichapishwa
kwa mara ya kwanza mwaka 1971. Kwa kiasi kikubwa, inaelezea maisha ya mhusika
mkuu, Rosa Mistika, tangu utoto wake, matukio na misukosuko aliyopitia katika
maisha yake, hadi kuamua kujiua kwake. Wahusika wengine ni pamoja na Flora,
Zakaria, Regina, Deogratias, na Charles Lusato. Hawa wamesaidia sana katika
kuikamilisha riwaya hii, kwani wamemjenga mhusika mkuu katika mapito ya maisha
yake, hadi kufikia hatua ya kuyakana maisha yake kwa kujiua.
Mandhari yanayosawiriwa katika riwaya hii, kwa kiasi kikubwa, ni ya Ukerewe,
ambako ni chimbuko la mwandishi na, kwa kiasi kidogo, Morogoro na Mwanza.
Morogoro ndiko Rosa Mistika alikosomea mafunzo yake ya Ualimu, na Mwanza ni
eneo alilopangiwa kufanya kazi yake ya Ualimu. Tunakubaliana na fikra za
Mulokozi (k.h.j) kuwa riwaya hii inadhihirisha mambo makuu matatu, ambayo ni:
athari ya maisha ya Seminari kwa mwandishi, ujana na ubalehe wake, na dalili za
mtazamo wa kukata tamaa katika kutafakari maisha.
Msingi wa riwaya hii ni tukio la kujiua kwa mhusika mkuu, Rosa Mistika. Ijapokuwa
anaacha ujumbe kwamba kujiua kwake kunasababishwa na tukio la kuachwa
kimapenzi na mchumba wake Charles, utafiti umebaini kwamba tukio hili
halikumtokea ghafla, bali ni kilele tu cha matukio kadhaa aliyoyapitia katika maisha
yake. Uthibitisho wa hoja hii ni kwamba mwishoni mwa riwaya, Rosa Mistika,
akiwa mbele ya Mungu, anatakiwa kujibu mashtaka kutokana na kujiua huko;
ambapo, badala ya kumtaja Charles kuwa ndiye chanzo cha kufanya hivyo,
46
anaelekeza lawama zake kwa baba yake, Zakaria. Mashtaka hayo ni kama
yanavyoelezwa na mwandishi katika dondoo lifuatalo:
Mungu: Rosa kwa nini umejiua?
Rosa: Ee Mungu wangu. Haya yote yametokea kwa sababu ya
baba yangu.
Mungu: Rosa, ninakuuliza tena, kwa nini umejiua?
Rosa: Ee Mungu wangu. Haya yote yametokea kwa
sababu ya baba yangu.
Mungu: Zakaria una usemi gani kujitetea?
Zakaria: Ee Mungu wangu. Haya yote yametokea kwa
sababu ya ubaya na udhaifu wake mwenyewe.
Mungu: Rosa. Una ushahidi?
Rosa: Ndiyo, Bwana. Ulimwengu mzima.
Mungu: Na Zakaria?
Zakaria: Ulimwengu mzima, Bwana Mungu wangu
(uk. 98).
Katika dondoo hili, Mungu anamuuliza Rosa swali la msingi: ―Rosa, kwa nini
umejiua?‖ Swali hili lilikuwa kiini cha utafiti uliofanyika. Ili kuonesha uzito na
ukubwa wa tukio hili, swali hilohilo linaulizwa mara mbili. Hata hivyo, badala ya
kujibu kwamba amejiua kwa sababu ya kuachwa na Charles, kama anavyoeleza
katika barua yake kabla ya kujiua kwake, anaelekeza lawama zake kwa baba yake,
Zakaria. Anapojitetea, ―Ee Mungu wangu. Haya yote yametokea kwa sababu ya baba
yangu‖ anatudokeza kwamba kinachosababisha kujiua kwake siyo tukio la kuachwa
na Charles peke yake, bali kuna matukio mengine. Kwa msingi huo, jibu hili lilimpa
msukumo zaidi mtafiti wa kuona kwamba kumbe kujiua ni mchakato
unaofungamana na matukio mengi ndani yake.
Aidha, kwa kuwa jambo hili linasawiriwa katika kazi za Fasihi, ni uthibitisho kuwa
Fasihi ina uhusino na jamii. Kutokana na hilo, mtafiti alipata msukumo wa kufikiri
kwamba, inawezekana pia watu wanapojiua katika jamii zetu huwa hawajiui kwa
sababu ya jambo au tukio moja tu, bali huwa ni mchakato unaofungamana na
matukio mengi ndani yake. Kwa msingi huo, matokeo yanaonesha kuwa matukio ya
mchakato wa kujiua kwa Rosa Mistika katika riwaya hii ni: kupigwa na baba yake,
kuwachongea wasichana wenzake, kuota ndoto, na kusimamishwa shule,
kufumaniwa na kufukuzwa chuo. Matukio mengine ni kutoa mimba, kujitenga na
kutengwa na jamii yake, na kuachwa na mchumba wake. Matukio haya yamejadiliwa
kama ifuatavyo:
47
4.2.1.1 Kupigwa na Baba yake
Utafiti umebaini kwamba, hili ni tukio la kwanza kabisa linalounda mchakato wa
kujiua kwa Rosa Mistika katika riwaya hii. Imebainika kwamba, akiwa mwanafunzi
wa darasa la sita, alipata kipigo kikali kutoka kwa baba yake, Zakaria, mara tu baada
ya kugundulika kwamba amepokea barua ya mapenzi kutoka kwa Charles Lusato.
Huu ndio ulikuwa mwanzo wa kukata tamaa ya maisha yake, kumwogopa,
kumkasirikia na kumchukia baba yake, kuwachukia na kuwakasirikia wavulana, na
kukataa kuwa karibu nao. Mwandishi anaeleza kuwa baada ya Zakaria kubaini kuwa
Rosa amepokea barua hiyo, alichafuka na kumwita:
Rosa alikuja hali shuka ikiteremka chini. Kabla hajasema
lolote alipigwa na kuanguka chini. Alijaribu kuamka na
kukimbia lakini shuka ilimtegatega na kumwangusha chini
tena. Alikuwa sasa mikononi mwa baba yake. ―Lete hiyo
barua iko wapi? Pamoja na shilingi ulizopewa. Unafikiri sisi
hapa maskini?‖ Rosa alipigwa tena na tena, makofi
yalikwenda mfululizo hata damu ikamtoka puani na mdomoni.
Alilia, ―baba nihurumie, sitarudia tena, nimekoma.‖ Rosa
alinyang‘anywa shuka (uk. 6).
Kinachobainika katika dondoo hili ni kwamba, Rosa hapewi nafasi ya kujitetea na
kueleza ukweli wa jambo hilo, badala yake anashushiwa kipigo kikali, kiasi cha
kumwacha akiwa nusu uchi. Matokeo yake ni kwamba tukio hili linamjengea chuki
dhidi ya baba yake kutokana na vitisho vyake vya kumbana na kumnyima uhuru kwa
kumchunga sana. Pia, linamfanya ajihisi kuwa hapendwi na hana usalama wowote,
kwani kipigo hicho kinatia pengo kubwa katika ujenzi wa maisha yake. Imebainika
kwamba baada ya kipigo hicho, Zakaria huku akiwa na fimbo mkononi, anaongozana
naye hadi chumba cha watoto hali akiunguruma na kusema: ―Lazima uonyeshe barua
hiyo! Unataka kuniletea umalaya wa mama yako hapa!‖ (uk. 7). Kauli hii ya dharau
na udhalilishaji dhidi ya mwanamke, inamjengea Rosa mtazamo wa kuona kuwa
kumbe mwanamke ni kiumbe duni na kisichokuwa na thamani yoyote mbele ya
mwanamume. Matokeo yake, anashindwa kuelewa maana ya maisha, na hivyo,
anaanza kukata tamaa kwa kuyaona kuwa hayana maana.
Mwandishi anathibitisha jambo hili anapoeleza kwamba kutokana na kubanwa na
Zakaria, Rosa anashindwa kujitetea na kujiokoa, hivyo analazimika kuonesha barua
na pesa alizopewa na Charles. Mwandishi anaeleza kwamba:
48
Rosa, akiwa na haya nyingi, alichukua mfuko wake wa
madaftari, na katika daftari la Jiografia alitoa barua hiyo
pamoja na shilingi tano. Alimpa baba shilingi hizo; lakini ile
barua aliikunjakunja na kuitupia mdomoni. Alijaribu kuitafuna
lakini babake alimkaba koo. Rosa hakuitema. Zakaria alikaza
mkono. Macho ya Rosa yalianza kuwa mekundu, ulimi
ulimtoka na barua ilianguka chini. Ilikuwa na utelezi kama
kuku aliyetapikwa na chatu. Zakaria aliiokota mara moja.
―Sema nani amekupa barua hii!‖ ―Charles,‖ Rosa alitamka
kwa shida (uk. 7).
Tukio hili la kikatili linafanywa na baba dhidi ya mtoto wake wa kike, ambaye yuko
katika hatua za balehe. Pambano hili linatokea Rosa akiwa hana welewa wa kutosha
kuhusu ulimwengu huo mpya wa mapenzi, huku akikabiliwa na mabadiliko kadhaa
yanayoendelea kutokea katika maisha yake kimwili na kiakili. Ni wakati huu
ambapo anahitaji kupewa mwanga na miongozo mbalimbali kuhusiana na suala la
maisha yake, na namna ya kuzikabili changamoto zilizoko mbele yake. Badala
yake, licha ya kupewa kipigo kikali na cha kikatili kiasi hicho, analazimishwa
kuongozana na baba yake hadi nyumbani kwa Ndalo, mjomba wake Charles. Huko,
Zakaria anampa Charles onyo na maneno makali na mazito. Anamwambia:
―Charles! Tangu leo ukome kutembea na binti yangu. Chukua
vishilingi vyako (alimtupia shilingi tano). Unafikiri sisi ni
maskini tusio na mikono!‖ Rosa alilia karibu usiku kucha (uk.
8).
Matokeo yanaonesha kuwa malezi haya ya vitisho, ukali na ukatili wa Zakaria
yanamfanya Rosa awachukie wanaume na kujitenga nao kabisa. Kwa wakati huu,
anashindwa kuelewa kwamba kuwachukia wanaume siyo suluhisho la maisha yake,
bali ni mtihani mgumu anaokabiliana nao ili kuwaelewa. Badala ya wazazi wake
(Zakaria) kuwa watu wa kwanza kumwelekeza ili aufalu mtihani huo, wao
wanakuwa kitisho zaidi kwake. Hili linadokezwa na mwandishi anaposema:
Hivi ndivyo Rosa alivyolelewa; hivyo ndivyo alivyotunzwa;
hivyo ndivyo alivyochungwa na baba yake. Tangu siku hiyo
alikoma kutembea na mvulana yeyote. Na Zakaria alipojua
hayo alifurahi sana. Alijidai kwamba yeye alifahamu jinsi ya
kulea binti zake – hasa alipokuwa amekunywa kidogo.
Hakufahamu kuwa Rosa alikuwa katika rika baya, na kwamba
ukali ulikuwa haufai; hakufahamu kuwa mabinti wanahitaji
uhuru fulani kutoka kwa baba zao; hakufahamu kwamba kwa
kumpiga bintiye alikuwa akiingilia utawala usio wake, na
49
kwamba kuhusu maoni ya ndoa yake alifahamu kidogo sana;
na hakufahamu kwamba Rosa alihitaji kuwafahamu wavulana.
Kwa hiyo, kutokana na malezi ya namna hii, Rosa alianza
kuwaangalia wavulana kama watu wasiopaswa kuandamana
nao, au hata kuzungumza nao (uk. 9).
Dondoo hili linaonesha kuwa malezi ya kunyimwa uhuru, ukali, vitisho na ukatili wa
Zakaria dhidi ya binti yake, ndiyo yanayojenga chuki na uhasama baina yao. Ni
kweli kwamba katika jamii kuna miiko na maadili mbalimbali yanayotakiwa
kufuatwa na kuzingatiwa. Hata hivyo, kutokana na kufungwa na sheria, taratibu na
miiko ya jamii, watu hulazimika kukengeuka misingi hiyo na kutafuta uhuru katika
kujiamulia mambo yao. Mambo haya ndiyo yanayozingatiwa sana katika nadharia ya
Udhanaishi, kwani mtu hutafuta uhuru binafsi na uwezo wa kujifikiria na kujiamulia
mambo yake mwenyewe. Pia, mtu huyo huwa na wajibu wake katika ulimwengu.
Utafiti ulibaini kwamba malezi ya ukali, ukatili na vitisho kwa mtoto hayafai, kwa
sababu humjengea nidhamu ya woga na husababisha akengeuke misingi ya malezi
aliyopewa kwa kutafuta uhuru binafsi. Kinachotakiwa ni kumwonya, kumwelekeza
na kumfunza namna ya kuishi na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha
zitokanazo na mazingira yake. Kama inavyojitokeza kwa Rosa Mistika, utafiti
umebaini kwamba kutokana na msichana huyo kukosa mwongozo imara wa namna
ya kuwafahamu na kukabiliana na changamoto zitokanazo na wanaume,
anapotambua kwamba kuna uzuri ndani yao, anazidisha chuki kwa baba yake. Hata
uhusiano wake na baba yake unabadilika baada ya kutambua ukweli kwamba chanzo
cha matatizo yake ni malezi kutoka kwa baba yake. Matokeo yake ni kwamba
uhusiano wao unageuka na kuwa uadui, huku akipinga waziwazi mfumo wa malezi
ya baba yake. Hii inajidhihirisha kupitia majibizano makali baina yake na Zakaria
anaposema kwamba: ―Rosa, tangu leo wewe si mwanangu‖, ambapo Rosa naye bila
kusita anamjibu baba yake kwamba: ―Tangu leo, wewe si baba yangu.‖ (uk. 58).
Mazonge na mikatale ya jamii yake inamsukuma kuutafuta uhuru binafsi alioukosa
kwa muda mrefu. Hata hivyo, uhuru huo kama unavyoelezwa katika msingi wa tatu
wa nadharia ya Udhanaishi, siyo kamili, bali ni wa kuogofya. Hii inatokana na
ukweli kwamba mwanadamu hata akiupata uhuru huo, huweza kuutumia vibaya na
baadaye humletea madhara. Matokeo yanaonesha kuwa tukio la kupigwa kwa Rosa
linasababisha autafute uhuru wake ambao unakuwa chanzo cha mchakato wa kujiua
50
kwake, kutokana na kuutumia vibaya. Hili linathibitishwa na Rosa mwenyewe
kupitia kalamu ya mwandishi anaposema:
―Sasa ninakufa: ninakufa sasa. Maisha yangu yalikuwa
magumu. Sasa nimeona wazi kwamba malezi yangu ndiyo
yalikuwa chanzo cha taabu. Malezi. Siyo malezi ya mama,
lakini malezi ya baba yangu. Kweli baba alinichunga.
Nilichungwa kama msichana wa jela. Nilipopata uhuru,
nilishindwa kuutumia. Deogratias, Thomas, Charles – wote
hao nimewapoteza. Kwa heri Flora, kwa heri Honorata, kwa
heri Stella, kwa herini Sperantia, Emmanuel kwa herini! Baba
na mama samahani kama nimefanya vibaya.‖ Juu ya kitanda
alikuwa amelala Rosa. Alikuwa amekufa (kur. 91 – 92).
Ni wazi kwamba Rosa anamlalamikia Zakaria na siyo mama yake, kutokana na suala
la malezi aliyopewa. Anaona kuwa mchakato wa kujiua kwake unatokana na ukatili
wa baba yake kwa kumlea kama mfungwa. Malezi hayo ndiyo yanayosababisha
kupigwa sana na kuwa ndilo tukio la kwanza la mchakato wa kujiua kwake. Hili
linasababisha akengeuke misingi ya malezi ya baba yake. Matokeo yake, kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi, anaamua kujitafutia uhuru binafsi. Hata
hivyo, uhuru huo unamwingiza katika mateso kiasi cha kuyaona maisha kama kitu
kisichokuwa na thamani kwake. Hivyo, anajilaumu kwa kuutumia uhuru huo vibaya
na kuyachukia malezi mabaya aliyopata kutoka kwa baba yake.
4.2.1.2 Kuwachongea Wasichana Wenzake
Matokeo yanaonesha kwamba tukio hili ni kiini cha mabadiliko ya tabia ya Rosa
aliyotoka nayo nyumbani kwao na ndilo linalomwingiza zaidi katika mchakato wa
kujiua kwake. Hii ni baada ya kuwataja wanafunzi wenzake wa shule ya sekondari
ya Rosary waliotoroka usiku na kwenda kulala mjini. Kufahamika kwa tukio hilo
kunasababisha wasichana hao wanapewe adhabu ya kusomba magari mia ya
mchanga. Wanapobaini kuwa Rosa ndiye aliyewachongea kwa mkuu wao wa shule,
wanaamua kumchania madaftari yake na kumchomea mashuka yake yote. Pia,
wanamwandikia ujumbe wa vitisho na kuuweka kwenye dawati lake. Kitendo hicho
kinasababisha Rosa azidi kuchukiwa na wasichana wenzake. Hali hiyo inamfanya
aishi maisha ya upweke na kukosa amani na furaha. Ujumbe huo unasema:
―Kumbe ndiyo maana uko mnyamavu namna hii! Ulifikiri
tutafukuzwa! Utakatifu wako uko wapi?‖ Wasichana
walikoma kumsumbua Rosa lakini chuki haikwisha. Rosa
51
alichukiwa sana. Alipojaribu kukaa na kuongea na wenziwe
walimkimbia na kumwacha peke yake. Rosa alikonda.
Alimaliza darasa la tisa kwa shida sana (uk. 29).
Katika dondoo hili, imebaini kwamba tukio la Rosa kutengwa na wenzake linampa
wakati mgumu pale shuleni na linamkondesha sana. Ifahamike kwamba Rosa
anaingia na kuanza masomo katika shule hiyo akiwa na tabia nzuri iliyojengwa
kutokana na malezi makali na ya ufungwa aliyoyapata kutoka kwa baba yake.
Imebainika kwamba katika malezi hayo, amejifunza kwamba mtu akifanya mambo
mabaya huadhibiwa, na akifanya mazuri ikiwa ni pamoja na kusema ukweli
hupongezwa. Hata hivyo, anashangaa kuona kwamba baada ya kusema ukweli
kuhusu wasichana waliotoroka kwenda kucheza disko, uongozi wa shule
haumpongezi kama alivyotarajia. Badala yake anachukiwa na kutengwa na
wanafunzi wenzake, wakiwemo wasichana hao. Kitendo hicho kinamkatisha tamaa
na kuamua kukengeuka misingi ya malezi aliyojengewa na baba yake. Matokeo yake
anaamua kujiingiza katika vitendo viovu kama wanavyofanya wasichana wenzake.
Mabadiliko ya tabia yake yanazidi kuchochewa na maneno ya vijana wawili wa
shule ya sekondari ya Bwiru. Rosa mwenyewe anawasikia wakimzungumzia na
kudai kwamba inawezekana yeye ni kilema kutokana na ukimya wake na kushindwa
kujihusisha na masuala ya wavulana (uk. 29). Maneno hayo yanamletea maumivu
makali, yanamkata maini na kumsumbua sana moyoni mwake (uk. 30). Yanakuwa
kichocheo cha kuanza kujihoji kutokana na malezi aliyopewa na baba yake.
Mwandishi anaendelea kujenga wazo lake kwa kusema: ―Hata alipokuwa kitandani,
maneno haya yaliendelea kuzunguka kichwani mwake. Alikata shauri. Alikata shauri
kwenda kucheza dansi‖ (uk. 30). Baada ya kuanza maisha ya kwenda kucheza dansi,
anaanza kupata hisia tofauti, hasa baada ya kucheza na Deogratias. Kitendo hicho
kinasababisha mgongano wa mawazo yanayomfanya ajiulize maswali haya:
Kama nikifanya urafiki na wavulana baba yangu atafahamu?
Yeye yuko Ukerewe, mimi niko Usukuma, baba anakaa
akinichunga anafikiri yeye atanioa? (uk. 32).
Dondoo hili linaonesha kwamba, ijapokuwa Rosa alitoka kwenye malezi ya baba
yake akiwa na tabia nzuri, tabia hiyo ilianza kubadilika alipokumbana na mazingira
ya sekondari, ambayo ni tofauti na yale ya nyumbani kwake. Matokeo yanaonesha
kwamba kumbe tabia hiyo ilikuwa ni ya woga uliotokana na kufungwa na sheria
52
kandamizi za baba yake zilizomnyima uhuru wa kufanya mambo yake kama kiumbe
razini. Mtafiti anaamini kwamba iwapo Rosa angepewa uhuru wake tangu mwanzo,
angejua namna ya kuutumia kwa kuchagua na kufikiri lipi la kufanya na lipi la
kuacha. Maelezo haya yanaungwa mkono na Kipacha (2019) anayeeleza kwamba:
Rosa anaamua kubadilika kitabia baada ya wanafunzi wenzake
kumtusi na kumwita kilema kwa kukataa vishawishi vya
kujiingiza katika tabia ya ufuska. Hata hivyo, anapoamua
kuendana na tabia za wanajamii waliomzunguka, anatumbukia
katika mtego wa kushutumiwa kwa tabia yake ya ufuska na
ulevi kupindukia. Rosa anapitia kipindi cha utambuzi kuwa,
mifumo ya uthamani ya kitamaduni na kimaadili
inayomzunguka haina mantiki wala haimsaidii; na yote ni ya
kidanganyifu. Hivyo, anaamua kuitupilia mbali na kuchukua
mkondo wake kwa kukata minyororo iliyokuwa ikimfunga
kama msichana, mwanamke na mwanajamii (kur. 423 - 424).
Kwa jumla, utafiti umebaini kwamba kitendo cha Rosa cha kuwachongea wasichana
wenzake kwa Mkuu wa shule, ndicho kinachokuwa chanzo cha mabadiliko ya tabia
yake kwa kukengeuka misingi ya malezi ya baba yake. Matokeo yake, anaamua
kukata tamaa baada ya kubaini kwamba kitendo cha yeye kuwa na tabia nzuri ndicho
kinachosababisha wenzake wamchukie na kujitenga naye. Hatimaye, anabaini
kwamba kuwa na tabia nzuri hakumsaidii lolote, bali kunamwangamiza. Anaamua
kufanya lolote analotaka kwa sababu alipofanya aliyoyataka baba yake hakupata
faida, na anapofanya kinachotakiwa na mfumo wa shule yake, bado hapati faida.
Mabadiliko hayo ndiyo yanayomwingiza katika mchakato wa matukio ya kujiua
kwake.
4.2.1.3 Kuota Ndoto
Tukio lingine la mchakato wa kujiua kwa Rosa ni ndoto mbili alizoota mara tu baada
ya kurudi kutoka kwenye disko. Ndoto hizo zinaonesha mabadiliko ya kimwili ya
Rosa na mwanzo wa kuingia katika mahusiano ya kimapenzi. Kwa mfano, katika
ndoto yake ya pili, anaona kuwa yuko na kijana mrefu, mwembamba na mwenye
ndevu nyingi, huku akimtazama kwa huruma. Mambo anayoota katika ndoto hiyo,
hatimaye, yanamtokea baadaye kama inavyosawiriwa katika ukurasa wa 75, pale
anapojiwa na Charles, akiwa chumbani kwake huko Mwanza na kukabidhiwa barua
ya kumwomba wawe wachumba. Mwandishi akisimulia ndoto hizo, anasema:
53
Baada ya muda usingizi ulimchukua. Alimwona baba yake
akitembea barabarani na mbwa. Mbwa huyo alikuwa
amefungwa kamba shingoni. Mbwa aliona mbuzi. Alikata
kamba na kukimbia. Alimrarua mbuzi vipande… Rosa aliamka,
alilala, na usingizi ulimchukua tena. Aliona kijana mwembamba
mwenye ndevu nyingi akimtazama kwa macho yenye huruma.
Rosa alipomwona alimkimbilia na kumkumbatia akisema kwa
sauti, lazima unioe, ukinikataa wewe maisha yangu
yamekwisha; sina tumaini tena! Rosa alitokwa na machozi.
Mvulana alimbusu na kumwambia: ―Nitakujibu baadaye kwa
barua; lakini unafikiri baada ya ku… Thereza alikuwa bado
hajaelewa Rosa alipomrukia na kumkumbatia. Waliangushana
kitandani. Rosa alianza kumbusu, lakini tamaa yake haikuweza
kupungua. Rosa alihitaji ule mkwaruzokwaruzo wa aina ya
pekee. Mkwaruzokwaruzo wa ndevu na manyoya ya tumboni.
Zaidi ya hayo, moto ulikuwa ukiwaka upande wa Kusini lakini
wao walikuwa wakizimisha upande wa Kaskazini (kur. 32 –
33).
Katika dondoo hilo, mwandishi anapoelezea kuhusiana na ndoto ya kwanza ya Rosa
kwamba anamwona baba yake akiwa amemshikilia mbwa aliyefungwa, analenga
kutoa taswira kuhusu maisha ya Rosa kwa jumla. Mbwa analinganishwa na Rosa,
ambapo, mara nyingi, mbwa huwa hapewi uhuru wa kutosha ili asiwarukie na
kuwadhuru watu. Hivyo, dawa ya mbwa huyo huwa ni kufungwa minyororo ili asiwe
na uhuru wa kutosha na kufanya atakavyo. Hivyo ndivyo inavyomtokea Rosa. Kama
ilivyo kwa mbwa, Rosa naye ananyimwa uhuru wa kufanya atakayo kutokana na
kufungwa na sheria, pamoja na malezi makali ya baba yake.
Ifahamike kwamba, mambo haya yanamtokea Rosa akiwa katika hatua nyingine za
mabadiliko ya kimwili na anahitaji mwongozo wa maisha yake na namna ya
kuyakabili. Imebainika kwamba ndoto anazoota zinachochewa na tukio la yeye
kwenda disko na kucheza muziki kwa mara ya kwanza, huku akiwa amekumbatiana
na kupapasana na mwanamume anayeitwa Deogratias. Ndoto hizi zinaamsha hisia na
hamu yake ya kufanya mapenzi, kiasi cha kuamka na kwenda kumkumbatia Thereza,
msichana mwenzake, kwa lengo la kutimiza na kuondoa hisia hizo. Kipacha (2019)
anaeleza kwamba Rosa anaamua kuvunja maadili kwa kujaribu kufanya mapenzi ya
jinsia moja na rafiki yake, Thereza, huku akimbusu, lakini tamaa yake haikuweza
kupungua. Utafiti umebaini kuwa baada ya tukio hili, Rosa anaamua kujiingiza rasmi
katika mapenzi na kuwa na mahusiano na wavulana wengi kwa wakati mmoja.
Mwandishi anasema:
54
Rosa alianza mapenzi. Alianza mapenzi lakini aliyaendea
haraka sana kama mbwa aliyekata kamba. Aliona mvulana
mmoja au wawili walikuwa hawamtoshi kwa urafiki. Mwaka
huo huo aliwakubalia wavulana watano (uk. 33).
Kutokana na dondoo hilo imebainika kuwa, kitendo cha Rosa kuyaendea mapenzi
kwa pupa, kinamfanya asiwe na tahadhari ya namna ya kuutumia uhuru alioutafuta
kwa nguvu. Matokeo yake, anajitapa na kujiona kwamba yu mshindi kwa hayo
anayoyafanya, huku akidai kwamba anawaendesha wavulana kama mtu aendeshaye
punda. Anasema:
Unafahamu, Thereza, siku hizi ninawachezea wavulana kama
mtu aendeshaye punda. Vuta kamba mkono wa kulia na punda
atakata kona: vuta mkono wa kushoto, pia atakata kona. Punda
hafahamu aendapo isipokuwa mwendeshaji tu. Ndivyo hivyo
ninavyowachezea wavulana siku hizi (uk. 33).
Hii ina maana kwamba, Rosa haoni tofauti ya wavulana hao anaowachezea na
kuwaendesha awalinganishapo na baba yake mzazi. Anakusudia kusema kwamba,
anamwendesha baba yake kwa sababu naye ni mwanaume sawa na wavulana hao, na
kwamba, anao uwezo na uhuru wa kumchezea mvulana au mwanaume yeyote baada
ya kuupata uhuru wake. Anaamua kuyafanya yote haya kama njia ya kumkomesha
baba yake kutokana na malezi ya kikatili aliyompa.
Kama inavyoelezwa katika msingi wa tatu wa nadharia ya Udhanaishi, Rosa anafikia
hatua ya kuutafuta uhuru wake binafsi na uwezo wa kujifikiria na kujiamulia mambo
yake. Anakata kamba na minyororo aliyofungwa na baba yake kwa muda mrefu
kama inavyosawiriwa katika ndoto ya kwanza. Anaamua kukengeuka misingi ya
malezi aliyowekewa na baba yake kwa kutoendelea kutii vigezo vya jamii kwa
jumla. Ndiyo maana mwishoni mwa riwaya hii, kigezo kimojawapo kikuu, ambacho
ni Mungu, kinajitokeza na kuendesha kesi juu ya uasi wa Rosa na tukio la kujiua
kwake. Hapa Mungu anataka kumwonesha binadamu kuwa mwisho wa maisha hapa
duniani kila mmoja atabainishiwa ukweli halisi wa namna anavyoishi. Mwandishi
ametumia ndoto ili kuendeleza wazo la malezi aliyoyapata Rosa ambayo ni ya
kukandamizwa na kuwekewa mikatale na makatazo mengi (Wafula, 2007). Ndoto
hizi zinabeba maana maalumu kwa kuwa zinaelezea maisha halisi ya mhusika Rosa
Mistika, kwa kufichua athari ya tajiriba za utotoni katika makuzi ya maisha yake.
55
Kwa hiyo, utafiti umebaini kwamba ndoto zote mbili za Rosa zinachangia na
kuchochea kwa kiasi kikubwa katika mchakato wake wa kujiua. Hii ni kwa sababu,
ndoto ya kwanza, inamsukuma katika kuasi sheria na kanuni za malezi aliyolelewa
na baba yake kwa kutafuta uhuru wake binafsi kama inavyoelezwa katika nadharia
ya Udhanaishi. Hata hivyo, imebainika kuwa uhuru huo anautumia vibaya na
unamwingiza katika mtanziko wa maisha yake. Hii ni baada ya kukiuka miiko na
maadili ya malezi aliyopewa na wazazi wake. Ndoto ya pili inamwingiza katika
mahusiano ya kimapenzi na Charles, ambapo baada ya penzi hilo kuvurugika, Rosa
anachukua maamuzi ya kujiua.
4.2.1.4 Kusimamishwa Shule, Kufumaniwa na Kufukuzwa Chuo
Kubadilika kwa tabia ya Rosa akiwa katika shule ya sekondari ya Rosary na
kukengeuka misingi ya malezi aliyopewa na baba yake, kunasababisha matokeo yake
mtihani kuwa mabaya. Hili linamfanya azidi kuchukiwa na kutengwa siyo tu na
marafiki zake pale shuleni, bali hata na walimu wake. Matokeo yake ni kwamba
Mkuu wa shule anaamua kumsimamisha masomo na kumrudisha nyumbani kwao,
huku akilazimika kurudi kwa ajili ya kufanya mtihani wake wa mwisho. Mwandishi
anasema:
Sista John alimsimamisha Rosa masomo kutokana na tabia
yake kubadilika na kuwa na wanaume tofauti. Alisimamishwa
masomo na kulazimika kuja kufanya mtihani wake wa
Cambridge. Rosa alilia. Rosa alikwenda nyumbani (uk. 35).
Matokeo yanaonesha kuwa tukio hili linazidi kumwingiza Rosa katika mchakato wa
kujiua kwake, kwani anazidi kukata tamaa na kuyachukia maisha yake kwa kukosa
matumaini ya kuwa na maisha bora na mazuri ya hapo baadaye. Hata hivyo, anapata
matumaini kidogo anaporudi na kufanya mtihani wake wa mwisho, ambapo anapata
ufaulu mdogo unaomsaidia kwenda kusomea mafunzo ya Ualimu huko Morogoro
(uk. 37).
Utafiti umebaini kuwa akiwa Chuoni Morogoro, Rosa kama kawaida yake
anaendelea na tabia yake ya umalaya hadi kufikia hatua ya kupewa jina la
‗laboratory‘, yaani sehemu ya kufanyia majaribio, huku akiufurahia zaidi uhuru
mpya alioupata, akiwa mbali na malezi ya baba yake. Hata hivyo, anapoamua
kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na Mkuu wake wa chuo, Bwana Thomas,
56
mapenzi yao hayadumu, kwani anafumaniwa na mke wa Mkuu huyo wakiwa ndani
ya nyumba yao. Rosa akiwa katika dimbwi hilo la mapenzi, anashtukia kumwona
mke wa Thomas akiwa na shoka mkononi mwake. Kisha, anaambiwa:
―Leo utanitambua! Unataka kuniletea hapa umalaya wako!‖
Rosa alijaribu kukimbia. Alishikwa na yule mwanamke. Rosa
aliangushwa chini. Yule mwanamke alimwinamia. Rosa
alitiwa jino. Palepale uso wa Rosa ulienea damu. Yule
mwanamke alionekana akitema kitu fulani chini. Rosa alilia.
Mwalimu alimtoa mke wake juu ya Rosa. Rosa alikimbia.
Kabla hajawahi kutoka redio ilimpata mgongoni. Ilianguka
chini na kupasuka (uk. 55).
Kutokana na dondoo hilo, imebainika kuwa tukio hili linakuwa sababu za
kumwondoa Rosa katika furaha aliyokuwa nayo muda mfupi kabla ya kufumaniwa.
Hivyo, anakosa mwelekeo kwa kuzidiwa nguvu na mke wa Thomas kutokana na
kipigo kizito, kinachomsababishia maumivu makali na ya kutokwa na damu.
Anapata maumivu zaidi anapogundua kwamba kipigo hicho kinamsababishia kilema
cha maisha kutokana na kung‘atwa sikio lake na mke wa Thomas na sura yake
kuharibiwa vibaya. Mwandishi anaeleza kwamba:
Rosa alipofika chumbani alijifungia humohumo kwa ufunguo.
Alikimbilia kioo. Alipojiangalia ndani ya kioo hakuweza
kuamini kwamba hiyo ilikuwa kweli sura yake. Alilia kwa
sauti. Alililia sikio lake. Yule mwanamke alimuuma sikio na
kutoa sikio lote la nje. Alianza kusikia maumivu makali (uk.
55).
Utafiti umebaini kuwa tukio la kufumaniwa na kupigwa kwa Rosa, linachangia sana
katika mchakato wa kujiua kwake, kwani linamjengea chuki akilini mwake dhidi ya
wanaume na maisha yake kwa jumla. Matokeo yanaonesha kwamba kitendo cha
kujifungia ndani akiwa na maumivu makali, huku akiijutia hali mbaya aliyo nayo, ni
usawiri wa tukio litakalompata baadaye, ambapo atajifungia chumbani kwake kabla
ya kuchukua uamuzi wa kujiua. Inaelezwa kwamba:
Rosa alipofika chumbani mwake alijitupa kitandani. Mambo
mengi yalimzunguka kichwani mwake. ―Rosa,‖ alisikia sauti
moyoni mwake ikimwita. Ilikuwa sauti kama ya mtu
anayetaka kufa. Ilikuwa sauti hafifu sana. Rosa peke yake
aliweza kuisikia. Rosa peke yake aliweza kuitambua (uk. 55).
57
Taswira inayosawiriwa katika dondoo hili, haitofautiani na ile inayompata katika
tukio halisi la kujiua kwake. Katika kipengele cha 4.4.3 kinachoelezea uhusiano wa
njia zinazotumika katika kujiua, imefafanuliwa kuwa wataalamu wa magonjwa ya
akili wanaeleza kwamba mtu anayetaka kujiua husikia sauti ikimwita na kumhimiza
kutekeleza kitendo hicho, pasipo kurudi nyuma wala kughairi uamuzi wake. Bila
shaka, sauti anayoisikia Rosa kwa wakati huo ni ya kifo inayotokana na maumivu ya
kuondolewa kwa sikio lake na kipigo kikali kutoka kwa mke wa Thomas. Hivyo,
anaingia katika mchakato wa kujiua kutokana na kukata tamaa ya maisha na kukosa
furaha na matumaini kwa namna maisha yanavyomwendea.
Hatimaye, mabadiliko ya uongozi wa Mkuu mpya wa chuo yanafanyika. Bwana
Thomas anaondolewa na kuletwa mkuu mwingine, Bwana Albert. Mabadiliko haya
yanakuwa mwiba mchungu kwa Rosa, kwani uongozi huo haufurahishwi na
mwenendo wa tabia yake na unaamua kumfukuza chuo. Tunaambiwa:
… Baada ya mkutano wake na wanafunzi, Bwana Albert
alikuwa amekuja kumwambia Rosa apange vitu vyake
sandukuni; kwamba amefukuzwa kabisa. Kwa namna fulani
alimwonea huruma; lakini alipaswa kufuata sheria. Rosa
alisikia uchungu wa kufukuzwa shule (kur. 67).
Kutokana na nukuu hii, imebainika kuwa Rosa anapoipokea barua ya kufukuzwa
kwake, haoni tena sababu ya kuendelea kuishi. Matokeo yake ni kwamba, anaingia
katika mchakato wa kujiua ili kuyakomesha maisha yake ya taabu. Hata hivyo,
imebainika kuwa uamuzi huo haumtokei kwa ghafla, bali analikabili tukio hilo hatua
kwa hatua. Mosi, anaonekana akipokea barua ya kufukuzwa chuo, halafu anafuatilia
kinachoendelea baina ya Mkuu wa Chuo na wanafunzi wake pale mistarini, kisha
anapanga njia ya kujiua kwake na kuandaa kifaa cha kujiulia. Yote haya yanamtokea
kutokana na kukata tamaa kwa kuchoshwa na mazonge mengi yanayomkabili na
kukosa matumaini ya kupata cheti cha ualimu anaousomea. Hata hivyo, akiwa katika
kilele cha kutimiza azma yake, anaokolewa na Mkuu wa Chuo mwenyewe, baada ya
kuingia ghafla chumbani kwa Rosa kwa lengo la kumhimiza afungashe mizigo yake
na kuondoka chuoni hapo. Hili linamfanya Mkuu huyo amwonea huruma na
kubatilisha uamuzi wake baada ya kushauriana na walimu wenzake. Kisha, Rosa
anaendelea na masomo yake, huku akiwa na chuki dhidi ya maisha kutokana na
matukio mengi anayokumbana nayo.
58
4.2.1.5 Kutoa Mimba
Tukio lingine la mchakato wa kujiua kwa Rosa ni la kutoa mimba mara kwa mara
kutokana na tabia yake ya umalaya. Vitendo hivi vinaanza akiwa katika shule ya
Sekondari ya Rosary na vinaendelea akiwa Chuo cha Ualimu Morogoro. Mwandishi
anaeleza:
Rosa akiwa Morogoro TTC aliendeleza tabia yake ya kufanya
mapenzi. Alilazwa hospitali mahututi kwa kutoa mimba ya
miezi miwili. Rosa alikaa hospitali muda wa majuma mawili.
Rosa alipona. Aliendelea na mchezo wake. Katika majuma
mawili yaliyofuata, Rosa alikonda sana. Vijana walikuwa
wakimzungumzia yeye katika vikundi; hata yeye mwenyewe
alifahamu. Alianza kuwa anaviziavizia vikundi hivyo ili
afahamu wanasema nini juu yake (uk. 45).
Kupitia katika dondoo hili, imebainika kwamba licha ya kulazwa hospitalini na
kunusurika kufa, Rosa anaendelea na mchezo huo wa kutoa mimba. Haoni thamani
ya viumbe hao wasiokuwa na hatia. Ama kweli, mazoea hujenga tabia, na sikio la
kufa halisikii dawa, kwani ielezwa kwamba akiwa mwaka wa pili wa masomo yake
huko Morogoro, alirudia tena kutoa mimba, kama anavyoeleza mwandishi
anaposema: Mwandishi anasema:
Rosa alitoa tena mimba alipoingia katika mwaka wake wa
pili. Wengine walisema kwamba ilikuwa mimba yake ya tatu;
wengine walisema kwamba ilikuwa ya nne. Tukio hilo la
kutoa mimba lilisababisha Rosa kuchukiwa na walimu
wote… (uk. 52).
Utafiti umebaini kwamba matukio ya kutoa mimba mara kwa mara yanasababisha
maisha ya Rosa kuwa ya mashaka, ya upweke na ya kuchukiwa na kila mtu kwa
sababu ya kukosa marafiki. Matokeo yake, anaishi maisha ya kuviziavizia kwa
kukosa mtu wa karibu wa kumpa taarifa ya mambo yanayoendelea hapo chuoni
kumhusu yeye. Haya yanampata kutokana na kukiuka wosia wa mama yake, kwani
kabla ya kwenda shuleni aliambiwa:
… Jambo moja hasa ningependa kukutahadharisha: wavulana
wakorofi. Huenda wakakutaka mapenzi, na nia yao ikiwa ni
kukupa mimba itakayokukatisha masomo yako. Daima
wakwepe hao. Na iwapo utakuwa mpumbavu ukapata mimba
usiitoe. Tunasikia kwamba siku hizi wasichana wengi
wanaosoma wanafanya hivyo ili wapate kuendelea na masomo
59
yao. Wanapenda masomo zaidi kuliko watoto wao. Hata hivyo
ni wauaji (uk. 11).
Dondoo hili linaonesha namna Rosa anavyoamua kukengeuka maadili na misingi ya
utu aliyoelezwa na mama yake kabla ya kwenda shule. Badala yake, anatoa mimba
nyingi na kumsababishia matatizo mengi. Matokeo yake ni kwamba matukio hayo
yanasababisha aishi maisha ya upweke na ya kuchukiwa na kila mtu pale chuoni.
Haya yanazidi kumwingiza katika mchakato wa kujiua kwake kutokana na kukata
tamaa ya maisha.
Aidha, utafiti umebaini kuwa Rosa anafikia uamuzi huo wa kukata tamaa kutokana
na wazazi wake kushindwa kumwandaa kuingia katika maisha ya utu uzima, ikiwa
ni pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha yake. Hii
ni kwa sababu, wanamlea katika hali ya upweke kwa kumweka mbali na wavulana,
ambao kimsingi, ni sehemu ya jamii yake. Matokeo yake ni kwamba,
anapobadilisha mazingira ya nyumbani kwake na kwenda mazingira mengine mbali
na wazazi wake, anabaini kuwa mazingira hayo yamezungukwa na wavulana. Hali
hiyo, ndiyo inayomsukuma kuanza kujitambua kuwa, yeye ni nani, na hivyo,
anaanza kuwatambua vijana wa kiume. Matokeo yanaonesha kuwa, akiwa katika
mazingira hayo anabaini kuwa, wavulana ni binadamu kama walivyo binadamu
wengine na wala si wabaya kama alivyolazimishwa na wazazi wake kuwa, hawa ni
watu wabaya. Aidha, anabaini kuwa wavulana wana uwezo wa kumpenda, kwani
mapenzi anayopata kutoka kwao, yanakuwa fidia ya mapenzi aliyokosa kutoka kwa
wazazi wake, hususani Zakaria. Hata hivyo, kwa upande mwingine mapenzi haya
haya ndiyo yanayomponza kwa sababu yanamfanya aharibike na kumkatisha tamaa
ya maisha yake kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi. Kutokana na
maumivu ya kuachwa na mpenzi wake, anakosa uvumilivu na anaamua kujiua.
4.2.1.6 Kujitenga na Kutengwa na Jamii yake
Kujitenga au kutengwa na jamii husababisha mtu kuwa na upweke3, ambao ni
miongoni mwa dalili za mchakato wa mtu anayetaka kujiua. Mara nyingi mtu huyo
hukwepa mwingiliano na watu wengine na kubaki mwenyewe, huku akitafakari na
3 Hali ya kiumbe kukaa bila ya kushirikiana na wengine (BAKITA, 2017).
60
kupima kama uamuzi anaotaka kuuchukua ni sahihi au la. Mtu huyo anapoachwa
katika hali hiyo kwa muda mrefu, huweza kumsababishia msongo wa mawazo,
ambao humkatisha tamaa na hata kufikia hatua ya kuchukua maamuzi ya kujiua.
Kujitenga kwa Rosa baada ya kukumbwa na matukio mengi akiwa katika Chuo cha
Ualimu Morogoro ni uthibitisho wa hoja hii, kama anavyoeleza mwandishi:
Rosa alikata shauri. Kwa sasa alikaa kimya. Moyoni alikuwa
amevurugika kama mtu aliyetaka kutapika. Kwa sasa
hapakuwa na mtu aliyefahamu mawazo yake (uk. 58).
Dondoo hili linathibitisha kwamba mtu anapojitenga na jamii yake, huweza kupata
msongo wa mawazo, ambao huchangia katika mchakato wa kujiua kwake. Kulingana
na utafiti huu, imebainika kuwa mtu anapofikia hatua hiyo, hutakiwa kushauriwa
mapema ili asijiingize katika fikra hizo, kwani anapokosa mtu wa karibu wa
kumweleza matatizo yake, hujiona kama hana thamani na ndipo huamua kujiua. Hii
ni kwa sababu msongo wa mawazo ni tatizo la kisaikolojia, ambalo humweka
mhusika katika hali ya hofu au wasiwasi kutokana na kuzidiwa na mawazo kwa
kukosa jibu la kitu kilichoko mbele yake au kichwani mwake (Freud, 1900; Ndosi na
wenzake, 2004; Glucksman & Kramer, 2017). Matokeo yanaonesha kuwa, watu
wengi hufikia uamuzi wa kujiua kwa sababu ya kukaa kimya na kuyakumbatia
matatizo mbalimbali wanayoyapitia.
Vilevile, imebainika kuwa mchakato wa kujiua kwa Rosa unatokana na kitendo cha
kutengwa na jamii yake, akiwamo baba yake, walimu wake, wanafunzi wenzake,
pamoja na mchumba wake, Charles. Kwa mfano, anaumizwa na maneno ya baba
yake anaposema: ―Rosa ndiye nani? Malaya hajawa mgeni wangu wala mtoto
wangu.‖ (uk. 57). Maneno haya yanamkatisha Rosa tamaa na yanamsumbua sana
moyoni mwake. Hali hiyo inasababisha aamue kukengeuka misingi ya jamii kwa
kumtamkia baba yake maneno mazito aliyokuwa ameyatunza moyoni mwake kwa
muda mrefu. Anasema: ―Kila wakati unatuchunga. Unafikiri utatuoa wewe!‖ (uk.
58). Mwandishi anaeleza kuwa, kimsingi, maneno haya yalitakiwa kusemwa na Rosa
siku ile ya kwanza alipopigwa na baba yake, baada ya kukutwa na barua ya mapenzi
iliyotoka kwa Charles. Matokeo yanaonesha kuwa, kitendo cha Rosa kumtukana
baba yake kutokana na kauli yake hiyo kinachochea hasira zaidi dhidi yake.
Kutokana na hilo, Zakaria anaamua kumtamkia maneno mabaya, ambapo Rosa naye
61
bila kusita, anamrudishia baba yake maneno kama hayo. Kupitia kalamu ya
mwandishi, Zakaria anasema: ―Rosa, tangu leo wewe si mtoto wangu.‖ Kwa upande
wake, Rosa naye anadakiza bila kukawia kwamba: ―Tangu leo wewe si baba yangu.‖
(uk. 58).
Kwa jumla, matokeo yanaonesha kuwa suala la kutengwa na kujitenga kijamii
huweza kusababisha mtu kupata msongo wa mawazo, ambao ni chanzo kikubwa cha
sonona. Aidha, msongo huo wa mawazo huweza kusababisha mhusika kukata tamaa
kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi. Hali hiyo huweza hata
kumsukuma mhusika kufikia hatua ya kuchukua maamuzi ya kujiua kama
ilivyotokea kwa Rosa Mistika.
4.2.1.7 Kuachwa na Mchumba Wake
Katika tukio hili, imebainika kuwa Rosa Mistika anachukua maamuzi ya kujiua
muda mfupi tu, baada ya kupokea barua ya kuachwa kimapenzi na mchumba wake,
Charles. Hili linatokea muda mfupi mara tu, baada ya Charles na Rosa kukubaliana
kutoka Mwanza kwenda nyumbani kwao, Ukerewe, kwa lengo la kuwajulisha
wazazi wao, kuhusiana na suala la uchumba wao. Hata hivyo, wanapokaribia kufika
Ukerewe, Charles anampa Rosa barua, ambapo:
Rosa kabla ya kuisoma alianza kuibusu. Alifungua kwa
makini. Mikono yake ilikuwa ikitetemeka. Mwishowe barua
ilifunguliwa. Mle ndani mlikuwa na kipande kidogo cha
karatasi ngumu, aina ya zile zitumikazo kuwekea sementi.
Rosa hakuamini alichokiona. Alijikaza. Alisoma ile barua; Ha!
Rosa, kweli wewe ulikuwa bikira! Unafikiri baada ya
kufahamu kwamba ulichezewa sana huko Morogoro, na baada
ya mimi mwenyewe kuona bonde la ufa na kuliona lile sikio,
unafikiri mimi ninaweza kukuoa! Ha! Dada yangu, sahau.
Haiwezekani hata kwa mizinga! Hata kama ukiwa wa bure!
(uk. 90).
Matokeo yanaonesha kuwa, mara tu baada ya Rosa kusoma barua hiyo, hakuamini
alichokiona ndani yake. Furaha yake aliyokuwa nayo muda mfupi kabla ya kufungua
barua hiyo, iligeuka na kuwa maumivu makali kwake. Mwandishi anaeleza kuwa
kabla ya kuanza kuisoma barua hiyo, alikwenda chumbani kwake upesiupesi ili aone
kilichokuwa kimeandikwa. Anafafanua zaidi kuwa, kabla ya kuisoma, alianza
kuibusu huku akiwa na furaha tele. Hata hivyo, furaha yake ilitoweka kutokana na
62
ndoto ya matamanio yake kupotea. Hatimaye, ujumbe ulikuwamo ndani ya barua
hiyo, unasababisha Rosa kuchukua uamuzi wa kujiua. Hii ni baada ya kugundua
kwamba, ndoto yake ya kuolewa na Charles haiwezi kutimia kama alivyotarajia.
Utafiti umebaini kuwa, kitendo cha Charles kuandika barua hiyo kwenye karatasi
ngumu kililenga kuonesha dharau kwa Rosa, na kwamba, baada ya kugundua
kwamba hakuwa bikira, hakuwa na thamani tena kwake na alimwona kama
takataka. Hali hii ndiyo iliyousukuma mbele mchakato wake wa kujiua kwa kuona
kuwa maisha yake hayakuwa na maana tena. Zaidi ya hayo, karatasi hiyo ngumu ni
ishara kuwa Rosa baada ya kusoma ujumbe huo atachukua uamuzi mgumu wa
kukatisha maisha yake. Haya yanasawiriwa na mwandishi anapoeleza mambo
yanayotokea mara tu, baada ya Rosa kuisoma barua hiyo. Anasema:
Rosa alipomaliza kusoma kichwa kilimwanga. Aliona
kizunguzungu. Jasho lilimtoka. Machozi yalimteremka mpaka
kifuani. Rosa aliona ulimwengu wote ulimwonea huruma,
lakini sasa aliona kama kwamba ulimwengu wote ulikuwa
ukimchekelea. Kuishi aliona hawezi. Aliona ni fedheha.
Alitafuta chupa. Aliona chupa iliyokuwa na mafuta ya nywele
ndani yake. Bila shaka yalikuwa mafuta ya nywele ya
Sperantia. Rosa aliyamwaga chini. Alichukua ile chupa na
kuisagasaga juu ya jiwe. Baada ya kuisaga aliweka ule
ungaunga wa vipande vya chupa ndani ya glasi. Aliweka maji
(uk. 90).
Maelezo haya ni uthibitisho kuwa tukio la kujiua siyo la ghafla kama ambavyo huwa
linatazamwa na watu mara wasikiapo kuwa mtu fulani amejiua, bali ni mchakato.
Suala hili pia, linathibitishwa na mwandishi anapoeleza kuwa:
Rosa alifikiri kwanza kabla ya kunywa. Alitubu dhambi zake.
Alitafuta karatasi nzuri sana halafu aljichanja mkononi na
wembe. Damu ilitoka. Kwa damu hiyo aliandika maneno
fulani juu ya karatasi. Alipomaliza kuandika maneno yake
Rosa alivuta hasira yake. Alifikiri juu ya maisha. Mara moja
alikunywa yale maji. Alilala juu ya kitanda cha Honorata.
Palepale damu ilianza kumtoka mdomoni. Vile vipande vya
chupa vilimkatakata kooni. Rosa alitema mate. Aliona damu.
―Asante. Kifo njoo upesi,‖ alisema. Baada ya muda mfupi
Rosa alisikia maumivu makali sana tumboni. Muda mrefu
haukupita Rosa alijiona anaanza kupoteza fahamu. Alianza
kuona kitu kama moshi mbele yake. Alisema maneno yake ya
mwisho. Hapakuwa na mtu yeyote aliyesikia isipokuwa
manyigu yaliyokuwa yamejenga paani (uk. 91).
63
Kama inavyojidhihirisha katika msingi wa nne wa nadharia ya Udhanaishi, Rosa
anaamua kukengeuka misingi ya jamii kwa kufanya tukio ambalo halikubaliki katika
jamii. Anaamua kukata tamaa na kuyaondoa maisha yake kwa kujiua. Anakifurahia
na kukiita kifo chake cha maumivu, huku akitokwa na damu pasipo kujuta wala
kuonesha nia ya kuahirisha tukio hilo. Huu ndio unakuwa mwisho wa maisha yake
baada ya kupitia misukosuko na matukio mengi katika maisha yake. Haoni tena
sababu ya kuendelea kuishi. Anaamua kujiua kama suluhisho la kuyakomesha
maisha ambayo ni kama adhabu kwake. Anaridhika kwamba kufa kwake, ndio uhuru
wake.
Utafiti umebaini kwamba tukio hili la kujiua halimtokei ghafla, kwani kabla ya
kuchukua uamuzi huo, anafanya kwanza maandalizi. Maandalizi hayo ni pamoja na
kutafuta karatasi na kuandika ujumbe, kutafuta na kupanga njia anayokusudia
kuitumia katika kufikia azma hiyo, kuandaa chupa, kuisagasaga, na hatimaye,
kufanya kitendo chenyewe. Hii inadhihirisha kwamba kujiua ni mchakato, na wala
siyo kitendo cha ghafla. Aidha, imebainika kuwa mchakato huo ni wa namna mbili:
mchakato kwa mawanda mapana ya maisha ya mtu anayejiua, na mawanda finyu ya
wakati au siku yenyewe ya kujiua.
Mawanda haya ndiyo yaliyomsaidia mtafiti kubaini kwamba wakati mwingine
mchakato huo huweza kuwa wa muda mrefu na wakati mwingine wa muda mfupi
kutegemeana na aina ya tukio au jambo linalomsibu mhusika kwa wakati huo.
Matokeo yanaonesha kuwa mchakato huo unajitokeza hata katika kitendo chenyewe
cha kufa, yaani baada ya kunywa vipande hivyo vya chupa, tukio la kufa halitokei
mara moja. Anaanza kutema mate na kuona damu ikimtoka, anakiita kifo kimjie
upesi, anasikia maumivu makali tumboni, anapoteza fahamu na kuona kitu kama
moshi mbele yake, kisha anasema maneno yake ya mwisho. Huu ni uthibitisho
kwamba kujiua ni mchakato na siyo tendo la ghafla. Maelezo hayo yanaungwa
mkono na Ilomo4 anayesema kuwa:
4 Mahojiano baina ya mtafiti na Bw. Flavian Ilomo Oktoba 2, 2019. Yalifanyika
katika viunga vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako anafundisha masomo ya
Fasihi.
64
Kujiua kwa Rosa Mistika hakukutokea ghafla bali mchakato
wake ulianza na suala la malezi ambayo, aliyapata nyumbani
kwake. Malezi hayo hayakumwandaa kwa maisha mengine ya
nje ya nyumbani kwake. Hata watu waliomwahidi kuwa naye,
baadaye walimtenga. Jamii yake ilimgeuka na kumwita
malaya. Kwa hiyo, anafikia hatua ya kuona kwamba hakuna
anayeweza kutatua matatizo yake. Hivyo, anaona kuwa
suluhisho lake ni kujiua.
Vilevile, maelezo haya yanaungwa mkono na Ponera5, ambapo katika ufafanuzi
wake anaeleza kuwa:
Ni kweli kwamba kujiua ni mchakato na siyo kitendo cha
ghafla. Nakupongeza kwamba unaliangalia suala la kujiua
kama mchakato na siyo kama tukio. Ungefanya kosa kubwa
sana kama ungefanya utafiti wako kwa kulichunguza suala hilo
kama tukio. Kwa hakika kujiua siyo tukio na hata kufa
kwenyewe kwa namna yoyote ile, siyo tukio bali ni mchakato.
Tunakufa polepole sana kama anavyoeleza Kezilahabi
mwenyewe katika Kichwamaji (uk.186) . Anasema tunakufa
polepole, hatufi mara moja. Nakupongeza kwa kuwa wewe
unafanya utafiti kuhusu mchakato wa kujiua. Unalipa uzito
suala lenyewe la kifo kwamba ni mchakato na siyo tukio. Watu
wanapoishi, wanakabiliana na mazonge mengi ya maisha yao
pamoja na watu wanaoamiliana nao. Hivyo, katika hali hiyo,
inafika hatua kwamba mazonge hayo yanatakiwa yafike
mwisho. Hatimaye, wengine huamua kujiua au kujiondoa.
Hivyo, hatua hiyo huwa ni kukamilisha tu matukio mengi
anayokuwa amepitia mhusika kabla ya tukio hilo. Mchakato wa
kujiua katika riwaya teule umesawiriwa vizuri sana. Kwamba,
watu hao, hawakurupuki tu na kujiua, bali mwandishi
anawapitisha katika hekaheka, matatizo, miiba, konakona na
hemwahemwa hadi kufika mahali mtu anaamua kusema, sasa
basi, inatosha.
Kwa jumla, imebainika kuwa maelezo ya Ponera na Ilomo katika madondoo hayo,
yanaunga mkono hoja iliyokwisha kuelezwa na mtafiti kwamba kujiua ni mchakato,
na siyo tukio la ghafla. Mfano mzuri wa mchakato huo ni tukio la kujiua kwa Rosa
Mistika kama linavyosawiriwa kupitia ujumbe aliouacha kabla ya kujiua kwake.
Fikra hizo hazikumjia mara moja, bali zinajitokeza mara kadhaa akiwa Morogoro na
5 Mahojiano baina ya mtafiti na Dkt. Athumani S. Ponera yalifanyika kwa njia ya
simu Februali 17, 2020. Dkt. Athumani S. Ponera ni Mhadhiri Mwandamizi wa
Fasihi, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
65
Mwanza. Imebainika kuwa, akiwa Mwanza anaamua kuachana na tabia yake ya
mwanzo ya umalaya na anabadilika, hadi anapoamua kujiingiza tena katika mapenzi
kwa kumkubalia Charles, huku akiahidi kwamba, akishindwana naye, huo ndio
utakuwa mwisho wa maisha yake. Anasema:
Kijana huyu lazima anioe; nikimkataa huyu basi maisha yangu
yamekwisha; sina tumaini tena. Alikata shauri kupiga mshale
wake wa mwisho. Mshale huu ukienda pembeni, basi jitu
maisha – litaniua, Rosa aliwaza moyoni. Rosa alikumbuka
jinsi alivyopigwa na baba yake; alikumbuka alivyopelekwa
nyumbani kwa Ndalo usiku… Kadri alivyopata nuru ndivyo
mapenzi yake yalivyoongezeka. Rosa aliona kwamba huyo
ndiye alikuwa mume aliyeandikiwa na Mungu tangu awali.
Rosa alikubali ombi la Charles la kutaka wawe wachumba.
Alimjibu kwa barua (uk. 76).
Ndoto yake ya kuolewa na Charles inaposhindikana, jitu maisha linamuua kama
alivyojisemea mwenyewe. Inaelezwa kwamba, wakati wa kuosha maiti yake,
karatasi safi sana iliyoandikwa na Rosa kwa kutumia damu aliyojichanja mkononi
kwa kutumia kiwembe, ilikutwa ndani ya kwapa lake. Juu ilikuwa imeandikwa jina
la Charles. Waliisoma:
Charles mimi nilikupenda. Ninakupenda hata sasa. Charles
ninajiua kwa ajili yako. Lakini kwa kuwa ninakupenda,
ninakwambia siri moja kubwa uzingatie. Charles kuoa bikira
ni bahati tu wala si kitu cha kutafuta: ukimwonja mchumba
wako kabla ya ndoa si bikira tena, hata kama alikuwa (uk. 93).
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa, kitendo cha Rosa kuandika ujumbe katika
karatasi nzuri, tofauti na ile iliyotumiwa na Charles, ni ishara kuwa anaamua kufa
huku akiwa na mapenzi ya dhati kwake na anamthamini. Hii inatokana na kauli yake
mwenyewe anaposema: ―Charles mimi nilikupenda. Ninakupenda hata sasa.‖ Kwa
upande mwingine, kutumiwa kwa karatasi hiyo nyeupe kuna lengo la kuusaili
uadilifu na usafi wa maisha ya Charles. Hii inatokana na kitendo chake cha
kumhukumu Rosa kuwa ni mtu mwovu na asiyekuwa na thamani yoyote ya kuolewa
naye, kwa sababu ya kutokuwa na ubikira (uk. 90). Kutokana na hilo, imebainika
kuwa Rosa anaamua kumwachia ujumbe unaodokeza ugumu wa kuupata ubikira
anaoutafuta kwa sababu, wenye kuwaharibu wasichana na kuwaondolea ubikira wao
ni watu kama yeye. Anayabainisha haya anaposema: ―… ukimwonja mchumba wako
kabla ya ndoa si bikira tena, hata kama alikuwa.‖ Maneno haya yanamshitaki Charles
66
kuwa, na yeye yumo katika kuondoa na kuharibu ubikira wa wasichana.
Kulithibitisha hili, mwandishi anaonesha namna Charles anavyotaka kumwonja Rosa
kwa kufanya naye mapenzi, kabla ya kumwoa. Anasema:
… siku moja wakiwa katika hali hii, Charles alimwangusha
Rosa juu ya kitanda. Charles alikuwa katika hali mbaya. Rosa
alikuwa amefumba macho: alikuwa naye amekwisha. Charles
alifunga milango na madirisha. Rosa alikuwa bado amelala juu
ya kitanda akipumua kama njiwa. Charles alianza kumbusu;
waligeuzana huku na huko juu ya kitanda. Charles alianza
kuvuta gauni la Rosa juu polepole sana. Rosa alihisi mkono wa
Charles ukimgusa. Ulikuwa umefika mbali mara wazo
lilipomjia Rosa kichwani. Alishika mkono huo na kuurudisha
polepole (uk. 78).
Dondoo hili linathibitisha kuwa, ijapokuwa Charles anamwona Rosa kama mtu
mwovu na asiyekuwa na thamani kwake, naye pia ni mwovu kama alivyo Rosa.
Uovu wa Charles unajidhihirisha pia kutokana na kitendo anachotaka kumfanyia
Rosa, yaani kutaka kufanya naye mapenzi kabla ya kumwoa. Pia, utafiti umebaini
kuwa, Charles ana uzoefu wa kuwafanyia kitendo kama hicho wasichana wengine.
Hii ni kutokana na namna anavyofanya maandalizi kabla ya kumwingilia Rosa
kimwili. Maandalizi hayo ni pamoja na kufunga milango na madirisha, kulivuta na
kulipandisha gauni la Rosa juu, na kuingiza mkono katika sehemu nyeti za Rosa.
Hata hivyo, Charles anapolazimisha kufanya kitendo hicho, anasababisha Rosa
kusema uongo kwamba yeye ni bikira. Anasema:
―… Charles siyo leo.‖
―Mpaka lini?‖
―Mpaka siku tutakayooana. Afadhali tungoje siku yenyewe.‖
―Haiwezekani.‖
―Vumilia kidogo muda umekaribia. Ninakuomba usiniharibu
kabla ya muda. Charles – mimi ni bikira.‖
Rosa alitamka maneno ya mwisho kwa shida na kusitasita.
Charles aliposikia maneno haya alikufa ganzi. Hakuwa na
hamu tena ya kumpapasapapasa Rosa (uk. 78).
Ikumbukwe kwamba Rosa anaposema kuwa yeye ni bikira, tayari Charles ana taarifa
nyingi zinazohusiana na umalaya wake, alizozipata kutoka kwa marafiki zake hata
kabla ya kumwomba Rosa uchumba. Kutokana na hilo, utafiti umebaini kwamba
kitendo cha Rosa kumdanyanya Charles kuwa yeye ni bikira, kinatokana na matakwa
ya jamii yake, ya kuwataka mabinti kuolewa wakiwa na ubikira. Hii ni kwa sababu
67
katika utamaduni wa Mwafrika, suala la kutunza ubikira hadi wakati wa kuolewa lina
hadhi na thamani kubwa. Aidha, wasichana ambao hutunza ubikira wao hadi hatua
ya kuolewa kwao, hutambuliwa na kupewa heshima kubwa kwa kuwa na msimamo
imara katika kutunza maadili ya jamii zao. Hata hivyo, matokeo yanaonesha kuwa
ijapokuwa jamii hizo zinataka mabikira, bado zinaonesha udhaifu mkubwa katika
kuwashughulikia na kuwachukulia hatua watu wenye tabia mbaya kama za Charles,
wanaowaharibu mabinti zao. Hatuoni zikiwakemea na kuwachukulia hatua kali
wanaume wanaowahitaji mabikira, ilihali wao wenyewe ndio wanaowaharibia
mabinti hao ubikira wao.
Kwa jumla, utafiti umebaini kuwa haya ni miongoni mwa matukio ya mchakato wa
kujiua kwa Rosa yanayosawiriwa katika riwaya hii. Tasinifu hii inaonesha kuwa,
ijapokuwa matukio haya yanamhusu Rosa, kimsingi msichana huyu ametumiwa na
mwandishi kama kiwakilishi tu cha wasichana wengi wanaoishi katika nchi ya
Tanzania, Afrika ya Mashariki, Afrika, na ulimwengu mzima. Mwandishi amejaribu
kuonesha kwamba kuharibika kwa Rosa Mistika kunatokana na athari za kijamii na
mazingira anayoishi. Anakusudia kuifikishia jamii elimu ya sosholojia kwamba
jukumu la kulea mtoto si la baba na mama peke yao, bali ni la asasi mbalimbali,
ambapo asasi hizo huweza kumwathiri mtoto tangu akiwa mdogo hadi anapokuwa
mtu mzima. Matokeo yanaonesha kuwa asasi ya kwanza, ambayo ni familia, inaibua
hisia za huzuni kutokana na malezi ya Rosa, kwa namna anavyolelewa na baba yake.
imebainika kuwa Zakaria anamlea Rosa kwa mkono wa chuma na kumnyima
mapenzi, usalama na huruma. Pia, anamchunga kama kuku achungavyo vifaranga
vyake na kumkosesha uhuru wa kujiamulia mambo yake. Baadaye, Rosa anapopata
uhuru, anashindwa kuutumia. Matokeo yake anakufa kifo cha maumivu makali, huku
akikifurahia kwa sababu huo kwake, ndio uhuru aliokuwa anautafuta kama suluhisho
la taabu zake.
Hivyo, kulingana na nadharia ya Udhanaishi utafiti umebaini kwamba, ulimwengu
ndio unakuwa chanzo cha kuharibu maisha ya Rosa kwa kushindwa kumweleza
bayana kosa lake. Hii inatokana na ukweli kwamba mabadiliko ya tabia yake
yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mazingira yanayomlea na kumkuza. Mwandishi
anaeleza kuwa, ―Rosa alikuwa msichana mzuri, mrefu kiasi, mnyenyekevu na
mnyamavu…‖ (uk. 4). Tabia hiyo nzuri ya Rosa Mistika inaharibiwa na mazingira
68
kama anavyoeleza Madumulla (2009) kwamba Kezilahabi anamuunda Rosa Mistika
kama fumbo linalokuja duniani kama bikira, lakini linachafuliwa na ulimwengu wa
misukosuko au dunia ya ―ubatili mtupu‖. Hii ina maana kwamba, ijapokuwa Rosa
alizaliwa bila hatia, lakini mazingira yake ndiyo yanayomharibia maisha yake.
Mfano mzuri ni Zakaria anayemnyima fursa ya kujifahamu na kuwafahamu watu
wengine, Sista John anayesababisha nguo na vitabu vyake kuchomwa moto,
Mwalimu Thomas anayesababisha Rosa kuondolewa sikio lake, pamoja na Charles
anayemlewesha, na kisha, kumbaka.
4.2.2 Muhtasari wa Riwaya ya Kichwamaji
Kichwamaji (1974) ni riwaya ya pili kuandikwa na Euphrase Kezilahabi na
imetumika katika kupata data za msingi za utafiti huu. Riwaya hii iliandikwa na
kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1974. Inasimulia kwa undani maisha ya
wahusika wawili, ambao ni Kazimoto na Manase. Vijana hawa baada ya kujipatia
elimu ya Kimagharibi, wanashindwa kueleweka vizuri kwa jamii kutokana na
matendo yao. Elimu ya Magharibi inawakengeusha na inakuwa sababu ya wao
kutazamwa tofauti na kizazi cha wazee na jamii kwa jumla.
Sakkos (2008) anaeleza kuwa Kichwamaji ni riwaya ya kwanza ya kidhanaishi katika
Kiswahili. Anafafanua zaidi kwamba katika riwaya hii, mwandishi anayachambua na
kuyasawiri maisha ya jamii yake kwa kina, huku akiegemea katika falsafa ya
Udhanaishi. Falsafa hii inatilia mkazo katika kuchunguza tajiriba ya mtu binafsi
katika kupambana na safari yake ya maisha. Sakkos anaongeza kuwa katika riwaya
hii, mwanadamu amesawiriwa kama kiumbe dhaifu, kinachoishi maisha magumu,
yaliyotawaliwa na vurugu na yasiyo na maana katika ulimwengu usiokuwa na
maana.
Kwa kiasi kikubwa, masimulizi na maudhui ya riwaya hii yanasawiri na kuelezea
maisha ya mhusika mkuu, Kazimoto, tangu akiwa mtoto mpaka anapoamua
kujisababishia kifo chake kwa kujiua. Mwandishi anaeleza kwamba kutokana na
Kazimoto kuwa na elimu ya Chuo Kikuu, anaamua kwenda kwa Mkuu wa Wilaya,
ambaye ni rafiki yake waliyekua pamoja, aitwaye Manase, kwa lengo la kuomba
kazi. Huko anafanikiwa kuonana naye, lakini anakataliwa. Baada ya hapo, Kazimoto
anaamua kurudi kijijini kwake akiwa na sononeko moyoni mwake. Anapokuwa
69
kijijini kwake, jamii pia inaonekana kujitenga na kuwa mbali naye. Pia, akiwa katika
hali hiyo ya mtanziko, anaumizwa sana kwa kitendo cha dada yake, Rukia, kutiwa
mimba na Manase. Kutokana na tukio hilo, anadhamiria kulipa kisasi kwa Manase,
pamoja na familia yake. Baada ya hapo, Kazimoto anapitia mikasa na matukio
mbalimbali yanayomsukuma na kumweka katika dimbwi la tafakuri kuhusu dhana na
maana ya maisha. Hatimaye, anayaona maisha kama adhabu, hali inayomsukuma
zaidi kutafakari na kuona kuwa hakuna Mungu.
Katika riwaya hii mwandishi anayasawiri na kuyapa uzito matatizo na matukio ya
kijamii, pamoja na mustakabali wake. Ili kumsawiri vyema Kazimoto, mwandishi
anaunda masimulizi yanayohusisha maisha ya wahusika wengine kama vile Sabina,
Pili, Vumilia, Moyokonde, Rukia, na Kabenga, ili kumjenga mhusika mkuu,
Kazimoto. Hatimaye, Kazimoto naye anafuata nyayo za Rosa Mistika. Anaamua
kujiua kwa kujipiga risasi kutokana na msongo wa mawazo, baada ya kupitia na
kukumbwa na matukio mengi katika maisha yake. Hapa tunabainisha baadhi ya
matukio ya mchakato wa kujiua kwake, ambayo ni: kunyimwa kazi, Rukia kutiwa
mimba, vifo vya Rukia na mama yake na kifo cha Kalia. Matukio mengine ni kifo
cha mtoto wake, kuugua ugonjwa wa ajabu, na kujitenga kijamii. Matukio haya
yamejadiliwa kama ifuatavyo:
4.2.2.1 Tukio la Kunyimwa Kazi
Matokeo yanaonesha kuwa mchakato wa kujiua kwa Kazimoto unaanza na tukio la
kwenda ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, Manase, kwa lengo la kuomba kazi ya muda.
Huyu ni mtu anayefahamiana naye kwa muda mrefu kutokana kukua pamoja na
kusoma shule na Chuo Kikuu wakiwa pamoja. Imebainika kuwa, Kazimoto akiwa
ofisini hapo, kabla ya kuingia ndani na kuonana na Mkuu wa Wilaya, anapanga
foleni miongoni mwa watu wengi wanaokusudia kumwona kiongozi huyo. Hata
hivyo, licha ya kufahamiana naye, Kazimoto anapofanikiwa kuingia ofisini humo,
anakumbana na changamoto kwani hapokelewi vizuri, bali anadharauliwa na
kutolewa nje kwa madai kuwa, hana adabu. Badala yake anaambiwa aingie tena
mwishoni mara tu watakapomalizika watu wote walioko kwenye foleni.
Kudharauliwa na kutothaminiwa huko, ndiko kunakoanza kujenga chuki na mtazamo
hasi kuhusu thamani na maana ya maisha yake. Mazungumzo yafuatayo baina ya
Kazimoto na Manase yanalisawiri vizuri jambo hili:
70
―Habari za asubuhi,‖ nilimsabahi.
―Asante, keti kitini.‖
―Mimi nilikuwa na shida kidogo.‖
―Ndiyo kusema sasa huna.‖
―Nina shida,‖ nilijisahihisha ili kumpendeza. ―Natafuta kazi ya
muda. Miezi mitatu hivi.‖
―Wewe nani?‖ Nilikasirika kidogo, lakini hasira yangu
niliimeza kwa kuuma meno. ―Mimi Kazimoto, mwanafunzi
wa Chuo Kikuu – Dar es Salaam.‖
―Huko ndiko mnakofunzwa jinsi ya kuwasabahi wakubwa
namna hiyo.‖
―Mimi ninatafuta kazi.‖
―Hata mimi nilipokuwa Makerere nilikuwa nikiwaheshimu
watu. Au kwa kuwa umesoma Chuo Kikuu unafikiri u mtu
tofauti.‖
―Kusoma Chuo Kikuu siyo dhambi,‖ nilimjibu. ―Lakini mimi
hayo hayakunileta hapa. Mimi ninatafuta kazi.‖
―Huna adabu! Kaa nje kwanza, unanichelewesha kazi bure.
Utaingia humu mtu wa mwisho (uk. 4).
Kinachobainika katika dondoo hili ni hasira ya Kazimoto kutokana na kiburi, dharau
na udhalilishaji anaofanyiwa na Manase. Anakasirika zaidi anaposhuhudia upendeleo
wa wazi unaofanywa na kiongozi huyo, kwani anawasikiliza kwa makini na kuwapa
kazi watu wa jinsia ya kike, wakiwemo Vumilia, Pili, na Salima, na kuwanyima wale
wa jinsia ya kiume, akiwamo yeye. Sambamba na hilo, anakasirishwa na tabia ya
Manase ya kutumia ofisi hiyo ya umma kama sehemu ya kupangia mipango na
vitendo vyake vya umalaya na wasichana hao, huku watu wengi wakiwa kwenye
foleni wakisubiri kuingia. Hata hivyo, Kazimoto anapoingia kwa mara ya pili, baada
ya kusubiri kwa muda mrefu, anaambiwa kuwa muda umekwisha na kutakiwa kurudi
kesho yake. Majadiliano yafuatayo baina yao, yanadhihirisha jambo hili:
―Samahani, ninataka kufunga ofisi. Saa nane na nusu sasa.
Utarudi kesho.‖ Nilimtazama machoni kwa mshangao.
―Kazimoto, fika kesho asubuhi.‖
―Mimi niliendelea kumkazia macho.‖
―Bwana Manase,‖ nilimwita.
―Ndiyo, unanifahamu; lakini sasa nimo kazini.‖
―Ndiyo.‖
―Manase,‖ nilimwita tena.
―Kazimoto,‖ aliniita (uk. 7).
Dondoo hili, linaonesha kiburi cha kiongozi huyu na namna anavyokiuka maadili na
misingi ya kazi yake, huku akitoa huduma kwa upendeleo na kuwanyanyasa watu
wake. Jambo hili linamkasirisha, linamuumiza, linamsumbua na kumuudhi sana
71
Kazimoto. Ndiyo maana anapoambiwa muda umekwisha, anaendelea kusimama
palepale, huku akimtazama kwa muda (uk. 7). Matokeo yake, anaamua kwenda
kunywa pombe nyingi ili alewe upesi kama njia ya kuyasahau mambo hayo. Kitendo
hicho cha kwenda kunywa pombe ni dalili mojawapo ya kukata tamaa ya maisha
kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi. Matokeo yake ni kwamba hasira
hii inapomzidi, anapanga kwenda ofisini kwa Manase kesho yake ili akamchome
visu. Mwandishi anaeleza kwamba:
Wazo la kufika tu ofisini nimchome Manase visu vya tumboni
lilinijia tena kichwani. ―Huenda nami nikanyongwa,‖ nilisema
moyoni. ―Sitapata faida yoyote isipokuwa kuwaacha wazazi
wangu taabuni. Jambo la maana ni kujaribu kumpa Manase
maisha magumu hapa duniani. Nisipoweza basi nitajilipiza
kisasi kwa njia nyingine.‖ (uk. 15).
Kinachojitokeza katika dondoo hili ni kwamba Kazimoto anaamua kuachana na
uamuzi wa kwenda kumchoma visu Manase kwa kuhofia madhara makubwa
yanayoweza kumpata. Anaachana na kitendo hicho, huku akiwa na kinyongo moyoni
mwake kutokana na Manase kumtia mimba dada yake, Rukia, (uk. 16). Hili
linathibitishwa na Kazimoto mwenyewe, baada ya kuamua kumuuliza Manase
kuhusu tukio hilo la kinyama (kur. 16 – 17). Matokeo ya kuuliza swali hilo,
yanasababisha apoteze na kunyimwa kazi ya kuhesabu ng‘ombe, aliyokuwa
amepewa na Manase muda huo huo. Mwandishi anaeleza kuwa, Manase akiwa na
hasira kali alimnyang‘anya Kazimoto karatasi yake na kumtamkia waziwazi kuwa:
―Sasa hata kazi hupati…‖ (uk. 17).
Utafiti umebaini kuwa tukio hili la kunyimwa kazi linaunda mchakato wa kujiua
kwake, kwani kitendo cha Kazimoto kupanga kumchoma visu Mkuu wa Wilaya ni
dalili ya kukata tamaa ya maisha yake. Suala hili kama linavyoelezwa katika
nadharia ya Udhanaishi, linamtokea akiwa katika harakati za kuutafuta uhuru wake
binafsi na uwezo wa kujifikiria na kujiamulia mambo yake mwenyewe. Hali hiyo
ndiyo inayosababisha akengeuke misingi ya maisha ya jamii yake na kupanga
kumuua kiongozi huyo wa Serikali. Kutokana na hilo, tumebaini kwamba iwapo
kitendo hicho kingefanikiwa, huo ungekuwa mwisho wa maisha yake ama kwa
kujiua mwenyewe au kwa kuuawa na nguvu ya umma. Hivyo, tukio hili la kunyimwa
72
kazi kwa Kazimoto, linajenga chuki na visasi moyoni mwake na linakuwa chanzo
kimojawapo cha mchakato wa kujiua kwake.
4.2.2.2 Rukia Kutiwa Mimba
Hili ni tukio lingine la mchakato wa kujiua kwa Kazimoto ambapo dada yake, Rukia
anatiwa mimba na Manase, wakiwa wanaishi pamoja huko Dar es Salaam. Haya
yanatokea baada ya Kazimoto kumwomba Manase, ambaye ni mtu wake wa karibu
na rafiki waliyesoma pamoja, kukaa na Rukia ili aendelee na masomo yake ya darasa
la tisa. Matokeo yake, Manase anautumia mwanya huo kumwingilia Rukia kwa
nguvu na kumtia mimba. Tukio hili linamkasirisha sana Kazimoto, kiasi cha
kumfanya ayachukie maisha yake, kumchukia Manase na kujenga uhasama dhidi
yake. Anakasirishwa zaidi na uongo wa Manase, anayedai kwamba Rukia ndiye
aliyemlazimisha kufanya naye mapenzi kutokana na umalaya wake. Haya
yanabainishwa katika mazungumzo baina ya Kazimoto na Manase kama ifuatavyo:
―Manase.‖ Nilimwita. Alinitazama. ―Jambo gani ulifanya?‖
Nilimuuliza hali nikimtazama usoni. Mara moja sura
ilimgeuka. Nilimwona anafungua mdomo polepole.
―Kazimoto, huelewi vizuri hadithi yenyewe.‖
―Halikuwa kosa langu.‖
―Ni kosa la nani?‖
―Hakika Rukia mchokozi sana. Yeye ndiye alinianza.‖
―Alikuanzaje?‖
―Unaona. Siku moja nilipokuwa nimelala usingizi nilisikia
mtu anagonga mlango wangu. ‗Nani huyo!‘ Nilisema kwa
sauti. ‗Ni mimi Rukia, fungua mlango!‘ ‗Kuna nini?‘
Nilimuuliza. ‗Wewe fungua mlango tu!‘ Nilipofungua mlango
aliingia chumbani mwangu; alilala juu ya kitanda changu. Sasa
wewe fikiri Kazimoto, mwanaume kama wewe ungefanya
nini?‖ … Bila shaka utakubalina nami kwamba Rukia alikuwa
malaya tangu alipoota maziwa (kur. 16 – 17).
Dondoo hili linabainisha uongo wa wazi wa Manase wa kumsingizia Rukia kwamba,
ndiye aliyemchokoza na kusababisha kufanya naye mapenzi. Aidha, kauli hii,
inaonesha namna wanaume wanavyowalaghai watoto wa kike kimapenzi, ambapo
mara tu wafanikiwapo katika nia yao ovu, huwakataa na kuwadharau. Kitendo cha
Manase kumwita Rukia malaya, ndicho kinachomkasirisha zaidi Kazimoto,
kinamkatisha tamaa ya maisha na kujenga chuki na visasi dhidi yake. Mwandishi
anabainisha majadiliano baina yao kama ifuatavyo:
73
―Unamwita malaya!‖ Nilisema kwa hasira.
―Ndiyo.‖
―Hebu sema tena!‖
―Rukia ni malaya. Kama umekasirika na jambo lililotokea kwa
bahati mbaya unaweza kufanya jambo lolote upendalo! Sijali
sasa!‖ Alisema kwa hasira. ―Sasa hata kazi hupati!‖ Karatasi
nilinyang‘anywa.
―Tutaona!‖ Alimwambia kwa hasira kubwa (uk. 17).
Katika dondoo hili, Kazimoto anakasirishwa na kitendo cha Manase cha
kumdhalilisha Rukia kwa kumwita malaya. Anapolitamka kwa hasira neno ―tutaona‖
ni dalili ya kukata tamaa kwake na kwamba yuko tayari kwa lolote linalomjia mbele
yake. Kukata tamaa huku ndiko kunakomwingiza katika mchakato wa kujiua
kutokana na kusongwa na mawazo mengi yanayotokana na tukio hili. Anazidisha
chuki kwa Manase anapopewa ujumbe na Rukia kwamba hayuko tayari kuendelea
kuishi na Manase na kwamba ataacha shule, iwapo hatatafutiwa sehemu nyingine ya
kuishi kutokana na vitendo anavyofanyiwa na Manase. Anasema:
―Sijui Manase ni mtu wa namna gani. … Kaka usiponitafutia
mahali pengine pa kukaa mimi nitarudi nyumbani. Heri
kuacha shule!‖ (uk. 19).
Kazimoto anazidi kuchanganyikiwa anapobaini kwamba Rukia amekata tamaa, hana
furaha na uvumilivu wake wa kuendelea na shule umekwisha. Kabla ya kuufanyia
kazi ujumbe huo, anasongwa zaidi na mawazo anapopokea barua inayoeleza matukio
na mapito yote ya Rukia. Katika barua hiyo, Rukia anasema:
Kaka mpendwa,
Moyo wangu siku hizi hauna raha. Lakini leo nimechukua
kalamu ili nikueleze mambo yote. Nimeona kwamba siwezi
kuwa nakuficha wewe mambo, hali mambo yenyewe sasa
hayawezi kufichika. Wewe ukiwa ndiye kaka yangu na ndiye
uliyenitafutia nafasi hii ya shule ninakupa heshima. Fahamu
kuwa mambo haya sijapata kumweleza mtu mwingine
isipokuwa wewe peke yako.
Kaka, uliponileta hapa nilikaa kwa raha kwa muda wa juma
moja tu. Baada ya juma hilo, niliona Manase anaanza
kunitazama kwa njia ya ajabu. Baada ya majuma mawili
mambo yalizidi kuwa mabaya, kwani nilipokuwa naoga siku
moja niliona jicho lake kwenye tundu la ufunguo. Mwishowe
aliniambia wazi alichokuwa anataka. Nilimwambia: Manase!
Kaka yangu akifahamu litakuwa jambo la aibu sana! Lakini
yeye alijibu kwamba wewe ni mwanaume kama yeye. Alifika
74
hatua ya kutumia nguvu! Na kweli alitumia nguvu bila utashi
wangu. Kaka, sitaki kukupotezea muda wako wa kujifunza kwa
kusoma barua ndefu. Mimi maisha yangu yameharibika. Shule
nimekwishaacha. Jambo ambalo limenisikitisha sana ni hili
lifuatalo: Jana usiku, Manase alirejea nyumbani mlevi.
Alikuwa na tikiti ya basi. Baada ya kunitukana kwa maneno
ambayo siwezi kukuandikia, alianza kupanga vitu vyangu
sandukuni. Leo atanisindikiza hadi kituo cha basi. Kaka,
machozi yananilengalenga, sijui nitasema nini kwa baba na
mama. Usifike kuja kuniaga kwenye kituo cha basi nisije
nikazimia.
Sina mengi,
Nduguyo,
Rukia Mafuru (kur. 19 - 20).
Kutokana na barua hii, imebainika kwamba Kazimoto anazidi kuchanganyikiwa na
kuongeza chuki na hasira mara tu, anapopata taarifa kwamba Rukia amekuwa akiishi
maisha ya taabu na mateso kwa muda mrefu, lakini hakutaka kuitoa siri hiyo
mapema. Matokeo ya usiri na uvumilivu wake huo, ndiyo yanayosababisha atiwe
mimba na kuvuruga maisha yake ya baadaye. Hapo ndipo Kazimoto anapobaini
kuwa, Rukia ameamua kuandika barua hiyo, baada ya kukosa furaha na matumaini
kwa kuona kwamba maisha yake sasa, hayana maana yoyote.
Kwa kuzingatia msingi wa kwanza wa nadharia ya Udhanaishi unaojadili matatizo
halisi yanayomkumba binadamu utafiti umebaini kwamba, watu wengi hujiua
kutokana na kuzidiwa na maumivu makali wayapatayo. Maumivu hayo
husababishwa na mrundikano wa mambo ambayo huwa wanayashikilia katika mioyo
yao, pasipokuwashirikisha watu wao wa karibu. Hili ndilo linalomtokea Kazimoto,
kwani mara tu baada ya kupata barua hiyo, anapatwa na msongo wa mawazo na
hasira yake inazidi kufura. Hafurahishwi na kiburi cha Manase cha kumdhalilisha na
kumnyanyasa dada yake kwa kumwita malaya, huku akimwambia kwamba
Kazimoto ni mwanaume kama yeye. Hali hiyo inasababisha ashindwe kuhudhuria
masomo kwa muda wa siku moja kutokana na kichwa chake kuvurugika. Tukio la
Rukia kutiwa mimba linamsababishia msongo wa mawazo unaomweka katika
mchakato wa kujiua kwake. Hii ni kwa sababu yeye ndiye aliyemwomba Manase
akae na Rukia. Hivyo, anajiona kuwa anastahili kubebeshwa lawama za uharibifu
huo.
75
4.2.2.3 Vifo vya Rukia na Mama Yake
Tukio lingine la mchakato wa kujiua kwa Kazimoto linatokana na vifo vya dada
yake, Rukia, pamoja na mama yake. Kama ilivyokwisha kuelezwa hapo awali,
matokeo yanaonesha kuwa tukio la kutiwa mimba kwa Rukia linapokelewa kwa
masikitiko makubwa na Kazimoto pamoja na familia ya mzee Mafuru, ambaye ni
baba yake Kazimoto. Kwa mfano, mama yake anapopata taarifa hii, anasononeka
sana moyoni mwake; na kama ilivyo kwa Rukia, wote wawili wanakataa kula kwa
muda mrefu. Hata Kazimoto anaporejea nyumbani kutoka Chuo, anawakuta wakiwa
katika hali hiyo, huku wakilia muda wote kwa masikitiko makubwa. Hali hii
inamsababishia maumivu moyoni mwake na inaendeleza chuki na msongo wa
mawazo. Anaumia na kusononeka zaidi anapofanya jitihada za kumbembeleza Rukia
ili ale chakula, lakini jitihada hizo zinashindikana. Kuhusiana na suala hili,
mwandishi anaeleza namna Kazimoto anavyombembeleza Rukia. Anasema:
―Rukia,‖ nilimwita polepole. ―Rukia,‖ niliita tena.
Hakuniitikia. Nilijaribu tena. ―Rukia, jaribu kula chakula
kidogo.‖ Hakuniitikia. Badala yake alianza kulia kwa kelele
(uk. 37).
Katika nukuu hii, mwandishi anajaribu kuisawiri hali aliyo nayo Rukia kutokana na
kitendo hicho cha kutiwa mimba pasipo ridhaa yake. Hali hiyo halimtokei Rukia
peke yake, bali hata mama yake anakuwa katika wakati mgumu kutokana na hali
aliyo nayo binti yake. Utafiti umebaini kwamba, muda mfupi baadaye, mama yake,
huku akiwa amejaa uchungu, anamwambia Kazimoto mambo yanayowasibu yeye
pamoja na Rukia. Anamweleza kuwa vijana wa siku hizi wanaangamiza maisha ya
wazazi na kwamba, kutokana na hilo, yeye hatakuwa na muda mrefu wa kuishi kwa
sababu atakufa pamoja na binti yake. Anasema:
―Kazimoto,‖ mama alisema. ―Kazimoto, tuache tupumzike,
tuache tulie. Huu ni ugonjwa umeletwa na vijana na
utatumaliza sisi kina mama wenye mabinti. Ninajiona kwamba
nitakwenda pamoja na binti yangu‖ (uk. 37).
Maneno haya yanazidi kumuumiza Kazimoto, kwa sababu hapendi kuwaona Rukia
na mama yake wakiendelea kulia na kuumia kiasi hicho. Anashindwa kuvumilia na
kuamua kuondoka, huku akiwaacha wote wawili wanalia wakiwa wamekumbatiana.
Imebainika kuwa, akiwa katika maumivu na sononeko hilo, mama yake huyu
76
anaendeleza mgomo wa kula kwa madai kwamba atakula mara tu atakapojifungua
binti yake. Jambo hili linathibitishwa na mwandishi anaposema: Saa sita, chakula
kilipoletwa, tulisikia kwamba mama alikataa kula mpaka binti yake atakapojifungua
(uk. 76).
Kazimoto anazidi kuumia, kwani kitendo cha Rukia na mama yake kukataa kula
kinasababisha afya zao kuzorota na kudhoofu sana. Matokeo yake, Rukia anakosa
nguvu wakati wa kujifungua na kusababisha kifo chake. Mazungumzo baina ya Tuza
na Kazimoto yanathibitisha jambo hili kama ifuatavyo:
―Kazimoto,‖ Tuza alisema, ―ndugu yako amekufa kwa sababu
amekosa nguvu; alikuwa hajala vizuri kwa muda mrefu
uliopita.‖
―Hayo usemayo ni kweli,‖ nilimwambia.
―Amekufa akitaja jina lako,‖
―Alisema nini kuhusu jina langu?‖
―Alikulilia; akikuomba umsamehe kwa yale yote yaliyotokea
kwake. Amekuomba usisikitike sana. Hata yeye alikuwa haoni
tena maana ya kuishi.‖
―Ndiyo hayo aliyosema?‖
―Nimesahau jambo moja. Amesema kwamba, maadam yeye
akitoweka kama yalivyokwisha kutimia, anakutakia uhusiano
mzuri na Manase. Yeye amemsamehe ni zamu yako
kumsamehe‖ (uk. 83).
Matokeo yanaonesha kuwa, Kazimoto anapoipokea taarifa ya kifo cha dada yake,
anapata uchungu, majonzi, masikitiko na maumivu yasiyomithilika. Hii ni kwa
sababu mama yake pia, anakufa muda mfupi baada ya kifo cha Rukia. Kauli yake
aliyoisema mara tu, baada ya Rukia kupata mimba kwamba atakufa pamoja na binti
yake, kutokana na ugonjwa ulioletwa na vijana, kuwaua akina mama wenye mabinti,
inatimia. Kifo hiki kinatokea muda mfupi mara tu baada ya Kazimoto kupata taarifa
ya kifo cha Rukia, ambapo anaitwa na baba yake, Mzee Mafuru na kuambiwa
kwamba mama yake amezimia, huku akimwagiwa maji kichwani (uk. 82). Kifo cha
mama yake kinatokana na uchungu na maumivu makali anayoyapata anaposhuhudia
kaburi la mtoto wake. Mwandishi anaeleza namna kifo hicho kinavyotokea.
Anasema:
Wakati wa kuchimba kaburi, mama alikuwa ndani ya nyumba
akizungumza mambo ambayo yalikuwa hayaeleweki. Lakini
kaburi lilipokwisha, Tuza na Tegemea walimshika na
77
kumsaidia kutoka nje ili aone binti yake akizikwa. Alipofika tu
mlangoni na kuona shimo lililokuwa limechimbwa tayari
kumzika binti yake alilia kwa sauti ya juu sana. ―Rukia!
Rukiaa!‖ hali akionyesha kwa mkono wake kaburini. Halafu
alianza kulia kwa namna ya pekee. ―Kichwa! Kichwa!‖
alitotoma na kuanguka chini. Wakati alipobebwa kupelekwa
kitandani alikuwa amekwisha kufa (uk. 85).
Katika dondoo hili tunabaini hisia za huzuni, masikitiko na majonzi yanayoibuliwa
na kuikumba familia ya mzee Mafuru. Maumivu na masikitiko ya mama yake
Kazimoto kutokana na kifo cha Rukia, yanamsonga na kusababisha kifo chake.
Tukio hili linasababisha Kazimoto kusongwa sana na mawazo na kutamka maneno
ya masikitiko na ya kuhuzunisha yanayoonesha wazi kwamba tukio hili ni mojawapo
ya matukio ya mchakato wa kujiua kwake. Tunaelezwa kuwa:
Huo ndio ulikuwa mwisho wa mama yangu. Nilikuwa siwezi
kumwona tena maishani. Nilikuwa siwezi kusikia tena sauti
yake. Mola alimnyima ile furaha kubwa wapatayo kina mama
wakati mtoto wao anapooa. Huo ndio ulikuwa mwisho wa
mama aliyempenda binti yake wa pekee kama pumzi na
mwanadamu. Alikuwa amenyang‘anywa pumzi yake.
Niliyakumbuka tena maneno yake, ―Kazimoto, tuache
tupumzike, tuache tulie. Huu ni ugonjwa umeletwa na vijana,
na utatumaliza sisi kina mama wenye mabinti. Ninajiona
nitakwenda na binti yangu‖ (uk. 85).
Ni kweli kwamba kauli ya mama yake inatimia, kwani anakwenda pamoja na binti
yake. Utafiti umebaini kwamba vifo hivi vinatokea kutokana na wahusika hao
kuyaona maisha kuwa hayana maana, kama inavyoelezwa katika nadharia ya
Udhanaishi. Kitendo cha kukataa kula muda wote ni uthibitisho kwamba, kwao
maisha hayakuwa na maana na walikuwa tayari kufa muda wowote. Hili
linathibitishwa na kauli ya Rukia aliyomwambia Tuza kabla ya kufa kwake kwamba,
―… Hata yeye alikuwa haoni tena maana ya kuishi…‖ (uk. 83).
Matokeo yanaonesha kuwa tafiti mbalimbali, ikiwamo ile ya Kubller-Rose (1991)
zinabainisha kuwa, kufikiri na kupenda kuongelea masuala ya kifo na kujiua ni dalili
mojawapo ya mtu kujiua. Hili linajitokeza kwa Kazimoto, ambaye, baada ya kifo cha
Rukia na kile cha mama yake, anatumia muda wake mwingi kuwaza juu ya tukio
hili. Huu ni mchakato wa kujiua, kwani hata katika ujumbe anaouacha kuhusu kujiua
kwake, anaongelea kuhusu suala la kifo. Mwandishi anaeleza kuwa, baada ya vifo
78
vya ndugu zake hao, Kazimoto alianza kufikiri jinsi kifo chake kitakavyokuwa.
Anasema:
―Usiku nilianza kufikiri juu ya kifo. Nilifikiri jinsi kifo changu
kitakavyonijia – kwa ugonjwa, kwa ajali au kwa
kukatwakatwa na wezi? Labda kwa uzee au kwa sumu!
Huenda nikajiua mwenyewe! Nilikumbuka ndoto ya Kalia.
Niliwakumbuka wale ng‘ombe, sisimizi, nyuki, na mengine
mengi niliyoyaona huko machungani. Niliona kwamba adhabu
kubwa ya mwanadamu ni maisha yenyewe. Nilimkumbuka
mlevi mmoja niliyemkuta akipiga mti mweleka mpaka
akaumia mwenyewe. Maisha ndiyo yaliyokuwa yakimsumbua,
wala siyo pombe. Wakati huo usiku niliyaona maisha chanzo
cha yote.‖ (uk. 84).
Dondoo hili linamwonesha Kazimoto akiwa katika kina cha tafakuri kuhusu kifo na
namna kitakavyomjia. Nadharia ya Udhanaishi inafafanua kuwa maisha ya mtu ni ya
kitanzia na hayana maana, kwani mwisho wa mwanadamu ni kifo. Pia, inamwona
binadamu kama kiumbe anayeteseka na anayeishi katika ulimwengu usiomjali;
aliyezungukwa na mateso na ubwege na anayeshindwa kukabiliana au kupatana
vyema na uhalisi huo. Haya ndiyo yanayoonekana kumsumbua sana Kazimoto
kutokana na matatizo mengi anayokabiliana nayo. Katika tafakuri yake, anaona kuwa
binadamu amepewa adhabu ya kuyatunza maisha yake. Hata hivyo, anaeleza kuwa
maisha yenyewe siyo rahisi, kwani ni adhabu kubwa kuyatunza kwa sababu huwa
hayashibishwi wala kuridhishwa. Zaidi ya hayo, huyo aliyetoa adhabu ya kuyatunza
maisha hayo, huyachukua wakati wowote aupendao.
Hatimaye, matokeo yanaonesha kuwa, baada ya Kazimoto kufikiri kuhusu kifo kwa
muda mrefu, anaamua kutamka waziwazi kuwa mwisho wa mwanadamu utaletwa na
mwanadamu mwenyewe. Hii inaonesha kuwa tukio la vifo vya Rukia pamoja na
mama yake, pia ni mojawapo ya matukio yanayomsukuma katika mchakato wa
kujiua kwake.
4.2.2.4 Kifo cha Kalia
Tukio la kuuawa kwa Kalia, ambaye ni mdogo wake Kazimoto, nalo linachangia
kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa kujiua kwa Kazimoto. Hii inatokana na
ukweli kwamba mambo mengi anayoyafanya yanamwathiri Kalia na kusababisha
tabia yake kubadilika. Miongoni mwa mambo hayo ni kumtuma mara kwa mara
79
kwenda kumwitia wasichana wake, na wakati mwingine kufanya vitendo vya ufuska
mbele yake. Kalia anapochoshwa na mwenendo wa Kazimoto, anaamua kukengeuka
na kumtamkia waziwazi kwamba naye anahitaji kuwa na mwanamke (uk. 73).
Mabadiliko ya tabia na mwenendo wake, yanamsababishia Kazimoto msongo wa
mawazo unaomwingiza katika mchakato wa kujiua kwake. Hii ni baada ya Kalia
kuuawa na wananchi kutokana na tabia yake ya umalaya iliyochangiwa kwa kiasi
kikubwa na mwenendo mbaya aliouiga kutoka kwa Kazimoto.
Matokeo yanaonesha kuwa tukio la kwanza linaloonesha mabadiliko ya tabia ya
Kalia linashuhudiwa na Kazimoto mwenyewe, ambapo Kalia anaamua kumtoroka
Kazimoto na kutaka kumbaka msichana mdogo, akiwa machungani. Hata hivyo,
msichana huyo anaokolewa na Kazimoto kabla ya kufanyiwa kitendo kibaya na
Kalia kama inavyobainishwa katika dondoo hili:
… alikuwa amekwishavutwa mpaka majanini. Niliona tu
majani yakitingishika. Niliweka kitabu changu mkononi halafu
nilishuka. Nilikimbia mara moja kwenda kumwokoa huyu
msichana, wakati huu nikihisi kwamba alikuwa ameshikwa na
chatu. Nilipofika pale mahali sikujua la kufanya. Msichana
alikuwa amelala kifudifudi akilia. Macho ya Kalia
yalipokutana na yangu aliona kwamba tendo alilofanya
halikunifurahisha (uk. 80).
Dondoo hili linaonesha namna Kazimoto alivyochukizwa na kusononeshwa sana na
tukio hili la Kalia, la kutaka kumbaka msichana huyo. Hili linasababisha Kazimoto
asikitike na kujilaumu kwamba kwa kuwa yeye ndiye chanzo cha mabadiliko ya
tabia ya Kalia, basi anastahili kuwajibika kwa hilo. Majibizano baina yake na Kalia
ni uthibitisho kwamba kuharibika kwa tabia ya Kalia, kunatokana na matendo maovu
aliyoyaiga kutoka kwa Kazimoto:
―Kalia, kwa nini umefanya hivi?‖ Nilimuuliza. Alinyamaza.
―Umefanya, umefurahi, lete mkono nikupe heko,‖
nilimwambia.
Alicheka kidogo wakati nikimsogelea. Nilipomsogelea
nilimpa vibao viwili vitatu akaanguka chini.
―Mbona wewe huwa unafanya. Mimi sijasema lolote hata kwa
baba. Leo mimi nafanya unanipiga. Kwa nini? Unanionea tu.
Unafikiri mimi mjinga kuwa natazama tu?‖ Alipomaliza
kusema hivi aliinuka kwenda nyumbani (uk. 80).
80
Katika dondoo hili, Kazimoto anashitakiwa na dhamiri yake anapobaini kuwa
mabadiliko ya tabia ya Kalia yanatokana na matendo yake maovu. Maneno ya Kalia
kwamba ―mbona wewe huwa unafanya‖, ndiyo yanayomzindua na kubaini kwamba,
kumbe yeye ndiye chanzo cha mkengeuko huo. Kalia anathibitisha ule usemi
usemao, mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu. Kazimoto anatoa kibanzi
katika jicho la Kalia wakati kwenye jicho lake kuna boriti. Hatimaye, anaanza kuona
ubaya na udhaifu wake wote ndani ya Kalia. Hii inamfanya aukumbuke msemo
usemao, mkuki humuua yule aliyeufua. Tabia na mwenendo wake mbaya ndio
unaomwingiza katika mchakato wa kujiua kwake kutokana na msongo wa mawazo
anaoupata. Hii ni baada ya kutambua kwamba, yeye ndiye sababu ya kifo cha Kalia.
Anasema:
Huu ndio ulikuwa mwisho wa nunda mla watu (Kalia).
Mwisho wake uliendelea kunisumbua moyoni; kifo chake
kilihusika sana na matendo yangu. Ilikuwa kama kwamba
mimi mwenyewe nilimuua mdogo wangu (uk. 114).
Dondoo hili linabainisha wazi mchakato wa kujiua kwa Kazimoto, kwani kifo cha
Kalia kinampa msongo wa mawazo na maumivu makali moyoni mwake. Maneno
haya ndiyo anayoyarudia katika ujumbe anaouandika kabla ya kujiua kwake.
Anatamka kuwa yeye ndiye aliyemuua mdogo wake, ingawa hakumgusa. Kazimoto
anayatamka maneno haya, mara tu baada ya Kabenga kuleta taarifa kwamba mwili
wa Kalia umekutwa ukielea majini. Baada ya taarifa hiyo, miji ya Mafuru na
Kabenga inaamua kwenda kuuchukua. Mwandishi anaeleza hivi:
Mji wetu na Kabenga tulikwenda kubeba maiti na kuleta
nyumbani. Kalia alikuwa amechomwa mikuki miwili, mmoja
tumboni, na mwingine kifuani. Ilikuwa kazi bure kueleza
polisi, baba hakutaka. Kila mtu kijijini alifikiri kifo
kilichompata kilikuwa cha haki na kwamba angeishi angeleta
maafa mengi zaidi (uk. 114).
Dondoo hili linaonesha tukio lingine gumu linalompata Kazimoto na kusababisha
ajielekezee lawama kwa kusababisha kifo cha mdogo wake. Ni kweli kwamba
hakumgusa kwa kumchoma mikuki hiyo, lakini ni wazi kwamba ndiye aliyemchoma
Kalia mikuki mingi zaidi ya hiyo miwili iliyokutwa mwilini mwake, kutokana na
tabia na mwenendo wake mbaya.
81
4.2.2.5 Kifo cha Mtoto Wake
Kufiwa na mtoto wake ni tukio lingine la mchakato wa kujiua kwa Kazimoto. Tukio
hili linatokea kwa sababu ya Sabina, ambaye ni mke wa Kazimoto kucheleweshwa
kupata huduma akiwa katika uchungu wa kujifungua, wakati huo daktari
akimhudumia mgonjwa mwingine. Mlolongo wa matukio yanayompata Kazimoto
unazidi kumpa msongo wa mawazo na kumchanganya kifikra. Mkanganyiko huo
anaupata mara tu baada ya kuwasili hospitalini, ambako anaelezwa na Yaya namna
mambo yalivyotokea:
―Poleni sana Kazimoto, mtoto wako amerudi. Hakuweza
kuishi. Wakati wa kujifungua ulipofika daktari alikuwa
akifanya upasuaji kwa mtu mwingine. Mke wako alipata shida
ya kuweza kupitisha kichwa cha mtoto ambacho kilikuwa
kikubwa kupita kiasi. Daktari alichelewa kufika. Alipokuja
mtoto alizaliwa lakini aliishi kwa muda wa saa moja tu.
Tulifanya tuliloweza ili kuokoa maisha yake, lakini kwa kuwa
hakuzaliwa ili apate kuishi, alirudi (uk. 179).
Dondoo hili linaonesha kuwa maelezo yanayotolewa na Yaya, yanamuumiza zaidi
Kazimoto, kwani yanamthibitishia na kuweka bayana kuhusu kifo cha mtoto wake
huyo. Maelezo hayo yanaonesha wazi kwamba licha ya mtoto huyo kuwa na kichwa
kikubwa, huenda angeweza kupona iwapo daktari angemhudumia mapema.
Maumivu yake yanazidi anapoingia katika chumba kimojawapo na kuwakuta Tuza
na Sabina wakiwa wanalia. Kilio chao kinazidi mara wanapomwona Kazimoto
anaingia. Kazimoto kupitia kwa mwandishi anaeleza:
―Nilikaa juu ya kitanda. Niliweka mkono wangu ndani ya
mkono wa mke wangu ambaye sasa alilia kwa kwikwi.
Sikuweza kusema neno lolote isipokuwa kusikitika kwa
unyamavu‖ (uk. 179).
Kitendo cha Kazimoto kukaa kimya bila kusema jambo lolote kinadhihirisha namna
alivyokuwa na maumivu ya ndani juu ya tukio hilo. Katika hali ya kawaida, ni vema
mtu kusema kitu kilichomo moyoni kuliko kukaa nacho, huku akiumia ndani kwa
ndani. Hili ndilo linalompata Kazimoto, kwani anaamua kukaa kimya. Zaidi ya hayo,
hata walimu wenzake alioongozana nao kwenda hospitalini, wanaporuhusiwa
kuingia ndani, nao wanaamua kukaa kimya. Kuhusu hili, mwandishi anasema:
82
―Waliingia. Wao pia walinyamaza baada ya kuyaona mambo
yalivyokuwa kwa macho yao wenyewe. Nani atamuuliza nani?
Na nani atasema nini? Chumba chote kilikuwa kimya
isipokuwa kwikwi za Tuza na mke wangu. Tulikesha
chumbani humo pamoja nao huzuni ilitawala chumba kizima‖
(uk. 179).
Dondoo hili linaonesha namna tukio hili linavyomchanganya Kazimoto, na hajui la
kufanya. Majonzi ya kufiwa na mtoto wake, yanamsukuma na kumzamisha katika
tafakuri ya kina kuhusu ukatili wa Mungu dhidi yake. Anaona kuwa mateso hayo
yote yangeweza kuepukwa iwapo Mungu angemwonea huruma. Anasema:
―Nilianza tena kufikiri juu ya Mungu. Kama kweli alikuwapo
kwa nini aliweza kufanya ukatili mkubwa kama huo.
Matumaini yetu yote; kazi na taabu tuliyopata – yote hayo
chini! Sikuona maana ya kuishi‖ (uk. 180).
Kinachobainika katika dondoo hili ni kwamba Kazimoto anatafakari kuhusu nafasi
ya Mungu katika mahangaiko yake. Kama inavyoeleza nadharia ya Udhanaishi,
anaonesha dalili za wazi za kukana nafasi na uwepo wa Mungu kwa madai kwamba
hamjali, ambapo hata ulimwengu wenyewe, nao pia hauko upande wake. Anaposema
kuwa haoni sababu ya kuishi ni dalili ya kukata tamaa. Hili ndilo analoandika pia
katika ujumbe anaouacha kabla ya kuamua kujiua kwake. Anasema kuwa anaamua
kujiua kwa kuwa haoni sababu ya kuendelea kuishi na kuzaa kizazi kibaya. Anakata
tamaa ya maisha kwa kuona kwamba hayana maana. Haya yanathibitishwa katika
majadiliano baina yake na Sabina kama ifuatavyo:
―Mimi nimekata tamaa,‖ nilimwambia mke wangu.
―Tamaa ya nini?‖ aliniuliza kwa sauti yenye masikitiko mengi.
―Ya kuishi – kupata watoto.‖
―Mimi nina matumaini bado. Mungu ni mkubwa; Anafahamu
kila kitu. Atatuwekea kitu kikubwa na kizuri zaidi.
Anatujaribu kwa mateso ili kuona utulivu wetu. Bwana‘ngu
inafaa tuvumilie. Tukubali na tupokee lolote lile
linaloporomoshwa na Mungu juu ya maisha yetu. Yeye ndiye
anafahamu mabaya na mazuri.‖
―Mimi siwezi kuishi tena,‖ nilimwambia.
―Kwa nini?‖
―Ulimwengu si pahala pa kuishi.‖
―Unataka kwenda kuishi wapi?‖
―Ninataka kwenda kuishi mahali ambapo ninaweza kuishi bila
kufikiri na bila kujua kwamba ninaishi‖ (uk. 180).
83
Majadiliano haya yanabainisha kwa uwazi namna Kazimoto na Sabina
wanavyotofautiana kimtazamo kuhusu Mungu na namna ya kuzikabili changamoto
zao. Wakati Kazimoto anaonesha kuwa maisha hayana maana na kuamini kwamba
ulimwenguni si mahali pazuri na salama pa kuishi, Sabina kwa upande wake bado
anaweka matumaini yake kwa Mungu. Kama inavyoelezwa katika nadharia ya
Udhanaishi, Kazimoto haamini kuhusu uwepo wa Mungu, anayedaiwa kwamba
ndiye muumba wa ulimwengu, ambao kimsingi kwa yeye anaona kuwa haumjali.
Matokeo yanaonesha kuwa kutofautiana kwao kimtazamo ndiko kunakozidi
kumsukuma Kazimoto katika mchakato wa kujiua anaposema ―mimi siwezi kuishi
tena.‖ Kauli hii inaonesha kwamba Kazimoto haoni tena thamani na maana ya
maisha yake. Kinachoonekana ni kwamba, kwa wakati huu yuko katika msongo wa
mawazo kutokana na tukio la kufiwa na mtoto wake. Kwa wakati huu, hapaswi
kuendelea kubishana na kuachwa peke yake, bali anahitaji kupata msaada wa karibu
kutoka kwa wataalamu wa saikolojia na magonjwa ya akili wa namna ya kulikubali
tukio hilo. Anapodai kwamba anataka kwenda mahali ambako hataweza hata kufikiri
na kujua kama anaishi, anaonesha kwamba yuko katika mchakato wa kujiua.
4.2.2.6 Kazimoto Kuugua Ugonjwa wa Ajabu
Tukio lingine la mchakato wa kujiua kwa Kazimoto ni la kuambukizwa ugonjwa wa
ajabu, baada ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na msichana anayeitwa Pili. Tabia
ya umalaya wa msichana huyu inasababisha Kazimoto kuambukizwa ugonjwa wa
huo wa ajabu, na hivyo, kuharibu kizazi chake. Kazimoto anapobaini kwamba tatizo
hili ndilo chanzo cha kifo cha mtoto wake, na kuzaliwa akiwa na kichwa kikubwa,
anakata tamaa ya maisha. Anapatwa na msongo wa mawazo unaomtesa sana na,
hatimaye, anaamua kujiua ili asiendelee kuzaa kizazi kibaya kama anavyoeleza
mwenyewe katika ujumbe anaouacha kabla ya tukio la kujiua kwake (uk. 195).
Ifahamike kwamba, Kazimoto na Pili wamekuwa katika mahusiano hayo kabla na
hata baada ya Kazimoto kufunga ndoa na Sabina. Hata hivyo, kwa muda wote huo,
Kazimoto hakujua kama ameambukizwa ugonjwa wa ajabu, hadi alipomwona mtoto
mwenye kichwa kikubwa katika familia ya Manase na Salima. Hatimaye, inabainika
kwamba familia hiyo pia, ina majonzi na masikitiko kutokana na kupata mtoto
mwenye kichwa kikubwa. Hii ni baada ya Manase kumwambukiza mke wake
ugonjwa huo wa ajabu alioupata kwa malaya, Pili. Jambo hili linampa msukumo
84
Kazimoto naye kumweleza Manase kinagaubaga kuwa, amekuwa katika mahusiano
ya kimapenzi na Pili, kabla na hata baada ya ndoa. Anaongeza kuwa, pamoja na yote
hayo, bado yeye na mke wake hawajisikii kuumwa chochote, kama ielezwavyo:
Manase alieleza kwamba ugonjwa huo ulikuwa hauwezi
kutambulika kwa urahisi. Alisema kwamba ugonjwa huo
unaingia ndani ya damu na kukaa bila kumdhuru mhusika.
Baada ya miaka kumi na minne hivi au zaidi unaanza
kumdhuru mhusika, lakini kabla yake ni vigumu kuusikia (uk.
192).
Maelezo haya yanasababisha Kazimoto kupata majonzi. Hii ni baada ya kuambiwa
kwamba ugonjwa huo huwa unaharibu kizazi kimoja hadi kingine. Pia, anakatishwa
tamaa zaidi anapoambiwa kuwa, daktari mwenye uwezo wa kutibu ugonjwa huo,
alifariki wiki moja tu iliyopita na hakuna mwingine wa kumsaidia. Yafuatayo ni
majadiliano baina ya Kazimoto na Manase:
―Daktari huyo alikupa dawa?‖ nilimuuliza.
―Ndiyo, alinipa.‖
―Ninaweza kumwona hata mimi?‖
―Bahati mbaya sana, Kazimoto, huyo daktari alikufa juma
lililopita, na watu waliopelekwa kusafisha nyumba yake ili
mwingine aingie walichoma vidonge vyote hivyo bila
kufahamu. Sasa hapatikani tena daktari ye yote.‖
―Wewe mwenyewe hukubakiza vidonge fulani?‖
―Bahati mbaya sana, Kazimoto, vyote vimekwisha.‖
Tulinyamaza kwa muda.
"Kazimoto,‖ Manase aliniita.
―Manase,‖ nilimwitikia.
―Maisha yangu yamekuwa magumu sana. Siwezi kutoka nje
ya nyumba hii isipokuwa wakati wa kazi. Nilikuwa nataka
kununua gari jipya lakini mke wangu amenizuia. Amesema
hataki kuona gari la kuchukulia malaya nyumbani kwake. Gari
lililolala hapo nje halikuharibika lenyewe. Lilichomwa na mke
wangu.‖
―Mimi maisha yangu yamekuwa magumu zaidi; dawa…
dawa,‖ nilimwambia (kur. 192 - 193).
Kinachobainika katika majadiliano haya ni kwamba wote wawili, Manase na
Kazimoto, wako katika msongo wa mawazo, kutokana na tukio hilo la
kuambukizwa ugonjwa wa ajabu. Tatizo hili linazidi kumweka Kazimoto katika
mchakato wa kujiua, kwani licha ya kusababisha mtoto wake kufa, hata huyo daktari
wa kumtibu anakosekana. Mtazamo wa Manase kuhusu kizazi chao kijacho kwamba
85
ni cha watoto wenye vichwa vikubwa, unazidi kumkatisha tamaa Kazimoto. Kwa
mantiki hiyo, haoni tena sababu ya kuendelea kuishi. Majadiliano yao ni kama
ifuatavyo:
―Unafikiri nini juu ya kizazi kijacho?‖ nilimuuliza.
Manase aliinama. Alifikiri. Halafu aliinua kichwa chake.
―Sijui,‖ alisema, ―lakini naona watoto wetu wanakuja na
vichwa vikubwa. Sijui kunaweza kuwa na nini ndani ya
vichwa hivyo.‖ Manase alitingisha kichwa chake kwa huzuni.
―Hata mimi naogopa,‖ nilisema.
Tulinyamaza kwa muda kila mmoja kati yetu akitazama
sakafuni.
―Kazimoto,‖ aliniita.
―Manase,‖ nilimwitikia.
―Kamwone mke wako, nami nikamwone wangu. Ulimwengu
unaozea mikononi mwetu. Mikono yangu naiona michafu‖
(uk. 193).
Mazungumzo haya yanaonesha kwamba Kazimoto hayuko tayari kuendelea kupata
aibu kwa kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa. Dalili za kujitenga na ulimwengu
zinajitokeza anapomwambia Manase kwamba kila mmoja aende akamwone mke
wake. Ujumbe tunaoupata hapa ni kwamba Kazimoto anataka kila mmoja awe tayari
kuibeba aibu inayomkabili, inayotokana na tabia yake ya umalaya na kuambukiza
vizazi vyao ugonjwa wa ajabu. Tukio hili linamzamisha katika fikra kuhusu maana
ya maisha. Kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi, anakata tamaa kwa
kukengeuka misingi ya jamii na kujitenga. Haya yanamwingiza katika mchakato wa
kujiua kwake kwa kuona kwamba ulimwengu unamwozea katika mikono yake
michafu kutokana na uovu wake.
4.2.2.7 Kujitenga Kijamii
Kujitenga kijamii ni hali nyingine ya mchakato wa kujiua kwa Kazimoto. Jambo hili
linaanza kujitokeza akiwa nyumbani kwa Manase. Hii ni baada ya kubaini kwamba
tabia yake ya umalaya ya kutembea na wasichana wengi akiwamo Pili, ndicho
chanzo cha kifo cha mtoto wake. Kujitenga huko kunamwingiza zaidi katika
mchakato wa kujiua kwa sababu anaanza kuishi maisha ya upweke, tofauti na maisha
yake ya kawaida aliyoyazoea. Hivyo, anaamua kukaa kimya na kujitenga na Sabina
muda wote wakiwa safarini. Tabia hii inaendelea hadi wanapofika nyumbani kwao.
Mambo haya yanathibitishwa kupitia kwa Kazimoto mwenyewe, anaposema:
86
Njiani sikuzungumza na Sabina maneno mengi. Kila mmoja
alikuwa akiwaza yake. Tulipofika shuleni tuliomba ufunguo
wa nyumba yetu kutoka kwa mwalimu aliyekuwa akitutunzia
nyumba. Tulifungua na kuingia ndani kimya kama kwamba
tulikuwa tukiingia kaburini. Nyumba ilionekana kuwa tofauti
kabisa. Tulipoingia ndani tulikaa juu ya kochi, kupumzika
kidogo. Tulikaa kimya. Tukawa tunaogopa kutazamana (uk.
194).
Utafiti umebaini kuwa, kujitenga kwa Kazimoto kunamweka katika mchakato wa
kujiua kwa sababu ya kusongwa na mawazo mengi, ambayo hana namna ya
kuyatatua. Mjadala anaouanzisha baina yake na Sabina baada ya kimya cha muda
mrefu, ndio unaoonesha kwamba kujitenga huko kunamsukuma katika mchakato wa
kujiua kwake kutokana na kukata tamaa ya maisha. Hali hiyo kama inavyofafanuliwa
katika nadharia ya Udhanaishi, ndiyo inayosababisha akengeuke misingi ya jamii
yake kwani anazama katika fikra nzito juu ya dhana ya maisha. Majadiliano
yafuatayo yanathibitisha jambo hili:
―Mke wangu,‖ nilimwita.
―Bwanangu,‖ aliitikia.
―Sijui kwa nini ninaishi.‖
―Nimechoka na maswali yako ya kijinga,‖ alisema.
―Huwezi kuishi kama watu wengine?‖ Wewe nani?‖
―Mimi sijijui,‖ nilimwambia.
―Hakika sikufahamu kwamba wewe ni kichwamaji namna hii!
Sikufahamu! (kur. 194 - 195).
Dondoo hili linaonesha dhahiri kwamba Kazimoto yuko katika mgongano wa
mawazo, ambapo haoni sababu ya kuendelea kuishi. Hata hivyo, kutokana na
kukosekana kwa elimu ya saikolojia, imebainika kuwa mtu anayemweleza matatizo
yake haelewi na hamsaidii, bali anamwita Kichwamaji, yaani mtu asiyekuwa na akili
au kichwa wazi, huku akiendelea kulia hadi macho yake kuwa mekundu na kuamua
kwenda kulala. Matokeo yake ni kwamba kitendo cha kumwacha Kazimoto peke
yake, kinamwongezea upweke na mwanya wa kuendelea kufikiria kuhusu maisha na
kuzidi kujitenga nayo. Kazimoto mwenyewe anasema:
―Nilisimama pale dirishani kwa muda mrefu nikifikiri.
Nilifikiri furaha; ilikuwa imetawaliwa sana na huzuni. Salima
ambaye siku moja alitwambia kwamba kwa jambo lile alikuwa
haoni tofauti yetu na ng‘ombe, yeye mwenyewe hana raha
sasa. Wakati nilipokuwa nikifikiri juu ya maisha nilisikia kitu
fulani kama sauti ikiniita‖ ―Kazimoto!‖ Sauti ilisikika
87
polepole. ―Naam,‖ nilijibu kimoyomoyo. Nilikwenda ndani ya
chumba cha kulala. Sabina alikuwa amejifunika shuka akilia
kwa kwikwi. Nilichukua kitu fulani. Nilikuwa sifahamu jambo
nililokuwa ninafanya, isipokuwa nguvu fulani zilikuwa
zikiniongoza – sauti! Sauti! (uk. 195).
Kinachobainishwa katika tasinifu hii ni kwamba mtu anayepanga kujiua huwa katika
hali ya mtanziko. Husikia sauti ikimwita na kumhimiza kutekeleza kitendo cha
kujiua na kwamba kama atachelewa, basi watu wengine watakuja na kumuua kabla
ya yeye mwenyewe kufanya hivyo. Sauti ya namna ndiyo inayomsukuma Kazimoto
kuingia katika mchakato wa kujiua kwake, kwani anaingia ndani na kuchukua silaha
pasipo kutambua tendo analokusudia kulifanya.
Wakati mchakato huu ukiendelea, Sabina akiwa amelala huku akilia kwa uchungu
kutokana na kauli ya mume wake kwamba haoni sababu ya kuendelea kuishi,
Kazimoto anaamua kuutumia mwanya huo kujiua kwa kujipiga risasi. Matokeo yake
ni kwamba Sabina anakuwa mtu wa kwanza kushuhudia kichwa cha mumewe
kikivuja damu, huku bastola ikiwa pembeni. Kikaratasi kidogo anachokiona juu ya
meza kinabainisha sababu ya kujiua kwake. Kilikuwa na ujumbe ufuatao:
Nimejiua. Siwezi kuendelea kuzaa kizazi kibaya. Pia sikuona
tofauti kati yangu na mdudu au mnyama. Akili! Akili! Akili ni
nini? Pia nikiwa duniani sikupata kukutana hata siku moja na
mtu anayeamini kwamba kuna Mungu. Watu wanaoogopa
kufa na kwenda motoni hao nimewaona, tena wengi sana. Mtu
ye yote asilaumiwe kwa kifo changu. Mimi, kabla ya kufa,
ninaungama mbele ya ulimwengu kwamba nilimwua mdogo
wangu ingawa sikumgusa (uk. 195).
Ujumbe huu ni uthibitisho tosha kwamba mara nyingi kujiua hakutokei ghafla, bali
ni mchakato ambao humtokea mhusika baada ya kukabiliwa na matukio mengi
maishani mwake. Mwandishi kupitia kwa mhusika wake Manase, anathibitisha suala
hili anaposema:
Ukweli ni kwamba sisi wanadamu tunakufa polepole. Watu
wengi wanafikiri kwamba kifo kinakuja mara moja. Hili ni
jambo la uongo. Tangu mwanadamu anapozaliwa anaanza
kufa polepole ingawa yeye anajiona yu sawa. Siku zake
zinakatwa moja moja. Kaburi ni hatua yetu ya mwisho.
Kazimoto, tunapoishi tunakufa polepole. Kwa hiyo, ―kufa ni
kuishi.‖ (uk. 186).
88
Kwa mujibu wa Kezilahabi, kufa na kuishi ni hali zinazoingiliana, kwani aliye hai
huenda pia amekufa. Kauli hii inalenga kuthibitisha kwamba kujiua siyo tukio la
ghafla, bali ni mchakato. Hii ni kwa sababu mtu anayepanga kujiua hudhamiria na
hufanya maandalizi kadhaa kabla ya kufikia uamuzi huo. Hata hivyo, kwa kuwa
mchakato huo hufanywa na mhusika mwenyewe kimya kimya, mara nyingi jamii
isikiapo kuwa mtu fulani amejiua, hulipokea suala hilo kwa mshtuko na huliona
kama ni tukio la ghafla. Hili linathibitishwa na mwandishi wa riwaya hii anaposema
kuwa ―Wengi waliosikia juu ya kifo cha Kazimoto walistuka sana‖ (uk. 195).
Matokeo yanaonesha kuwa, kujiua kwa Kazimoto kunatokana na kukata tamaa ya
maisha na kutotambua nafasi ya Mungu kama inavyoelezwa katika msingi wa pili wa
nadharia ya Udhanaishi. Anaondoka na msimamo walio nao wadhanaishi wanaokana
kuhusu uwapo wa Mungu kwa madai kwamba woga ndio unaowasukuma watu
kuamini kuhusu Mungu. Aidha, anaeleza kuwa hajaona watu wakiwa na imani ya
kweli kuhusu Mungu, bali waoga ndio wengi kwa sababu huogopa adhabu ya moto.
Utafiti huu, basi, umebaini kwamba kujiua kwa Kazimoto kunatokana na mchakato
wa matukio mbalimbali anayoyapitia katika maisha yake. Matukio hayo ndiyo
yanayompa msongo wa mawazo na kusababisha akate tamaa kwa kuona kwamba
maisha kwake hayana maana tena. Hatimaye, anaamua kujiua kama suluhisho la
matatizo na taabu nyingi alizozipitia katika maisha yake.
4.2.3 Muhtasari wa Riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo
Dunia Uwanja wa Fujo (1975) ni riwaya ya tatu ya Euphrase Kezilahabi katika
mfululizo wa kazi zake. Ilichapishwa mwaka 1975. Riwaya hii pia, imetumika katika
utafiti huu kwa kumpatia mtafiti data za msingi. Kwa kiasi fulani, inaendeleza
mjadala kuhusu tatizo la maisha ya binadamu, maana yake, pamoja na kusudi lake,
mjadala unaoanza katika Kichwamaji (Mbatiah, 1998). Mulokozi (1983) anafafanua
kuwa katika riwaya hii mwandishi analitazama tatizo la maisha kwa viwango viwili.
Mosi, kwa kiwango cha jamii. Katika kiwango hiki, anashughulikia tatizo la maisha
katika ngazi tatu, yaani, ngazi ya familia, ngazi ya kijiji na ngazi ya taifa. Pili, kwa
kiwango cha mtu binafsi. Hapa anabainisha kuwa mara nyingi kanuni na miiko ya
jamii huweza kumfunga mtu binafsi na hata kuingilia uhuru na matamanio yake.
89
Riwaya hii, kwa kiasi kikubwa, inasimulia na kueleza kuhusu maisha ya mhusika
mkuu, Tumaini, tangu akiwa mtoto hadi kuuawa kwake. Mulokozi (k.h.j) anadokeza
kuwa matendo na tabia ya Tumaini inatokana na sababu kuu tatu. Mosi, malezi
mabaya. Huyu ni mtoto pekee katika familia ya Kapinga na Muyango, anayelelewa
kwa kudekezwa na kuengwaengwa. Pili, urithi mkubwa wa shilingi elfu hamsini
anaoachiwa na wazazi wake. Hela hiyo anaitumia kwa anasa na uasherati. Tatu, aibu
inayotokana na wazazi wake kugeuzwa vizuu kutokana na uchawi wa Mugala. Kama
ilivyo kwa riwaya nyingine zilizotangulia, mhusika mkuu, Tumaini, amejengwa na
wahusika wengine wanaosaidia kusogeza mbele dhamira za mwandishi katika
kufanikisha maudhui yake. Riwaya hii inabainisha kuwa maisha ya mwanadamu ni
vurumai inayotokana na mwanadamu huyo kuitafuta furaha maishani mwake.
Vurumai hizi, kwa kifupi, huletwa ulimwenguni na watu fulani, ambao, hujitokeza
katika nyakati mbalimbali za historia ya maisha ya binadamu huyo.
Aidha, imebainika kuwa katika riwaya hii mwandishi anaishughulikia na kuibua
migogoro, matatizo, pamoja na mikinzano mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na hata
ya kifalsafa katika jamii ya Tanzania, hususani, baada ya kutangazwa kwa Azimio la
Arusha. Pia, anaisawiria taswira ya maisha ya mwanadamu kama kiumbe kilicho
dhaifu na kisichoweza kuudhibiti ulimwengu wake, kuufanya ukitumikie na
kumletea furaha katika maisha yake. Matokeo yanaonesha kuwa jitihada za Tumaini
kuisaka furaha hiyo zinashindikana kutokana na kuandamwa na matukio na
mitanziko kadha wa kadha kuhusu mali na mashamba yake, ambayo sasa yanatakiwa
kutaifishwa. Kitendo hicho kinamkatisha tamaa. Hivyo, anaamua kumuua Mkuu wa
Wilaya akiwa mkutanoni akiwahutubia wananchi. Hata hivyo, nguvu ya dola
inafanikiwa kumtia Tumaini hatiani. Hatimaye, naye anauawa kwa kunyongwa
kutokana na kosa hilo la mauaji. Yafuatayo ni matukio ya mchakato wa kujiua
yanayosawiriwa katika riwaya hii: matukio ya aibu na fedheha, na tukio la Tumaini
kumuua Mkuu wa Wilaya.
4.2.3.1 Matukio ya Aibu na Fedheha
Matokeo yanaonesha kuwa, chanzo kimojawapo cha mchakato wa kujiua ni matukio
ya aibu na fedheha yanayompata mhusika au jamii yake. Mhusika au watu wake wa
karibu huamua kujiua ili kukwepa aibu, dharau na fedheha kutokana na kushindwa
kufanya au kutimiza jambo binafsi au la kijamii. Katika riwaya hii, tukio mojawapo
90
la aibu na fedheha linamhusu Kapinga. Hili linasababishwa na kitendo chake cha
kukosa nguvu za kufanya tendo la ndoa kwa takribani siku tatu, mara tu baada ya
kufunga harusi yake. Aibu na fedheha hii haimpati yeye peke yake, bali inawapata
pia, wazazi wake. Tukio hili linasababisha mama yake mzazi kushindwa kuvumilia
aibu hiyo kwa sababu ya umati mkubwa wa watu kumzomea, huku Kapinga
akiendelea kuhangaika ndani. Ili kuikwepa aibu hii, mama yake anaamua kuchukua
uamuzi wa kutaka kujiua, lakini anashikwa na kuokolewa. Mwandishi anasema:
―… Kapinga alikata tamaa. Alitoka nje kwenda kumwambia
kaka yake kwamba alishindwa. Rudi tena! Kaka yake
alimsukumia ndani ya nyumba kwa ghadhabu. Kapinga alirudi
ndani. Alijaribu tena lakini hakuweza. Usiku huo ngoma
hazikuchezwa, kwani arusi ilikuwa bado kuthibitishwa kwa
kitendo.‖ Kesho yake watu walikuwa wakiwazomea wazazi
wake. ―Mama yake nusura ajiue kama asingalishikwa‖ (uk.
10).
Kinachobainika katika dondoo hili ni kwamba tukio la kutaka kujiua kwa mama yake
Kapinga, halitokei ghafla, bali ni mchakato unaomtokea baada ya kuvumilia kwa
muda mrefu. Kutokana na hilo, anaamua kukata tamaa baada ya kubaini kwamba
Kapinga mwenyewe amekata tamaa na kukiri kwamba jambo hilo ni gumu kwake na
hawezi kufanikiwa. Hata jitihada zinazofanywa na bibi arusi za kuvunja sheria za
jamii yake ili kumsaidia Kapinga kwa kuhofia suala la usalama wa ndoa yake,
zinashindikana. Mwandishi anaeleza kwamba:
Alijitahidi kumsaidia bwana wake. Akiwa amevaa shanga
nyingi sana kiunoni, alimchomachoma Kapinga kwa matiti
kifuani; alimtekenya tumboni, mgongoni na kisogoni lakini
Kapinga alikuwa baridi, alikuwa akiguna tu. Bibi arusi
alitokwa na machozi. ―Kapinga! Kapinga kweli nirudi kwetu!‖
Alilia. Kapinga ingawa jasho lilikuwa limemtoka, alishindwa.
Alinyang‘anywa mwanamke. Kesho yake bibi arusi alirudi
kwao. Kapinga aliaibisha kijiji kizima (uk. 10).
Dondoo hili linaonesha kwamba kukatishwa tamaa huko hakutokei kwa Kapinga na
ndugu zake peke yao, bali hata mke wake anakumbwa na jambo hili. Ama kweli
sikio la kufa halisikii dawa, na kisicho riziki hakiliki, kwani licha ya mwanamke
huyo kumpa vionjo na manjonjo yote, Kapinga anashindwa kutimiza jukumu lake.
Hivyo, mama yake naye anaamua kukata tamaa kwa kutaka kujiua ili kuikwepa aibu
91
na fedheha hiyo. Furaha ya kumpokea mwali wake inapotea, kwani kabla ya kufikia
maamuzi ya kutaka kujiua inaelezwa hivi:
―… siku ambayo Kapinga alimleta bibi arusi nyumbani kwa
shangwe kubwa, vijana na wageni wengi walikuwapo. Kimila,
usiku ulipowadia, Kapinga aliambiwa kuingia ndani ya
nyumba baada ya bibi arusi kuoshwa vizuri na kupakwa
mafuta. Kapinga alipofika kitandani alimkuta bibi – arusi
tayari kwa ajili yake – amejifunika kanga moja (kur. 9 - 10).
Tunachokibaini ni kwamba ujio wa bibi arusi huyu unampa furaha ya muda mfupi
mama yake Kapinga, lakini furaha hiyo inageuka na kuwa majonzi na masikitiko
kutokana na Kapinga kushindwa kufanya tendo la ndoa. Jamii yake inapomcheka na
kumzomea, inachochea na kumpa msukumo mama yake kukata tamaa na kutaka
kujiua kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi. Kwa msingi huo, matukio
ya aibu na fedheha ni chanzo kimojawapo cha mchakato wa kujiua kama
inavyotokea kwa mama yake Kapinga.
Tukio lingine la aibu na fedheha ni la mwanasiasa kumwaibisha na kumvunjia
heshima Tumaini mbele za watu mkutanoni. Katika hali ya kawaida, kila mtu
anastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake. Tukio la kumsema vibaya
Tumaini hadharani linalofanywa na mwanasiasa huyo, linamkasirisha sana Tumaini
na linamjengea chuki inayomsukuma na kumchochea kuingia katika mchakato wa
kujiua. Mwanasiasa huyo, kupitia kalamu ya mwandishi, anasema:
―… lakini wanyonyaji wapo. Kwa mfano, mnamwona huyu!
Ebu simama Bwana watu wakuone!‖ Tumaini alisimama na
watu walimzomea. Mwanasiasa aliendelea, ―haya ndiyo
manyonyaji haya!‖ Watu walimcheka na kumzomea. Tumaini
alikaa (uk. 117).
Kitendo cha kudhalilishwa na kuitwa mnyonyaji, siyo tu kwamba kinasababisha
Tumaini kuchekwa na kuzomewa na watu, bali pia kinamvunjia heshima, utu na
thamani yake katika jamii. Ifahamike kwamba utajiri wake haukutokana na
kuwanyonya watu kama anavyodai mwanasiasa huyo, bali unatokana na jitihada
zake za kufanya kazi kwa bidii baada ya kuanzisha mashamba makubwa. Kutokana
na kudhalilishwa huko, Tumaini haoni tena faida ya kuendelea kupambana na
kufanya kazi kwa bidii, badala yake anakata tamaa kwa kusongwa na mawazo
mengi. Mwandishi anasema:
92
Tumaini aliporudi nyumbani kichwa kilikuwa kikimwanga
kwa sababu ya mambo yaliyotokea kwake mkutanoni.
Tumaini alijiona mtu mkubwa; na maneno ya mwanasiasa
kuhusu kitambi chake yalimuudhi sana. Aliona udhia sana
kuambiwa maneno kama hayo mbele ya wafanyakazi wake wa
shambani na mbele ya watu waliokuwa wakimheshimu na
kumwita mzee. Hakuona kwa nini mwanasiasa yule
alimchagua yeye tu kati ya watu wote wenye vitambi
waliokuwako mkutanoni (uk. 119).
Mwandishi anaeleza namna Tumaini alivyosongwa na mawazo mara tu baada ya
kurudi nyumbani kwake, akitokea mkutanoni. Kitendo cha kudhalilishwa mbele ya
wafanyakazi wake pamoja na watu wengine mkutanoni, kinamfanya akate tamaa ya
maisha. Mchakato wa kujiua kwake unaongezeka akiwa chumbani kwake, kwani
anakosa usingizi na kubaki akizungukazunguka, huku mawazo yakimzunguka
kichwani mwake. Tumaini, kupitia kalamu ya wandishi, anasema:
―Siwezi kutukanwa na mwanasiasa anayetegemea kura yangu!
Haiwezekani! Kuniambia mimi, ―Mnaliona hilo; haya ndiyo
manyonyaji haya!‖ Mimi Tumaini! Mimi sikumkataza
kunenepa! Na hata hivyo ninakula jasho langu. Tabu
niliyopata zamani imenifunza jinsi ya kutafuta pesa. Nilikata
shauri kufanya kazi; nikawa nashinda shambani asubuhi na
jioni. Na sasa nimepata mali. Halafu huyu mwanasiasa
ananiita mnyonyaji! Mali niliyoisumbukia mwenyewe wakati
watu wengine wanashinda kwenye kangara! Haiwezekani!
Potelea mbali vijiji vyao vya ujamaa ambavyo vimerudisha
nyuma maendeleo ya watu wengi. Haiwezekani!‖ (uk. 120).
Kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi, Tumaini anakosa furaha na
anakata tamaa ya maisha kwa kuyaona kuwa hayana maana yoyote. Ithibati ya hali
hiyo ni kauli yake kwamba: ―Haiwezekani! Potelea mbali vijiji vyao vya ujamaa,
ambavyo vimerudisha nyuma maendeleo ya watu wengi. Haiwezekani!‖ Kauli hiyo
inaonesha kuna kitu anakusudia kufanya kutokana na msongo wa mawazo alio nao.
Kitu hicho, kwa muktadha wa tasinifu yetu, ni mchakato wa kujiua kwake au
kuhatarisha maisha ya huyo aliyemtia aibu na fedheha.
4.2.3.2 Tukio la Tumaini Kumuua Mkuu wa Wilaya
Tukio lingine la mchakato wa kujiua linatokana na kitendo cha Tumaini kumuua
Mkuu wa Wilaya. Tukio hilo nalo halitokei ghafla, bali linaambatana na matukio
kadhaa anayoyapitia Tumaini, yanayomkatisha tamaa na kumsababishia msongo wa
93
mawazo. Tukio hili linatokea mara tu baada ya kupokea barua kutoka kwa Mkuu wa
Wilaya, ikidai kwamba Serikali imetaifisha mashamba yake yote ili kujenga kijiji
cha Ujamaa. Jambo hili linamuumiza na kumkatisha tamaa. Mazungumzo baina yake
na mke wake, mama Bahati, ni uthibitisho wa jambo hili:
―Mama Bahati, hawa wanasiasa wanajua sasa kuwatania
wenzao. Eti wananiambia nijiunge nao! Eti baada ya kuchukua
mashamba yangu nijiunge nao! Siyo utani huo kitu gani?‖ …
mimi naona afadhali tuonyeshane nao. Watashinda. Lakini
nitakuwa nimewafunza somo.
―Somo gani?‖ Aliuliza mama Bahati.
―Kwamba Ujamaa ni ndoto!‖ Alijibu Tumaini kwa haraka na
kwa msisitizo (kur. 126 - 127).
Hapa dalili za wazi za mchakato wa kujiua kwa Tumaini zinajidhihirisha. Ukweli
wake ni kwamba anapanga kupambana na nguvu ya dola, huku akitambua dhahiri
kuwa, hana uwezo huo. Hata hivyo, licha ya kuufahamu ukweli huo, bado anaamua
kumuua Mkuu wa Wilaya wakati akihutubia wananchi. Mwandishi anaelezea kuwa:
… kelele za watu zilikuwa hazijatulia mlio wa bunduki
uliposikika. Hapo hapo Mkuu wa Wilaya alitotoma chini
akaanguka. Mlio wa pili ulisikika pale pale. Tumaini ambaye
alikuwa akijaribu kutoroka alianguka chini. … Askari
walimzunguka Tumaini. Akiwa amelala chini, mitutu kama
sita ya bunduki ilikuwa imelenga kichwa chake, akaambiwa
asijitingishe. Askari wengine walimbeba Mkuu wa Wilaya
upesi upesi, akaingizwa ndani ya gari kupelekwa hospitali (uk.
128).
Dondoo hili linabainisha namna Tumaini anavyokengeuka misingi ya jamii kwa
kukata tamaa na kusababisha kifo. Kama inavyoelezwa katika nadharia ya
Udhanaishi, anakumbwa na fadhaa, mashaka, pekecho na uchovu. Anaamini
kwamba, mwisho wa mwanadamu ni mauti. Kitendo anachokifanya ni uthibitisho wa
mchakato wa kujiua au kuuawa kwake. Hata hivyo, anakamatwa na askari mara tu
baada ya kutenda tukio hili wakati akitafuta mwanya wa kutoroka. Muda mfupi
baadaye, taarifa ya tukio la kuuawa kwa Mkuu wa Wilaya inasambaa na kusomwa
katika vyombo vya habari, huku ikieleza kwamba ameuawa na jambazi wakati
akihutubia wananchi kuhusu vijiji vya ujamaa, na kwamba, jambazi hilo
limekatamtwa.
94
Hatimaye, Tumaini anaamua kukiri kosa lake na kuhukumiwa kunyongwa baada ya
mwaka mmoja. Hata hivyo, kabla ya kufanyiwa kitendo hicho, anaelekeza lawama
zake kwa Dennis kwa madai kwamba ushauri wake wa kumtaka afanye kazi kwa
bidii, ndio uliosababisha aingie katika matatizo hayo. Anayasema haya mara tu,
baada ya kutembelewa na Dennis huko gerezani, wakati akisubiria kunyongwa:
―Dennis, unayakumbuka maneno uliyoniambia siku ya kwanza
tulipokutana hapa Shinyanga?‖
―Sikumbuki vizuri. Zamani sana.‖ Dennis alisema.
―Muda mrefu umepita. Lakini nitakukumbusha. Ulisema
kwamba dunia uwanja wa fujo, kwamba kila mtu lazima
atumie kichwa chake ajitahidi, afanye kazi kwa bidi ili apate
kujiendeleza.‖
―Ninayakumbuka sana maneno hayo,‖ Dennis alisema.
―Mimi nimefanya fujo hiyo: nimeweza kuwa tajiri. Lakini sasa
niko wapi?‖ … Dennis, sasa nitazame. Nitakufa kama
ng‘ombe. Nitatupwa pembeni kama gunia zee niliwe na
mchwa.‖ … Mimi nilifuata maoni yako. Nilikuwa tajiri.
Lakini kwa utajiri nilioupata nimelazimika kuua. Sikuweza
kuvumilia.
―Lakini hukulazimika kuua, Tumaini! Kwa nini uliua!‖
―Mali yangu, Dennis. Mali ambayo kwa muda mrefu
nilisumbukia… Ulikuwa wakati mbaya kwangu, Dennis.
Wakati nilipokuwa tu naanza kuchanua. Sikuweza kuvumilia
kukatwa kama ua la njiani lichumwavyo na msafiri
asiyejulikana‖ (kur. 129 - 130).
Ifahamike kwamba, Dennis alipomwambia Tumaini kuwa dunia uwanja wa fujo,
alimaanisha kwamba, kila mtu lazima atumie kichwa chake na ajitahidi kufanya kazi
kwa bidii ili apate kujiendeleza. Hata hivyo, Tumaini anapofanya jitihada za kutafuta
mali kwa bidii na kutajirika, anakutana na vikwazo vya jamii, kwani anashindwa
kutambua kwamba mtu hupata utu wake awapo katika jamii. Matokeo yake, kanuni
za jamii zinamfunga na kuingilia matakwa yake na shughuli zake za kujinufaisha,
kujiendeleza na kujitafutia furaha. Ndiyo maana, Dennis anamwambia Tumaini
kwamba hakupaswa kuua, bali kuvumilia. Hii ni kwa sababu anaishi katika jamii,
ambapo nguvu za mtu binafsi mara zote huwa haziwezi kushindana na nguvu za
jamii. Salamu anazompa Dennis kumpelekea mke na watoto wake ni uthibitisho
kwamba anakifurahia kifo chake. Anasema:
―Ukirudi. Waambie nitawakumbuka daima. Waambie
nitakufa. Lakini nitakufa kiume. Sitatoa hata chozi moja.
Waambie sina masikitiko kwa jambo nililolitenda. Nitakufa na
95
heshima yangu. Kama nilifanya kosa vizazi vitaamua (uk.
130).
Hivi ndivyo Tumaini alivyoingia katika mchakato wa kifo chake. Ni kweli katika
hali ya kawaida hakujiua kama ilivyotokea kwa Kazimoto na Rosa Mistika. Hata
hivyo, utafiti umebaini kwamba anapitia matukio yote ya mchakato wa kujiua kama
vile kukata tamaa, kupata msongo wa mawazo na kukubaliana na lolote linaloweza
kumtokea. Tunalithibitisha hili kutokana na kauli yake kwamba atakufa kiume,
hatatoa hata chozi moja, hana masikitiko kwa jambo alilotenda na kwamba atakufa
na heshima yake. Hivyo, kwa kuwa anajua madhara yatakayompata baada ya tukio la
kumuua Mkuu wa Wilaya, basi tunahitimisha kwamba Tumaini alijiua kwa sababu
alijisababishia kifo chake.
Kwa jumla, mjadala katika sehemu hii ulilenga kubainisha usawiri wa matukio
yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi. Kabla
ya kubainisha matukio hayo, muhtasari wa riwaya teule umetolewa. Baada ya hapo,
ubainishaji wa matukio hayo umefanyika kwa mfuatano kwa kuanza na riwaya ya
Rosa Mistika, Kichwamaji, na Dunia Uwanja wa Fujo. Mjadala umebainisha
kwamba matukio yanayosawiriwa katika riwaya hizo, ndiyo yanayounda mchakato
wa kujiua kwa wahusika. Aidha, mjadala umeonesha kwamba wahusika hao kabla ya
kuchukua uamuzi wa kujiua kwao, wanapitia matukio na changamoto nyingi
zinazowakatisha tamaa ya maisha ambapo mwishowe wanachukua maamuzi ya
kujiua. Wahusika waliojadiliwa kwa kina ni Rosa Mistika, Kazimoto, mama yake
Kapinga na Tumaini.
Katika ubainishaji wa usawiri wa matukio hayo ya mchakato wa kujiua katika riwaya
hizo, mtafiti ameongozwa na nadharia ya Udhanaishi. Nadharia hii imemwongoza
katika kubainisha kwamba mtu hufikia uamuzi wa kujiua, kutokana na kukata tamaa
ya maisha kwa kuyaona kuwa hayana maana. Aidha, imemwongoza katika kueleza
kwamba binadamu hutafuta uhuru wake kwa kutetea ubinafsi wake; na hufikia hatua
ya juu kabisa ya ubinafsi huo, yaani kujiua. Hivyo, hulazimika kukengeuka misingi
na kanuni zinazoiongoza jamii ili kujitafutia uhuru huo.
Sehemu inayofuata inawasilisha data kuhusu sababu za mitanziko ya wahusika
zinazosawiriwa katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi.
96
4.3 Sababu za Mitanziko ya Wahusika katika Riwaya Teule za Euphrase
Kezilahabi
Sehemu hii inajadili sababu za mitanziko ya wahusika zinazosawiriwa katika riwaya
teule za Euphrase Kezilahabi. Sababu hizo zimegawanywa katika makundi makuu
manne, ambayo ni sababu za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kifalsafa. Mwisho,
kuna sehemu inayotoa muhtasari wa jumla kuhusiana na mjadala uliofanyika.
4.3.1 Sababu za Kijamii
Kulingana na TUKI (2014), jamii ni mkusanyiko wa vitu au watu wenye asili au
kitovu kimoja. Kwa kuwa Fasihi huwakilisha maisha, basi katika sehemu hii,
tunajadili sababu ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya kila siku ya
jamii. Sababu hizo ni mahusiano ya kimapenzi na mfumo wa malezi.
4.3.1.1 Mahusiano ya Kimapenzi
Mahusiano ya kimapenzi ni sababu kubwa inayochangia watu wengi kuingia katika
mitanziko. Hali hii huwapata zaidi vijana ambao huwa katika rika la kubalehe,
ambapo hupitia changamoto mbalimbali za kimaisha. Wengi wao hujaribu kufanya
mambo mengi na makubwa ili kufikia matarajio na matamanio yao. Inapotokea kuwa
matarajio na matamanio hayo hayakufikiwa, huweza kukumbwa na msongo wa
mawazo, na hivyo, kujikuta katika hali ya kushindwa kuelewa nini kifanyike. Mara
nyingi, msongo huo wa mawazo huweza kusababisha mhusika kufikia hatua ya
kukata tamaa, na hata kuchukua uamuzi wa kujiua, hasa pale anapokosa ushauri na
miongozo sahihi. Kipengele hiki kinajikita katika mahusiano ya kimapenzi baina ya
mvulana na msichana.
Katika riwaya ya Rosa Mistika, suala la mahusiano ya kimapenzi linajitokeza kwa
kiasi kikubwa na linasababisha wahusika kuingia katika mitanziko ya kimaisha. Kwa
mfano, Rosa Mistika anajiingiza katika mtanziko wa mahusiano ya kimapenzi na
watu mbalimbali. Hatimaye, anaamua kujiua baada ya kukosa jibu sahihi juu ya
maisha yake. Mtanziko huo anaanza kuupata akiwa darasa la sita, mara tu baada ya
kuandikiwa barua ya mapenzi na Charles (uk.8). Barua yenyewe ni hii ifuatayo:
97
Namagondo,
P.O.Box Mpenzi,
Ukerewe.
Mpenzi Rosa Mistika
Ewe ua waridi lenye fumbo! Ewe dada wa makao yangu uliye
kitulizo changu! Fungua macho uone makala hii fupi ya
mapenzi. Nakuota kila siku wakati wa usiku, sipati usingizi
kwa ajili yako. Kuvumilia nimeshindwa. Tafadhali unijibu
upesi. Nakutakia ushindi mzuri katika mtihani wako.
Wako katika mapenzi na matumaini,
Charles Lusato.
Barua hii fupi na yenye maneno machache, imebeba ujumbe unaoibua na kuchochea
hisia, msisimko na fikra nzito ndani ya moyo wa Rosa Mistika, zinazomwingiza
katika mahusiano ya kimapenzi na Charles. Hata hivyo, mahusiano yenyewe
hayadumu, kwani yanaingia dosari mara tu baada ya Zakaria, baba yake Rosa, kupata
taarifa kuhusiana na barua hiyo. Zakaria hafanyi uchunguzi, badala yake, anampa
Rosa kipigo kikali kinachomfanya ajutie, ajilaumu na kujishuku kwa kuona kuwa
hapendwi, na hana usalama.
Utafiti umebaini kuwa kipigo hicho kinamsababishia Rosa mtanziko, ambapo
anatakiwa kuchagua ama kukubaliana na kutii sheria ngumu, kali, kandamizi na
zinazomnyima uhuru, kutoka kwa baba yake, ama kuzitupilia mbali na kuendelea na
mahusiano ya kimapenzi na Charles. Kukosekana kwa uhuru wa kujiamulia mambo
yake mwenyewe, kunamkatisha tamaa ya mapenzi na kumsababishia woga wa
maisha yake. Hali hiyo inasababisha amkasirikie na kumwogopa sana baba yake
pamoja na kuwakasirikia na kuwaogopa wavulana. Hatimaye, anaamua kumtii baba
yake, huku akiingiwa na chuki na kinyongo dhidi ya Charles na wanaume wengine
kwa jumla. Hivyo, kitendo cha Rosa kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi
kinachojidhihirisha ndani ya barua hii kinasababisha mtanziko kwake, kwani
kinampa wakati mgumu wa kufikiri uamuzi wa kuuchukua na kuufuata.
Pia, Rosa anapata mitanziko zaidi anapotoka katika sheria ngumu za kunyimwa
uhuru kutoka kwa Zakaria. Hii ni kwa sababu anakumbana na sheria nyingine ngumu
za masista katika shule ya Sekondari ya Rosary. Uvumilivu wake wa kuendelea
kufungwa katika minyororo hiyo ya ukandamizaji unamwishia na kuamua kujitafutia
uhuru wake binafsi. Matokeo yake ni kwamba anaanza kuiga tabia za wasichana
98
wenzake kwa kutoroka usiku na kwenda kucheza dansi. Msukumo huu anaupata
baada ya kuumizwa na maneno ya wavulana wawili wa shule ya sekondari ya Bwiru
wanaomjadili na kumwita kilema kwa sababu hana uhusiano na wavulana.
Mwandishi anasema:
Hata alipokuwa kitandani, maneno haya yaliendelea
kuzunguka kichwani mwake. Alikata shauri. Alikata shauri
kwenda kucheza dansi (uk. 30).
Imebainika kwamba msuguano wa mawazo anaoupata kuhusiana na suala hili la
mapenzi unamweka katika mtanziko, kwani anapata wakati mgumu wa kuamua
jambo lipi alifanye na lipi asilifanye.
Kitendo cha kuamua kwenda kucheza dansi kinamsababishia mtanziko, kwa kuwa
kinachangia sana katika mabadiliko yake kitabia. Pia, kinaibua hisia kali za mapenzi
anazozipata mara tu baada ya kucheza dansi na Deogratias. Tukio hili ndilo
linalosababisha aingie katika mgongano wa mawazo zaidi na kuanza kujiuliza
maswali yanayoumiza akili yake. Kupitia kwa mwandishi anasema:
Kama nikifanya urafiki na wavulana baba yangu atafahamu?
Yeye yuko Ukerewe, mimi niko Usukuma, baba anakaa
akinichunga anafikiri atanioa? (uk. 32).
Matokeo yanaonesha kuwa uamuzi anaouchukua wa kujiingiza na kuanza mapenzi
kwa madai kwamba baba yake yuko mbali na hamwoni, unampa wakati mgumu
zaidi anapobaini kwamba kunyimwa uhuru huko kumemcheleweshea mambo mazuri
ambayo hakuyafahamu kabla. Hivyo, anaamua kujiingiza katika bahari ya mapenzi
kwa pupa, pasipo kufanya maandalizi ya kutosha. Tabia na mwenendo wake sasa
vinatawaliwa na kukumbwa na nguvu ya mazingira yake mapya, tofauti na yale
aliyoyazoea. Mbatiah (1998) anaeleza kuwa Rosa anaamua kutumbukia katika bahari
iliyochafuka ya mapenzi bila kujua kuogelea. Haya yanajitokeza akiwa katika shule
ya Rosary. Mwandishi anasema:
Rosa sasa alianza mapenzi. Alianza mapenzi lakini aliyaendea
haraka sana kama mbwa aliyekata kamba. Aliona mvulana
mmoja au wawili hawamtoshi kwa urafiki. Mwaka huo huo
aliwakubalia wavulana watano (uk. 33).
99
Kutokana na dondoo hili tumebaini kwamba, uhuru anaojitafutia anautumia vibaya
na unamzamisha katika bahari ya mapenzi, ambayo haikati na wala haimalizi hamu
yake ya mapenzi. Kitendo cha kucheza dansi na kukumbatiana na Deogratias
kinamwamshia hisia kali za mapenzi zinazomweka katika mtanziko. Hali hiyo
inamfanya ashindwe kupata jibu sahihi la mtu, yaani mwanaume wa kuweza
kumaliza na kutatua tatizo lake. Badala yake, anavunja maadili ya jamii yake na
kwenda kwa msichana mwenzake, Thereza, na kutaka kumbaka. Mwandishi
analithibitisha jambo hili anaposema:
… Thereza alikuwa bado hajaelewa Rosa alipomrukia na
kumkumbatia. Waliangushana kitandani. Rosa alianza
kumbusu, lakini tamaa yake haikuweza kupungua. Rosa
alihitaji ule mkwaruzokwaruzo wa aina ya pekee.
Mkwaruzokwaruzo wa ndevu na manyoya ya tumboni. Zaidi
ya hayo, moto ulikuwa ukiwaka upande wa Kusini lakini wao
walikuwa wakizimisha upande wa Kaskazini (kur. 32 – 33).
Kitendo cha Rosa kwenda na kumparamia msichana mwenzake na kutaka kumaliza
hisia zake kinathibitisha kwamba yuko katika mtanziko. Ndiyo maana anashindwa
kupata jibu sahihi la uamuzi anaouchukua. Jambo hili linazidi kumtatiza na kumpa
wakati mgumu zaidi. Hii ni kwa sababu Thereza anashindwa kummalizia hamu na
hisia zake za mapenzi na kusababisha azidi kuchanganyikiwa. Yote haya yanampata
kutokana na kukengeuka misingi ya malezi na maadili aliyoyapata kutoka kwa
wazazi wake kwa kutafuta uhuru wake mwenyewe kama isemavyo nadharia ya
Udhanaishi. Uhuru huo ndio unaomwingiza katika mtanziko, kwani anaposhindwa
kutimiza na kumaliza hisia zake kwa Thereza, anaamua kufanya mapenzi na
wanaume wengi. Hata hivyo, bado hawamalizi kiu yake na kuzidi kumzamisha
katika bahari hiyo, ambayo kwa wakati huo, hajui urefu wa kina chake.
Kutokana na kuendekeza na kuendeleza tabia yake ya umalaya, mtanziko wa
mahusiano ya kimapenzi haumtokei akiwa katika shule ya Rosary pekee, bali hata
akiwa katika Chuo cha Ualimu Morogoro. Matokeo yanaonesha kuwa akiwa huko
pia, anajiingiza katika mahusino ya kimapenzi na watu wengi, akiwemo Mkuu wa
Chuo hicho, Bwana Thomas. Matokeo yake, Rosa anazidi kupatwa na masaibu ya
kimapenzi anapofumaniwa na mke wa Thomas, akiwa ndani ya nyumba ya Mkuu
huyo wa Chuo, huku akiwa katika ulimwengu wa mapenzi (uk. 54). Imebainika
kuwa tukio hili linazidi kumweka katika mtanziko zaidi anapoona kuwa, thamani
100
yake inazidi kupungua baada ya kuumizwa na mwanamke huyo, kwa kukatwa sikio
lake. Mwandishi anaeleza kuwa Rosa alilia na kulililia sikio lake kutokana na
maumivu makali aliyoyapata (uk. 55). Inaelezwa kwamba mambo mengi
yalimzunguka kichwani mwake, kiasi cha kusikia sauti hafifu sana kama ya mtu
anayekufa, ikimwita moyoni mwake. Sauti hiyo haisikiki kwa kila mtu, bali ni Rosa
peke yake ndiye anayeisikia na kuitambua. Matokeo yake, anajikuta katika wakati
mgumu wa kuamua jambo la kufanya, kutokana na mvutano na mvurugiko wa fikra
anaokabiliana nao. Mvutano na mvurugiko huo wa fikra, ndio unaosababisha
baadaye, afikie hatua ya kukata tamaa ya maisha na kukengeuka misingi ya malezi
aliyoipata kwa baba yake.
Sambamba na hilo, tumebaini kwamba baada ya kufanikiwa kuhitimu mafunzo yake
ya Ualimu huko Morogoro, Rosa anapangiwa kazi ya kufundisha katika shule ya
Msingi Nyakabungo, Mkoani Mwanza. Akiwa huko, anaamua kuachana na tabia ya
umalaya na kuchagua maisha ya ndoa, ili kupata utulivu wa maisha. Hatimaye,
anafanikiwa kumpata Charles Lusato, mpenzi wake wa zamani aliyesababisha
apigwe sana na baba yake, baada ya kumwandikia barua ya mapenzi akiwa darasa la
sita. Hata hivyo, anapopata matumaini mapya ya kuishi na kijana huyo, ndoto zake
zinapotea baada ya Charles kufichuliwa siri ya maisha ya umalaya wa Rosa.
Matokeo yake ni kwamba Charles anapobaini kuwa Rosa hana bikira, anamkataa na
anamwacha. Kitendo hicho cha kukataliwa kinamsababishia mtanziko, kwani
anapata ugumu wa kuamua jambo sahihi la kufanya. Hali hiyo inamkatisha tamaa ya
kuendelea kuishi na kufikia hatua ya kuchukua maamuzi ya kujiua huku akiacha
ujumbe unaoelekeza lawama zake kwa Charles, kwamba anajiua kwa ajili yake (uk.
93).
Hali hii inathibitisha kwamba kuvurugika kwa mahusiano kimapenzi huweza
kumsababishia mhusika mtanziko. Hali hiyo hutokea pale ambapo mhusika hujikuta
katika wakati mgumu wa kuamua jambo la kufanya kwa sababu uamuzi wowote
huwa na athari mbaya kwake. Kutokana na mitanziko hiyo, wahusika wengine
huweza hata kuchukua maamuzi ya kujiua. Hili ndilo linalomtokea Rosa, kwani
anafikia uamuzi huo baada ya kukata tamaa kwa kuona kwamba maisha hayana
maana tena kwake. Anapanga kuchukua uamuzi huo kama suluhisho la maisha yake
ili asiendelee kuumizwa tena na masuala ya mahusiano ya kimapenzi. Hii
101
inatudhihirishia kuwa, haoni sababu ya kuendelea kuishi, kama inavyoeleza adharia
ya Udhanaishi kwa sababu maisha yake yamekosa matumaini.
Vilevile, mtanziko unaotokana na mahusiano ya kimapenzi unajitokeza katika riwaya
ya Kichwamaji. Baadhi ya wahusika wanaokumbwa na mtanziko huo ni: Rukia,
Sabina, Kazimoto, Manase, Vumilia, na Moyokonde.
Utafiti umebaini kwamba Rukia anapatwa na mtanziko kwa kushindwa kujua hatima
ya maisha yake ya shule kutokana na vitendo vinavyohusiana na mapenzi,
anavyofanyiwa na Manase. Anazidi kutatizika anapobaini kwamba mahusiano hayo
yanamsababishia mimba pasipo matarajio yake. Barua anayomwandikia kaka yake,
Kazimoto, inaonesha wazi kwamba yuko katika mtanziko. Barua hiyo inasema:
Kaka mpendwa,
Moyo wangu siku hizi hauna raha. Lakini leo nimechukua
kalamu ili nikueleze mambo yote. Nimeona kwamba siwezi
kuwa nakuficha wewe mambo, hali mambo yenyewe sasa
hayawezi kufichika. Wewe ukiwa ndiye kaka yangu na ndiye
uliyenitafutia nafasi hii ya shule ninakupa heshima. Fahamu
kuwa mambo haya sijapata kumweleza mtu mwingine
isipokuwa wewe peke yako.
Kaka, uliponileta hapa nilikaa kwa raha kwa muda wa juma
moja tu. Baada ya juma hilo, niliona Manase anaanza
kunitazama kwa njia ya ajabu. Baada ya majuma mawili
mambo yalizidi kuwa mabaya, kwani nilipokuwa naoga siku
moja niliona jicho lake kwenye tundu la ufunguo. Mwishowe
aliniambia wazi alichokuwa anataka. Nilimwambia: Manase!
Kaka yangu akifahamu litakuwa jambo la aibu sana! Lakini
yeye alijibu kwamba wewe ni mwanamume kama yeye. Alifika
hatua ya kutumia nguvu! Na kweli alitumia nguvu bila utashi
wangu. Kaka, sitaki kukupotezea muda wako wa kujifunza kwa
kusoma barua ndefu. Mimi maisha yangu yameharibika. Shule
nimekwishaacha. Jambo ambalo limenisikitisha sana ni hili
lifuatalo: Jana usiku, Manase alirejea nyumbani mlevi.
Alikuwa na tikiti ya basi. Baada ya kunitukana kwa maneno
ambayo siwezi kukuandikia, alianza kupanga vitu vyangu
sandukuni. Leo atanisindikiza hadi kituo cha basi. Kaka,
machozi yananilengalenga, sijui nitasema nini kwa baba na
mama. Usifike kuja kuniaga kwenye kituo cha basi nisije
nikazimia.
Sina mengi,
Nduguyo,
Rukia Mafuru (kur. 19 - 20).
102
Barua hii inadhihirisha wazi kwamba masaibu anayoyapata Rukia katika maisha
yake, yanamsababishia mtanziko kutokana na kushindwa kupata majibu sahihi ya
mambo hayo. Uamuzi wake wa kumwandikia kaka yake barua, na maneno yaliyomo
ndani ya barua hiyo ni uthibitisho kwamba, uvumilivu wake wa kuendelea kuishi na
Manase umemwishia, na hayuko tayari tena kuendelea na shule. Udhaifu na uduni
wa maisha ya familia yake unakuwa chanzo cha kuingia katika mtego wa kuishi na
Manase na kumsababishia matatizo kwa kutiwa mimba, ambayo hakuitarajia. Tukio
hili, kama inavyoelezwa katika Udhanaishi, linasawiri picha halisi ya mwanadamu
ambaye ni kiumbe dhaifu kinachoishi maisha yasiyo na maana, katika ulimwengu
usio na maana.
Matokeo yake, anapata msongo wa mawazo unaomsababishia kifo chake kwa kukosa
nguvu za kusukuma mtoto wakati wa kujifungua. Hii ni baada ya kukaa muda mrefu
bila kula chakula kwa sababu ya mtanziko aliokuwa nao. Suala hili, kama
lilivyokwisha kujadiliwa katika kipengele cha 4.2.2.3 kinachohusu vifo vya Rukia na
mama yake hapo awali, linathibitishwa kupitia mazungumzo baina ya Tuza na
Kazimoto (uk. 83).
Hivyo, ni kweli kwamba Rukia anakufa kwa sababu ya mtanziko unaotokana na
kukosa mapenzi ya dhati kutoka kwa mtu aliyemtia mimba, yaani Manase. Uamuzi
wake wa kukataa kula kwa muda mrefu na kukosa nguvu za kusukuma mtoto wakati
wa kujifungua ni uthibitisho kwamba, haoni sababu ya kuendelea kuishi kutokana na
kuathiriwa na suala la mahusiano ya kimapenzi. Kwa hiyo, anachagua kufa kama
njia ya kuyakwepa matatizo hayo, kwa kuwa haoni tena sababu ya kuendelea kuishi.
Hivyo basi, matokeo ya utafiti yamebaini kuwa mahusiano ya kimapenzi ni sababu
mojawapo ya mtu kupata mtanziko, kwa kuwa humpa wakati mgumu wa kuamua la
kufanya pale anaposongwa na mawazo. Mtanziko huo wakati mwingine husababisha
mtu kuchukua maamuzi ya kujiua kutokana na kukata tamaa ya maisha kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi.
Vilevile, mahusiano ya kimapenzi yanajitokeza kwa Sabina na yanamsababishia
mtanziko. Hii ni baada ya kudanganywa na mvulana aliyewekeana naye ahadi
kwamba wataoana. Suala hili linamweka katika wakati mgumu, kwani linasababisha
aonekane na kutazamwa tofauti na jamii yake. Miongoni mwa watu wenye mtazamo
103
tofauti dhidi yake ni Kazimoto. Huyu, anahoji sababu za Sabina kutopenda kuolewa,
licha ya uzuri alio nao. Hata hivyo, majibu ya Sabina yaliyojaa masikitiko, huzuni,
maumivu na majonzi aliyo nayo moyoni mwake, yanathibitisha mtanziko alionao juu
ya jambo hili. Anasema:
―Kazimoto,‖ alianza kuzungumza. ―Kama ungefahamu taabu
ambayo nimekwishapata usingeniambia vile. Mimi nimo
katika huzuni. Usifikiri kwamba mimi sipendi kuolewa au
kwamba mimi sipendi wanaume. Kazimoto, ni vigumu kupata
wanaume. Nilikuwa na mchumba wangu. Kijana huyo
nilimpenda kweli na nilimpa moyo wangu wote, lakini siku
moja niliona picha yake gazetini ameoa msichana mwingine.
Ninawaombea maisha mazuri. Nilipata kijana mwingine,
nilitaka kumfanya mchumba, lakini nilipokataa mambo
aliyokuwa akipenda, yeye alinitukana kwamba nilikuwa
sifahamu mapenzi na kwamba sikuwa mchangamfu. Tangu
siku hiyo sijapata kumwona tena kijana huyo (uk. 103).
Dondoo hili linaonesha kwamba suala la ulaghai na udanganyifu katika mapenzi
limekuwa likisababisha mitanziko kwa watu wengi. Sabina ni mfano mzuri wa watu
hao, kwani licha ya kuendelea na shughuli zake za kijamii za kila siku, maisha yake
yanatawaliwa na maumivu na huzuni kubwa kutokana na kushindwa kujua hatima ya
maisha yake.
Mtanziko mwingine wa mahusiano ya kimapezi unaomkumba Sabina unatokana na
kubanwa na misingi na kanuni za jamii yake, ambapo, licha ya kuwa na hamu ya
kutaka kuolewa, utamaduni haumpi nafasi ya kumtongoza mwanaume amtakaye.
Hali hii inamweka katika wakati mgumu, kwani anabaki akisubiria mtu aje
pasipokuwa na uhakika wa kumpata. Ushahidi wa hili unatokana na maelezo ya
Sabina mwenyewe, anayeeleza kuwa, endapo atatokea mwanamume ambaye
ataamua kuomba uchumba kwake, atampenda na kumheshimu sana. Hii inaonesha
wazi kuwa vikwazo vya kijamii vinamzuia kumtafuta mwanamume amtakaye, hivyo
kusubiri kudra za Mungu. Anasema:
―… Lakini naona kwamba siwezi kuishi bila mume. Nikipata
mchumba sasa sijui nitampendaje! Nitamng‘ang‘ania kufa na
kupona. Siku ya kuolewa nafikiri bwana wangu nitakuwa
namlisha kwa mikono yangu mwenyewe‖ (uk. 104).
104
Ni wazi kwamba, watu wengi katika jamii zetu wana mitanziko inayotokana na
mahusiano ya kimapenzi. Hali hiyo inapozidi, huweza kusababisha msongo wa
mawazo, ambapo wengine huweza hata kujiua kutokana na kukata tamaa ya maisha
kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi.
Tasinifu hii imebaini kwamba watu wengi wana mitanziko ya mahusiano ya
kimapenzi inayotokana na sababu na visingizio mbalimbali. Miongoni mwa sababu
au visingizio hivyo ni umri, msimamo wa kiimani, udanganyifu na kukata tamaa ya
maisha. Watu wa namna hii wanahitaji kufarijiwa na kupata ushauri wa kisaikolojia.
Kufanyika kwa mambo kama hayo kutawaondoa katika msongo wa mawazo, na hata
kujisikia kuwa wao pia, ni sehemu ya jamii.
Vilevile, matokeo ya utafiti yamebaini kuwapo kwa wahusika wengine
wanaokumbwa na mtanziko wa mahusiano ya kimapenzi katika riwaya hii ya
Kichwamaji. Wahusika hao ni pamoja na Kazimoto, Manase, Vumilia, na
Moyokonde. Kwa upande wa Kazimoto na Manase, pamoja na mambo mengine,
imebainika kuwa mtanziko wao pia, unatokana na wote wawili kuwa na mahusiano
ya kimapenzi na msichana malaya anayeitwa Pili, ambapo anawaambukiza ugonjwa
wa zinaa. Nao, Kazimoto na Manase, kutokana na tabia yao ya uzinzi na umalaya,
wanawaambukiza ugonjwa huo wake zao. Athari za ugonjwa huo zinasababisha
wake zao kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa. Matokeo yake ni kwamba kila
mmoja wao anaingia katika mgogoro na mafarakano na mwenzi wake kwa
kusababisha janga hilo. Imebainika kuwa, hatimaye, mgogoro huo unasababisha
mtanziko kwa familia zote mbili, na unamsukuma Kazimoto kuamua kujiua kama
inavyoeleza nadharia ya Udhanaishi kutokana na kukata tamaa ya maisha.
Kuhusiana na familia ya Manase, matokeo yanaonesha kuwa, Salima, ambaye ni
mke wa Manase, anaamua kulichoma moto gari la Manase ili asiendelee kulitumia
katika masuala ya anasa. Vilevile, Manase anapotaka kununua gari jipya, Salima
hakubaliani na uamuzi huo. Hivyo, Manase anakuwa ni mtu wa kukaa ndani muda
wote kutokana na kukata tamaa ya maisha na kukosa majibu ya mambo
yanayomkabili (uk. 193). Hii inaonesha kwamba yuko katika mtanziko na unampa
wakati mgumu wa kujua maisha yake ya baadaye yatakavyokuwa. Imebainika
kwamba mara nyingi mtu akiwa katika hali kama hiyo, huweza hata kuchukua
105
maamuzi ya kujiua kutokana na kukata tamaa ya maisha kama ielezavyo katika
nadharia ya Udhanaishi.
Vilevile, mahusiano ya kimapenzi yanamsababishia Kazimoto mtanziko kutokana na
mtoto wake kufariki. Suala hili linaongeza simanzi na majonzi katika familia yake.
Tukio hili linamweka katika mtanziko, kwa sababu linamwingiza katika fikra nzito
na kumtafakarisha sana kuhusu maisha, pamoja na kizazi kijacho. Mahusiano ya
kimapenzi anayoyafanya na Pili na kumsababishia ugonjwa wa ajabu, ndiyo
yanayomzamisha katika mtanziko huu. Kwa kurejelea nadharia ya Udhanaishi,
imebainika kuwa hali hiyo ya mtanziko inamweka na kumzamisha katika dimbwi la
fikra, kwa sababu hajui maisha yake baadaye yatakavyokuwa. Hatimaye, anaamua
kujiua kwa madai kwamba haoni sababu ya kuendelea kuzaa kizazi kibaya (uk. 195).
Pia, kabla ya kujiua kwake anabainisha wazi kwamba, yeye ndiye aliyesababisha
kifo cha mdogo wake, Kalia, ingawa hakumgusa. Haya yanatokana na vitendo vyake
vya kujihusisha na masuala ya mapenzi, ambapo tabia yake hiyo inasababisha Kalia
kuuawa baada ya kuiga vitendo na tabia yake.
Aidha, Kazimoto anapata mtanziko mwingine unaotokana na mahusiano ya
kimapenzi baina yake na Sabina. Mtanziko huu unasababishwa na Mzee Fungameza
kutokana na kitendo chake cha kumshawishi Kazimoto kuachana na mpango wake
wa kumwoa Sabina kwa madai kwamba, jamii yake ina asili ya magonjwa na
uchawi. Suala hili linampa Kazimoto wakati mgumu wa kuamua hatima ya
mahusiano yake na Sabina, ikizingatiwa kwamba Mzee Fungameza ni baba mkubwa
wa Sabina. Anasema:
… ingawa Sabina ni jamaa yangu, bado ninaona kwamba
lisingekuwa jambo zuri wewe kumwoa… Sabina – nikwambie
mtoto wangu – ni tunda baya na nisingependa wewe ulile.
Tukitazama katika ukoo wao kwa makini, hasa jamii yao
utaona kwamba ulikuwa na sifa mbaya tangu zamani. Babu
yake wa pili – ninyi hamkumwona – alikuwa mgonjwa wa
ukoma. Alikufa bila vidole vya mikono na miguu. Nyanya
yake – nyinyi hamkumkuta anaishi – alikuwa mchawi wa
kustaajabisha. Alikufa macho mekundu kama umeme.
Ukimtazama vizuri Sabina utaona kwamba anaweza kurithi
mambo haya mawili. Ukitazama vizuri mwili wake, utaweza
kudadisi kwamba anaweza kupata ukoma katika miaka yake
ya uzee. Na hali ya unyamavu aliyonayo inaonyesha wazi
106
kwamba amekwishafahamu siri za watu wengi. Yaani siri za
usiku (kur. 146 - 147).
Katika dondoo hili, Mzee Fungameza, siyo tu kwamba anaisema vibaya jamii ya
Sabina kwa masuala ya uchawi na magonjwa, bali pia anamnasibisha Sabina na
masuala hayo. Kutokana na hilo, anazidi kumweka Kazimoto katika mtanziko
anapoelezea mambo yanayodaiwa kufanywa na Sabina akiwa Tabora. Anasema:
… huko Tabora, mtoto wangu, ndiko tunda lilikoozea. Jambo
huenda likakushangaza, Sabina aliwahi kuchukuliwa na
kutunzwa kama kimada. Akaishi na jambazi fulani kwa miaka
miwili. Lile jambazi baada ya kumtafuna, lilimwacha na kuoa
msichana mwingine wa kwao huko – sijui wapi… Lakini hili
pia ni jambo dogo, labda jambo ambalo siwezi kumsamehe ni
lile la kutoa mimba mara mbili. Mimba hizi alizitoa alipokuwa
Tabora. Kama ataweza kuzaa tena sijui… (kur. 145 - 146).
Ifahamike kwamba uongo na ulaghai huu unafanywa na Mzee Fungameza wakati
Kazimoto akiwa katika mchakato wa kufunga ndoa na Sabina. Katika hali ya
kawaida, maneno haya siyo tu kwamba yanamkatisha tamaa Kazimoto, bali pia
yanampa wakati mgumu wa namna ya kulikabili jambo hili. Ushauri unaotolewa na
Mzee Mafuru, ambaye ni baba yake Kazimoto, kwamba ajihadhari na watu wenye
nia mbaya, kwa sababu wanaweza kuvunja uchumba wa watu, kwa kiasi fulani
unamwondoa Kazimoto katika mtanziko huo, kwani unamsaidia kubaini hila za
Mzee Fungameza (uk. 147). Pia, anatiwa moyo na kuendelea na mchakato wake wa
kumwoa Sabina, baada ya Sabina mwenyewe kumwomba asisikilize maneno ya
watu, kwa sababu si kila mtu hupenda watu wafanikiwe. Anasema:
Kazimoto, wewe sasa ni mtu mzima. Sidhani kwamba
unaweza kushtushwa na mambo kama haya. Jambo
linalotupendeza sisi haliwezi kumpendeza kila mtu. (uk.
148).
Ni kweli kwamba mahusiano ya mapenzi baina ya Kazimoto na Sabina
yanasababisha mtanziko kwa Kazimoto kutokana na changamoto zinazojitokeza
katika mchakato wa kuoana kwao. Hata hivyo, mtanziko huo unaondoka baada ya
kubaini hila, uongo na ulaghai wa Mzee Fungameza. Jambo muhimu lialopaswa
kufahamika ni kwamba mtu akiwa katika mtanziko, huwa na wakati mgumu wa
kuamua la kufanya. Hali hiyo husababisha hata kuchukua maamuzi ya kujiua
kutokana na kukata tamaa kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi.
107
Sababu ya mtanziko wa mahusiano ya mapenzi pia inajitokeza kwa Vumilia na
mumewe, Moyokonde. Watu hawa, licha ya kuwa na maisha magumu kutokana na
hali yao duni ya kipato, wanaamua kuishi kwa kupendana na kuvumiliana. Tegemea
ambaye ni mama yake Vumilia, akiwa na Kazimoto baada ya kumtafuta Vumilia
kwa muda mrefu, hatimaye, wanafanikiwa kumpata huko Mabatini, Mwanza akiwa
anaishi na Moyokonde kama mke na mume. Kutokana na mazingira hayo, Tegemea
anakata shauri la kuondoka na binti yake. Kauli hiyo inasababisha mtanziko kwa
wote wawili, Vumilia na Moyokonde. Kwa upande wake, Moyokonde anamweleza
Tegemea kwamba, kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo kwa mke wake, Vumilia,
hawezi kuishi pasipo kuwa naye. Anaongeza kuwa, iwapo uamuzi wake ni kuondoka
pamoja na Vumilia, basi akubali kuondoka nao wote wawili, kwa sababu akiachwa
peke yake, yuko tayari hata kufa kwa ajili yake. Mazungumzo baina ya Moyokonde
na Tegemea yanabainisha jambo hili:
―Tukuchukue wewe tukupeleke wapi?‖
―Hata kama ni kuniua,‖ alijibu Moyokonde.
―Nimekuja kumchukua binti yangu, na kesho nasafiri naye.‖
Moyokonde aliinama kwa masikitiko. Aliinua kichwa.
―Hata kama mnataka kumchukua, afadhali mngoje ajifungue,
kwa sababu sasa ni mjamzito.‖
―Mimi nitamchukua mtoto wangu tu. Mtoto wako
atakayezaliwa tutakurudishia.‖
―Hapana. Wewe ni mtu mzima mwenzangu. Mimi nilikuwa
sijapata mtoto maishani. Kumchukua Vumilia sasa ni
kuchukua maisha yangu. Mwanizika kaburini bila nguo.‖ (uk.
174).
Majadiliano haya yanaonesha namna Moyokonde anavyopata wakati mgumu
kutokana na Tegemea kutaka kumnyang‘anya na kuondoka na binti yake. Suala hili
la mahusiano ya mapenzi halimpi wakati mgumu Moyokonde pekee, bali hata
Vumilia mwenyewe anapata ugumu wa kuamua ama akubaliane na matakwa ya
mama yake au akatae na kuendelea kuishi na mumewe. Hatimaye, anachukua
uamuzi mgumu na kumweleza mama yake waziwazi kuwa hayuko tayari kuondoka
naye, bali kubaki na Moyokonde (uk. 174). Msimamo huu wa Vumilia unamsukuma
mama yake kuridhishwa na upendo uliopo baina yao. Kutokana na hilo, anaamua
kuwaondolea mtanziko huo kwa kuwapa baraka zake ili waendelee kuishi pamoja
kama mume na mke (uk. 174). Hivyo, ni wazi kwamba mahusiano ya kimapenzi
huweza kusababisha mitanziko kwa wahusika, hususani pale ambapo mahusiano
108
hayo yatakumbwa na vikwazo mbalimbali. Mtanziko huo huweza hata kusababisha
mhusika kuchukua maamuzi ya kujiua kutokana na kukata tamaa ya maisha kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi, hususani pale anapokuwa haoni
mwanga wa maisha yake ya baadaye. Maelezo ya Moyokonde kwamba yuko tayari
hata kufa iwapo mama yake Vumilia ataamua kuondoka na mtoto wake, ni ithibati
juu ya jambo hili.
Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo, mtanziko wa mahusiano ya kimapenzi pia,
unajitokeza kwa wahusika mbalimbali. Miongoni mwao ni Leonila, Anastasia, Vera,
na Dennis. Matokeo yanaonesha kuwa wahusika hawa walipitia changamoto nyingi
za kimahusiano, kiasi cha kupata wakati mgumu wa kuamua kuhusu hatima ya
mahusiano na maisha yao kwa jumla.
Mtanziko wa mahusiano ya mapenzi kwa Leonila unatokana na hila na udanganyifu
wa Tumaini unaomwingiza katika mahusiano ya kimapenzi. Tumaini anamhadaa
Mugala, ambaye ni bibi yake Leonila, kwa kumpa ugoro na pipi ili amfanyie mpango
wa kuwa na mahusiano na mjukuu wake. Kwa kuwa Mugala huwa analala nyumba
moja na wajukuu zake, anakubaliana na ulaghai wa Tumaini. Anatengeneza
mazingira ya kumruhusu Leonila kwenda kulala kwa Tumaini usiku kwa siri (kur. 18
- 19). Tumaini anapomkuta Leonila akiwa na bikira yake, anampongeza na anampa
shilingi kumi zaidi. Mahusiano yao yanaendelea vizuri kwa muda mrefu. Matokeo
yake, Leonila anapata mimba na kusababisha mgogoro na mafarakano katika familia
ya Kasala, ambaye ni baba yake Leonila.
Hata hivyo, licha ya Tumaini kukiri kwamba alimkuta Leonila akiwa bikira, Leonila
anapopata mimba, Tumaini anamgeuka na kumkataa kwamba mimba hiyo siyo yake,
na kamwe hawezi kumwoa. Anasema: ―Mimi siwezi kumwoa Leonila, mimba si
yangu. Hata kama akizaa, mtoto wake mnaweza kumtupia mbwa‖ (uk. 26). Badala
yake, Tumaini anaanzisha mahusiano ya kimapenzi na Anastasia na kusababisha
Leonila kuwa na wakati mgumu, kwa sababu licha ya Tumaini kuikataa mimba hiyo,
anakataa hata kumwoa (uk. 26). Hivyo, hii ni ithibati kwamba mahusiano ya
kimapenzi ni sababu mojawapo ya watu kupata mitanziko katika maisha yao,
ambapo wengine huamua hata kujiua kutokana na kukata tamaa ya maisha kama
inavyoeleza nadharia ya Udhanaishi.
109
Kwa upande wa Anastasia matokeo yanaonesha kuwa, naye anakumbwa na mtanziko
unaotokana na mahusiano ya kimapenzi kwa kutakiwa, ama akubaliane na matakwa
ya wazazi wake ya kuolewa na Mzee Tembo, au akubaliane na ulaghai wa Tumaini
na kutoroka naye. Jambo hili linatokea mara tu baada ya Mzee Tembo kufiwa na
mke wake, ambaye ni dada yake, Anastasia. Hivyo, Anastasia mwenye umri wa
miaka kumi na sita tu, analazimishwa na wazazi wake kuolewa na Mzee Tembo
mwenye umri wa miaka hamsini, ili aweze kuwatunza watoto walioachwa na
marehemu dada yake. Kutokana na hilo, anajikuta akishindwa kupata maamuzi
sahihi ya nini cha kufanya ikizingatiwa kwamba, yuko katika mahusiano ya
kimapenzi na Tumaini. Zaidi ya hayo, tayari Tumaini amepanga kumtorosha ili
kumwepusha na balaa hilo. Ifahamike kwamba, msukumo wa wazazi wa Anastasia
wa kumlazimisha aolewe na Mzee Tembo, haukuwa kwa ajili ya kwenda kuwalea
watoto walioachwa na dada yake tu, bali pia, ni kwa sababu ya mali nyingi alizo
nazo mzee huyo. Mazungumzo baina ya Mzee Tembo na wazazi wa Anastasia
yanaonesha furaha yao kwake na wanampa nafasi ya kuongea na Anastasia,
ijapokuwa yeye mwenyewe hapendi. Haya yanabainishwa katika mazungumzo baina
yao kama ifuatayo:
―Ninashukuru sana kwa wema wako. Ninafurahi sana kama
ningeweza kumchukua upesi. Watoto wa dada yake
wanasumbuka sana.‖
―Ndiyo maana nilikwambia ufike upesi. Sisi tu tayari kukupa
binti yetu huyu kwa sababu ya wema wako uliotutendea.
Hatutaki kuomba mahari makubwa sana. Ng‘ombe watatu,
mbuzi wawili na shilingi mia nne zatosha.‖
―Baba mkwe, asante sana, asante sana,‖ Tembo alisema kwa
unyenyekevu akipiga makofi polepole.
―Basi, ukazungumze naye. Bukehele! Njoo hapa nikutume!
Wewe nenda jikoni‖ (uk. 39).
Dondoo hili linaonesha namna wazazi wa Anastasia wanavyomgawa binti yao kama
zawadi kwa Mzee Tembo kwa kigezo cha wema alio nao, pasipo ridhaa ya
mwolewaji. Hii inasababisha mtanziko kwa Anastasia, kwani hata anapoambiwa
akae ndani ili azungumze na Mzee Tembo, yeye anakataa na kukimbilia nje huku
akilia na kumwacha peke yake ndani. Kitendo hiki kinamuudhi sana baba yake na
anamlazimisha arudi ndani ili azungumze na mchumba wake. Kauli ya baba yake
inasema: ―Rudi ndani! Unaogopa wanaume!‖ Baba yake alifoka (uk. 40). Kauli hii
inazidi kumweka Anastasia katika mtanziko. Hatimaye, anachagua kuwasaliti wazazi
110
wake na kuamua kutoroka na Tumaini ili kukomesha utamaduni wa wazazi wa
kuwachagulia watoto wao wachumba na kuwalazimisha kuoa au kuolewa na watu
wasiochaguo lao na wasiowataka. Tumaini analielezea suala hili anaposema:
―Anastasia, usilie. Lazima tuwaonyeshe wazee kwamba
mpango wa zamani wa kugawa mabinti wapendavyo wao,
umekwisha. Huu ni ulimwengu wa ndoa za mapenzi; siyo tena
ulimwengu wa kugawa mabinti kama zawadi kwa watu
wasiowapenda… (kur. 42 - 43).
Dondoo hili linaonesha kwamba mahusiano ya kimapenzi yanamsababishia
Anastasia mtanziko, kwa kuwa yanampa wakati mgumu wa kuamua jambo sahihi la
kufanya kwa wakati huo. Kulingana na utamaduni wa jamii yake, kitendo cha
kuwatoroka wazazi wake, siyo tu kwamba kinawadhalilisha, bali pia kinawaletea
aibu mbele ya watu. Mwandishi anaeleza kwamba kitendo hiki kinamkasirisha sana
baba yake, kwa sababu kinatokea huku jamaa zake wakiwa wamekwishakusanyika
kwa ajili ya arusi. Matokeo yake, jamaa za Mulele wanaanza kudharau na
kutawanyika, huku wakisema:
Watu wasiofahamu kulea binti zao matokeo yao haya haya.
Lakini watu wengine walimtetea Anastasia kwamba alifanya
vizuri kutoroka. Tumaini aliposikia habari hizi alicheka
moyoni (uk. 53).
Hapa tunaona kuwa, Tumaini anafanikiwa kumtorosha Anastasia na kwenda naye
kuanza maisha mapya kama mke na mume huko Shinyanga. Hili linafanikiwa baada
ya kumshawishi Anastasia kuwalaghai wazazi wake kwamba anataka kwenda kijiji
cha Lutare kuangalia ngoma. Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, ndipo
anapoamua kutoroka na Tumaini. Kwa kurejelea nadharia ya Udhanaishi, matokeo
yanaonesha kuwa Anastasia anaamua kufanya hivyo kama njia ya kuusaka uhuru
wake binafsi kwa kufanya yale anayoona yanafaa dhidi ya mikatale ya jamii,
inayomkandamiza na kumnyima uhuru wake.
Kwa jumla, utafiti umebaini kwamba mahusiano ya kimapenzi, husababisha watu
wengi kuwa na mitanziko. Suala hilo huwaweka katika hali ya kutatiza, kukanganya
au kuhangaisha. Aidha, huwapa wakati mgumu wa kuchagua la kufanya kutokana na
mkinzano wa mawazo waupatao. Hii ni kwa sababu uamuzi wowote wapangao
kuchukua, huwa na madhara kwao. Hili linathibitishwa katika gazeti la Mtanzania la
111
Novemba 30, 2019 linaloeleza kuwa, sababu mojawapo ya watu kujiua ni msongo
wa mawazo unaotokana na mahusiano ya kimapenzi. Haya ndiyo yanayojitokeza pia,
kwa wahusika Rosa Mistika, Rukia, Sabina, Kazimoto, Manase, Vumilia,
Moyokonde, Leonila, na Anastasia kama tulivyojadili katika sehemu hii.
4.3.1.2 Mfumo wa Malezi
Mfumo wa malezi na namna watoto wanavyolelewa katika jamii huweza
kusababisha mitanziko kwa wahusika. Malezi ni mchakato wa kumtunza na
kumsaidia mtoto, tangu kuzaliwa hadi utu uzima, kwa kuhusisha maumbile, hisia,
jamii na uwezo wa kiakili. Mchakato huo hulenga kumkuza na kumfundisha mtoto
kabla au baada ya kuzaliwa hadi anapofikia umri wa utu uzima ili kufuata tabia na
mwenendo unaostahiki. Kwa mujibu wa BAKITA (2017), malezi ni mafundisho
mazuri yanayotolewa na mzazi au mlezi katika makuzi ya mtoto. Katika jamii nyingi
za Kiafrika, mfumo wa malezi hupitia michakato mbalimbali. Hatimaye, mifumo
hiyo humtoa mhusika katika hali ya utoto na kuwa mtu mzima anayetambua wajibu
wake. Kutokana na hilo, ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha kuwa mtoto
anaandaliwa mapema na kutambua mambo yote muhimu kama binadamu mkamilifu.
Katika riwaya teule, mwandishi anabainisha ugumu uliopo kuhusiana na suala la
malezi ya watoto, hususani wa kike. Anaona kuwa, malezi ayapatayo mtu akiwa
mtoto mdogo, huwa na athari kubwa sana katika maisha yake ya baadaye. Hii ina
maana kuwa, endapo mtoto atalelewa maisha ya ukali, manyanyaso, ukatili, mateso,
vitisho na masimango, bila shaka mambo hayo yataweza kujidhihirisha kwenye
maisha yake ya baadaye. Aidha, kama atapata malezi ya kudekezwa, ya upendo,
furaha, na kuthaminiwa, anaweza kusawiriwa hivyo hivyo maishani mwake. Kwa
mantiki hiyo, wazazi au walezi wanapotofautiana katika misimamo ya namna ya
kuwalea watoto wao, huwaweka watoto hao kwenye mitanziko ya maisha yao ya
baadaye kama inavyojitokeza katika riwaya teule zilizotumika katika utafiti huu.
Katika riwaya ya Rosa Mistika, tumebaini kuwa malezi aliyopata Rosa kutoka kwa
wazazi wake, hususani kutoka kwa Zakaria, yanamsababishia mtanziko katika
maisha yake. Hii inatokana na kunyimwa uhuru wa kuchangamana na wavulana
kutokana na kulelewa katika hali ya ukali, ukatili, kubanwa na kuchungwa sana.
Musau (1995) anaeleza kuwa Zakaria anaamini kuwa hayo ni malezi bora ambayo
112
ufanisi wake utaonekana pale binti huyo atakapomletea mahari baba yake, baada ya
kuolewa. Hata hivyo, imebainika kwamba malezi ya namna hiyo yanasababisha Rosa
kutofahamu namna ya kukabiliana na matatizo yanayotokana na maisha ya kisasa nje
ya kijiji chao, na mbali na jicho la baba yake. Matokeo yake, akiwa katika shule ya
sekondari ya Rosary, anapata mtanziko pale anapofikiria kukengeuka misingi ya
malezi aliyojengewa na baba yake. Hili linathibitishwa kupitia kauli yake,
anaposema:
Kama nikifanya urafiki na wavulana baba yangu atafahamu?
Yeye yuko Ukerewe, mimi niko Usukuma, baba anakaa
akinichunga anafikiri atanioa? (uk. 32).
Kinachobainika kupitia kauli hii ni kwamba, Rosa hakurupuki tu na kukengeuka
misingi ya malezi aliyojengewa na baba yake, bali anasongwa na mawazo
yanayompa wakati mgumu wa kufikia uamuzi anaopanga kuuchukua. Hata hivyo,
anapobaini kuwa malezi hayo ndicho chanzo cha matatizo yake, anamchukia baba
yake na kujibizana naye hadharani. Zakaria anamkana Rosa kuwa si mtoto wake na
wakati huohuo Rosa naye, anamkana Zakaria kuwa si baba yake (uk. 58).
Utafiti umebaini kuwa kitendo cha Rosa kujibizana na baba yake, ni ishara ya wazi
ya kupinga mfumo wa malezi ya baba yake. Anafikia hatua hii kutokana na Zakaria
kumbana katika suala la malezi na kumnyima uhuru. Hivyo, anaamua kuutafuta kwa
nguvu kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi, ili kupata mwanga na
kujitimizia haja ya matamanio yake. Mwandishi analisawiri jambo hili anaposema:
Maisha ya binadamu ni kama mti. Mti unahitaji maji, hewa na
mwanga. Kama mti ukinyimwa mwanga wa kutosha na miti
mingine, utarefuka. Utajaribu kupita miti yote ili upate
mwanga. Zakaria aliwanyima binti zake mwanga wakati ule
walipokuwa wakiuhitaji sana. Aliwapiga; aliwakataza
kuzungumza na mvulana yeyote. Nao kama mti walijaribu
kujirefusha ili wapate mwanga, na walirefuka kweli; kiasi cha
kutoweza kuonywa na mtu yeyote (uk. 47).
Ni kweli kwamba Rosa anakosa mwanga na njia sahihi kwa sababu ya kunyimwa
uhuru, pamoja na vitisho vingi anavyofanyiwa na baba yake. Kitendo hicho
kinamuumiza sana na kinamjengea chuki moyoni mwake, dhidi ya baba yake.
Matokeo yake anafikia hatua ya kukengeuka misingi ya jamii na kukata tamaa ya
maisha kwa kuamua kuutafuta uhuru wake kwa nguvu kama inayoelezwa katika
113
nadharia ya Udhanaishi. Anayathibitisha haya katika mazungumzo yake na Charles
wakiwa huko Mwanza. Anasema:
―Charles, tendo la baba limeniumiza kuliko unavyofahamu.
Ah Charles, kama tu wazazi wangalifahamu kwamba tendo lao
moja linaweza kuharibu maisha ya watoto wao wangejua
ugumu wa madaraka yao na uangalifu uwapasao (uk. 77).
Maneno hayo ni uthibitisho tosha kwamba Rosa yuko katika mtanziko unaotokana na
malezi kutoka kwa baba yake. Mtanziko huo unasababisha achukue uamuzi wa
kujiua, kama anavyoeleza mwenyewe kabla ya kuchukua uamuzi huo, huku
akielekeza lawama zake kwa Zakaria. Anasema:
―Sasa ninakufa: ninakufa sasa. Maisha yangu yalikuwa
magumu. Sasa nimeona wazi kwamba malezi yangu ndiyo
yalikuwa chanzo cha taabu. Malezi. Siyo malezi ya mama,
lakini malezi ya baba yangu. Kweli baba alinichunga.
Nilichungwa kama msichana wa jela. Nilipopata uhuru,
nilishindwa kuutumia… Baba na mama, samahani kama
nimefanya vibaya.‖ (uk. 91).
Rosa anaposema kwamba maisha yake yalikuwa magumu, na kwamba, malezi ya
baba yake ndiyo sababu ya taabu zake, anakusudia kuthibitisha kwamba aina ya
malezi anayoyapata mhusika huweza kumsababishia mtanziko, ambao pia, huweza
kusababisha mtu kujiua kutokana na kukata tamaa kama inavyoelezwa katika
nadharia ya Idhanaishi. Ndiyo maana, Rosa anamwelekezea lawama baba yake
kutokana na aina ya malezi aliyompa, na kumkosesha mwanga wa namna ya
kuzikabili changamoto za maisha yake.
Suala hili la malezi linasawiriwa pia katika maiti ya Rosa, ambapo uso wake
unaonekana kama wa mtu anayetabasamu, ijapokuwa amekufa kwa maumivu
makali. Mwandishi anasema:
Uso wa Rosa ulionekana kama wa mtu anayetabasamu.
Ingawa alikufa kwa maumivu aliweza kufunga na kufumba
mdomo na macho yake vizuri. … siri ya malezi (uk. 93).
Uso wa Rosa unabeba siri ya maisha yake yaliyogubikwa na madhila yatokanayo na
malezi na matendo mabaya aliyoyapitia. Tabasamu lake ni ishara kwamba anaicheka
jamii yake, kutokana na malezi mabaya kwa watoto wao, hususani, wa kike. Kauli
114
hii inaungwa mkono na Mbatiah (1998) anayeeleza kuwa riwaya hii ya Rosa Mistika,
imetawaliwa na kicheko cha uchungu. Anaongeza kuwa mwandishi anaicheka jamii
yake kwa kushindwa kuwalea watoto wake, hususani watoto wa kike. Anaenda mbali
zaidi kuwa malezi haya mabovu yanakiangamiza kizazi kizima cha watoto wa kike.
Kwa msingi huo basi, ni wazi kwamba Rosa anawakilisha maisha ya vijana wengi
katika jamii, ambao maisha yao kwa jumla yameathiriwa kutokana na mifumo ya
malezi wanayoyapitia katika jamii zao. Aidha, uso huo unaonesha kwamba Rosa
anakifurahia kifo chake, kwa sababu maisha yake hayakuwa na maana tena. Ndiyo
maana ameamua kujiua kuliko kuendelea kuishi. Kulingana na nadharia ya
Udhanaishi, kwake huo ndio uhuru aliokuwa anautafuta kwa muda mrefu, ijapokuwa
uhuru huo ndio ulioyaangamiza maisha yake.
Kwa jumla, utafiti umebaini kwamba kitendo cha kuwabana na kuwanyima uhuru
watoto kwa kuwawekea sheria ngumu na kandamizi, si kigezo madhubuti cha
kuwajengea tabia njema kwao. Kitendo hicho kama inavyoeleza nadharia ya
Udhanaishi, husababisha watoto hao kukengeuka misingi ya malezi wayapatayo na
kuamua kutafuta uhuru wao binafsi na uwezo wa kujifikiria na kujiamulia mambo
yao wenyewe. Hivyo, wazazi na jamii kwa jumla wanatakiwa kuwaeleza watoto wao
ukweli ulivyo kuhusu changamoto za maisha yao. Kitendo cha kuwazuia na
kuwabana wasione mwanga wa mambo yatokeayo ulimwenguni husababisha
mivutano baina yao na wazazi wao, na ndipo hufikia uamuzi wa kuutafuta uhuru wao
kwa nguvu. Mfano mzuri wa kulithibitisha hili ni Rosa Mistika anayejaribu kuutafuta
uhuru wake. Anafanya hivyo ili kuondokana na mfumo wa malezi kandamizi wa
kufungwa na minyororo, uliokita mizizi katika familia ya Zakaria na jamii kwa
jumla. Hata hivyo, uhuru huo unamsababishia matatizo mengi, likiwamo suala la
mapenzi, na hivyo kumpa wakati mgumu wa kuamua na kuchagua la kufanya.
Hatimaye, anachagua kujiua, huku akilalamikia suala la malezi makali, kutoka kwa
baba yake.
Katika riwaya ya Kichwamaji, mitanziko inayosababishwa na suala la malezi,
inasawiriwa pia, hususani kwa vijana. Mitanziko hiyo inatokana na mabadiliko
makubwa ya kitabia kwa vijana, yanayosababishwa na aina ya malezi wanayoyapitia.
Kukosekana kwa malezi bora kunachangia kwa kiasi kikubwa vijana wengi wa
kiume kuwapatia mimba wasichana, wengi wao wakiwa katika umri mdogo.
115
Matokeo yake, wengine hukumbwa na mitanziko kutokana na kushindwa kupata njia
ya kukabiliana na matatizo wanayoyapata. Matilda analithibitisha hili anaposema:
―Haya yote ni sawa,‖ Matilda alisema, lakini nionavyo mimi
sababu yenyewe hasa ni kwamba malezi ya watoto wa siku
hizi yamelegea sana. Wakati mimi nilipokuwa kama wao
ilikuwa mwiko kukutwa na kaka nimesimama na mvulana
yeyote; siku hizi kaka anaweza kumletea ndugu yake barua
kutoka kwa mvulana mwenziwe. Maana yake nini? Wengine
wanaweza kushikana viunoni dansini – kaka na dada! (uk. 58).
Katika nukuu hiyo, Matilda anaonekana kukasirishwa na kitendo cha kulegea kwa
malezi ambako hakutokei kwa vijana wa kiume pekee, bali hata kwa vijana wa kike.
Kulegea huko ndiko kunakosababisha kuharibika kwa vijana, hususani wa kike, na
kuwasababishia mitanziko kutokana na kukosa njia madhubuti za kutatua na
kukabiliana na mitanziko hiyo. Maelezo ya Matilda, yanaungwa mkono na kijana
mwingine anayeona kuwa, kuporomoka kwa malezi ya vijana wa siku hizi,
kunatokana na vijana wengi kuwa na dharau. Anasema:
Sababu kubwa ilikuwa vijana wa siku hizi wanadharau wazazi
wao. Dharau hii imeletwa na elimu. Wanafikiri kwamba
mawazo yote ya wazee ni ya kijadi (uk. 58).
Utafiti umebaini kwamba mabadiliko katika malezi ya vijana wa siku hizi, kwa kiasi
kikubwa yamechangiwa na mwingiliano wa tamaduni, hususani zile za Kimagharibi.
Athari kubwa imetokana na mfumo wa elimu itolewayo kwa vijana hao. Vijana
wengi wa kiume wamekuwa wakiwalaghai na kusababisha mitanziko kwa mabinti
kwa kuwatia mimba na wakati mwingine kuzikataa. Vitendo hivyo vimekuwa
vikiwasababishia mabinti wengi mitanziko katika maisha yao, ambapo wengi wao
hufikia hata uamuzi wa kujiua kutokana na kukata tamaa kama inavyoelezwa katika
nadharia ya Udhanaishi. Manase ni mfano mzuri wa vijana wenye kiburi cha elimu
itokanayo na athari hizo za Kimagharibi. Kutokana na kiburi hicho, anamtia mimba
Rukia na kuikataa kwa kusingizia kwamba alikuwa malaya tangu alipoota maziwa
(uk. 17). Kitendo hiki kinasababisha Rukia kupata mtanziko na baadaye kuchangia
katika tukio la kifo chake.
Kitendo kingine cha vijana wa kiume kuwatia mimba watoto wa kike
kinachohusishwa na mabadiliko ya malezi ya vijana wa siku hizi, kinasawiriwa
116
katika mazungumzo baina ya Kazimoto na wenzake nyumbani kwa Kamata. Jambo
kubwa linalokusudiwa kuibuliwa na mwandishi ni namna watoto wa kike
wanavyopata mimba na, wakati mwingine, kushindwa kumbainisha mhusika wake.
Haya yanajidhihirisha katika majadiliano baina yao, kama ifuatavyo:
―Nasikia binti Kasembe ana mimba ya miezi saba,‖ mmoja
kati yao alisema.
―Mama yake anasema ni mitano.‖
―Mimi nasikia saba na ametiwa mimba hiyo na kijana fulani
mchafumchafu. Sijui wasichana hawana macho?‖
―Msichana alikuwa darasa la kumi na mbili na ametiwa mimba
na kilevi kama sisi.‖
―Wazazi wa msichana huyu wamekataa kumkubalia kijana
huyo kumwoa binti yao.‖ (uk. 57).
Matokeo ya utafiti yanaonesha kwamba vitendo vya vijana wa kiume kuwahadaa na
kuwatia mimba watoto wa kike, vimeshamiri sana katika jamii zetu. Wengi wao
wakishafanikiwa kukipata wanachokitafuta, huwakana na kuwasingizia mambo
mengi, kama vile umalaya, kutokuwa na sifa ya kutembea nao, na nyinginezo. Hali
hiyo ya kukataliwa, husababisha mitanziko kwa wasichana hao. Wengine hukata
tamaa n ahata kujiua kama ielezwavyo katika nadharia ya Udhanaishi. Suala hili
linaungwa mkono na Msigala6 anayeeleza kwamba:
Wasichana wengi wana msongo wa mawazo unaotokana na
athari za mahusiano ya kimapenzi. Hata hivyo, suala la
kuachwa katika mapenzi ni safari tu kwa sababu atakuja
mwingine. Hivyo, wasichana hao wanapaswa kuwa
wavumilivu. Ukizidiwa tafuta mtu mweleze shida yako kwa
sababu kadiri unavyomwelezea mtu shida hiyo, ndivyo
unavyozitema zile sumu.
Vilevile, utafiti umebaini kwamba wakati mwingine wasichana hao huweza hata
kutoa mimba hizo, huwatupa watoto wao, na mara nyingine huchukua maamuzi ya
kujiua, kutokana na kukata tamaa ya maisha kwa kuyaona kuwa hayana maana tena
6 Mahojiano baina ya mtafiti na Bw. Selestino Helman Msigala Septemba 30, 2019.
Yalifanyika Ofisini kwa mtafitiwa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako
anafundisha masomo ya Fasihi.
117
kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi. Haya yote hutokea pale
wanapopitia wakati mgumu na kukosa majibu sahihi ya uamuzi wa kuchukua.
Aidha, kwa kuwa vijana wengi wamekuwa wakijiingiza katika vitendo hivyo pasipo
kujiandaa vema, matokeo yanaonesha kwamba wamekuwa wakisababisha watoto
wengi kutowafahamu baba zao, hivyo kupata malezi ya upande mmoja tu, yaani
upande wa mama. Matokeo yake, jamii imekuwa ikishuhudia migongano, migogoro
na kukosekana kwa maelewano baina ya mama na watoto hao, pale wanapotaka
kujua baba zao waliko. Mwandishi analisawiria suala hili kupitia kwa Vumilia,
anayemtaka mama yake amwambie ukweli kuhusu mahali aliko baba yake.
Mwandishi anasema:
Vumilia alikuwa hajapata kumwona baba yake. Jambo hili
lilimfanya apoteze wachumba, kwani wengi walimwita mtoto
wa vichakani. Hili halikuwa kosa lake. Lawama yote
ilimwendea Tegemea mama yake. Tegemea alipokuwa bado
mwanamwari alifanya kazi ya umalaya. Alikuwa ametembelea
miji mingi ya mwambao, Mombasa hadi Mtwara. Katika
kurandaranda kwake alizaa watoto kadhaa, lakini wote hao
walichukuliwa na baba zao (uk. 68).
Matokeo yanaonesha kwamba, matukio kama haya ya vijana kuwatia mimba
wasichana na kusababisha watoto kupata malezi ya upande mmoja, yamekithiri
katika jamii zetu. Jamii imefikia hata kuwaita ombaomba au watoto wa mitaani.
Hivyo, kutokana na watoto hao kukosa malezi thabiti, maisha ya wengi wao
yamekuwa ni ya kukatisha tamaa, yasiyo na matumaini, na yaliyokosa mwanga.
Aidha, imebainika kuwa watoto wanapotaka kujua baba zao waliko na mama
kushindwa kutoa majibu sahihi, huweza kusababisha migogoro na mizozo baina yao
na wazazi wao. Mfano mzuri ni Vumilia anayemwelekezea lawama mama yake,
Tegemea, kwa kushindwa kumwonesha baba yake na kusababisha mtanziko katika
maisha yake kutokana na kukosa malezi ya baba yake. Inaelezwa kwamba:
Wakati huu Vumilia aliinua uso wake kwa mara ya kwanza.
Alimtazama mama yake, halafu alinitazama mimi (Kazimoto).
―Kati yenu hakuna anayenipenda,‖ alisema. ―Maisha yangu
yaliharibika tangu zamani wakati huo hamkusema lolote.
Imekuwaje kwamba leo mmeota kuja kunitafuta na
kunichukua! Mwili nilionao ni wangu; moyo nilionao ni
wangu. Niacheni nife na masumbuko. Na nitakapokufa
118
ninawaombeni mpige ngoma, mkatangaze kote kijijini
kwamba mbwa wa masikini amelamba mchanga‖ (uk. 166).
Mwandishi anaeleza kuwa maneno haya yaliwakata maini wote wawili, yaani
Tegemea na Kazimoto. Kilichokibainika hapa ni kwamba Vumilia anaamua
kuyasema haya kwa uchungu, kwa sababu mama yake hakumpa mwongozo upasao
juu ya maisha yake kutokana na kushindwa kumwambia ukweli kuhusu mahali aliko
baba yake. Kwa upande wa Kazimoto, yeye analaumiwa kwa kuwa ni miongoni
mwa watu waliomharibia maisha yake kwa kumchezea kingono. Utafiti umebaini
kwamba hata pale ambapo Tegemea anamng‘ang‘ania Vumilia kwa kutaka
kuondoka naye, Vumilia anakataa na kusema:
―Mimi sitaki maneno mengi,‖ Vumilia anasema, ―Ninataka
kukuuliza swali moja ambalo ulikataa kunijibu tangu zamani.
Je, baba ni nani?‖ Tegemea alinyamaza. ―Basi fahamu
kwamba maisha yangu yalianzia hapo kuharibika. Kutofahamu
nani baba yangu.‖ (uk. 167).
Huu ni ukweli mchungu kwa Tegemea. Vumilia anaamua kumpasulia jipu ambalo
kwa wakati huo limekwishakuiva, baada ya kuteseka nalo kwa muda mrefu, yaani
kutaka kumjua baba yake mzazi. Hadi kufikia hatua hii, ni wazi kwamba Vumilia
amekuwa katika mtanziko mkubwa unaotokana na tatizo la malezi ya upande mmoja
tu wa mama yake, pasipo kumjua baba yake. Hili linamwia vigumu Tegemea
kuendelea kuhoji ubaya wa Vumilia wa kupata mimba na kuishi na Moyokonde
pasipo ridhaa ya wazazi wake, kwa sababu naye amezaliwa katika mazingira yasiyo
rasmi na pasipo kumjua baba yake mzazi. Hali hii inaonesha kwamba, ijapokuwa
Vumilia hafikii hatua ya kuchukua maamuzi ya kujiua kutokana na kukatishwa
tamaa na namna alivyolelewa, ukweli ni kwamba mtu akiwa katika mtanziko,
huweza kujiua kwa kuyaona maisha hayana maana kama ielezwavyo katika nadharia
ya Udhanaishi.
Utafiti umebaini kwamba aina ya malezi wapewayo watoto wetu ni mojawapo ya
masuala yanayosababisha mitanziko katika jamii. Hii ni kutokana na vijana wengi
kukengeuka misingi na kanuni za jamii husika. Hali hiyo inatokana na vijana wengi
kukengeushwa na elimu ya kimagharibi na kuharibiwa na uozo ulioletwa na
mabadiliko ya kijamii, kutokana na kumomonyoka kwa mfumo wa kimaadili wa
kijadi (Mbatiah, 1998). Mfano mzuri ni Manase na Kazimoto ambao ni wasomi wa
119
Chuo Kikuu lakini wanashindwa kufikia matarajio ya maisha yao; badala yake, kwa
sababu ya umalaya wao, wanakiambukiza kizazi chao ugonjwa wa zinaa walioupata
kutoka kwa Pili. Matokeo yake, wanazaa kizazi kibaya na kusababisha mitanziko
kwao wenyewe na kwa familia zao. Kutokana na mitanziko hiyo, Kazimoto anaamua
kujiua kutokana na kukata tamaa na kwa kuona kuwa, huo ndio uhuru kwake kama
ielezavyo nadharia ya Udhanaishi.
Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo, imebaini kwamba kutofautiana kwa
mitazamo ya wazazi katika malezi huweza kusababisha mitanziko kwa watoto wao.
Hii ni kwa sababu watoto hao hupata wakati mgumu wa kujua upande sahihi wa
kuegemea, kutokana na kujengewa tabia tofauti na wazazi wao. Kutokana na hilo,
mwandishi anaibua mitazamo mikuu miwili inayojitokeza katika riwaya hii
kuhusiana na suala la malezi ya watoto. Mtazamo wa kwanza, ni malezi ya
kuwadekeza, kuwaengaenga na kuwatimizia watoto kila wanachohitaji. Malezi ya
namna hii tunayapata kwa Tumaini kutoka kwa wazazi wake — Kapinga na
Muyango. Mtazamo wa pili, ni malezi ya ukali, vitisho, ukatili, kuwachunga na
kuwafuatilia sana. Mfano mzuri ni familia ya Kasala na Mungere. Matokeo
yanaonesha kwamba kutofautiana kwa mitazamo ya namna ya kuwalea watoto,
ndiko kunakosababisha mitanziko katika makuzi na malezi yao, kwani mabadiliko
yao kitabia hujengeka kadiri wanavyopewa aina fulani ya malezi.
Mwandishi anasawiria aina ya malezi anayoyapata Tumaini kutoka kwa wazazi
wake, hususani baba yake, yanavyochangia katika kuharibika kwa tabia yake.
Anasema:
… alikuwa bado mtoto mdogo, alitunzwa vizuri. Alitafutiwa
mvulana mdogo wa kumtunza kwa mshahara. Tumaini alikua
kwa kuengwa. Alinunuliwa vijigari vidogo vidogo vingi; kila
alicholilia alipewa. … Muyango alipokuwa akifanya kosa la
kumpenda Tumaini kupita kiasi, Kapinga alifanya kosa la
kujali sana Tumaini atarithi nini. … Hivyo basi, ndivyo
Tumaini alivyotunzwa; ndivyo alivyokua … Tumaini
alipokuwa akipigwa na walimu alizoea kuwatukana
―Washenzi ninyi! Baba hajapata kunipiga! Mna haki gani
ninyi ya kunipiga!‖ (kur. 11 - 12).
Dondoo hili linaonesha namna wazazi wa Tumaini wanavyotofautiana kimtazamo
katika kumlea mtoto wao. Kutofautiana huko ndiko kunakosababisha Tumaini kuwa
120
na tabia mbaya kiasi cha kuwadharau na kuwatukana hata walimu wake kwa madai
kwamba, hata baba yake mwenyewe huwa hampigi. Kauli hii inatopa picha kwamba,
kuharibika au kujengeka kwa tabia ya mtoto huchangiwa sana na malezi ayapatayo
kutoka kwa wazazi wake. Malezi hayo, wakati mwingine, husababisha mkinzano wa
mawazo ambayo humpa wakati mgumu mhusika wa kuchagua la kufanya na
humkatisha tamaa. Muyango anathibitisha kutofautiana na Kapinga katika suala la
malezi ya Tumaini, hususani katika suala la urithi wa mali, anapomwambia Tumaini
hivi:
… funguo hizo hapo mezani. Utalifungua sanduku la
marehemu baba yako, na humo utakuta kitabu kidogo cha
benki. Hizo zote ni pesa zako. Lakini ninaogopa kwamba
zitakuangamiza. Kumbuka kwamba mwanadamu harithi pesa;
mwanadamu hurithi hekima na busara ya babu. Mimi
mwenyewe nilitaka tukuachie nusu, na nusu nyingine
tuwapatie yatima. Watoto wote yatima ni watoto wangu.
Lakini baba yako alikataa. Nilimwambia, ―Kapinga, ni vibaya
mtoto kurithi pesa nyingi; afadhali mjengee nyumba ya kukaa
arithi. Apande mibuyu na michungwa ambayo ataendelea
kutunza kwa jasho. Ni vizuri mtoto kurithi vitu kama hivyo,
licha ya hekima na kumrithisha mtoto ni kumvisha taji la
uovu.‖ Baba yako alikataa kabisa; na kwa kuwa nilishindwa
kugeuza mawazo ya baba yako alipokuwa mzima, siwezi sasa
geuza tamshi lake. Pesa hizo zote ni zako (kur. 14 - 15).
Kitendo cha Kapinga kumwachia urithi mkubwa Tumaini kinamjengea mwenendo
na tabia mbaya kutokana na kiburi cha urithi wa mali hizo. Hali hii inampa wakati
mgumu wa ama kuuzingatia na kuufuata wosia anaopewa na mama yake, au
kuegemea upande wa malezi ya baba yake. Hatimaye, anaamua kufuata aina ya
malezi aliyopewa na baba yake na kujiingiza katika vitendo vya anasa. Anaamua
hata kuacha shule na kujiingiza katika vitendo vya kuwaharibu wasichana kwa
kutembea nao ovyo, na wengine kuwatia mimba (kur. 21 - 22).
Aidha, kiburi chake kinamweka katika wakati mgumu na kusababisha kuchukiwa na
watu wote kijijini hapo kutokana na mwenendo na tabia yake mbaya. Kutokana na
hilo, anaamua kutoroka na Anastasia na kukimbilia Shinyanga (uk. 53). Akiwa huko,
anaendelea na tabia yake mbaya ya umalaya, ambapo anajiingiza katika mahusiano
ya kimapenzi na malaya, Hadija, na kusababisha ugomvi baina yake na Anastasia.
121
Ugomvi huo unazidi kumpa wakati mgumu kutokana na mkinzano wa mawazo
anaoupata, hususani baada ya Hadija kumpiga risasi Anastasia (uk. 84).
Pia, Tumaini anazidi kutatizika na kukosa uamuzi sahihi wa jambo la kufanya
anapoishiwa na mali hiyo, huku akikabiliwa na hali ngumu ya maisha ambayo
hajawahi kuyapitia. Mtanziko huo unamsukuma hadi kwa Dennis, ambako anaomba
kibarua kinachomwingiza katika mtego wa majambazi, ambapo anapigwa na
kutupwa karibu na hospitali ya Shinyanga. Kitendo hiki kinazidi kumtatiza na
kumfanya ayachukie maisha, kama anavyosema yeye mwenyewe kuwa:
―Msizungumzie tena juu ya maisha. Msizungumzie juu ya kitu chochote kile. Maisha
yangu yameharibika‖ (uk. 97).
Hivyo, utafiti umebaini kuwa malezi mabaya anayoyapata Tumaini kutoka kwa baba
yake ni sababu mojawapo ya mtanziko wake. Kauli yake ya huzuni, masikitiko na
majuto anayoitoa, huku akiwa na maisha magumu, tofauti na maisha yake ya awali,
ni uthibitisho wa jambo hili. Kuhusiana na hali hiyo, mtafiti anaona kuwa Kapinga,
ndiye anayestahili lawama hizi kwa kumpa Tumaini malezi mabaya, ikiwa ni pamoja
na kumvisha taji la uovu wa mali ya urithi mkubwa, pasipo kumwandaa kwanza na
kumsababishia mtanziko katika maisha yake. Kwa kujiegemeza katika nadharia ya
Udhanaishi, imebainika kwamba Tumaini anakata tamaa ya maisha kutokana na
mtanziko unaomkabili. Hii inasababisha ashindwe kuona mwanga katika maisha
yake ya baadaye. Mtanziko huo, ndio unaomsukuma katika hatua ya kuyaona maisha
kutokuwa na maana na kukifurahia kifo chake.
Vilevile, imebainika kuwa mwandishi anasawiria aina nyingine ya malezi
inayojitokeza katika riwaya hii, ambayo ni ya ukali na vitisho. Malezi ya namna hii
ambayo ni ya kuwanyima uhuru, kuwabana na kuwachunga sana watoto, wanayapata
Leonila na wenzake kutoka kwa baba yao, Kasala. Malezi haya, siyo tu kwamba
yanawanyima watoto uhuru wao, bali yanawajengea pia mienendo na tabia ya hofu
na woga kama isawiriwavyo katika nadharia ya Udhanaishi. Mambo haya
yanawasababishia mitanziko katika maisha yao. Kauli anayoambiwa Leonila na
mama yake baada ya kubainika kwamba ana mimba ni uthibitisho wa jambo hili.
Anasema:
122
Leonila, baba yako atakuwa mkali kama simba aliyepigwa
mkuki mguuni. Hakika jambo ulilotenda si la busara. Baba
yako atakurarua vipandevipande… (uk. 6).
Maelezo haya yanasawiri tabia ya ukali wa Kasala katika kuwalea watoto wake.
Jambo muhimu ni kwamba jamii inatakiwa kuhakiki ni aina gani ya malezi
yanayofaa kutolewa kwa watoto, na nani anatakiwa kuwajibika katika suala hilo.
Matokeo yanaonesha kuwa watoto hawatakiwi kupewa malezi ya ukali, vitisho,
ukatili, na ya kuegemea upande mmoja, bali jamii nzima inatakiwa kushirikiana
katika suala hili la malezi. Hii inatokana na ukweli kwamba maelezo ya mama yake
Leonila yanaibua wazo linaloonesha kwamba mtu mmoja tu, ambaye ni Kasala,
ndiye aliyeachiwa jukumu la kuwalea na kuwadhibiti watoto wake. Mama huyu
haoneshi dalili za waziwazi za kukichukia kitendo hicho, badala yake, anasubiri
hatua zitakazochukuliwa na Kasala. Mwandishi anaelezea suala la malezi ya Kasala
kwa watoto wake kama ifuatavyo:
―... ilikuwa vigumu sana kuwapata wasichana hawa (Leonila
na Aurelia) kwa sababu baba yao – Kasala – aliwatunza kama
maji ndani ya mtungi. Siku moja alimpiga Leonila mpaka
akazirai kwa sababu ya kukawia sana kisimani. Lakini mtungi
wa Kasala ulikuwa na tundu kubwa. Maji yaliweza kupita.
Tundu liliwekwa na Mugala – mama yake.‖ (uk. 17).
Katika dondoo hili, mwandishi anakusudia kuionesha jamii kuwa malezi ya vitisho,
ukali, ukatili, na ya kuwanyima uhuru watoto, mara nyingi, siyo msingi wa
mwenendo na tabia njema kwao. Pia, suala la malezi halipaswi kuwa la mtu mmoja
pekee, bali jamii nzima inatakiwa kushirikiana. Sambamba na hilo, mwandishi
anaonesha kuwa, licha ya ukali wa Kasala, bado malezi yake yanaingia dosari
kutokana na kukosekana kwa ushirikiano katika familia yake. Utafiti umebaini kuwa
Mugala, ambaye ni mama yake Kasala, ndiye anayesababisha Leonila kupata mimba
baada ya Tumaini kumhonga ugoro na pipi, kisha, kumfanyia mpango wa kuingia
katika mahusiano ya kimapenzi naye kwa siri (kur. 19 - 20).
Hivyo, malezi ya Kasala na ya Mugala yanampa Leonila wakati mgumu wa kuamua
la kufanya kutokana na mkinzano wa mawazo anaoupata, yaani kufuata malezi ya
baba yake, au ya bibi yake. Hata hivyo, msukumo wa malezi ya bibi yake
unamwingiza katika mtanziko zaidi, inapobainika kwamba Tumaini amemtia mimba.
123
Kitendo hiki kinasababisha Kasala kukasirika na kumpa kipigo kikali. Inaelezwa
kuwa:
Kasala alichukua kamba. Alimfunga Leonila kuambatana na
mti wa mchungwa. Leonila alijaribu kukataa; lakini baada ya
muda alikuwa amefungwa tayari akingojea adhabu yake.
Kasala alikwenda kuchukua fimbo ndani ya nyumba. Kasala
alirudi, fimbo mkononi. Alimtandika Leonila fimbo mbili
matakoni (kur. 21 - 22).
Utafiti umebaini kuwa, malezi ni mojawapo ya sababu zinazochangia katika
mitanziko ya wahusika. Hii ni kutokana na kukosekana kwa uwiano mzuri wa namna
ya kuwalea. Hii ina maana kwamba watoto hawatakiwi kulelewa katika hali ya ukali,
vitisho na kuwanyima sana uhuru, kwa sababu kufanya hivyo, siyo kigezo thabiti cha
kudhibiti tabia na mienendo yao. Aidha, hawatakiwi kudekezwa na kuengwaengwa,
kwani huo pia, siyo msingi bora wa malezi, na huweza kuchangia katika kuziharibu
tabia zao na kuwasababishia mitanziko. Suala la muhimu ni kwamba, kutokana na
mwingiliano wa tamaduni, pamoja na mabadiliko ya kijamii na ya kiwakati, malezi
yanatakiwa kwenda sambamba na mabadiliko hayo pasipokuathiri utamaduni halisi
wa jamii husika. Hivyo, jamii inatakiwa kushirikiana na kuungana katika suala hili ili
kuepusha mitanziko kwa watoto wetu. Mitanziko hiyo mara nyingi huweza
kuwasukuma wahusika katika hatua ya kukata tamaa na hata kujiua kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi.
4.3.2 Sababu za Kiutamaduni
Utamaduni ni uzoefu wa kimaisha wa watu fulani unaohusisha michakato ya kijamii,
ambayo huiwezesha jamii hiyo kujielezea na kujitambulisha, pamoja na kufanya
shughuli za kila siku. Kila jamii ina utamaduni, mila na desturi zake ambazo
hutumiwa kama mojawapo ya utambulisho wake. BAKITA (2017) linaeleza kwamba
utamaduni ni mwenendo wa maisha unaohusisha asili, mila, desturi, jadi au itikadi
unaotawala katika jamii fulani; mtindo wa jumla wa maisha ya jamii fulani. Mbiti
(1969) anaeleza kuwa Waafrika wanaamini katika mila na desturi zao, ambazo
hujidhihirisha kwa njia mbalimbali, kama vile vyakula, utoaji majina, dini, nyimbo,
ngoma zao na kadhalika. Katika utafiti huu imebainika kuwa, miongoni mwa
vipengele vya utamaduni wa Kiafrika vinavyoweza kusababisha mitanziko kwa
124
wahusika ni masuala ya mila na desturi, masuala ya dini na tatizo kuhusu ndoa na
uzazi. Vipengele hivi vimejadiliwa kwa kina kama ifuatavyo:
4.3.2.1 Suala la Mila na Desturi
Miongoni mwa vipengele vya kiutamaduni vilivyojadiliwa katika sehemu hii, ni
masuala ya mila na desturi. Vipengele hivi vimejadiliwa kwa namna tatu: urithi wa
mali, utoaji wa mahari, na utani. Kuhusiana na suala la urithi wa mali za marehemu,
usiozingatia usawa na miongozo sahihi ya ugawanyaji wake, utafiti umebaini kuwa,
jambo hili huweza kusababisha mitanziko na mafarakano makubwa katika jamii.
Suala hili linajitokeza katika riwaya ya Rosa Mistika, ambapo ndugu wa Zakaria
wanaamua kugawana mali zake mara tu, baada ya kifo chake. Kitendo hiki
kinasababisha mtanziko kwa watoto wake, kwa sababu ndugu hao hawazingatii
wosia aliouacha kabla ya kifo chake, kwamba mali zote ni za mke wake, Regina,
pamoja na watoto wake. Mwandishi anaeleza:
Lakini Zakaria alikuwa mwalimu. Alifahamu kwamba
matatizo yatatokea kuhusu urithi wa mali yake. Jamaa hawa
baada ya kukosa funguo za kufungulia masanduku,
waliyapasua kwa shoka. Mle ndani walikuta shilingi hamsini
ndani ya bahasha iliyokuwa imeandikwa jina la Regina juu.
Katika sanduku jingine walikuta kijibarua kidogo, nacho
kilieleza habari yote kuhusu watu watakaorithi vitu. Zakaria
aliandika zamani (uk. 96).
Utafiti umebaini kuwa, licha ya Zakaria kuacha wosia unaonesha warithi wa mali
zake, ndugu zake hao wanaugomea kwa madai kwamba haukuandikwa naye.
Matokeo yake, wanaendelea na mpango wao wa kugawana mali hizo na kusababisha
mtanziko kwa watoto wa marehemu. Mwandishi analithibitisha hili anaposema:
Hawa jamaa walirithi. Walirithi hawa jamaa. Walirithi,
walirithi. Jamaa waligawana vitu. Walirithi kila kila
kilichokuwa ndani ya nyumba. Walirithi michungwa na
miembe. Walirithi migomba yote. Walirithi paka na mbwa.
Walirithi majani yaliyokuwa juu ya paa, na miti yote
iliyofanya nyumba isimame. Walirithi mashamba yote.
Walirithi kuku; walirithi hata mbolea ya ng‘ombe. Walirithi.
Hawa jamaa walirithi. Lakini hapakuwa na mtu mmoja
aliyeweza kusema atamchukua mtoto fulani amtunze. Badala
yake walimdai John alipe mahari ili pia wagawane (uk. 96).
125
Kitendo kinachofanywa na ndugu wa Zakaria kinawakera, kinawakanganya na
kuwachanganya sana watoto wake, kwa kuwa wanapata wakati mgumu na hawajui
jambo la kufanya. Hii ni kwa sababu hawahusishwi kabisa katika mgao huo na kila
wanachogusa wanaambiwa siyo mali yao. Matokeo yake wanaachwa katika
mtanziko, kwa sababu hakuna hata mmoja miongoni mwa ndugu hao, anayetaka
wajadili namna ya kuwalea. Mwandishi wa riwaya hii pia, anaonesha kukerwa na
kitendo hicho. Ndiyo maana analirudiarudia neno ‗walirithi‘.
Hata hivyo, utafiti umebaini kuwa pamoja na mitanziko hiyo, si kila mhusika
anayeipitia huchukua maamuzi ya kujiua, bali wengine huistahimili na kuendelea na
maisha yao kama kawaida. Mfano mzuri ni Flora, ambaye ni mdogo wake Rosa
Mistika. Matokeo yanaonesha kuwa, msichana huyu licha ya kupitia changamoto
nyingi katika maisha yake, zilizomsababishia mitanziko mbalimbali, bado
anaendelea kupambana na maisha yake na hachukui maamuzi ya kujiua kama ilivyo
kwa dada yake, Rosa Mistika. Hii inaonesha kwamba wahusika wengine, kama vile
Rosa Mistika huamua kujiua kutokana na udhaifu wao wenyewe, kama anavyoeleza
Zakaria katika ukurasa wa 98, anapotoa sababu za kujiua kwa Rosa Mistika.
Aidha, katika kulielezea zaidi suala hili la urithi katika jamii ya Wakerewe, Bununja7
anasema:
Katika jamii yetu masuala ya urithi hususani miaka ya nyuma
lilikuwa jambo la kawaida sana. Urithi huo ulikuwa ni wa
mwanamke mjane kurithiwa na jamaa za marehemu na urithi
wa mali za marehemu. Kwa upande wa kurithi wajane, suala
hilo kwa sasa limepungua sana. Hii ni kwa sababu mara nyingi
mwanamke mjane apatapo taarifa ya kurithiwa na jamaa hao,
hukimbia na kuiacha nyumba yake. Kwa upande wa mali za
marehemu, hizi zilirithiwa na jamaa za marehemu pamoja na
watoto wa kiume wa marehemu. Kwa Wakerewe mke wa
marehemu na watoto wa kike hawakurithi chochote. Jamii
hiyo iliwachukulia kuwa, wao ni wapita njia na kwamba
wataondoka na kwenda kuishi sehemu nyingine baada ya
kuolewa. Aidha, mali nyingi za marehemu zilirithiwa na
7 Mahojiano baina ya mtafiti na Bi. Rozina Mugabe Bununja Desemba 18, 2019.
Yalifanyika katika Kijiji cha Namagondo kisiwani Ukerewe. Bi. Rozina Mugabe
Bununja ni mwalimu wa Shule ya Msingi Mwitongo iliyoko katika kata ya
Namagondo.
126
ndugu wa marehemu na mara nyingi suala hili lilizusha
ugomvi mkubwa katika familia na ukoo kwa jumla. Watoto
wa kiume walirithi mashamba na baadhi ya mali za
marehemu. Ili kutatua suala hili, mara nyingi mzee wa ukoo
alihusika katika kulishughulikia na kulitafutia ufumbuzi.
Kwa mujibu wa Bununja, masuala ya urithi katika jamii ya Wakerewe, hususani
urithi wa mali bado yapo. Mara nyingi ndugu wa waliofiwa, hung‘ang‘ania mali
zilizoachwa na marehemu. Jambo hili husababisha mizozo na migogoro katika
familia na ukoo wa marehemu. Mizozo na migogoro hiyo mara nyingi ndiyo
husababisha mitanziko kwa wahusika na kwa jamii kwa jumla. Jambo muhimu hapa
ni kwamba kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi, wakati mwingine
mitanziko hiyo husababisha wahusika kukata tamaa na hata kuamua kujiua.
Tofauti na inavyosawiriwa katika riwaya ya Rosa Mistika, ambapo ndugu wa Zakaria
wanarithi mali zote za marehemu na kusababisha mtanziko kwa watoto wake,
ijapokuwa wao hawajiua, suala hili la urithi wa mali linasawiriwa kwa namna tofauti
katika riwaya ya Kichwamaji. Katika riwaya hii, mwandishi anaonesha kuwa suala la
urithi wa mali likizingatiwa na kufanyika vizuri, siyo lazima liwe sababu ya
mitanziko katika jamii, bali mali hiyo inaweza kutumika katika kutatua matatizo
makubwa yanayomkumba mhusika. Kwa mfano, Kamata anaitumia mali ya urithi
kulipia mahari kubwa aliyopangiwa na wazazi wa Matilda, inayolenga kumkomoa
kwa sababu, wazazi hao, hawapendi binti yao aolewe na Kamata. Mwandishi
anasema:
Mwishowe wazazi wake walikubali, lakini moyoni kitu fulani
kilikuwa bado kikiwachoma. Kwa kutaka kumkatisha tamaa
Kamata walidai mahari kubwa sana. Kamata alikuwa tayari
kulipa, kwani baba yake alipofariki alimwachia pesa nyingi
kutokana na kazi ya uvuvi‖ (kur. 47 - 48).
Katika dondoo hili, mwandishi anakusudia kueleza kuwa mali ya urithi siyo haramu,
bali uharamu wake unatokea pale ambapo mhusika huamua kuitumia ovyo tofauti na
utaratibu. Hili linathibitishwa na mwandishi kupitia kwa Kamata, ambaye licha ya
kurithi pesa nyingi, pesa hiyo haikumtumbukiza katika anasa, bali aliitunza na
hatimaye, ilimsaidia katika majukumu mengine ya kijamii, likiwamo suala la kulipia
mahari. Hivyo, kulingana na utafiti huu imebainika kuwa mali ya urithi inaweza
kusababisha mitanziko na hata kumfanya mhusika akate tamaa na kuamua kujiua
127
kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi. Kwa upande mwingine, mali
hiyo inaweza kutumika katika kutatua matatizo mbalimbali na kumwepusha mhusika
na mitanziko katika maisha yake.
Pia, suala la urithi wa mali linajitokeza katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo.
Jambo kubwa linalojadiliwa ni kwamba suala la urithi lisipowekewa misingi imara,
huweza kumletea mrithi matatizo makubwa, na hata kumsababishia mtanziko.
Mwandishi anaelezea namna wazazi wa Tumaini wanavyomrithisha mtoto wao pesa
nyingi pasipo kumwachia miongozo imara ya namna ya kuitumia. Matokeo yake
Tumaini anaitumia pesa hiyo kwa anasa na kusababisha migongano na migogoro
baina yake na jamii yake kama inavyoelezwa katika ukurasa wa 14 na 15.
Matokeo yanaonesha kuwa Tumaini mwenyewe akiwa katika mazungumzo na
Dennis na mama Resi, anakiri kwamba pesa za urithi alizoachiwa na wazazi wake,
ndizo zilizomharibia maisha yake na kumsababishia mtanziko. Mama Resi kwa
upande wake, anaona kwamba urithi wa Kiafrika haufai kwa sababu huwaacha
watoto wa marehemu bila kitu chochote na huwasababishia mitanziko. Haya
yanabainishwa katika mazungumzo yao kama ifuatavyo:
―Mimi ninafahamu kitu kilichokufanya ukawa na maneno
mengi namna hii,‖ Dennis alisema.
―Ni kitu gani?‖ Tumaini aliuliza.
―Pesa za urithi ndizo zimekufanya ukawa na maneno mengi
namna hiyo. Zamani ulikuwa mnyamavu ajabu.
―Wewe unafikiri nini juu ya urithi?‖ Tumaini aliuliza.
―Urithi wa Kiafrika haufai,‖ Mama Resi alidakia. ―Mtu akifa
jamii za marehemu wanachukua mali yote na kuwaacha
watoto bila kitu chochote.‖
―Mimi pesa zangu zimo benkini. Na atakayerithi ni mtoto
wangu, au labda watoto wangu,‖ Dennis alisema.
―Dennis,‖ Tumaini alisema, ―ninashangaa kuona kwamba
mawazo yako yanapingana. Mara unasema kwamba pesa za
urithi ndizo zinaniharibu, mara kwamba watoto wako ndio
watarithi kila kitu.‖
―Wewe Tumaini zimekuharibu kwa sababu ulikuwa peke yako
na pesa ulizorithi zilikuwa nyingi,‖ Dennis alijibu.
―Hata mimi ninafikiri hivyo,‖ Mama Resi aliingia ndani.
―Hata mimi nakubali kwamba pesa za urithi ndizo
zimeniharibia maisha yangu…‖ (uk. 80).
128
Dondoo hili linaonesha namna pesa za urithi zilivyo na madhara na zinavyoweza
kusababisha mtanziko kwa mhusika. Hata hivyo, tasinifu hii inaona kuwa madhara
hayo yanaweza kutokea iwapo pesa hizo hazitatumika kwa umakini na kwa
uangalifu. Mfano mzuri ni Tumaini ambaye baada ya kukengeuka maagizo na
miongozo aliyopewa na mama yake ya namna ya kuitumia pesa hiyo, anakata tamaa
ya maisha yake kutokana na mtanziko anaoupata. Mtanziko huo ndio unaomsukuma
katika mchakato wa kujiua kwake kutokana na kukata tamaa ya maisha kwa kuyaona
kuwa, hayana maana kama ielezwavyo katika nadharia ya Udhanaishi.
Ulipaji wa mahari ni suala lingine linalosawiriwa na mwandishi katika riwaya teule,
ambalo huweza kusababisha mtanziko kwa wahusika. Mtanziko huo huwapata
kutokana na wazazi wa mwolewaji kupanga mahari kubwa, hasa pale wanapotaka
kumkomoa mwoaji. Kwa mujibu wa TUKI (2014), mahari ni mali au fedha
inayotolewa na mwanamume kupewa mwanamke au wazazi wa mwanamke
anayetaka kumwoa. Kulingana na mila na desturi nyingi za Kiafrika, ikiwamo
Tanzania, hususani kwa jamii zinazofuata mfumo dume, mtoto wa kike kabla ya
kuolewa, hulazimika kulipiwa mahari. Jukumu la ulipaji wa mahari hiyo huwa ni la
jamaa wa mwoaji au mwanaume na hulazimika kulipa mahari hiyo kwa kuzingatia
makubaliano ya familia ya mwolewaji. Mahari hiyo hutolewa kama ishara ya
shukrani au zawadi kwa wazazi wa binti anayeolewa. Pia, huwa ni amana kwa
wazazi na ukoo mzima wa binti anayeolewa. Mahari hiyo huhusisha vitu mbalimbali,
ikiwa ni pamoja na wanyama, vifaa vya kazi, pamoja na hela. Wakati wa utoaji wa
mahari hiyo, watu teule wa ukoo hualikwa kushiriki katika kikao cha kuamua
kiwango cha mahari inayotakiwa kutolewa. Kuwapo kwa watu hao ni muhimu ili
maamuzi yanayoafikiwa yasitawaliwe na tamaa za kibinafsi (Wango, 2009). Kwa
msingi huo, kiwango hicho mara nyingi huwa si cha juu sana bali huendana na
uwezo wa aila husika.
Reed (1975) anaeleza kuwa desturi ya kulipa mahari ilianza pale jamii za jadi
zilipoanza kufuga mifugo, hususani ng‘ombe. Wakati huu, wanaume walikuwa na
hamu kubwa ya kutambuliwa kama baba wa watoto wa wake zao. Anaongeza kuwa,
baada ya muda, wanawake walianza kuwa chini ya mamlaka ya wanaume. Kwa hiyo,
wanaume pia, walianza kumiliki watoto waliozaliwa na wake waliowalipia mahari.
Kutokana na hilo, mume alilazimika kumlinda na kumdhibiti mke wake ili amzalie
129
watoto alio na uhakika nao kuwa ni damu yake na wawe warithi halali. Hivyo,
kulingana na mila na desturi za Kitanzania na Kiafrika, kwa upana wake, tendo la
ulipaji wa mahari ndilo linalohalalisha ndoa yoyote itakayofungwa. Hata hivyo,
tendo hili lisipofanyika kwa uangalifu, huweza kusababisha mitanziko kwa
wahusika, kama anavyobainisha mwandishi wa riwaya teule.
Katika riwaya ya Kichwamaji, mwandishi anabainisha namna suala la mahari
linavyosababisha mtanziko katika familia ya Mzee Mafuru. Mtanziko huo
unasababishwa na familia ya Kabenga kupanga mahari kubwa inayotakiwa kulipwa
kabla ya Kazimoto kuanza kuishi na Sabina. Suala hili halisababishi mtanziko kwa
familia ya Mzee Mafuru pekee, bali hata kwa Sabina mwenyewe. Mazungumzo
baina ya Kazimoto na Sabina yanathibitisha jambo hili:
―Unafahamu wazazi wetu walikwenda kuandikisha vitu vya
mahari. Mpaka sasa bado hawajakubaliana ingawa
wameandikisha mbele ya padre. Nilipofika hapa ndilo lilikuwa
jambo la kwanza kuambiwa. Baba yako amedai mahari
ambayo nilikuwa sijapata kusikia. Baba pia mkaidi. Amesema
hata kama ninaweza kutoa hawezi kuniruhusu nitoe na nikuoe
wewe kwa mahari kama hayo, kama kwamba kuna uadui kati
yetu na ninyi. Kabenga ni mtu ambaye tunasikilizana sana
naye, hasa katika siku chache zilizopita. Hatuoni kwa nini
atudai mahari makubwa namna hiyo. Ndoa ni uungwana siyo
uadui.‖
―Baba ameomba kiasi gani?‖
―Ameomba shilingi elfu moja; ng‘ombe watatu, dume na jike
wawili; mbuzi watano; visu vinne, kinu, nafikiri vilevile na
mchi wake, na kitanda.‖
―Kweli, baba hawezi kudai hayo yote kama kwamba ananiuza.
Kwani anafikiri anaweza kutajirika siku moja! Mahari ni
mazuri lakini lazima yakadiriwe. Mahari yanapoteza maana
kama wazazi wakianza kupata wazo la faida vichwani
mwao…‖ (kur. 142 - 143).
Kinachoonekana katika majadiliano haya ni kwamba Kazimoto na Sabina wako
katika mtanziko unaotokana na Kabenga kupanga mahari kubwa. Suala hili linawapa
wakati mgumu ikizingatiwa kwamba Mzee Mafuru naye, licha ya kuwa anatoka
katika utamaduni sawa na Kabenga, hayuko tayari kulipa kiasi hicho cha mahari,
ijapokuwa anao uwezo wa kufanya hivyo. Sabina, kwa upande wake, haoni sababu
ya baba yake kupanga mahari kubwa, kwa kuwa suala la mahari halitakiwi hulenga
katika kuwapa faida wazazi.
130
Ifahamike kwamba katika jamii nyingi za Kiafrika, kushindwa kulipa au kukamilisha
mahari huweza kusababisha mhusika kunyimwa ridhaa ya kukaa na binti huyo, au
kuzuiliwa kabisa kuendelea na michakato mingine ya ndoa. Itokeapo hivyo,
wahusika huwa katika mitanziko na huweza hata kupata msongo wa mawazo. Hali
hiyo huweza hata kusababisha wengine kukata tamaa na hata kujiua kama
inavyoeleza nadharia ya Udhanaishi, kwa sababu hukosa matumaini na mwanga wa
maisha yao ya baadaye. Matokeo yanaonesha kuwa suala hili linampata Moyokonde
na linamsababishia mtanziko, ambapo kutokana na kushindwa kulipa mahari ili
kuhalalisha ndoa yake na Vumilia, mama yake Vumilia anaamuru mtoto wake
asiendelee kuishi naye. Hili linajitokeza katika mazungumzo baina ya mama yake
Vumilia na Moyokonde, kama ifuatavyo:
―Wewe ndiye umemwoa binti yangu?‖ Alimuuliza
Moyokonde.
―Ndiyo.‖ Moyokonde alijibu kwa unyenyekevu.
―Ulifika nyumbani kuleta posa?‖
―Hapana.‖
―Unafikiri Vumilia ameanguka kutoka angani?‖
―Hapana.‖
―Basi fahamu kwamba Vumilia alizaliwa. Ukifahamu hivyo
fahamu pia kwamba mama yake amekuja sasa kumchukua.‖
―Kusema haki sasa Vumilia nimekwisha mpenda, vile
kwamba siwezi kuishi bila yeye. Kama mkitaka kumchukua
basi nichukueni na mimi.‖ (uk. 173).
Majadiliano haya yanaonesha jinsi Moyokonde anavyopata mtanziko anapoambiwa
kwamba hapaswi kuendelea kuishi na Vumilia. Yote hayo yanatokana na
Moyokonde kukiuka mila na desturi za jamii kwa kushindwa kulipa mahari na kuishi
na Vumilia pasipo ridhaa ya wazazi wake. Hivyo, huu ni uthibitisho kwamba
kushindwa kukamilisha utaratibu wa mahari huweza kusababisha mtanziko kwa
wahusika. Matokeo yanaonesha kuwa, wakati mwingine, mitanziko husababisha
mhusika kukata tamaa ya kuishi na hata kufikia maamuzi ya kujiua kama
inavyoelezwa katika msingi wa nne wa nadharia ya Udhanaishi.
Vilevile, tatizo hili la mahari linajitokeza katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo.
Humu mwandishi anamwonesha Mulele, ambaye ni baba yake Anastasia,
akimlazimisha bintiye, Anastazia, kuolewa na Mzee Tembo. Imebainika kuwa
Mulele anampangia Mzee Tembo mahari, huku akionesha kama anafanya takrima
131
kwake kwa sababu ya wema alio anao. Suala hili linamsababishia mtanziko
Anastasia, kwani licha ya mzee huyu kuwa na umri wa miaka hamsini na yeye miaka
kumi na sita tu, vilevile hampendi. Jambo hili linabainishwa kama ifuatavyo:
―… Tembo alifika nyumbani kwa Mulele ili kufanya mpango
wa mahari na kuweka siku ya arusi…‖
―… Ndiyo maana nilikwambia ufike upesi. Sisi tu tayari
kukupa binti yetu huyu kwa sababu ya wema wako
uliotutendea. Hatutaki kuomba mahari makubwa sana.
Ng‘ombe watatu, mbuzi wawili na shilingi mia nne zatosha.‖
―Baba mkwe, asante sana, asante sana,‖ Tembo alisema kwa
unyenyekevu akipiga makofi polepole…‖ (uk. 39).
Kitendo cha Mulele kumtoa Anastasia kwa Mzee Tembo kama takrima na
kumpangia mahari pasipo ridhaa yake, kinazidi kumpa wakati mgumu Anastasia.
Matokeo yake, anaamua kukubaliana na ulaghai wa Tumaini na kutoroka naye.
Anapanga kwenda kuishi pamoja naye huko Shinyanga kama njia ya kuusaka uhuru
wake binafsi kama inavyoelezwa katika msingi wa tatu wa nadharia ya Udhanaishi.
Hii ni baada ya kushindwa kuvumilia mazonge na mikatale ya jamii yake
inayomlazimisha kufanya mambo pasipo ridhaa yake. Matokeo yanaonesha kuwa,
mara nyingi ndoa za kulazimishwa na wazazi au walezi ni chanzo komojawapo cha
mitanziko kwa wahusika na husababisha hata kujiua kutokana na kulazimishwa
kuishi na watu wasiowataka.
Kipengele kingine cha mila na desturi kinachojadiliwa na mwandishi katika riwaya
teule ni utani. Kipengele hiki pia huweza kusababisha mitanziko kwa wahusika
katika maisha yao kama taratibu zake zitakiukwa. TUKI (2014) inaeleza kuwa utani
ni taratibu za kimila ambazo zinawafanya watu kuambiana au kutendeana jambo
lolote bila ya chuki. Kwa upande wake, Mulokozi (2017) anaeleza kuwa mila ya
utani imeenea sana katika makabila mengi ya Afrika Mashariki. Aghalabu, watani
wanapokutana hutaniana kwa maneno (na hata vitendo), huku wakizingatia masharti
yanayotawala uhusiano wao wa kiutani. Anabainisha michepuo ya utani kuwa ni:
utani wa mababu au mabibi na wajukuu, utani wa mashemeji, utani wa makabila au
ya kiukoo, utani wa wanarika, na utani wa marafiki. Anaongeza kuwa kila mojawapo
kati ya michepuo hii huwa na kanuni zake, miktadha yake na mipaka yake katika
jamii zinazohusika.
132
Mara nyingi, utani huonesha uhusiano uliopo baina ya wahusika ambapo watendaji
humithilisha hali na maisha ya wahusika hao. Maelezo haya yanafanana na yale ya
Sengo (2009) anayeeleza kuwa, utani ni uhusiano wa kijamii uliojengeka baina ya
pande mbili, wenye lengo la kufurahisha, kufunza, kukosoa na kukuza uhusiano kwa
kuzingatia mila na desturi za jamii husika. Wanjala (2013) anakazia maelezo hayo
kwamba, malumbano ya watani ni maneno ya kufanyiana mzaha au dhihaka kwa
kueleza mwenendo au utaratibu wa maisha ya jamii husika. Kwa kawaida utani
huambatana na ubadilishanaji wa maneno au misemo ambayo wakati mwingine,
huonekana kama kero au matusi. Hata hivyo, mwandishi wa riwaya teule anabainisha
kuwa, utani huweza kusababisha mtanziko kwa wahusika kwa kuwa, si kila mtu
hupenda kutaniwa. Hii ni kwa sababu, mara nyingi, utani huambatana na mizaha,
kejeli na maudhi kwa kutegemeana na tukio lililopo. Kutokana na hilo, baadhi ya
watu hukosa uvumilivu na huzua migogoro, na hatimaye, huweza hata kusababisha
mhusika kukata tamaa na kujiua kama ielezwavyo katika nadharia ya Udhanaishi.
Katika riwaya ya Rosa Mistika, suala hili linasawiriwa kupitia tabia ya Zakaria, ya
kupenda utani na mizaha. Hii inasababisha mtanziko katika jamii yake kwa kuwa
utani huo, anaufanya mbele ya watu wengi kwenye msiba wa Ndalo. Zakaria
anawatania watu hao kwa kusema:
―Watu wote mliopo hapa, mnatafuta nini! Mnafikiri hapa kuna
arusi! Ondokeni hapa! Ndalo amekwisha kufa kesho ataoza!
Sitaki kusikia mtu akilia bwe! Bwe! Hapa!‖ (uk. 89).
Utani huu unafanywa na Zakaria kwenye msiba wa mtani wake Ndalo, huku akijua
dhahiri kwamba jamii hiyo iko katika majonzi, uchungu na maumivu makali kwa
kuondokewa na ndugu yao. Katika hali ya kawaida, maneno anayoyatamka yanakera
na kuudhi, hasa anaposema, ―Ndalo amekwisha kufa kesho ataoza.‖ Mwandishi
anaeleza kwamba, katika utani huo, Zakaria anavua hadi kofia yake kichwani, akiwa
amepanda juu ya kaburi na kuanza kusema:
―Uhuru wananchi! Wananchi uhuru…! Mimi, nikiwa hapa
kama mwenyekiti wa walevi, ni…‖ Zakaria hakumaliza
maneno yake kitu kama fimbo ndefu iliposimama wima juu ya
kifua chake (uk. 89).
133
Ni kweli kwamba jamii nyingi hutaniana kwa lengo la kuburudisha, kutambulisha
asili na utamaduni wa jamii fulani, pamoja na kurithisha mila na desturi za jamii.
Hata hivyo, baadhi ya watu huchukizwa na kitendo hicho kwa kuwa huambatana na
mizaha, kejeli, ubadilishanaji wa maneno na matusi makali pamoja na kukashifu.
Hili ndilo linalomtokea mtu anayemchoma mkuki Zakaria na kusababisha kifo
chake, kwani maneno yake yanathibitisha hasira kali aliyo nayo dhidi yake.
Mwandishi anaeleza kuwa baada ya Zakaria kutupiwa mshale huo, mtu mmoja
alisikika akiapa, huku akitamka majina ya mababu akisema: ―Kwa jina la Mkaka na
Kamera! Nimemuua mbwa! Mtu hawezi kudharau mji wa watu namna hii!‖ (uk. 90).
Baada ya tukio hili, ndipo inapobainika kuwa:
Zakaria alikuwa mtani wao (mtani wa ukoo wa akina Ndalo).
Na kufuatana na desturi ya Wakerewe, mtani anaweza
kumtania mtani wake wakati wowote na mahali popote
isipokuwa mahakamani. Anaweza pia kuchukua chochote
kisichozidi thamani ya mbuzi mmoja. Mtani hapaswi
kuhamaki wakati huu. Na hivyo ndivyo Zakaria alivyowatania
watani zake (uk. 90).
Kinachobainika kutokana na dondoo hili ni kwamba, kitendo kinachofanywa na
muuaji wa Zakaria kinaleta mtanziko kwa jamii, kwa sababu utani anaoufanya
Zakaria ni sehemu ya utamaduni wa jamii yake. Ndiyo maana kuuawa kwake
kunasababisha mkinzano wa mawazo, kwa kuwa haieleweki iwapo jamii nzima
inakubali na kuelewa umuhimu wa utani au la. Matokeo yake jamii hiyo inabaki
katika mtanziko, kwani hata baada ya Zakaria kuuawa, hatuoni nguvu na hatua
zozote zikichukuliwa dhidi ya mhusika wa kitendo hiki. Badala yake, jamii inazidi
kutatizwa na kukanganywa linapotokea tukio lingine la mke wa Zakaria kufa ghafla,
mara tu anaposhuhudia kifo cha mume wake (uk. 90). Mkanganyiko huu unaiweka
jamii katika wakati mgumu kwa sababu inashindwa kuamua na kujua jambo la
kufanya kutokana na mambo yanayotokea. Tunaambiwa:
Katika kijiji cha Namagondo maafa kama haya yalikuwa bado
hayajatokea hata siku moja. Watu wanne kufa siku moja! Na
wote majirani! Na watatu wakiwa wa mji mmoja! Kijiji kizima
kilijaa masikitiko (uk. 92).
Maelezo haya yanaonesha namna suala la utani linavyosababisha jamii hiyo kuwa
katika mtanziko, kwani siyo tu kwamba linasababisha kifo cha Zakaria, bali
134
linasababisha pia, kifo cha mke wake, Regina. Hii inathibitisha kuwa, wakati
mwingine, mitanziko husababisha mtu kuchanganyikiwa na kupata mshituko, ambao
husababisha mhusika kujiua au kufa kama ilivyomtokea Regina, mara tu baada ya
kifo cha Zakaria.
Vilevile, suala la utani linajitokeza katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo.
Mwandishi anaonesha kuwa, ijapokuwa utani ni sehemu ya maisha ya jamii, si kila
mtu hupenda kutaniwa au kutaniana. Hii ina maana kwamba utani huweza
kusababisha mkinzano wa mawazo, kutokana na watu wengine kukosa uvumilivu wa
mambo. Hili linajitokeza katika riwaya hii, ambapo Kasala anashindwa kuvumilia
utani unaofanywa na Makaranga na kusababisha ugomvi baina yao. Mazungumzo
yafuatayo yanasawiri jambo hili:
―…haya ni mambo ya waliosoma!‖ Kasala alijitetea.
―Sisi mambo ya Kizungu hatuyafahamu, ndiyo maana mke wa
Makaranga alikojoa ndani ya motakaa.‖
―…Mimi sitaki maneno ya kijinga kama hayo!‖ Alifoka.
―Kama wewe una akili mbona Tumaini alimpa mimba binti
yako! Tena alikuwa akilala ndani ya nyumba yako! Ndiyo
maana mama yako alikuwa mchawi!‖
―Unataka tupigane!‖ Kasala aliamka. ―Mimi sijataja jina la
mama yako! Unataka tupigane!‖
―Nani anakuogopa!‖ Makaranga alisema. Waliamka wote ili
wapigane. (uk. 36).
Dondoo hili linaonesha namna utani unavyosababisha mgongano wa mawazo kati ya
Kasala na Makaranga kutokana na Makaranga kuvuka mipaka ya utani wao. Kitendo
cha kumtania Kasala kwa kumtaja mama yake kutokana na uchawi wake,
kinamsababishia mtanziko. Matokeo yake, anachukua uamuzi mgumu wa kutaka
kupigana naye. Kinachojitokeza hapa ni kwamba, licha ya kuwapo kwa umuhimu
wa suala la utani katika jamii, ni wazi kwamba si kila mtu hupenda utani. Hii ni kwa
sababu utani una mipaka yake. Utafiti umebaini kwamba, endapo mipaka na
mazingira ya utani hayatazingatiwa, utani huo huweza kugeuka na kusababisha
mitanziko kwa wahusika. Hali hiyo, huweza hata kusababisha mizozo na migororo,
ambayo pia, huweza kuwa chanzo cha watu kukata tamaa na hata kujiua kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi.
135
Aidha, matokeo yanaonesha kuwa suala la utani kama linavyoelezwa na mwandishi
katika riwaya teule, bado lipo katika jamii yake na ni miongoni mwa vipengele
muhimu vya mila na desturi za jamii hiyo. Pia, imebainika kwamba suala hili ni
miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha mtanziko kwa wahusika, kwa kuwa
wengine kushindwa kuistahimili hali hiyo, na huweza hata kuchukua maamuzi ya
kujiua. Akithibitisha kuhusu kuwapo kwa suala la utani katika jamii ya mwandishi,
Nagane8 anasema:
Kwa sisi Wakerewe, suala la utani ni la muda mrefu sana.
Huwa tunataniana tukiwa humuhumu kisiwani. Mara nyingi
huwa tunataniana na wenzetu kutoka kisiwa cha Ukara. Katika
jamii yetu utani uko katika kila ukoo. Utani huo hufanyika
katika misiba au sherehe mbalimbali. Wakati mwingine,
watani huweza kuchukua nyama ya mbuzi au ya ng‘ombe na
kumwachia mtani wao nyama kidogo tu kwa ajili ya
kuwapikia watu waliokuja kwenye tukio husika. Hata hivyo,
akishachukua mtani mmoja, basi mwingine huwa hachukui
tena.
Kwa jumla, matokeo yanaonesha kwamba suala la utani bado lipo katika makabila
mengi ya Tanzania na unathaminiwa sana. Hii inatokana na ukweli kwamba, pamoja
na mambo mengine, utani husaidia kujenga umoja na mshikamano, udugu, na huibua
mambo mazuri na maovu yaliyopo katika jamii. Hata hivyo, matokeo yanaonesha
kwamba jamii inatakiwa kuelimishwa zaidi juu ya suala hili. Hii ni kwa sababu kama
haitakuwa na welewa wa kutosha, suala hili linaweza kusababisha mitanziko ambayo
wakati mwingine huwa chanzo cha mafarakano katika jamii. Pia, mitanziko hiyo
huweza kusababisha wahusika kujiua au hata kuwaua wenzao kama ilivyotokea kwa
jamii ya Zakaria.
4.3.2.2 Suala la Dini
Dini ni mfumo wa imani wa kuabudu na kuheshimu Muumba. Asasi hii hutawala
mfumo wa maisha ya mtu katika idara zake, kwa kuwa humwekea misingi muhimu
ya maisha. Hii inatokana na kuwa na nguvu kubwa kuliko asasi nyingine za kiitikadi,
8 Maelezo haya yalitolewa na Mzee Pantaleo Vicent Tilibuzya Nagane katika
mahojiano na mtafiti Desemba 18, 2019. Yalifanyika katika Kijiji cha Namagondo
kisiwani Ukerewe. Mzee Pantaleo Tilibuzya Vicent Nagane ni kaka mkubwa wa
Euphrase Kezilahabi.
136
kwa sababu huathiri fikra za watu. Kwa mujibu wa TUKI (2017), dini ni imani
inayohusiana na mambo ya kiroho, kwamba kuna muumba, ambaye aliuumba
ulimwengu huu na kwamba ndiye mtawala wa kila kilichomo. Mbiti (1969)
anafafanua kuwa, pamoja na ujio wa dini za Kikristo na Kiislamu, Waafrika wana
dini zao za jadi. Katika ufafanuzi wake kuhusu dini za jadi, Awolalu (1976)
anasema:
… tunapozungumzia dini za jadi ya Kiafrika tunamaanisha
imani na desturi ya dini ya asili ya Waafrika. Ni dini ambayo
inatokana na kushikilia imani za mababu wa Waafrika wa leo,
na inayoabudiwa nyakati hizi kwa namna na vivuli tofauti vya
uzito, na idadi kubwa ya Waafrika, wakiwamo wale wanaodai
kuwa ni Waislamu au Wakristo.
Waafrika huamini katika miungu yao, na kwamba jambo fulani likitokea vinginevyo
hutazamwa kama ni laana au mwiko. Kutokana na hilo, wengi wao wanapokumbwa
na majanga mazito hukimbilia katika dini zao za jadi ama dini za kigeni kwa imani
kuwa hii ndiyo asasi yenye ulinzi kamili. Kwa hiyo, dini za jadi ni imani za mababu
ambazo zinafuata miiko na maadili halisi ya taifa au kabila fulani. Matokeo
yanaonesha kuwa dini huweza kumsababishia mhusika mtanziko, hasa pale
anaposhikilia sana misingi ya imani yake na kuibua mitazamo inayokinzana baina
yake na jamii inayomzunguka.
Suala hili linajitokeza katika riwaya ya Kichwamaji na linasababisha mtanziko kwa
Sabina, kwa kuwa inamfanya aonekane mtu tofauti kulingana na mitazamo ya
kawaida ya jamii yake. Hii inatokana na msimamo wake wa kushikilia sana misingi
ya dini yake ya Kiprotestanti. Kutokana na hilo, vijana wenzake wanamwogopa na
kumtenga. Kitendo hiki kinampa wakati mgumu wa kujua hatima ya maisha yake.
Anashindwa hata kupata mtu wa kuwa naye katika mahusiano ya kimapenzi. Hii ni
kwa sababu kila mtu anamwogopa kwa namna alivyo. Jambo hili linasababisha
akose mwelekeo wa maisha yake ya baadaye, na anakata tamaa ya maisha kama
isawirivyo nadharia ya Udhanaishi. Mwandishi anathibitisha hili anaposema:
Sabina alikuwa anaogopwa na vijana wengi kutokana na
msimamo wake kwa kuwa alikuwa Mprotestanti halisi. Dini
ilimkaa sana moyoni. Wale waliomnyemelea aliwajibu kwa
misemo ya Biblia. Kweli watu waovu huogopa wacha-Mungu.
137
―Msichana mcha Mungu huyo utamwezaje?‖ Vijana
walijiuliza (uk. 101).
Ni kweli kwamba, mara nyingi, mtu aliyeshikilia sana misingi ya dini au imani yake,
hutazamwa kwa namna tofauti na watu wasiokuwa na misingi hiyo. Msimamo wa
Sabina kuhusu dini yake, ndio unaomsababishia mtanziko. Hali hiyo ya mtanziko
huweza kusababisha mhusika kujiona hafai na hastahili, hususani kwa wale ambao
huwa tofauti na msimamo wake. Msimamo huo humfanya pia, ashindwe kujua
maisha yake ya baadaye yatakavyokuwa, kwani hukata tamaa na huweza hata kujiua
kama isawirivyo nadharia ya Udhanaishi. Hii husababishwa na mhusika kutengwa
na jamii kama anavyothibitisha Sabaina anapoulizwa na Kazimoto, ni kwa nini
hapendi kuolewa, licha ya uzuri wake alionao:
―Kazimoto,‖ alianza kuzungumza. ―Kama ungefahamu taabu
ambazo nimekwishapata usingeniambia vile. Mimi nimo
katika huzuni. Usifikiri kwamba mimi sipendi kuolewa au
kwamba sipendi wanaume. Kazimoto, ni vigumu kupata
wanaume. Nilikuwa na mchumba wangu. Kijana huyo
nilimpenda kweli na nilimpa moyo wangu wote, lakini siku
moja niliona picha yake gazetini ameoa msichana mwingine.
Ninawaombea maisha mazuri. Nilipata kijana mwingine,
nilitaka kumfanya mchumba, lakini nilipokataa mambo
aliyokuwa anapenda, yeye alinitukana kwamba nilikuwa
sifahamu mapenzi na kwamba sikuwa mchangamfu. Tangu
siku hiyo sijapata kumwona tena kijana huyo. Tangu hapo
sijapata tena kijana mwenye nia.‖ (uk. 103).
Katika dondoo hili, utafiti umebaini mawili yanayomtatiza Sabina, licha ya kuwa na
hamu ya kuolewa. Mosi, udanganyifu wa vijana wengi wa kiume kuhusiana na suala
la mapenzi. Pili, ni msimamo wa dini yake, unaosababisha atengwe na vijana
wenzake na kukosa mtu wa kuolewa naye. Kitendo cha kukimbiwa na mchumba
wake kinatokana na msimamo wake wa dini unaomfanya atofautiane naye
anapomwomba afanye naye tendo la ndoa. Misingi na minyororo ya dini yake
inamnyima uhuru wa kukubaliana na kufanya kile anachokihitaji, ijapokuwa naye
ana uhitaji sawa na kijana huyo. Tunalithibitisha hili kupitia maneno ya Sabina
mwenyewe anaposema kuwa, alitamani kuishi na mwanamume, lakini hakubahatika
kumpata. Hii inaonesha kwamba Sabina yuko katika mtanziko wa muda mrefu na
amekata tamaa ya maisha yake kutokana na kukumbwa na hofu na mashaka kama
138
ielezavyo nadharia ya Udhanaishi juu ya maisha yake ya baadaye. Madai yake ni
kwamba siku atakayompata, hatathubutu kumpoteza. Anasema:
―… Lakini naona kwamba siwezi kuishi bila mume. Nikipata
mchumba sasa sijui nitampendaje! Nitamng‘ang‘ania kufa na
kupona. Siku ya kuolewa nafikiri bwana wangu nitakuwa
namlisha kwa mikono yangu mwenyewe.‖ (uk. 104).
Kinachojitokeza katika dondoo hili ni mtanziko alio nao Sabina kwa sababu ya
kufuata sana misingi ya dini na kusababisha aogopwe na kukosa wanaume. Kitendo
hicho kinasababisha akate tamaa na kuamua kuikata minyororo hiyo ya dini ili
kuutafuta uhuru binafsi kama inavyoelezwa katika Udhanaishi. Anapanga kumpa
nafasi mtu yeyote anayetaka kuwa naye katika mahusiano ya mapenzi. Hatimaye,
misingi hiyo inabomolewa kwa urahisi sana na Kazimoto, ambapo, anaanza kufanya
naye mapenzi kabla hata ya kufunga naye ndoa (uk. 104). Matokeo yanaonesha
kwamba mtu akiwa katika mtanziko, huweza kupata msongo wa mawazo, ambao
huathiri uwezo wa akili na hata kumsababisha achukue maamuzi magumu likiwamo
suala la kujiua.
Mtafiti anaamini kwamba dini ni asasi muhimu sana katika kujenga maadili ya mtu
na jamii kwa jumla. Hata hivyo, anaona kuwa misingi ya dini haitakiwi kumtenga
mtu na jamii yake, kiasi cha kusababisha aogopwe na kushindwa kufungamana nayo.
Utafiti umebaini kuwa maumivu anayoyapata Sabina kiasi cha kuogopwa na vijana
wengi, yanaonesha namna dini ilivyomweka katika mtanziko wa maisha yake.
Ndiyo maana Kazimoto anapomgusa tu, anapewa kile anachokihitaji, tofauti na
msimamo wake wa awali. Hii ni baada ya Sabina kuamua kukengeuka misingi ya
dini yake na kujitafutia uhuru binafsi wa kujiamulia mambo yake mwenyewe kama
inavyoelezwa katika msingi wa tatu wa nadharia ya Udhanaishi. Mtafiti anaona
kuwa, iwapo Sabina angebaki katika hali hiyo pasipokubadilika, angeweza hata
kupata msongo wa mawazo, ambao ungemweka katika upweke, na hatimaye,
angeweza hata kujiua au kuishi kwa kuyavumilia maumivu
4.3.2.3 Tatizo la Ndoa na Uzazi
Matatizo yatokanayo na migogoro ya ndoa na masuala ya uzazi husababisha
mitanziko katika jamii. Mitanziko hiyo hutokea pale ambapo wahusika hushindwa au
kukosa uwezo wa kuzaa, kuzaa watoto wa jinsia fulani, au kulazimishwa kuingia
139
katika mahusiano ya ndoa na watu wasiowataka. Kwa mujibu wa TUKI (2014), ndoa
ni makubaliano rasmi ya mwanamke na mwanamume kuishi pamoja kama mume na
mke. Katika jamii nyingi za Kiafrika, heshima ya ndoa hukamilika pale wanandoa
wanapopata watoto, hususani wa kiume. Aidha, ndoa huchukuliwa kama sehemu ya
faraja kwa mtu aliyefikia umri wa utu uzima.
Kimsingi, Waafrika huthamini sana watoto. Pia, thamani ya mwanamke wa Kiafrika
hupatikana kutokana na kuwa na uwezo wa kuzaa watoto, tena wengi (Temples,
1959; Wiredu, 1980; Magesa, 1999; na Mbiti, 2011). Hivyo, mwanamke mwenye
uwezo wa kuzaa huthaminiwa na kupendwa sana kwenye ndoa, ikilinganishwa na
mwanamke asiyekuwa na uwezo wa kuzaa. Kulingana na Thatiah (2018), kutoweza
kuwa na watoto huchukuliwa kuwa ni balaa na nuksi. Hii ni kwa sababu watoto
huchukuliwa kuwa baraka katika ndoa na jamii kwa jumla. Kwa mantiki hiyo, iwapo
ndoa haikubarikiwa kupata watoto kutokana na utasa au kutokuwa na uwezo wa
ujauzito, shauri hilo mara nyingi, huzungumzwa na wanaukoo ili kutafuta suluhisho.
De Beavoir (1985) anaeleza kuwa asasi ya ndoa inampa mwanamke majukumu
mawili muhimu, ambayo ni: kuzaa watoto na kuhakikisha kuwa anamtimizia mume
wake mahitaji ya kimapenzi, pamoja na kuangalia nyumba yake. Maelezo ya
mtaalamu huyu yanaonesha namna suala la ndoa na uzazi lilivyo muhimu katika
maisha.
Imebainika kuwa mtazamo wa jamii nyingi za Kiafrika ni kwamba, tatizo la kukosa
watoto au kuzaa watoto wa jinsia fulani tu, husababishwa na mwanamke hata kama
tatizo hilo litakuwa linatokana na mwanamume mwenyewe. Mambo hayo
yanapotokea, huiweka ndoa husika katika mtanziko, na hata kusababisha wakati
mwingine kuwa na migogoro na wakati mwingine ndoa hizo kuvunjika, kama
anavyoeleza Euphrase Kezilahabi katika riwaya teule.
Katika riwaya ya Rosa Mistika, mtanziko wa ndoa unaojitokeza ni baina ya Zakaria
na Regina. Mtanziko huu unahusishwa na kitendo cha Regina kuzaa watoto wa kike
tu. Kitendo hiki kinaiweka ndoa hiyo katika mtanziko, kwani Zakaria anapanga
kumwacha iwapo ataendelea kuzaa watoto wa kike. Kutokana na hilo, Regina
anakosa amani na kujiona kama mwanamke ambaye hajakamilika kwa kutokuwa na
mamlaka katika familia yake. Hii inatokana na mtazamo wa jamii nyingi za Kiafrika
140
kumchukulia mtoto wa kike kama kiumbe duni na kisichokuwa na nafasi na thamani
kubwa, kilinganishwapo na mtoto wa kiume. Mwandishi analisawiri suala hili
anaposema:
Lakini Regina tangu aolewe hakuwa na raha: alikuwa
akisumbuliwa na kuteswa na mumewe kwa kosa lisilo lake.
Regina alikuwa na watoto watano wasichana; wote wazuri
kama yeye. Matumaini yake ya kukaa pamoja na watoto hao
kama alivyoambiwa na bwanake yalikaa katika mimba ya
miezi mitano aliyokuwa nayo sasa… siyo mimba peke yake
iliyomfanya Regina asimwache bwanake; ilikuwa pia na moyo
aliokuwa nao juu ya watoto wake. Hakutaka kuachana na
watoto hao; bila yeye, mumewe alikuwa hawezi kuwatunza.
Mawazo yake yalikuwa juu ya furaha ya watoto wake katika
maisha yao ya baadaye (uk. 3).
Katika dondoo hili, tunapata mitanziko mikuu mitatu aliyonayo Regina. Mosi, hali
yake ya ndoa itakavyokuwa iwapo atazaa mtoto mwingine wa kike, tofauti na
matakwa ya mumewe. Jambo hili linampa wakati mgumu, linamtesa na kumkosesha
furaha, kwani hajui matokeo yake yatakuwaje. Pili, anatatizwa na kukanganywa na
hali ya watoto wake itakavyokuwa, kwani atashindwa kutimiza jukumu lake la
malezi. Kulingana na tamaduni nyingi za Kiafrika, jukumu la malezi ya mtoto ni la
mama. Hili linajidhihirisha kupitia misemo mbalimbali ikiwemo methali isemayo:
Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Ndiyo maana hata mtoto
anapofanya makosa, mara nyingi lawama nyingi huelekezwa kwa mama yake. Tatu,
ni kukosa furaha katika maisha yake kwa kosa lisilo lake, kwani, licha ya kumzalia
Zakaria watoto watano wa kike, bado anaonekana kutokuwa na thamani kwake
kutokana na kukosa mtoto wa kiume.
Matokeo yanaonesha kuwa mambo haya matatu, ndiyo yanayomweka Regina katika
mtanziko na yanamnyima uhuru wa kuamua la kufanya mbele ya Zakaria. Pia,
yanamkatisha tamaa ya maisha kama isawiriwavyo katika nadharia ya Udhanaishi,
na hajui maisha yake ya baadaye yatakavyokuwa. Hii inamaana kwamba, ijapokuwa
Regina haoneshi dalili za wazi za kujiua, ukweli ni kwamba yuko katika mtanziko na
ana msongo wa mawazo, ambayo ni dalili mojawapo inayoweza kusababisha
mhusika kujiua. Kimsingi, Regina anaonekana kutokuwa na furaha katika maisha
yake kutokana na vitendo anavyofanyiwa na Zakaria.
141
Ponera (2010) anaeleza kuwa furaha ni kionjo cha kisaikolojia ambacho huhusu hali
ya ukunjufu wa moyo na bashasha, ambayo aghalabu, hutokana na ridhiko la moyo
au nafsi. Aidha, anamnukuu Shaaban Robert (1954) anayeelezea dhana hiyo ya
furaha kwa kusema:
… Furaha ya kweli huja kwa akili yetu wenyewe. Twaweza
kuhuzunika hata wakati tumekaa juu ya mlima wa dhahabu na
kufurahi hata kama hatuna senti moja ya shaba mfukoni
mwetu. Nadhani kwamba furaha ya kweli huja si wakati
tuwapo matajiri au maskini; lakini ni wakati tuwezapo
kutimiza haja na faraja zetu zipasazo katika maisha yetu. Kwa
hiyo, furaha na akili au ya moyo ndiyo furaha ya kweli, tukiwa
matajiri au maskini, mjini au vijijini (uk. 13).
Ni wazi kwamba maisha ya Regina yanakosa furaha kutokana na kutokuwa na
utulivu wa moyo na akili kunakosababishwa na manyanyaso, masimango pamoja na
kipigo cha mara kwa mara kutoka kwa mumewe. Kwa hali hiyo, imebainika kuwa
kukosekana kwa furaha katika ndoa ni sababu mojawapo ya mtu kuwa katika
mtanziko kama ilivyo kwa Regina. Hata hivyo, matokeo yanaonesha kuwa pamoja
na mtanziko huo, Regina hachukui maamuzi ya haraka ya kujiua, ijapokuwa
anaonesha dalili za kukata tamaa ya maisha kama isawiriwavyo katika nadharia ya
Udhanaishi. Hii ni kwa sababu mtanziko humweka mtu katika njia panda na
hulazimika kuchagua la kufanya, ambapo kila uamuzi auchukuao mhusika huwa na
madhara kwake. Hii inayakinisha hoja iliyokwisha kuelezwa hapo awali kuwa,
mtanziko huweza kusababisha mhusika kujiua au kuendelea kuishi katika hali ya
kukata tamaa lakini kwa uvumilivu.
Hata hivyo, matokeo yanaonesha kuwa mtanziko wake unaanza kupungua mara tu,
baada ya kujifungua mtoto wa kiume na kutimiza ndoto na matamanio ya muda
mrefu ya mume wake. Suala hili linamfanya Zakaria anafurahi na kumpongeza
Regina kwa kumzalia mtoto wa kiume. Hii inasaidia kurejesha kidogo amani na
furaha katika familia yake. Anasema:
―Regina! Sasa mji huu umekuwa wako.‖ ...
Usiku huo Zakaria aliimba aleluya karibu usiku kucha. Kesho
yake alikwenda posta. Mke wake alishangaa kumwona jioni
anarudi na vitu vyote alivyokuwa ametaja. Alianza kupata
sauti. Alianza kuzungumza kwa furaha. Hata watu wa kijijini
waliona ajabu... (kur. 24 – 25).
142
Matokeo yanaonesha kuwa kuzaliwa kwa mtoto huyu wa kiume kunaikamilisha ndoa
ya Zakaria na Regina, kwani kwa Waafrika, kuzaa watoto wa kiume ni fahari kubwa
na jambo linalopewa heri na baraka zote. Furaha ya Zakaria inajidhihirisha pia,
katika maana ya jina la Emmanuel analopewa mtoto huyu. Senkoro (2006) anaeleza
kuwa katika dini ya Kikristo, Emmanuel ni jina lingine la Yesu Kristo, likiwa na
maana ya ―Mungu yu pamoja nasi‖. Imebainika kuwa jina hili lina heshima kubwa
kwa Wakristo. Hii ni kwa sababu huchukuliwa kuwa ni jina la mwana pekee wa
Mungu. Huyu, alitumwa na Mungu baba kuja duniani kuleta wokovu na ukombozi
kwa kuwapatanisha wanadamu na Mungu. Ushahidi wa hoja hii unapatikana katika
Biblia Takatifu, ambapo, katika utabiri wake, Isaya anasema: ―Tazama, Bikira
atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita jina lake Emmanuel, yaani
Mungu pamoja nasi‖ (Isaya 8: 8, 10; Mathayo 1: 23). Akielezea zaidi kuhusiana na
jina hilo, Ngassa9 anasema kuwa:
Emmanuel ni jina lenye asili ya Kilatini, yaani ―Mungu
pamoja nasi‖. Jina hili lina fundisho kubwa sana katika imani
ya Kikristo, kwani linamtambulisha Yesu kama Mungu kati
yetu. Ndiyo maana tunasema, Yesu ni Mungu na, kwa hakika,
suala hili linahitaji imani kubwa sana ili kulielewa. Ni Mungu
aliyetwaa mwili, kwani hapo mwanzo alikuwapo hata kabla ya
kuumbwa kwa ulimwengu, lakini siyo katika hali ya
kibinadamu au kimwili. Hii ni teolojia ya umwilisho
inayoonesha kwamba huyo aliyekuwapo anatwaa mwili.
Kwa msingi huu, ni dhahiri kuwa mwandishi analitumia jina hili kwa makusudi ili
kuonesha umuhimu na thamani ya mtoto huyo anayechukuliwa kama mkombozi na
mpatanishi kati ya Zakaria na Regina. Hii ni kwa sababu kuzaliwa kwa Emmanuel
anayetumiwa na mwandishi katika riwaya yake, kunamwezesha Regina kuendelea
kuishi pamoja na familia yake. Tunaambiwa kuwa matumaini yake ya kukaa pamoja
na watoto hao kama alivyoambiwa na bwanake yalikaa katika mimba ya miezi
mitano aliyokuwa nayo sasa (uk.3). Hatimaye, mimba hiyo ndiyo inayowezesha
9 Mahojiano baina ya mtafiti na Padre Ibrahimu Ngassa, yalifanyika Desemba 17,
2019 katika viunga vya Seminari ya Mtakatifu Maria huko Nyegezi. Hapa ndipo
aliposomea pia, Euphrase Kezilahabi, mwandishi wa riwaya teule. Padre Ibrahimu
Ngassa ni mlezi wa wanafunzi wanaoandaliwa kuwa Mapadre.
143
kuzaliwa kwa mtoto wa kiume na kupewa jina la Emmanuel kama ishara ya kuleta
upatanisho baina ya Zakaria na Regina. Hii inaonesha kuwa, ijapokuwa Regina
alikuwa katika mtanziko uliomkosesha furaha na ulimfanya awe msongo wa
mawazo, ambao ungeweza hata kusababisha ajiue, mtoto huyu anasaidia kuuondoa
mtanziko huo. Aidha, anasaidia kumwondoa Regina katika hali ya kukata tamaa
kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi, badala yake anakuwa huru
kuendelea kuishi kwa furaha na utulivu pamoja na watoto wake. Huu ni uthibitisho
kuwa suala la ndoa na uzazi huweza kusababisha mtanziko kwa mhusika, ambao
humpa wakati mgumu wa kuamua jambo la kufanya, kwani wakati mwingine
humsukuma mhusika katika ukingo na fikra za kujiua.
Ifahamike kwamba, kabla ya kuzaliwa kwa Emmanuel, Zakaria alimfokea Regina
kwa kumtolea kauli mbaya, za maudhi, kashifa, lawama na manyanyaso. Haya
yalimkosesha furaha katika maisha yake yote. Yalimfanya akate tamaa na kuyaona
maisha hayana maana kama inavyoelezwa katika Nadharia ya Udhanaishi. Kwa
mfano, kauli anayoitoa Zakaria baada ya kuwafukuza na kuwakimbiza vijana
wanaojifanya wanataka kununua mayai, inathibitisha mojawapo ya kauli hizo mbaya.
Mwandishi anasema:
Wale vijana walikimbia bila kuangalia nyuma. Walifikiri
bado anawafuata. Zakaria aliwasikia kwa mbali
wakimtukana.
Mshenzi, utaoza na binti zako!‖
Zakaria hakuwajibu lolote. Regina na Rosa walikuwa
wamenyamaza tu.
―Mshenzi, unanizalia wasichana tu! Unaniletea taabu
nyumbani bure tu!‖ Zakaria alifoka. Regina hakujibu;
aliogopa kumdhihaki... (uk. 23).
Regina anaamua kukaa kimya ili kumtunzia heshima mumewe na kuepusha
mitanziko zaidi katika ndoa yake. Aidha, kukaa kimya huko kunaonesha hulka
waliyonayo wanawake wengi ya uvumilivu na utii kwa waume zao. Maoni ya mtafiti
kuhusiana na ukimya wa Regina ni kwamba, yawezekana anafanya hivyo kwa
kuogopa kumdhihaki na kumdhalilisha mumewe kutokana na ujinga wake wa
kuelekeza lawama kwake, kwa kitendo cha kumzalia watoto wa kike tu, wakati
kibaiolojia, anayeamua jinsia ya mtoto ni mwanaume, na wala siyo mwanamke
(Taylor na wenzake, 1995; Allan, 2003; Mwaniki & Geoffrey, 2009). Kwa hiyo,
144
mtafiti anaona kuwa Zakaria, ndiye anayestahili lawama zote kwa kumzalisha
mkewe watoto wa kike mara zote na kusababisha mtanziko katika familia yake.
Mtanziko huo unamkatisha tamaa na anayaona maisha hayana maana kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi Hata hivyo, matokeo yanaonesha kuwa,
ijapokuwa mtanziko huweza kusababisha msongo wa mawazo na kumkatisha tamaa
ya maisha mhusika na hata kujiua, Regina anaonesha ujasiri na uvumilivu na
hachukui maamuzi ya kujiua.
Katika riwaya hii, pia, mtanziko unaosababishwa na uzazi na ndoa unajitokeza baina
ya Ndalo na Bigeyo. Wanandoa hawa wanajikuta katika mkinzano wa mawazo na
kupata wakati mgumu kutokana na kuhangaika kwa muda mrefu wakitafuta watoto
pasipo mafanikio. Hali hii inasababisha ndoa yao kukosa furaha na amani, kwa
sababu kwa asili, uimara wa ndoa na ufahari wa Mwafrika huonekana kwa kuzaa
watoto, tena wengi. Pia, imebainika kuwa uzazi ndiyo njia ya uzima wa milele, na
ugumba ni laana mbaya kuliko zote, kwa kuwa huondoa thamani ya mtu duniani.
Methali ya Kibantu inayosema: ―Nyumba ya mgumba haina matanga‖ ni uthibitisho
kwamba mgumba hana thamani katika jamii, kwa sababu ya kukosa uzazi. Hoja hii
inaungwa mkono na Shaaban Robert (2013) anayeeleza mtazamo wa Waafrika
kuhusiana na watu wasiokuwa na uwezo wa kuzaa na athari zake, anaposema:
Ustawi uliofanyika katika nchi hii tangu mwanzo wa ufalme
wangu, umeniletea heshima. Lakini ugumba umemeza
heshima na utasa umetia wimbi fahari ya Malkia. Sina mtoto
wa kurithi kiti changu cha ufalme, kutoa mashauri ya hekima
barazani kama mababu zake (uk. 3).
Mwandishi anaonesha thamani na heshima inayotokana na uzazi ambao huwezesha
kupatikana watoto wa kurithi hata kiti cha ufalme. Anaonesha mtanziko aupatao mtu
asiyekuwa na uzazi, ambapo hata heshima yake hutoweka mbele ya jamii, kwa
sababu hutazamwa kama mtu ambaye hajakamilika bado. Hii inatokana na ukweli
kwamba mtu anapooa au kuolewa, matarajio ya jamii yake huwa ni kumwona
mwanamke akiwa mjamzito mapema iwezekanavyo. Chuachua (2016) anaeleza
kuwa, kwa kawaida, minong‘ono huanza baada ya mwaka mmoja au miezi michache
tu, tangu kufunga ndoa, endapo hakuna dalili za kupatikana kwa mtoto. Matokeo
yanaonesha kuwa, minong‘ono hiyo husababisha wahusika kupata mitanziko na
hujiona kama watu duni na wasiokuwa na thamani katika jamii. Kutokana na hilo,
145
imebainika kwamba wengine hufikia hatua ya kukata tamaa na huyaona maisha
hayana maana tena kwao kama isemavyo nadharia ya Udhanaishi. Hivyo, huamua
kujiua ili kuikwepa aibu na fedhea kutoka kwa jamii inayowazunguka. Ifuatayo ni
taarifa inayothibitisha kuwa mtanziko wa ndoa na uzazi huweza kusababisha
mhusika kujiua kama inavyoripotiwa na (https://www.eatv.tv/news/current-affairs/).
Taarifa hiyo inasema:
Askari polisi wa Kituo cha Polisi, Wilaya ya Kahama, H.1363
PC Gideon Clement (miaka 30), Mkazi wa Muleba, Mkoani
Bukoba, amejiua kwa kujipiga risasi shingoni Alhamis, April
4, 2019 majira ya saa moja na nusu asubuhi akiwa kwenye
lindo mjini Kahama. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,
ACP Richard abuwao, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo,
ambapo amesema sababu za askari huyu kujiua, ni kutokana
na kutofanikiwa kupata mtoto, licha ya kuishi kwenye ndoa na
mkewe kwa kipindi cha miaka mitano. Kamanda huyo
ameeleza kuwa sababu hizo, zilibainishwa katika ujumbe
alioutuma kwa mke wake. Ujumbe huo ulisema kwamba hana
sababu za kuendelea kuishi kwa kuwa hajajaliwa kupata mtoto
na amekaa katika ndoa na mke wake, ambapo jana yake
alilalamikia sana jambo hilo na alianza kuonesha dalili kwa
kumtumia mkewe ujumbe wa simu akieleza kuhusu mali zake,
vikiwamo viwanja (www. Eatv.tv).
Hapa taarifa hii inatoa ithibati juu ya umuhimu wa suala la ndoa na uzazi katika
jamii, na namna linavyopewa kipaumbele. Aidha, taarifa hii inaonesha namna
mhusika anavyoweza kupata mtanziko na kukata tamaa ya kuendelea kuishi kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi kutokana na kukosa uzazi, na hivyo,
kuamua kujiua. Utafiti umebaini kuwa, hili ni tukio moja tu miongoni mwa mengi
yanayotokea katika jamii yanayowapata wahusika kutokana na mitanziko ya ndoa na
kukosa uwezo wa kuzaa.
Kwa upande wake, Mbiti (1969) anaeleza kuwa suala la kuoa na kuolewa kwa
Mwafrika, si hiari, bali ni la lazima. Anafafanua zaidi kwa kusema:
… therefore, it is a duty, religious and ontological for everyone
to get married; and if a man has no children or only
daughters, he finds another wife so that through her, children
(or sons) may be born who would survive him and keep him
(with the other living dead of the family) in personal
immortality (pg. 26).
146
… kwa hiyo ni jukumu la kidini na kijamii, kwa kila mmoja
kuoa au kuolewa; na kama mwanaume hana mtoto au ana
watoto wa kike pekee, atafute mke mwingine, ili kupitia
kwake, watoto (wa kiume) waweze kuzaliwa, ambao
wataendeleza ukoo wake na kumweka (pamoja na wafu
wengine katika familia) katika dhana ya uhuishwaji (uk. 26)
(Tafsiri ya Mtafiti).
Maelezo haya yanatoa picha kwamba ndoa haiwezi kukamilika mpaka mwanamke
anapoonesha kuwa na uwezo wa kuzaa. Pia, mtazamo wa Mbiti unaonesha kwamba
tatizo la kutozaa au kupata watoto wa jinsia moja husababishwa na mwanamke.
Ndiyo maana anaona kwamba mwanaume akibaini tatizo hili, anapaswa kutoka nje
ya ndoa yake na kutafuta mwanamke mwingine wa kuzaa naye watoto wa kiume.
Mawazo ya Mbiti hayatofautiani sana na ya Faustine (2017) anayeeleza kuwa, katika
jamii za Kiafrika wanandoa wasiobahatika kupata watoto, huwa hawathaminiwi
katika jamii. Aidha, mara nyingi, ndoa zao huwa hazidumu; au mwanaume huamua
kuoa mke mwingine ili kupata watoto. Hali hiyo ya kutodumu kwa ndoa hizo,
husababisha wahusika kuwa katika mitanziko, na wengine huishi kwa woga, hofu na
wasiwasi kama ielezwavyo katika nadharia ya Udhanaishi. Aidha, wengine huamua
kujiua kama suluhisho la mitanziko hiyo.
Mawazo ya Mbiti na Faustine yanaeleza mambo halisi, kwani mitazamo hiyo ndiyo
iliyoshamiri katika jamii zetu. Hata hivyo, utafiti huu unaona kuwa kushamiri kwa
mitazamo hiyo ni mwendelezo tu wa mfumo dume wa kumkandamiza mwanamke.
Mfumo huu mara zote humtazama mwanamke kama kiumbe duni na kisichokuwa na
thamani na uwezo wa kufanya lolote. Ukweli ni kwamba wanandoa wanapokosa
uzazi, wote wawili hupata mtanziko ambao huwaondolea thamani yao katika jamii.
Hivyo, hufanya jitihada mbalimbali kama vile kwenda kwa waganga wa jadi au
kutumia madawa ya asili kabla ya kwenda hospitalini, ili kupewa dawa za
kufanikisha tatizo lao (Kitereza, 1980). Hufanya hivyo kwa kuamini kuwa, uganga
ndilo suluhisho la matatizo mengi yanayomsibu mtu, likiwamo tatizo la uzazi.
Tatizo hili la uzazi ndilo linalowakumba pia, Ndalo na Bigeyo katika riwaya ya Rosa
Mistika. Wao, wanahangaika na kwenda kwa waganga mbalimbali, huku wakipoteza
pesa nyingi ili kutafuta dawa ya uzazi. Mahangaiko yao yanatokana na mtanziko
walionao wote wawili kutokana na kukosa watoto na kukosa thamani katika jamii.
Mwandishi anasema:
147
Ndalo pamoja na Bigeyo walikuwa wanakula nyama ya kuku
hali wanakimbia kuzunguka nyumba. Ndalo na mkewe
walikuwa wanasumbuliwa na jambo moja – uzazi. Walikuwa
wamekwishapoteza fedha nyingi kutafuta dawa ya uzazi.
Mwaka mmoja walikwenda nchi za mbali kuitafuta. Walirudi
na nusu debe la mizizi ya miti. Mizizi ilikwisha na wala
hapakuwa na alama yoyote ya Bigeyo kupata mimba. Mwaka
uliofuata walikwenda pengine. Huko walimkuta mganga
mmoja wa kienyeji aliyewaambia kwamba Bigeyo alikuwa
hazai kwa sababu alipokuwa bado msichana alikataa
kuwabeba wadogo zake mgongoni. Dawa ya uzazi sasa
ilikuwa lazima kupata mkojo wa wadogo zake ajimwagie
mgongoni. Lakini jambo hili halikuwa rahisi; wadogo zake
sasa walikuwa watu wazima. Waliporudi nyumbani, haukupita
muda mrefu mdogo wake akamtembelea. Bigeyo alifurahi
sana. Wakati wa kulala ulipofika alimpelekea mdogo wake
kopo. Alimwambia kwamba katika kijiji hicho ilikuwa hatari
kutoka nje wakati wa usiku. Alimwambia akojoe ndani ya
kopo. Asubuhi na mapema Bigeyo alichukua lile kopo na
kwenda kujimwagia mgongoni. Mwaka ulipita. Bigeyo
alipokuwa anashiba sana mumewe alimuuliza kama amepata
mimba. Miaka miwili ilipita; hapakuwa na alama yoyote kwa
Bigeyo kuchukua mimba…. Mwishowe, walikata shauri
kwenda Kaskazini, huko walimkuta mganga mwingine
aliyewaambia wale nyama ya kuku mweupe wakikimbia
kuzunguka nyumba ili kutakasa mji (kur. 17 - 18).
Dondoo hili linaonesha umuhimu wa uzazi, na namna unavyowapa wakati mgumu
Ndalo na Bigeyo. Furaha ya ndoa yao inakosekana kwa sababu ya kukosa uwezo wa
kupata watoto. Wanahangaika huku na kule ili kulinda heshima yao, kwani uzazi ni
njia pekee ya kumletea mtu heshima na thamani katika kuendeleza familia na ukoo
wake. Hatimaye, uvumilivu wao unafika mwisho. Kama inavyoeleza katika nadharia
ya Udhanaishi, wanakata tamaa kutokana na maisha yao ya kukosa matumaini ya
kufanikiwa. Kiashiria cha wazi cha kukata tamaa huko ni kauli ya Bigeyo (uk. 18)
kwamba kitendo cha wao kukosa watoto ni laana. Hata hivyo, matokeo yanaonesha
kuwa, pamoja na mtanziko wa ndoa na uzazi wanaoupata, Ndalo na Bigeyo
hawachukui maamuzi ya kujiua, bali wanaendelea kuishi kwa uvumilivu, huku
wakiwa wamekata tamaa.
4.3.3 Sababu za Kiuchumi
Miongoni mwa matatizo ya kiuchumi yanayosababisha mtanziko ni umaskini, hali
ngumu ya maisha, na ukosefu wa kazi. BAKITA (2017) linaeleza kuwa uchumi ni
mfumo wa uzalishaji mali wa nchi kwa shughuli za biashara, viwanda na kilimo,
148
pamoja na matumizi ya mali hizo. Kwa maneno mengine, uchumi ni jumla ya
shughuli zote za binadamu zinazolenga kutosheleza mahitaji yao. Unajumuisha njia
za uzalishaji, usambazaji, ugawaji na matumizi ya bidhaa na huduma. Hali ya
uchumi inapokuwa mbaya, huweza kusababisha mtu au taifa kushindwa
kujitosheleza katika mahitaji yake, na hata kusababisha mtanziko wa namna ya
kuyaendesha maisha kwa jumla. Mwandishi wa riwaya teule anabainisha namna
sababu za kiuchumi zinavyoweza kuwa chanzo cha mitanziko kwa wahusika.
Katika riwaya ya Rosa Mistika, umaskini na hali ngumu ya maisha katika familia ya
Zakaria vinasababisha mtanziko kwa Rosa na mama yake, Regina. Hali hiyo
inawatokea mara tu baada ya Rosa kufaulu masomo yake ya darasa la saba na
kutakiwa kwenda kujiunga na sekondari ya Rosary. Barua inayoonesha mahitaji
anayotakiwa kwenda nayo shuleni, inazidi kumweka katika wakati mgumu zaidi
anapojibiwa na Zakaria kwamba hana hela hiyo (uk. 9). Uduni wa maisha yao
unasababisha Rosa kuchelewa kuripoti shuleni kwa muda wa mwezi mmoja. Suala
hili linachangiwa pia na kitendo cha Zakaria kuiba fedha iliyoandaliwa kwa lengo
hilo na kwenda kuitumia katika masuala ya ulevi (uk. 11). Mwandishi anaeleza
kuwa:
Zakaria alikuwa mwalimu zamani, lakini alifukuzwa kazi kwa
sababu ya ulevi. Jirani zake walisema alijali pombe kuliko
watoto. … Sasa watoto walikuwa shuleni, heko kwa mama
yao (uk. 11).
Zakaria anaonesha kutowapenda wala kuwajali watoto wake. Hataki kuwalipia ada
ya shule kwa madai ya kukosa pesa, lakini siku zote anazo za kunywea pombe.
Kitendo cha kuiba fedha iliyoandaliwa kwa ajili ya ada ya Rosa kinawasababishia
mtanziko Rosa na mama yake, kwani wanapata wakati mgumu wa namna ya
kulitatua tatizo hili (uk. 16). Wanapoamua kubuni biashara ya kuuza mihogo
(udaga), hawafanikiwi kwa sababu ya kukosekana kwa wanunuzi. Ugumu
wanaoupata kutokana na kushindikana kwa biashara hiyo unawasukuma kubuni
biashara nyingine, ambayo ni ya kuuza pombe ya mihogo iitwayo mapuya.
Hatimaye, wanafanikiwa kupata pesa hiyo (uk. 18).
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa umaskini na hali ngumu ya maisha hukatisha
tamaa na huweza kumsababishia mhusika mtanziko. Hii ni kwa sababu mtu huyo
149
hujikuta katika wakati mgumu na hushindwa kujua la kufanya. Matokeo yake,
huweza hata kujiingiza katika vitendo vya ulevi kama njia ya kuondoa msongo wa
mawazo unaokuwa unamkabili. Suala hili linasawiriwa na mwandishi anapoelezea
hali ngumu ya maisha ya Zakaria. Kutokana na hali hiyo anashindwa hata kujenga
nyumba ya maana na kuamua kuishi maisha ya ulevi. Mwandishi anasema:
Zakaria alikuwa ameshindwa hata kujenga nyumba ya maana.
Katika nyumba alimokuwa akilala sasa pamoja na watoto
wake, nyota zilikuwa zikiwashangilia kila siku usiku. Tangu
Ijumaa mpaka Jumapili Zakaria alikuwa anakwenda kunywa,
na siku nyingine za juma alijifanya mgonjwa kitandani (uk. 6).
Kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi, dondoo hili linaonesha namna
Zakaria alivyokata tamaa na kuamua kujiingiza katika vitendo vya ulevi. Hii ni
kutokana na umaskini na hali ngumu ya maisha yake. Mambo haya yanamweka
katika mtanziko na kushindwa kupata majibu sahihi ya maisha yake. Mwandishi
anaeleza zaidi kuhusu umaskini na hali ngumu ya Zakaria, anaposema, ―… usiku huo
mvua ilinyesha kwa wingi sana. Lo! Nyumba ilikuwa kama mti. Ilivuja
kustaajabisha…‖ (uk. 13). Imebainika kwamba mambo haya yanachangiwa na tabia
yake ya kuendekeza ulevi na uvivu kwa visingizio vya kuumwa. Hatimaye, anajikuta
katika mtanziko unaomkatisha tamaa ya maisha yake. Hata hivyo, hachukui
maamuzi ya kujiua kama iwatokeavyo watu wengine, ambao husukumwa katika
hatua ya kujiua kama suluhisho la kumaliza matatizo yao, wanapokuwa katika hali
kama hiyo.
Hii ndiyo picha halisi ya maisha ya familia ya Zakaria, anayoisawiri mwandishi wa
riwaya hii. Mateso, mahangaiko na maumivu ya familia hii yanasababishwa na tabia
ya Zakaria ya kutumia pesa zake nyingi katika ulevi. Anashindwa kuwajibika na
kutimiza majukumu yake kama baba wa familia. Mtafiti anaamini kuwa, kama
angeitumia pesa hiyo kwa uangalifu, angeweza hata kujenga nyumba nzuri ya kuishi
na familia yake. Hata hivyo, matokeo yanaonesha kwamba kwa jamii ya Wakerewe
150
kama zilivyo jamii nyingine za Tanzania, kwao suala la unywaji wa pombe ni jambo
la kifahari. Hili linathibitishwa na Kadala10
kama ifuatavyo:
Wakerewe wana kawaida ya kunywa pombe na huwa
wanalewa sana. Kwa Wakerewe pombe ni jambo la kawaida
na halina uzito wala makatazo yoyote. Ndiyo maana hata
katika riwaya ya Rosa Mistika, mwandishi mwenyewe
ametusawiria kwamba pombe imetumika kama nyenzo ya
kupatia uchumi ili watoto (Rosa Mistika) waende shule au
wasome.
Matokeo yanaonesha kwamba katika jamii nyingi za Kiafrika, pombe huchukuliwa
kama kiburudisho na kitu cha fahari na heshima kubwa miongoni mwao. Hata
hivyo, unywaji usio wa kistaarabu na unaozidi kiwango, humpoteza na kumharibu
mtu na, wakati mwingine, huweza hata kumfanya kuwa mtumwa wake. Mambo
haya, ndiyo yanayojitokeza kwa Zakaria, kwani anashindwa hata kutimiza
majukumu ya kuilea familia yake, kwa sababu ya unywaji wa pombe unaozidi
kipimo. Anajali pombe kuliko familia yake. Mbali na hilo, anathubutu hata kuiba
pesa iliyoandaliwa kwa ajili ya Rosa kwenda shule. Matokeo yake, anaitumia pesa
hiyo katika ulevi na nyingine anawanunulia marafiki zake pombe (kur. 18 - 19). Kwa
kufanya hivyo, anaisababishia mitanziko familia yake na kuikosesha amani, furaha
na upendo.
Vilevile, masuala ya umaskini na hali ngumu ya maisha yanajitokeza katika riwaya
ya Kichwamaji. Humu yanasababisha mtanziko katika familia ya Mzee Mafuru.
Umaskini wa familia hii unakuwa ndicho chanzo cha mtanziko wa Rukia kutokana
na familia hii kumwomba Manase aishi naye ili kuendelea na masomo yake. Hii ni
baada ya kukosa mahali pa kuishi. Kitendo hiki kinamsababishia mtanziko kutokana
na usumbufu wa Manase wa kumtaka kimapenzi. Hili linathibitishwa na Rukia
mwenyewe katika ujumbe anaomwandikia kaka yake, Kazimoto (uk. 19).
10 Mahojiano baina ya mtafiti na Dkt. Ramadhani Thomas Kadala Oktoba 1, 2019.
Yalifanyika katika viunga vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Dkt. Ramadhani
Thomas Kadala ni Mhadhiri wa Fasihi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
151
Nadharia ya Udhanaishi inatilia mkazo harakati au hali ya kukata tamaa, ambapo
huendana na kuyaona maisha kuwa ni kitu kisichokuwa na maana. Hili ndilo
tunaloliona kwa Rukia ambaye anaonekana kukata tamaa kutokana na mtanziko
unaotokana na vitendo anavyofanyiwa na Manase. Hatimaye, anajikuta katika wakati
mgumu anapobaini kuwa, ametiwa mimba pasipo ridhaa yake.
Kitendo hiki kinasababisha familia yote ya Mzee Mafuru kuwa katika mtanziko,
mara tu inapopata taarifa kwamba Rukia kuacha shule, baada ya kupata mimba.
Matokeo yake, kinasababisha Kazimoto kufikia hatua ya kutoa kauli inayoonesha
namna anavyotatizika juu ya suala hili. Anasema, ―Kulikokuwa na mwanga sasa
giza! Manase ana kiburi namna gani! Mimi ni mwanamume kama yeye!‖ (uk. 20).
Matokeo yanaonesha kuwa, hata mama yake anakumbwa na mtanziko kutokana na
tatizo hili. Kauli anayomweleza Kazimoto kwamba, ―… tuache tupumzike, tuache
tulie. Huu ni ugonjwa umeletwa na vijana na utatumaliza sisi kina mama wenye
mabinti…‖ (uk. 37), inathibitisha suala hili.
Kauli hii nzito na yenye masikitiko makubwa ndani yake, inatolewa na mama yake
Rukia, huku akilengwalengwa na machozi, kutokana na mtanziko alio nao baada ya
Rukia kutiwa mimba. Suala hili linamkosesha furaha na kumkatisha tamaa ya
maisha. Anakosa matumaini katika maisha na kuyakatia tamaa. Anaelekea kujutia
umaskini na hali ngumu ya maisha yake, inayosababisha mtanziko kutokana na
kumpeleka Rukia kuishi na Manase na kumsababishia tatizo hili.
Aidha, umaskini na hali ngumu ya maisha ya familia ya Mzee Mafuru, vinasababisha
mtanziko kwa Kazimoto ambaye anashindwa kuendelea na masomo yake akiwa
darasa la kumi kutokana na kukosa pesa. Hili linatokea mara tu baada ya kutoka
hospitalini alikokaa kwa muda wa mwaka mmoja kutokana na kuumwa ugonjwa wa
kifua kikuu. Mambo yanazidi kumwendea vibaya anaposhindwa kutimiza ndoto yake
ya kumaliza shule mwaka huo na kulazimika kutafuta kibarua. Anaeleza hivi:
Nilipotoka hospitalini nilikuwa na nia ya kusoma kufa na
kupona, lakini mwaka huo baba akashindwa kulipa ada ya
shule; shule nikaacha, nikatafuta kazi. Manase akawa sasa
miaka miwili mbele yangu (uk. 10).
152
Ni wazi kwamba hali hii ya umaskini inampa wakati mgumu Kazimoto, kwa sababu
anashindwa kutimiza malengo yake. Hivyo, nalazimika kuacha shule kwa muda ili
akatafute kazi ya kumwezesha kupata fedha kwa ajili ya kuendelea na masomo yake
ya chuo. Yote haya yanatokea kwa sababu ya umaskini na hali ngumu ya maisha ya
familia ya Mzee Mafuru.
Pia, umaskini na hali ngumu ya maisha vinamsababishia mtanziko Moyokonde
kutokana na kitendo cha Tegemea, ambaye ni mama yake Vumilia, kutaka kuondoka
na mwanaye, kwa sababu ya umaskini wake. Uamuzi huu unakuja baada ya Tegemea
kuwakuta Vumilia na Moyokonde wakiishi katika kijumba kidogo cha mabati, huku
Vumilia akiwa mjamzito. Mwandishi anaeleza:
Nyumba hii ilikuwa na vyumba viwili: cha kulala na cha
maongezi. Paa lilikuwa karibu, vile kwamba nilikaribia
kuligusa kwa kichwa. Madebe yalikuwa na matundu mengi na
nilishangaa kama kweli waliweza kulala humo wakati wa
mvua. Katika chumba cha maongezi niliona viti viwili vya
kuegemea; mtungi wa maji na kabati dogo ambamo niliona
sahani na vikombe vya chai (uk. 165).
Picha inayochorwa na mwandishi katika dondoo hili ni ya umaskini na maisha
magumu waliyo nayo Moyokonde na Vumilia. Kuishi katika nyumba ya namna hiyo
kunatokana na kukosa kipato na uwezo wa kugharamia nyumba nzuri na yenye
hadhi. Pia, afya zao dhaifu zinadhihirisha hali ya umaskini na ngumu waliyo nayo.
Mahojiano baina ya Tegemea na Vumilia yanatupa picha ya maisha wanayoishi
Vumilia na Moyokonde.
―Ulikuwa mgonjwa? Kwa nini umekonda namna hii?‖
Tegemea aliuliza. Vumilia hakujibu. ―Ulikuwa hupati chakula
cha kutosha?‖ Vumilia aliendelea kunyamaza. ―Husemi!
Mtoto huyu namna gani! Umekuwaje? Ulikuwa mgonjwa?‖
―Hapana,‖ Vumilia alijibu.
―Nimesikia umeolewa?‖ Tegemea aliuliza tena. Vumilia
alinyamaza.
―Labda wanakusingizia?‖ Tegemea aliendelea.
―Nimeolewa,‖ alijibu.
―… Unapenda kukaa naye?‖ Vumilia alinyamaza. ―Vumilia
huwezi kusumbuka hivi.‖ Tegemea alisema. ―Nimekuja
kukuchukua twende Ukerewe. Nyumbani kwetu huwezi
kukuta watu wanasumbuka hivi. Huwezi kukuta mtu anaishi
katika nyumba kama hii japokuwa ni shamba. Hivi nani
alikufukuza?‖ (uk. 165).
153
Hapa, Tegemea anakerwa sana na maisha wanayoishi Vumilia na Moyokonde. Azma
yake ya kutaka kuondoka na Vumilia kwenda naye Ukerewe inamtatiza na
kumkanganya Moyokonde, kwani anapata wakati mgumu kwa kuwa hajui la
kufanya. Anadiriki hata kulisema suala linaloleta aibu na fedheha kwa kutaka
Tegemea aondoke nao wote wawili ili akawatunze. Kama inavyoelezwa katika
nadharia ya Udhanaishi, hali hii inaonesha kuwa, amekata tamaa ya maisha kutokana
na mtanziko alio nao. Kutokana na mtanziko huo, Moyokonde anamweleza Tegemea
kuwa, yuko tayari hata kufa kama ataachwa peke yake pasipo kuishi na mke wake
Vumilia. Haya yanajitokeza katika majadiliano baina yake na Tegemea kama
ifuatavyo:
―…Mimi nitamchukua mtoto wangu tu. Mtoto wako
atakayezaliwa tutakurudishia.‖
―Hapana. Wewe ni mtu mzima mwenzangu. Mimi nilikuwa
sijapata mtoto maishani. Kumchukua Vumilia sasa ni
kuchukua maisha yangu. Mwanizika kaburini bila nguo.‖
―Lakini kama unampenda, mbona umekwishashindwa
kumlisha? Mtoto wangu hakuwa mwembamba namna hii. Na
kwa nini mnaishi katika nyumba ya kuku. Siwezi kumwacha
mtoto wangu humu.‖
―Mimi ninakubali kwamba ni maskini. Lakini hata maskini pia
hupenda. Isipokuwa siwezi kuwazuia kama mmekata shauri
kuninyang‘anya mwenzangu. Muulizeni mwenzangu.
Akikubali, basi mimi sina la kusema.‖ (uk. 174).
Majibu yanayotolewa na Moyokonde katika majadiliano haya yanaonesha namna
alivyo na wakati mgumu kutokana na mkinzano wa mawazo alio nao. Anakiri hali
yake ya umaskini kwa masikitiko makubwa yanayomfanya Tegemea amwonee
huruma kutokana na hali aliyo nayo. Kauli yake kwamba hawezi kuwazuia kama
wamekata shauri kumnyang‘anya mwenzake inaonesha wazi kuwa amekata tamaa,
na hana namna nyingine ya kufanya. Hii inadhihirisha kuwa umaskini na hali ngumu
ya maisha huweza kusababisha mtanziko. Pia, humkosesha mtu uhuru wa kujiamulia
mambo yake kama inavyoelezwa katika msingi wa tatu wa nadharia ya Udhanaishi.
Hili linathibitishwa kupitia kwa Moyokonde ambaye anafikia hatua ya kuwaeleza
Tegemea na Kazimoto kwamba, hana la kufanya kama wao wameamua
kumnyang‘anya mwenzake, yaani Vumilia. Hii inaonesha kuwa amekosa uhuru wa
kupanga na kujiamulia mambo yake mwenyewe.
154
Vilevile, tumebaini kuwa ukosefu wa ajira au kufukuzwa kazi ni tatizo lingine
linaloweza kumsababishia mhusika mtanziko. Kuhusiana na hili ni kwamba,
inapotokea mtu aliyekuwa na kazi fulani akafukuzwa au kuachishwa kazi hiyo, au
mtu anapotafuta kazi kwa muda mrefu na kuikosa, huweza hupatwa na wakati
mgumu wa kufikiria namna atakavyojikimu kimaisha. Hali hiyo husababisha
mhusika kupata msongo wa mawazo na kukata tamaa. Kutokana na hilo, wengine
huamua kujiingiza katika matukio ya ulevi wa pombe na matumizi ya madawa ya
kulevya kama njia ya kuondoa msongo wao wa mawazo. Pia, wengine huamua hata
kujiua kama njia ya kutanzua mtanziko wao. Hufikia haua hiyo kutokana na kukata
tamaa kwa kuona kuwa maisha yao hayana maana tena kama inavyoeleza nadharia
ya Udhanaishi.
Pia, tatizo la kukosa kazi linasawiriwa katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo. Hili
linamkumba Tumaini mara tu baada ya kutumia ovyo na kumaliza pesa ya urithi
aliyokuwa nayo. Kutokana na hilo, anahangaika huku na huko kutafuta kazi, bila
mafanikio yoyote. Hatimaye, anaamua kwenda kwa Dennis kumweleza kuhusu tatizo
hilo. Yafuatayo ni majadiliano baina yao:
―Siku hizi niko katika hali mbaya sana. Nimejaribu kutafuta
kazi lakini sikufanikiwa. Nimekuja kuomba msaada wako,
maana ninyi mlioko juu mna nguvu zaidi.‖
―Kazi?‖ Dennis alisema hali ameweka mkono wake juu ya
shavu, alijifanya kufikiri.
―Ndiyo, kazi,‖ Tumaini alisema, ―isipokuwa isiwe kazi ya
kufagia barabara.‖
―… nitafurahi sana kama utaweza kunipa jibu lako leo au
kesho. Niko katika hali mbaya sana bwana.‖ (uk. 81).
Matokeo yanaonesha kuwa baada ya majadiliano haya, Dennis anaamua
kumshirikisha jambo hilo mke wake, Vera, ambaye kwa wakati huo ana chuki na
hampendi Tumaini kutokana na kuwa maarufu zaidi kumzidi mume wake. Hivyo,
anafurahishwa na kitendo chake cha kwenda kuomba kazi kwa mumewe kwa
kuamini kwamba tangu wakati huo, umaarufu wake utaisha na mume wake, ndiye
atayepata umaarufu zaidi na kumzidi yeye. Kwa hiyo, baada ya majadiliano yao
wanakubaliana kwamba, apewe kazi ya kupeleleza watu wapingao serikali katika
mabaa. Hivyo, Tumaini anakubali kufanya kazi hiyo, kwa kuwa hana namna
nyingine ya kufanya. Hata hivyo, kazi hiyo inamweka katika wakati mgumu na
155
kusababisha achukiwe sana na watu, hususani wenye mabaa, pamoja na wateja wao,
kwa sababu ya kuingilia na kugusa maslahi yao. Mwishowe, anajikuta akiingia
katika mgogoro na Vera, pamoja na mmiliki wa Africans’ Royal Bar. Hawa
wanamtafutia Tumaini majambazi ambao wanampiga na kumuumiza vibaya sana
(uk. 97). Tumaini anakumbwa na matatizo haya kwa sababu ya mitanziko aliyo nayo,
inayotokana na hali yake mbaya ya kiuchumi. Hii ni baada ya kuishiwa pesa yake ya
urithi na kukata tamaa ya maisha kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi.
Utafiti umebaini kwamba, ijapokuwa mtanziko huo wa kiuchumi haumsukumi
Tumaini moja kwa moja kwenye tukio la kujiua kwa wakati huo, ni wazi kwamba
huo ulikuwa ni sehemu ya mchakato wake wa kukata tamaa ya kuendelea kuishi
kutokana na namna maisha yalivyo.
4.3.4 Sababu za Kifalsafa
Mitazamo ya kifalsafa juu ya ukweli kuhusu maisha huweza kusababisha mitanziko
kwa wahusika, na hata kwa jamii kwa jumla. TUKI (2014) inaeleza kuwa falsafa ni
elimu ya asili, maana na sababu za mambo au vitu. Nayo, Wizara ya Elimu na
Utamaduni (1992) inafafanua kuwa falsafa ni taaluma inayojishughulisha na kutafuta
ukweli wa jambo kwa njia ya kutafakari. Mantiki iliyomo katika fasili hizo ni
kwamba falsafa ni taaluma au mtazamo unaochunguza matumizi ya dhana, kupima
hoja pamoja na mbinu za ujengaji hoja. Pia, hufanya uhakiki au tathmini na
kuthibitisha au kutoa ushahidi wa hoja zinazozungumzwa na nadharia mbalimbali
zinazohusu hali halisi ya maisha kwa kuzingatia imani, mila, Desturi, pamoja na
mienendo aliyo nayo binadamu. Katika riwaya teule, Euphrase Kezilahabi anaibua
vipengele vikuu vitatu juu ya mtazamo wa kifalsafa kuhusu maisha. Vipengele hivyo,
ambavyo ni dhana ya maisha, dhana ya kifo na dhana kuhusu Mungu, vinaibua
mjadala na kusababisha mtanziko kwa wahusika kama inavyojitokeza katika kazi
hizo.
4.3.4.1 Dhana ya Maisha
Dhana ya maisha ni swali linalowashughulisha na kuwatatiza watu wengi wakiwamo
Wanatheolojia, Wanasayansi na Wanafalsafa (Muller 1964; Lepp 1968 katika
Mungah 1999, na Freeman 1971). Majibu mbalimbali yanayopingana na hata
kutofautiana yamekuwa yakitolewa kuhusiana na swali hilo. Kwa upande wa dini,
suala hili limekuwa likihusishwa na masuala ya kidhanifu yanayodai kuwa, chanzo
156
cha maisha ni Mungu au nguvu zilizo nje ya fikra za binadamu. Haya
yanathibitishwa kupitia kitabu cha Mwanzo 1: 26 - 27 katika Biblia Takatifu, 1997).
Hoja hii inaungwa mkono na Jaspers (1883 – 1986) na Darwin (1809 – 1832)
wanaodai kuwa Mungu ana nafasi kubwa katika kuyafanya maisha ya mwanadamu
yawe kama yalivyo au yanavyoonekana. Kwa mtazamo wao, maisha ya mwanadamu
hupangwa na Mungu. Aidha, kwa msingi wa dini ya jadi ya Waafrika, maisha ni
mapito kutoka ulimwengu wa kawaida kuelekea ulimwengu wa mizimu. Kwa
upande wa Wanasayansi, hususani wale wa karne ya ishirini, wakiwamo Richard
Dawkins (1941) na David Haig (1955), majibu yao yamekuwa yakihusishwa na
masuala ya utafiti, yanayojikita katika mabadiliko ya mwanadamu.
Nao Wanafalsafa, hususani wadhanaishi, wamekuwa wakidai kuwa maisha hayana
maana, na wakati mwingine hayapo, kwa sababu ni ya kuwazika tu (Camus 1954;
Beckett, 1975). Pia, hudai kwamba hakuna Mungu kabisa kwani kama angekuwapo,
angeingilia kati na kutatua shida na matatizo yanayomkumba binadamu katika
maisha yake ya kila siku. Aidha, hudai kwamba kila jambo alifanyalo mwanadamu
katika ulimwengu wake, ni kutokana na asili yake tu ya kimaumbile, hivyo Mungu
hayupo. Wanaongeza kuwa kuamini katika nguvu za Mungu ni kupoteza muda wa
kufikiri na kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Kimsingi, kutofautiana kwa mitazamo kuhusu falsafa ya maisha kumesababisha
mtanziko mkubwa kwa binadamu; na wengine wameshindwa kabisa kuamini juu ya
dhana mbalimbali zinahohusiana na maisha kwa jumla. Euphrase Kezilahabi ni
miongoni mwa watu wenye mtanziko kuhusu dhana ya maisha. Anadhihirisha jambo
hili waziwazi katika kazi zake. Kwa mfano, katika dibaji ya diwani yake ya Kichomi
(1974: xv) anasema: ―Wazo moja hasa lilinisumbua. Jambo lenyewe lilikuwa ni
swali linalohusu maana ya maisha. Swali hili liliukera sana moyo wangu.‖ Nukuu hii
inaonesha namna Kezilahabi anavyopata wakati mgumu na kukanganywa na dhana
ya maisha, kwa kuwa hata chanzo chake chenyewe hakieleweki. Mtazamo wake
kuhusu maana ya maisha kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi
unamkatisha tamaa. Hapa anawatumia wahusika kama vile Rosa Mistika, Kazimoto,
Manase, na Tumaini katika kazi zake kuendeleza mtanziko wake kwa kuyaona
maisha kama kitu kisichokuwa na maana.
157
Katika riwaya ya Kichwamaji, dhana ya maisha inasababisha mtanziko kwa Manase
na Kazimoto. Hawa wanapata mkinzano wa mawazo wa namna ya kuielewa maana
halisi ya maisha kwa jumla. Mtanziko huo unasababisha wayaone maisha kama kitu
kisichokuwa na maana, kwa kuwa hata binadamu mwenyewe anachukuliwa kama
kiumbe dhaifu na duni, na kinachoishi katika ulimwengu usiomjali. Hoja hii
inaungwa mkono na Mbatiah (1998) anayeeleza kuwa maisha ya mwanadamu
hayana maana yoyote, ni batili, ya kuudhi na ya kutatanisha. Haya ndiyo
yanayojitokeza katika nyumba ya Manase, ambapo watu wanaoishi ndani ya nyumba
hiyo, hawaoni tena thamani ya maisha. Wanayafananisha na ngozi ya simba
iliyotundikwa ndani ya nyumba hiyo. Manase anayabainisha haya anaposema:
―… mtu yeyote aonaye ngozi hii atafikiri juu ya maisha yake
lakini kwa kuwa haoni kitu tena kwa sababu ya woga,
polepole ataanza kuona kwamba maisha yake hayana maana.
Mnyama kama huyu anaweza kutunyang‘anya maisha haya
kwa urahisi sana. Kazimoto, kwa ufupi ni kwamba watu
wanaoishi katika nyumba hii hawaoni tena maana ya maisha.‖
(uk. 188).
Katika dondoo hili, Manase anadokeza hali ya kukanganya inayoikumba nyumba
yake, kiasi cha kufikia hatua ya kukata tamaa juu ya maisha. Kama inavyoelezwa
katika nadharia ya Udhanaishi, matatizo yanayoikumba nyumba yake yanakatisha
tamaa na kufikia wakati wa kuona kuwa maisha hayana maana tena. Pia, anaichora
picha ya maisha ya binadamu yalivyo magumu kwa kuhusisha na mistari iliyomo
katika picha mojawapo, iliyotundikwa ndani ya nyumba yake. Anafafanua kuwa:
―Katika picha hii utaona mistari inakwenda juu na mingine
inashuka chini; halafu mingine inatoka pembeni na
kuchanganyika katikati mfano wa mtego. Picha hii inaonyesha
jinsi maisha ya binadamu yalivyo magumu. Ukitazama vizuri
unaweza kuona picha ya mwanadamu ameshikwa katika
mtego huu kama samaki. Inaonyesha kwamba matatizo ya
binadamu magumu na hayawezi kutafutiwa jawabu kwa
urahisi. Mwanadamu kama samaki, atajaribu kujikakamua
lakini kazi bure.‖ (uk. 188).
Kuhusiana na dondoo hili tumebaini kuwa, maisha ya binadamu yanasawiriwa kama
mateso na yanasababisha mtanziko kwake, kutokana na kushikwa katika mtego kama
samaki. Anapata wakati mgumu wa kuyaelewa na kuyatunza kwa sababu ya
kupotoshwa na kuangamizwa katika kutafuta furaha. Hali hiyo ya ugumu wa maisha
158
yake ndiyo inayosababisha ayaone kama kitu kisichokuwa na maana na
kumsababishia mtanziko. Mtanziko huo unamkosesha furaha kiasi cha kuyaona
maisha yake kama adhabu inayoshinda mambo mengine yote anayokumbana nayo.
Hii inatokana na ukweli kwamba binadamu hana uwezo wa kuyaendesha na
kuyapanga maisha yake, ambayo hayajulikani mwanzo na mwisho wake. Maelezo
haya yanalandana na ya Mbatiah (1998) anayeelezea maisha ya binadamu kama
fumbo linalohitaji jitihada kubwa ili kulifumbua.
Pia, dhana ya maisha inamsababishia mtanziko Kazimoto. Huyu anafikia hatua ya
kuyaona maisha kuwa hayana maana. Hii ni kutokana na kupitia matatizo mengi
yanayompa wakati mgumu, hasa anaposaili maisha na maana yake, kama
inavyojitokeza katika majadiliano yafuatayo baina yake na Sabina.
―Mke wangu,‖ nilimwita.
―Bwana‘ngu,‖ aliitikia.
―Sijui kwa nini ninaishi.‖
―Nimechoka na maswali yako ya kijinga,‖ alisema.
―Huwezi kuishi kama watu wengine?‖ Wewe nani?‖
―Mimi sijijui,‖ nilimwambia.
―Hakika sikufahamu kwamba wewe ni kichwamaji namna hii!
Sikufahamu! (uk. 194 - 195).
Kutokana na dondoo hili, tunapata sababu mahususi zinazotufanya tuelewe ni kwa
nini Kazimoto anapata mtanziko kuhusu maisha yake. Anayaona maisha kuwa ni
adhabu na tanzia kali, ambapo anashindwa kupata njia sahihi ya kujinasua nayo.
Maswali anayohojiana na mkewe yanaonesha namna alivyokumbwa na fadhaa,
mashaka, pekecho na uchovu wa maisha kama inavyoelezwa katika msingi wa nne
wa nadharia ya Udhanaishi. Yote haya yanatokana na mtanziko kuhusiana na dhana
ya maisha unaomsukuma katika hatua ya kujiua kama suluhisho la kumaliza matatizo
yake.
Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo, dhana ya maisha pia inajitokeza na
inasababisha mtanziko kwa Tumaini. Matatizo anayopitia katika maisha yake,
yanamfanya atafakari kwa kina juu ya dhana hii. Tafakuri hiyo inamweka katika
mkinzano wa mawazo kiasi cha kukosa majibu sahihi ya nini hasa maana ya maisha.
Matokeo yake, anafikia hatua ya kukata tamaa kwa kuona kwamba kumbe maisha
hayana maana. Hii ni kwa sababu hayampi furaha anayoihitaji baada ya kuhangaika
159
kwa muda mrefu akitafuta mali. Furaha ya muda mfupi anayoipata baada ya kujipatia
mali zake inatoweka. Hii ni baada ya kuambiwa kwamba mali hizo pamoja na
mashamba yake yanataifishwa kutokana na sera ya vijiji vya ujamaa. Hali hiyo
inamkatisha tamaa na kuona kuwa furaha ni wazo tu; ni kitu kisichoweza kupatikana,
kwani kuendelea kuitafuta ni namna ya kujitafutia maangamizo. Hili linabainishwa
kupitia mazungumzo baina yake na Dennis anapomwambia:
Tumaini la furaha ni wazo tu ambalo linaweza kusukuma
mwanadamu mbele ili kumwangamiza ama kumwendeleza.
Lakini hatalishika mkononi (uk. 163).
Dondoo hili linaonesha kwamba furaha ni wazo tu, na wala siyo hali ambayo
mwanadamu ataifikia. Hii ni kwa sababu hakuna mtu aliyewahi kufikia kiwango cha
juu kabisa cha furaha katika maisha yake. Hoja hii inaungwa mkono na Camus
(1954) anayedai kwamba furaha ya kudumu, kamwe, haiwezi kupatikana katika
maisha ya binadamu. Dhana ya maisha ya binadamu kutokuwa na furaha inaelezwa
pia na Kezilahabi kwamba:
Mwanadamu ni kiumbe ambaye amejaribu kutafuta njia nyingi
zitakazomwezesha kupata furaha. Kwa kuwa ameshindwa
kupata furaha hapa duniani amejenga kichwani mwake kitu
kama mbingu, yaani mahali anapotegemea kupata furaha
baada ya kufa (uk. 123).
Hivyo, dhana ya maisha inasababisha mtanziko kwa Tumaini, kwa kuwa anakosa
furaha; na anayaona hayana maana tena kwake. Kutokana na hilo, anaamua
kupambana na nguvu ya jamii, huku akijua kabisa kwamba, kamwe, mtu binafsi
hawezi kushindana na nguvu hizo. Anasema, ―…mimi naona afadhali tuonyeshane
nao. Watanishinda. Lakini nitakuwa nimewafunza somo…‖ (uk. 127). Kauli hii
inaonesha dhahiri kwamba amekata tamaa, na anaamua tu kupambana na nguvu
ambayo, kamwe, hawezi kuishinda. Suala hili la mtu binafsi kushindana na nguvu za
umma, linaelezwa na Mulokozi (1983) kwamba kanuni za jamii wakati mwingine
humfunga mtu binafsi na kuingilia matakwa yake na shughuli zake za kujinufaisha,
kujiendeleza, na kujitafutia furaha. Hata hivyo, anaeleza kuwa katika hilo, ni wazi
kwamba mtu binafsi, kamwe hawezi kushindana na nguvu ya umma.
Hili ndilo linaloshuhudiwa kwa Tumaini kwani, ijapokuwa anafanikiwa kumuua
Mkuu wa Wilaya matokeo yanakuwa mabaya kwake kwa sababu anaishia gerezani,
160
ambapo katika ukurasa wa 129, mwandishi anaonesha kuwa, Tumaini pia anauawa
kwa kunyongwa (uk. 129). Yote haya yanampata kutokana na mtanziko aliokuwa
nao kuhusu suala la maisha na namna yalivyo. Hivyo, maisha ya Tumaini yanaishia
katika kutokuwa na maana kama inavyoeleza nadharia ya Udhanaishi.
4.3.4.2 Dhana ya Kifo
Dhana ya kifo imemshughulisha binadamu kwa muda mrefu kiasi cha kumpumbaza
kwa karne nyingi, na kumsababishia mtanziko katika maisha yake. Mtanziko huo
unatokana na mkanganyiko anaoupata katika kuielewa dhana hiyo. Hii inatokana na
kuwapo kwa mitazamo mbalimbali ya kuachana miongoni mwa watu kuhusu dhana
hii. Baadhi ya watu huamini kwamba kuna maisha baada ya kifo, na wengine hudai
kwamba hakuna maisha baada ya kifo. Kwa mfano, Temples (1959) anaeleza kuwa,
fikra kuhusu uhai na kifo ni masuala yanayowashughulisha sana Waafrika. Hii
inatokana na kuamini kwao kwamba kifo ni matokeo ya laana inayotokana na
kupungua kwa nguvu-hai. Nao, Marealle (2002) na Mbiti (2011) wanaeleza kuwa,
Waafrika huamini kwamba kifo siyo mwisho wa maisha na kuwapo kwa mtu.
Wanafafanua zaidi kwamba, kwa Waafrika kifo ni mwanzo tu wa maisha mengine ya
mtu katika ulimwengu wa wafu hai. Naye, Menkiti (1984) anakubaliana na mawazo
ya Mbiti na anafafanua kuhusu mila na desturi za Waafrika. Anaeleza kuwa
Waafrika wanaamini kwamba kifo siyo mwisho wa uhai bali ni mwanzo tu wa
maisha menngine. Anasema:
Following John Mbiti, we can call the inhabitants of the ancestral
community by the name of the living dead. For the ancenstral dead
are not dead in the world of spirits nor are they dead in the memory of
the living men and women who continue to remember them, and who
incessantly ask their help through various acts of libation and
sacrificial offering. (uk. 174).
Kwa kufuatia mawazo ya John Mbiti, tunaweza kuwaita wakazi wa
jumuiya ya wahenga kwa jina la wafu wanaoishi. Wahenga hao
hawajafa katika ulimwengu wa kiroho, kadhalika hawajafa katika
kumbukumbu za waliohai, wake kwa waume, ambao wanaendelea
kuwakumbuka na huendelea kuomba msaada wao kupitia matendo
mbalimbali ya matambiko na kutoa sadaka. (Tafsiri ya mtafiti)
Katika andiko hili, Menkiti amefafanua juu ya imani za Waafrika katika kifo,
ambapo anaona kuwa mtu akifa anaendelea kuishi katika ulimwengu mwingine wa
kiroho. Hii ina maana kuwa mwili ndio unaotengana na roho lakini roho inaendelea
161
kuwepo na kuwatembelea walio hai. Fikra hizi zinashabihiana kwa kiasi kikubwa na
Stumph na Fierser (2008) ambao wanaona kuwa roho ya binadamu ni muunganiko
wa mwili na roho.
Matokeo yanaonesha kuwa, kwa Waafrika mtazamo kuhusu maisha baada ya kifo
unakitwa katika dhana kuwa mtu anapokufa, hurudi duniani kwa kuzaliwa upya
ndani ya ukoo huo, au katika mazingira tofauti na yale aliyokulia. Hoja hii inaungwa
mkono na Faustine11
anaposema kuwa:
Imani ya Waafrika juu ya dhana hiyo ni kwamba kifo si
mwisho wa maisha, bali ni mwanzo tu wa maisha mapya
katika ulimwengu mwingine tofauti na waliouzoea.
Wanaamini kuwa mtu akifa bado huendelea kujidhihirisha
katika jamii kwa njia mbalimbali kama vile, majina, ndoto,
maono, na wakati mwingine, kwa kumwingia mtu na kumtia
wazimu.
Kwa upande wake, Mpalanzi (2019) anaeleza kwamba, misingi ya ontolojia ya
Kiafrika inazingatia imani kuwa baada ya kifo, roho za watu waliokufa huendelea
kuishi ulimwenguni. Anafafanua zaidi kuwa, kulingana na ontolojia hiyo, nafsi ya
mtu imejengwa na elementi mbili za msingi, ambazo ni mwili na roho, ambapo
wakati wa kuzaliwa mtu, mwili na roho huungana. Roho hiyo huendelea kuwapo
katika mwili wa mtu katika kuishi kwake. Baada ya mwili kufa, roho huendelea
kuwapo ulimwenguni na kuungana na miili mingine. Naye, Mihanjo (2004)
anafafanua dhana hii kuwa:
… roho ya binadamu hutoka katika ulimwengu wa roho. Roho
hiyo hushiriki katika akili na mawazo ya jumla na huunganishwa
na mwili, lakini huwa si kitu kimoja na mwili. Hata hivyo, baada
ya kifo, roho haifi. Kwa sababu hiyo, roho hutoka katika mwili
mmoja na kuingia mwili mwingine. Hii ni kwa sababu roho ni
kitu ambacho hakina umbisho. Hivyo, roho ni kitu ambacho
hakiwezi kuharibika…
11 Mahojiano baina ya mtafiti na Dkt. Stella Faustine Novemba 9, 2019. Yalifanyika
katika viunga vya Chuo Kikuu cha Dodoma. Dkt. Stella Faustine ni Mhadhiri wa
Fasihi, Chuo Kikuu cha Dodoma.
162
Katika dondoo hili, kama ilivyo kwa Faustine (keshatajwa) na Mpalanzi
(keshatajwa), matokeo yanaonesha kuwa Mihanjo pia, anakubaliana na hoja
inayoeleza kuwa, Waafrika wanaamini kwamba kuna maisha baada ya kifo. Hii ina
maana kwamba kwa asili Waafrika hulichukulia suala la kifo katika hali ya thamani
kubwa sana. Pia, huamini kwamba kifo ndiyo njia inayomfanya mwanadamu aingie
katika sehemu mpya ya maisha yake katika awamu nyingine. Vilevile, huamini kuwa
mtu hufa mwili tu na roho yake hubaki hai. Hivyo, jamaa zake huendelea
kuwasiliana naye kwa njia mbalimbali kama vile kufanya matambiko. Hii ina maana
kwamba tofauti na Wanyama wengine, Waafrika huamini kwamba hakuna kifo kwa
mwanadamu. Wao huamini kuwa, kifo ni badiliko la kiasili ambapo mtu hubadili tu
mahali pake pa kuishi. Kwa hiyo, matokeo yanaonesha kuwa kwa jumla, kifo kwa
Waafrika hutazamwa kama mchakato wa kuhama kutoka katika ulimwengu halisi na
kwenda ulimwengu dhahania.
Aidha, utafiti umebaini kwamba dini za kigeni zinaamini kuhusu kuwapo kwa
maisha ya kiroho baada ya kifo. Imebainika kwamba kulingana na imani ya dini
hizo, mtu aliyeishi hapa duniani bila dhambi, atakapokufa ataishi maisha mengine
yaliyo bora zaidi katika ulimwengu wa kiroho. Mpalanzi (2019) analielezea hili kwa
kurejelea katika Kurani na Biblia. Anafafanua kuwa Kurani inatetea hoja ya kuwapo
kwa maisha baada ya kifo na kwamba mtazamo huo, unatetewa na kauli ya Allah
anaposema: ―Kila kilicho juu ya ardhi ni chenye kufa‖ (taz. Surat Al-Rahman, aya ya
27). Kwa kuzingatia mtazamo huo, ni dhahiri kwamba Uislamu unaamini maneno ya
Allah yanayosema kuwa: ―Kila nafsi itaonja mauti.‖ (taz. Surat Anbiya, aya ya 35).
Hii ni kwa sababu kwa desturi, hakuna uhai usiokuwa na mauti. Hivyo, Uislamu
unaamini kuwa siku ya kufufuka, mfu atarudishiwa uhai wake na kuhukumiwa
kutokana na matendo yake aliyoyafanya hapa duniani. Kuhusiana na hili wao
huamini kwamba watenda mema watakwenda mbinguni, na waovu watakwenda
motoni kuadhibiwa kutokana na kushindwa kumtii Mungu na Mtume wake.
Hali kadhalika, suala la kifo na maisha baada ya kifo linaelezwa katika imani ya dini
ya Kikristo. Kwa mfano, Biblia Takatifu inafundisha kuhusu theolojia ya imani ya
kuwapo kwa maisha baada ya kifo. Hapa tutatoa mifano michache, katika (Luk. 16:
19 – 31), ambapo katika kifungu hicho kuna kisa kinachohusu mtu tajiri na maskini
Lazaro. Inaelezwa kwamba watu hawa walipokufa, tajiri alikwenda kuzimu na
163
Lazaro akaenda mbinguni au paradiso. Pia, katika Injili ya Yohana, Yesu anasema:
―Mimi ndiye ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi ajapokufa, atakuwa anaishi‖
(Yoh. 11: 23 – 27). Mifano hii michache inaonesha kuwa kundi hili kama ilivyo kwa
Waafrika na kwa Waislamu, nalo linaamini kuwa mtu akifa hupumzika tu kaburini
akisubiri ufufuo wa Yesu, na kwamba baada ya hapo maisha yake yataendelea tena.
Maandiko hayo yanasema: ―… nao waliokufa watafufuliwa kwanza. Kisha, sisi tulio
hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao‖ (1Thes. 4: 13 – 18) katika Biblia Takatifu,
(1997).
Kwa jumla, matokeo yanaonesha kwamba suala la kuwapo kwa maisha baada ya
kifo, lilikuwapo tangu enzi na lilikuwa na msingi wa imani za kijadi za Waafrika.
Kutokana na maelezo hayo imebainika kwamba suala hili limeendelea kupewa
msukumo mpya na dini za kigeni, yaani dini zilizoletwa na wakoloni kwa mwavuli
wa Umisionari. Hata hivyo, utafiti umebaini kwamba ujio wa dini hizo, pamoja na
jitihada za kujaribu kuidhoofisha imani ya Waafrika kuhusu suala la kifo na maisha
baada ya kifo, haitofautiani na mtazamo uliojengeka katika imani hiyo ya dini za
kigeni.
Kwa upande mwingine, Kipacha (2019) anaelezea mtazamo wa wadhanaishi kama
vile Nietzsche (1844) na Kezilahabi (1944), wanaoonesha mawazo tofauti juu ya
dhana ya kifo. Wao wanapinga suala la kuwapo kwa maisha baada ya kifo na
kuwako kwa uwili wa mwili na roho. Hoja hii inaungwa mkono na Kahigi na
Mulokozi (1979) katika Mnenuka (2011) wanapoeleza kuwa, maisha ya binadamu
yanaanza na kuishia hapahapa duniani. Wanafafanua zaidi kuwa, kama ilivyo kwa
viumbe vingine, baada ya kufa binadamu huoza na kuwa udongo, na huo ndio
unakuwa mwisho wa historia ya maisha ya binadamu huyo. Hii ni sawa na kusema
kuwa maisha ya mwanadamu hupotea kama moto unavyopotea ukizimika. Kwa
upande mwingine, Mulokozi (2017) anaona kuwa pamoja na kuwapo kwa fikra za
maisha baada ya kifo, maisha hayo ni dhahania kwa kuwa maisha halisi ni ya hapa
duniani. Anafafanua zaidi kuwa, hakuna pepo wala jehanamu na wala hakuna tunzo
wala adhabu baada ya kufa. Kwamba mtu hutunzwa au kuadhibiwa awapo hapahapa
duniani. Hivyo, mwanadamu akifa ndio mwisho wa maisha yaliyo halisi. Kwa hiyo,
utafiti umebaini kwamba kuwapo kwa mitazamo inayoachana juu ya dhana ya kifo,
ndiko kunakosababisha mtanziko miongoni mwa wahusika katika riwaya teule.
164
Mitanziko hiyo huweza kusababisha wengine kuchukua maamuzi ya kujiua kama
suluhisho la maisha yao.
Katika riwaya ya Kichwamaji, utafiti umebaini kuwa dhana ya kifo inasababisha
mtanziko kwa Kazimoto. Anajikuta katika mkinzano wa mawazo anapoambiwa na
Kalia kwamba mtu akifa, huendelea kuishi, kwa kuwa kufa ni kubadilika hali. Kalia
anayasema haya wakati akimsimulia Kazimoto kuhusu ndoto yake aliyoota akijikuta
yuko Mbinguni, huku akiwa na watu wengine waliokwisha kufa, lakini wakiwa hai.
Anasema:
―… Hata! mara fulani fulani Mungu mpenzi alikuwa
anaturuhusu kuja ulimwenguni. Tuliwaona watu, lakini wao
walikuwa hawawezi kutuona. Halafu tulirudi. Tulipokuwa
tunafika mahali fulani mara hali yetu iligeuka tulikuwa
tumezoea kuiita ―kupokelewa na Mungu mpenzi.‖ ―Bado
sijaelewa, yaani mlikuwa mnatembea kwa miguu?‖
―Hapana, tulikuwa tunakwenda tu, hali yetu ilizoea kugeuka
na tukajiona mbinguni tena.‖ (uk. 75).
Dondoo hili linaonesha namna Kazimoto anavyopata wakati mgumu kuelewa dhana
ya kifo. Hii inatokana na mtazamo alio nao kwamba mtu akifa hawezi kuendelea
kuwa hai tena. Anasema: ―Mimi naamini kila kitu kilicho na mwanzo kina mwisho.
Na kifo ndio mwisho kwa mwili wa binadamu, roho inabaki lakini haigeuki tena‖
(uk. 123). Hivyo, kutofautiana kwa mtazamo wake na Kalia kunamfanya ashindwe
kupata majibu sahihi kuhusiana na dhana hii ya kifo. Tunaelezwa kwamba, baada ya
majadiliano yao, Kazimoto anajikuta katika mtanziko, huku akifikiria mambo kama
vile: Mosi, kwamba kufa ni kugeuka hali. Pili, kwamba waliokufa tuko karibu nao,
lakini hatuwezi kuwaona kwa sababu hali yetu haijageuka (uk. 75). Udadisi na
mkanganyiko anaoupata juu ya dhana ya kifo unamweka katika mtanziko kutokana
na mkinzano wa mawazo anaoupata.
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa mtanziko wa Kazimoto hauishii katika
majadiliano yake na Kalia pekee, bali anatatizwa pia na dhana hii baada ya
kukumbwa na matatizo ya kufiwa na dada yake, Rukia. Hapa anaikumbuka ndoto ya
Kalia na inamfanya azidi kutatizika. Kutokana na ndoto hiyo anajikuta akizama
katika tafakuri nzito kuhusiana na namna kifo chake kitakavyomjia. Anaeleza hivi:
165
―Usiku nilianza kufikiri juu ya kifo. Nilifikiri jinsi kifo changu
kitakavyonijia - kwa ugonjwa, kwa ajali au kwa kukatwakatwa
na wezi? Labda kwa uzee au kwa sumu! Huenda nikajiua
mwenyewe! Niliikumbuka ndoto ya Kalia. Niliwakumbuka
wale ng‘ombe, sisimizi, nyuki na mengine mengi niliyoyaona
huko machungani. Niliona kwamba adhabu kubwa ya
mwanadamu ni maisha yenyewe. Nilikumbuka mlevi mmoja
niliyemkuta akipiga mti mweleka mpaka akaumia mwenyewe.
Maisha ndiyo yaliyokuwa yakimsumbua, wala siyo pombe.
Wakati huo usiku niliyaona maisha kuwa chanzo cha yote.‖
―Hii ni adhabu ambayo kila mwanadamu amepewa kutunza
maisha yake. Maisha ambayo hayashibishwi wala
kuridhishwa. Zaidi ya hayo mwenye nguvu anatunyang‘anya
wakati wote bila hata kutuarifu.‖ (uk. 84).
Katika dondoo hili, tunaona namna Kazimoto anavyopata wakati mgumu katika
kuitafakari dhana ya kifo. Anakatishwa tamaa na dhana yenyewe, kwani, licha ya
kushindwa kueleweka kwake, bado mwanadamu hana hiari na uamuzi juu ya kifo
chenyewe. Anafikia hatua ya kuona kwamba: ―Mwisho wa mwanadamu utaletwa na
mwanadamu mwenyewe‖ (kur. 84 - 85). Kauli hii siyo tu kwamba inaonesha kukata
tamaa kwake katika kutafakari juu ya kifo kama inavyoelezwa katika nadharia ya
Udhanaishi, bali inaonesha pia, namna dhana yenyewe inavyomweka katika
mtanziko.
Vilevile, dhana ya kifo inamsababishia mtanziko Kazimoto, hususani, anapoihusisha
na mtazamo wa wazee walioishi hapo zamani. Kinachomsumbua zaidi ni namna
wazee hao walivyoyatazama maisha ya mtu baada ya kufa. Kutofautiana kwake na
wazee hao kimtazamo juu ya dhana hiyo kunampa wakati mgumu kwa kuwa, hapati
jibu sahihi kuhusiana na jambo hilo. Hili linathibitishwa katika majadiliano baina
yake na Manase kama ifuatavyo:
―Zamani wazee wetu walikuwa wakiamini kwamba mtu
alikufa na kuzaliwa tena. Yaani, kulikuwa na hali kama ya
duara. Lakini mimi nimeanza kuamini kwamba hali yenyewe
ni mstari usio na mwisho. Ni hali ya kwenda mbele bila kurudi
nyuma.‖
―Ninaamini kwamba kufa ni kugeuka hali. Kama kufa ni
kugeuka hali ninaamini kuwa kuna kugeuka na kugeuka na
kugeuka. Ndiyo maana ya mstari usio na mwisho. Kwa hiyo
sioni kwa nini mbingu iwepo baada ya kufa ambayo ni hatua
moja tu, na labda ya kwanza katika kugeuka kwa viumbe.
Kwa nini isiwepo baada ya hatua ya pili?‖
166
―Mimi ninaamini kila kitu kilicho na mwanzo kina mwisho.
Na kifo ndio mwisho kwa mwili wa binadamu, roho inabaki
lakini haigeuki tena. Kwani huo mstari usio na mwisho
ulianzaje? Kama una mwanzo basi utakuwa na mwisho.‖
―Tunaweza kusema kwamba mstari huo una mwanzo, lakini
mwisho wake haujulikani. Kifo siyo mwisho wa binadamu, ni
tukio fulani katika mfululizo wa kugeuka kwa viumbe.‖ (uk.
123).
Kwa kuzingatia ujumbe uliomo katika dondoo hili tumebaini kuwa, mwandishi
anaonesha namna dhana ya kifo inavyosababisha mtanziko kwa Kazimoto. Hii
inatokana na mtazamo wake kuhusiana na dhana hiyo, kutofautiana na ule wa wazee
wanaoamini kuwa, kifo ni mwanzo wa maisha mapya. Kazimoto kwa upande wake
anatofautiana nao, kwa sababu anaona kuwa kifo ndio mwisho wa maisha ya
mwanadamu hapa duniani. Mkinzano huu wa mawazo, ndio unaompa wakati mgumu
wa kuielewa dhana ya kifo. Matokeo yake ni kwamba mtanziko huo unamsukuma
katika kufikia maamuzi ya kujiua kwake.
4.3.4.3 Dhana Kuhusu Mungu
Dhana ya kuwako au kutokuwako kwa Mungu imeishughulisha akili ya mwanadamu
tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu hadi sasa, na ni miongoni mwa sababu za
mitanziko ya wahusika katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi. Hii inatokana na
ugumu uliopo katika kuielewa na kuielezea dhana hii, kwa sababu inahusiana na
mambo ya asili, pamoja na ukweli wa maarifa. Hoja hii inaungwa mkono na
Chuachua (2016) anayeeleza kuwa Mungu ni mojawapo ya dhana ngumu za
kifalsafa, na kwamba inaweza kuelezeka kiontolojia. Hii ni kwa sababu, Mungu
anasawiriwa na kuelezwa na jamii mbalimbali duniani kote kuwa, ni mwanzo wa
kuwapo na kuendelea kwa vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Falsafa ya
Kiafrika inadhihirisha kuwa jamii za Kibantu huamini kuhusu uwepo wa Mungu.
Inaeleza kuwa, hata kabla ya majilio ya wageni kutoka nje ya bara hili la Afrika,
Wabantu walikuwa na Mungu wao waliyemwamini, waliyehusiana na kushirikiana
naye katika shughuli zao za kila siku. Kwa mtazamo wa kiontolojia, Mungu
anasawiriwa na kuelezwa na jamii mbalimbali duniani kote kuwa ni mwanzo wa
kuwapo na kuendelea kwa vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.
Chuachua (k.h.j) anaelezea mtazamo wa Idowu (1973) kuhusu Mungu kwamba:
Katika utamaduni wa Kiafrika, Mungu ndiye kiumbe mkuu na kibainishi cha dini
167
yao. Pia, ni mtawala, muumbaji wa dunia, na chanzo cha kuwapo kwake. Anaongeza
kuwa, katika utamaduni wa Kiafrika, Mungu ni halisi zaidi ya vitu vyote na hutajwa
mara nyingi katika sala, hususani wakati wa matatizo. Mawazo ya Idowu
hayatofautiani na ya Temples (1959) anayedai kwamba dhana kuhusu Mungu
inapoelezwa kwa mtazamo wa Kiafrika, yafaa ieleweke kwamba Mungu ni nguvu
kuu kuliko nguvu zote, na ni chanzo cha kuwapo kwa kila kitu ulimwenguni.
Kwa upande mwingine, Mbiti (1995) anabainisha namna jamii za Kiafrika
zinavyoielezea dhana kuhusu Mungu. Anaeleza kuwa, kwa Wazulu na
Wanyarwanda, Mungu hujulikana kama ni ―Mwenye Hekima‖, kwa Waakan ni
―Mjua Yote au Mwona Yote‖, Wayoruba huamini kwamba ―Mungu pekee ndiye
aliye na busara, na ndiye huamua mwelekeo wa moyo wa mtu‖ na ndiye huona yale
yote yaliyomo moyoni mwa mtu. Wakikuyu wao huamini kuwa Mungu hana baba
wala mama, pia hana mke wala watoto. Aidha, Mungu siyo mtoto wala mzee, na
kamwe huwa habadiliki. Aonekanavyo leo, ndivyo alivyokuwa jana na juzi. Kwa
mtazamo wa Mbiti, Mungu ana umri mkubwa kuliko dhana ya nyakati za zamani; na
kwamba yupo nje ya uumbaji wake. Pia, hadhi yake inaupita huo uumbaji wake.
Kwa maneno mengine, kwa kila hali, Mungu ana hadhi ya juu sana kupita vitu na
viumbe vyote alivyoviumba.
Kwa jumla, katika kujibu swali la Mungu ni nani, Katekisimu ya Kanisa Katoliki
(1998) inasema: ―Mungu ni muumba wa mbingu na dunia, muumba wa watu na vitu
vyote na ni Baba mwema.‖ Katika fundisho hilo la kanisa Katoliki, Mungu
anaelezwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi na Baba mwema wa wanadamu.
Kimsingi, katika dini ya Kikristo, Mungu anaitwa majina mengine kama vile
Mwenyezi, Mwenye Enzi, Bwana, Yehova, na Yahwe. Kwa upande wake, Mpalanzi
(2019) anaeleza kuwa, kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, kuna majina 99 ya
kumrejelea Mungu. Baadhi ya majina hayo ni Allah, Al Rahman, Rabuka, na Maliki.
Anafafanua zaidi kwamba kwa kawaida majina hayo huwa na maana ya ndani ya
kuelezea sifa na tabia zake. Kwa mfano, katika Kurani Tukufu, Mungu anaelezwa
katika sura ya 40 (Al Ghafir). Aya ya 64 inasema:
Ni Mwenyezi Mungu aliyekufanyieni ardhi kuwa ni pahala pa
kukaa na mbingu kuwa dari. Na atakutieni sura, na akazifanya
nzuri sura zenu, na akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndiye
168
Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Basi ametukuka
Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Nukuu hii inaonesha dhahiri kuwa Mungu ndiye muumba wa binadamu na vitu vyote
vya duniani na mbinguni. Pia, ni Mtukufu na mtunzaji wa watu na vitu vyote
alivyoviumba. Hivyo, utafiti umebaini kuwa mitazamo ya kidini na ya watu
mbalimbali kuhusiana na dhana waliyo nayo juu ya Mungu, ndiyo inayosababisha
pia, wahusika katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi kupata mitanziko juu ya
dhana hiyo, na wengine kujiua kwa kuona kuwa hakuna Mungu.
Katika riwaya ya Kichwamaji, dhana kuhusu Mungu inasababisha mtanziko kwa
Kazimoto kutokana na madai yake kwamba hakuna Mungu. Hoja hii inamweka
katika wakati mgumu, kwa sababu mtazamo wake unakinzana na mawazo ya wazee
anaojadiliana nao, kiasi cha kuvuruga hata mazungumzo baina yao. Kutokana na
mkinzano huo, mzee mmoja miongoni mwao anaamua kuondoka, huku akitupatupa
mikono yake juu kuonesha kuwa hakubaliani na fikra za Kazimoto. Anasema:
―Mnazungumza na mwehu!‖ Alisema kwa kelele. ―A!
Anasema kwamba hakuna Mungu. Hakuna Mungu! Mtoto wa
nani? Mababu na mababu wamekwenda; wamechukuliwa na
nani? Bangi!‖ (uk. 51).
Hapa mwandishi anaonesha kuwa suala la kuamini juu ya uwepo wa Mungu ni
gumu, kwani kuna mitazamo inayotofautiana juu ya dhana hii. Kutofautiana huko
ndiko kunakosababisha Kazimoto akose jibu sahihi kuhusiana na kuwapo au
kutokuwapo kwa Mungu. Mtanziko wake hauishii katika majadiliano na wazee hao
pekee, bali unajitokeza pia katika majadiliano baina yake na Kalia. Mtanziko huo
anaupata kutokana na namna Kalia anavyoisimulia ndoto yake inayoelezea kuhusu
Mungu. Maelezo yake yanamkanganya Kazimoto na anashindwa kuelewa vizuri
kuhusiana na Mungu anayeelezwa na Kalia. Hili linabainishwa kupitia majadiliano
yao kama ifuatavyo:
―Ulivyoona wewe mbingu iko mbali na dunia?‖
―Hata! Mara fulani fulani Mungu mpenzi alikuwa anaturuhusu
kuja ulimwenguni. Tuliwaona watu, lakini wao walikuwa
hawawezi kutuona. Halafu tulirudi. Tulipokuwa tunafika
mahali fulani mara hali yetu iligeuka tukajiona mbinguni tena.
Hali ya kugeuka tulikuwa tumezoea kuiita kupokelewa na
Mungu Mpenzi.‖
169
―Bado sijakuelewa, yaani mlikuwa mkitembea kwa miguu?‖
―Hapana, tulikuwa tunakwenda tu, hali yetu ilizoea kugeuka
na tukajiona mbinguni tena.‖
―Mlikuwa mnakwenda tu namna gani?‖
―Kwa nini huelewi?‖
―Kwa nini kila mara unasema Mungu Mpenzi?‖
―Kwa sababu tulipokuwa mbinguni tuliona kwamba Mungu
anatupenda vile kwamba tuliona vigumu kumkosea kwa
sababu ya aibu kubwa.‖ (uk. 74).
Majadiliano haya yanaonesha namna Kazimoto anavyopata mtanziko kuhusu dhana
ya Mungu, kwani licha ya kupewa ufafanuzi wa kutosha, bado anaonekana kuwa
mgumu kuielewa. Kutofautiana kwake kimtazamo na namna Kalia anavyoielezea
dhana hiyo inayohusu Mungu, ndiko kunakompa wakati mgumu wa kuielewa dhana
hii. Hii ni kwa sababu haamini kuhusu kuwapo kwa Mungu anayedaiwa kwamba,
ndiye muumba wa ulimwengu kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi.
Vilevile, mtanziko wa Kazimoto kuhusiana na dhana ya Mungu unajitokeza katika
majadiliano baina yake na Manase. Maelezo ya Manase kwamba Mungu hawezi
kufahamika kwa kutumia akili za kawaida yanampa Kazimoto wakati mgumu na
anakosa jibu sahihi kuhusu dhana ya Mungu. Kwa Kazimoto, maelezo ya Manase
yanaonekana ni kama imani ya kinjozi tu, juu ya maana halisi ya maisha kwa
kuyahusha na Mungu kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi.
Majadiliano yafuatayo yanabainisha mtanziko wake juu ya dhana hii:
―Unafikiri nini juu ya watu wasioamini kwamba Mungu
yupo?‖
―Ni wajinga,‖ Manase alisema mara moja.
―Hivi wewe unafikiri mtu asiyeamini Mungu ni mtu gani?‖
Nilimuuliza.
―Ni mtu ambaye anataka kumfahamu Mungu kwa kutumia
kichwa chake. Mungu hawezi kueleweka kwa akili.‖
―Hapo ndipo sikubaliani nawe. Mtu asiyeamini Mungu ni mtu
asiyeamua kuwako kwa Mungu kwa kutumia milango ya
fahamu peke yake. Licha ya milango ya fahamu mtu
asiyeamini Mungu anatumia akili zake. Mimi naona kwamba
bongo pia zaweza kukosea.‖
―Ndiyo, lakini milango ya fahamu ni zaidi. Ndiyo maana
ninasema kwamba lazima vyote viwili viafikiane. Na ndivyo
mtu asiyeamini Mungu afanyavyo. Milango ya fahamu ipo
kusaidiana na ubongo, lakini bongo lazima zikuchukue nafasi
kwanza baada ya kuafikiana.‖
170
―Sioni kwa nini umeingiza ndani mambo ya milango ya
fahamu?‖ Aliuliza.
―Unaona, Manase; mwanadamu ameamua kwamba kuna
Mungu kwa sababu ya hali yake ya woga iletwayo na milango
ya fahamu. Kwa hiyo mtu anayeamini kwamba Mungu yupo
ni yule aamuaye kwa kufuata milango ya fahamu zake. Kwake
fahamu zinatawala bongo.‖
―Kama ni vile basi, ninaona kwamba awezaye kutueleza vizuri
zaidi juu ya jambo hili la Mungu ni yule ambaye fahamu zake
zinakubaliana na bongo. Hakuna kinachochukua nafasi ya
kwanza.‖ Kazimoto aliendelea:
―Woga umeleta Mungu,‖ niliendelea kufikiri, ―Na woga
umeletwa na mambo yote yanayomzunguka mwanadamu. Na
ujasiri je unaleta nini? Nafikiri unaleta kutoamini Mungu.
Ujasiri umeletwa na juhudi ya mwanadamu katika kuyashinda
mambo mabaya. Kwa hiyo sayansi inaweza kutusaidia
kuelewa jambo hili ingawa ni polepole (kur. 124 - 125).
Pia, Kazimoto anaonekana kuwa ni mfuasi mzuri wa nadharia ya Udhanaishi,
ambayo haiamini kuhusu uwapo wa Mungu anayedaiwa kuwa ndiye muumba wa
ulimwengu kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi. Mazungumzo baina
yake na Manase yanaonesha namna anavyopata mtanziko katika kuamini kuhusu
uwapo wa Mungu. Kauli ya Manase kwamba wasioamini Mungu ni wajinga, kwa
sababu hutumia vichwa vyao tu ili kumwelewa, inampa wakati mgumu zaidi.
Anatofautiana naye kimtazamo kuhusiana na dhana ya Mungu kutokana na fikra
zake kwamba wanaofikiri kuwa kuna Mungu ni waoga. Hii ni kwa sababu
husukumwa tu, na milango yao ya fahamu kuamini na kufikiri hivyo. Mkinzano wa
mawazo baina yake na Manase unasababisha mtanziko na anakosa jibu sahihi la
kumfanya aamini iwapo kuna Mungu au la. Matokeo yanaonesha kuwa,
mkanganyiko anaoupata Kazimoto kuhusu kuwapo au kutokuwapo kwa Mungu, ndio
unaochangia katika mchakato wa baadaye wa kujiua kwake.
Aidha, dhana kuhusu Mungu inasababisha mtanziko kwa Kazimoto kutokana na
kupitia changamoto mbalimbali katika maisha yake. Changamoto hizo zinampa
wakati mgumu kiasi cha kuhoji nafasi ya Mungu katika maisha yake, ambaye haoni
wala hamtatulii matatizo yake kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi.
Kitendo cha kufiwa na mtoto wake kinampa msukumo zaidi wa kutafakari juu ya
Mungu. Mwandishi kupitia kinywa cha Kazimoto anasema:
171
―Nilianza tena kufikiri juu ya Mungu. Kama kweli alikuwapo
sikuona kwa nini aliweza kufanya ukatili mkubwa kama huo.
Matumaini yetu yote; kazi na taabu tuliyopata yote hayo chini!
Sikuona maana ya maisha.‖ (uk. 180).
Msingi wa kwanza wa nadharia ya Udhanaishi unajadili matatizo halisi
yanayomkumba binadamu, kiasi cha kumkatisha tamaa na hata kusababisha mauti.
Hili ndilo linalompata Kazimoto, kwani anakata tamaa kuhusu maisha kwa kuwa,
haoni tena thamani na nafasi ya Mungu kwake. Anafikia hatua hii kutokana na
mtanziko alio nao kuhusu dhana ya Mungu. Matokeo yake anapanga kuchukua hatua
ya kwenda mahali atakakoishi bila kufikiri wala kujua kwamba anaishi. Kulingana
na utafiti huu, uamuzi huo ni mchakato wake wa kujiua. Suala hili kama
lilivyojadiliwa katika kipengele cha 4.2.2.3, linasawiriwa kupitia majadiliano baina
yake na Sabina (uk. 180).
Majadiliano hayo ni uthibitisho wa wazi kwamba, dhana kuhusu Mungu
inamsababishia Kazimoto mtanziko na anakata tamaa ya maisha kama inavyoelezwa
katika nadharia ya Udhanaishi. Haamini kuhusu uwapo wa Mungu anayedaiwa
kwamba ndiye muumba wa ulimwengu. Hii ni kwa sababu uwapo huo kimsingi
haumjali, bali unampa wakati mgumu kwa sababu ya kupitia changamoto nyingi
katika maisha yake. Kutokana na hilo, anajikuta katika wakati mgumu wa kufanya
uchaguzi wa ama kuendelea kuishi, au kuondoka duniani na kwenda mahali ambako
ataishi bila kufikiri na kuishi pasipo kujua kama anaishi. Hivyo, utafiti umebaini
kwamba mtanziko alio nao Kazimoto kuhusu kuwapo au kutokuwapo kwa Mungu,
ndio unampa msukumo wa kujitafutia uhuru wake kwa nguvu kama inavyoelezwa
katika nadharia ya Udhanaishi na kumwingiza katika mchakato wa kujiua kwake. Hii
ni kwa sababu haoni na haamini kuhusu kuwapo kwa Mungu.
Vilevile, dhana kuhusu Mungu inajitokeza katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo.
Humu inasababisha mtanziko kwa Tembo na wenzake. Hawa wanapata wakati
mgumu kuelewa kuhusu Mungu kutokana na vitendo vinavyohusiana na Mungu,
vinavyofanywa kanisani. Mjadala huo unabainishwa na mwandishi kama ifuatavyo:
―Lakini mimi jambo moja linanishangaza. Siku moja niliingia
kanisani nikaona watu wanapewa vijidudu fulani mdomoni,
hivi ni nini?‖
172
―Mimi zamani nilifikiri ni shilingi. Lakini nilisikia
wanavitafuna,‖ mtu mmoja alisema.
―Wanasema kuna Mungu‖ mwingine aliongeza.
―Ha! Ha!‖ watu walicheka.
―Mbona mtoto wangu Dennis alikaleta nyumbani
tukakachoma kakaungua! Mungu wao yukoje? Kasala alisema.
―Mtoto wangu,‖ Mulele alisema, ―Alipokuwa karibu kupewa
vijitu hivyo alizoea kunung‘unika kwamba mapadre wachoyo
wanakula kipande kikubwa kuliko wengine.‖ (uk. 37).
Kutokana na dondoo hili, tunabaini namna dhana kuhusu Mungu inavyosababisha
mtanziko kwa Tembo na wenzake. Kauli ya mmoja wao kwamba ―… Wanasema
kuna Mungu‖ ni uthibitisho wa wazi kwamba watu hawa hawaielewi vizuri dhana
hiyo inayohusiana na Mungu. Utafititafiti umebaini kwamba, Wakristo, hususani wa
dhehebu la Katoliki, wana desturi ya kula chakula hicho kinachowatatiza Tembo na
wenzake. Kanisa hilo huamini kuwa katika maumbo ya mkate na divai, ndimo
anamopatikana Yesu Kristo, ambaye ni mwana wa Mungu na Mungu kweli. Hili
linathibitishwa katika Biblia Takatifu (1997). Tunaelezwa kuwa:
Nao walipokuwa wakila, Yesu alitwaa mkate, akabariki,
akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, ―Twaeni, mle;
huu ndio mwili wangu.‖ Akakitwaa kikombe, akashukuru,
akawapa, akisema, ―nyweeni nyote katika hiki; kwa maana hii
ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi
kwa ondoleo la dhambi…‖ (Mathayo 26: 26 - 29; Marko 14:
22 - 24; Luka 22: 17 - 20).
Kitendo hiki cha kula mwili wa Yesu, ndicho kinachosababisha mtanziko kwa
Tembo na wenzake. Hii ni kwa sababu, katika hali ya kawaida kinachoonekana
katika macho yao ya kawaida ni mkate halisi, lakini maelezo yanayotolewa yanadai
kuwa, huo ni mwili wa Yesu. Aidha, inaelezwa kwamba tukio la kuugeuza mkate
kuwa mwili wa Yesu, na divai kuwa damu yake, lilifanywa na Yesu mwenyewe
alipokula karamu ya mwisho pamoja na wanafunzi wake. Tukio hili lilifanyika siku
moja kabla ya kufa kifo cha mateso na cha aibu msalabani. Hivyo, kumbukumbu
hiyo hufanyika kupitia mkate na divai, ambavyo kwa imani yao, hugeuzwa na kuwa
mwili na damu ya Yesu. Kwa msingi huo, tukio hili hupewa heshima na thamani
kubwa, kwani mara nyingi waumini hao wapokeapo mwili na damu hiyo, wakati
mwingine hulazimika kupiga magoti na kusali kwa utulivu. Kwa muktadha huo,
dhana hii ni ngumu kueleweka hata kwa baadhi ya madhehebu ya dini, yenye
mtazamo tofauti juu ya imani hiyo.
173
Aidha, katika mafundisho ya imani ya Kikristo, inaaminika kwamba Mungu ni
mmoja, lakini amegawanyika katika nafsi tatu; Mosi, Mungu Baba ambaye ndiye
muumbaji wa mbingu na dunia (Mwanzo 1: 1- 31 katika Biblia Takatifu, 1997). Pili,
Mungu Mwana, yaani Yesu Kristo, ambaye ndiye aliyetumwa na Mungu Baba kuja
duniani kuwakomboa wanadamu kutokana na dhambi zao (Mathayo 3: 16 - 17 katika
Biblia Takatifu, 1997). Na, tatu, Mungu Roho Mtakatifu, ambaye huwaimarisha
waumini kwa kuwafundisha na kuwakumbusha mafundisho ya Yesu (Yohana 20: 19
- 23 katika Biblia Takatifu, 1997). Waumini hao hukiri fumbo hili wanaposali sala ya
Kanuni ya Imani inayosema:
Nasadiki kwa Mungu mmoja, Baba Mwenyezi, Muumba
mbingu na nchi, na vitu vyote vinavyoonekana na
visivyoonekana. Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo,
Mwana wa pekee wa Mungu, aliyezaliwa kwa Baba tangu
milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa
mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila
kuumbwa, mwenye Umungu mmoja na baba, ambaye vitu
vyote vimeumbwa naye. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili
yetu sisi wanadamu, na kwa ajili ya wokovu wetu; akapata
mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kwake yeye Bikira
Maria, akawa mwanadamu. Akateswa kwa mamlaka ya
Ponsyo Pilato, akasulubiwa, akafa akazikwa, akashukia
kuzimu, akafufuka siku ya tatu, kama ilivyoandikwa. Akapaa
mbinguni, amekaa kuume kwa Baba, atakuja tena kwa
utukufu, kuwahukumu wazima na wafu, nao ufalme wake
hautakuwa na mwisho. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu Bwana
mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana, anayeabudiwa na
kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana, aliyenenwa kwa
vinywa vya Manabii. Nasadiki kwa kanisa moja Takatifu
Katoliki la Mitume, naungama ubatizo mmoja, kwa
maondoleo ya dhambi. Nangojea na ufufuko wa wafu na
uzima wa milele ijayo. Amina (Misale ya Waumini, 1993:
424).
Kwa hakika, dhana kuhusu Mungu ni ngumu kueleweka na inasababisha mtanziko
kwa Tembo na wenzake. Matokeo yake wanajikuta katika wakati mgumu wa kupata
jibu sahihi kuhusiana na dhana hiyo kutokana na mkinzano wa mawazo,
unaowakanganya na kuwatatiza. Wanakosa jibu sahihi kuhusu Mungu anayepatikana
katika umbo la mkate, na ndiyo maaana wanacheka, huku wakikejeli na kuonesha
dharau juu ya chakula hicho. Hivyo, kwa kuzingatia nadharia ya Udhanaishi katika
msingi unaopinga kuhusu kuwapo kwa Mungu, imebainika kwamba dhana hii ni
ngumu kueleweka na inawaweka Tembo na wenzake katika mtanziko.
174
Kwa jumla, sehemu hii imejadili sababu mbalimbali za mitanziko ya wahusika kama
zinavyosawiriwa katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi. Sababu hizo
zimegawanywa katika makundi makuu manne, yaani sababu za kijamii, kiutamaduni,
kiuchumi na kifalsafa. Kuhusiana na sababu za kijamii, tumejadili suala la mfumo
wa malezi na mahusiano ya kimapenzi. Katika kipengele cha mfumo wa malezi,
tumeeleza kwamba ili kujenga maadili na misingi bora ya maisha ya watoto, suala
hili linatakiwa kuwa ni jukumu la jamii nzima. Kwa upande wa mahusiano ya
kimapenzi, tumeeleza kuwa hili ni janga, kwa kuwa linasababisha mitanziko na hata
kuwakengeusha wahusika kwa kukiuka misingi na maadili ya jamii. Matokeo yake ni
kwamba wengine hufikia hata hatua ya kuchukua maamuzi ya kujiua kutokana na
kukata tamaa ya kuendelea kuishi.
Kuhusiana na sababu za kiutamaduni tumeeleza kwamba jamii inatakiwa kuenzi na
kudumisha mila na desturi zake. Hata hivyo, ili kuepusha mitanziko kwa wahusika,
imeelezwa kwamba suala hili linatakiwa kufanyika kwa umakini na kwa kuzingatia
miktadha inayotawala na kuongoza jamii husika. Kwa upande wa sababu za
kiuchumi, mambo makubwa yaliyojadiliwa ni umaskini na hali ngumu ya maisha, na
suala la ukosefu wa kazi. Tumebaini kuwa mambo haya husababisha mitanziko kwa
wahusika, kwani huwapa wakati mgumu pale wanaposhindwa kutatua matatizo yao,
kutokana na kuwa katika hali duni za maisha. Vilevile, tumebaini sababu za
kifalsafa. Hizi zimegawanywa katika sehemu kuu tatu; yaani mtanziko kuhusu dhana
ya maisha, dhana ya kifo na dhana kuhusu Mungu. Kuhusiana na masuala haya
matokeo yanaonesha kwamba, kuna mkanganyiko mkubwa wa namna ya kuzielewa
dhana hizi. Hii ni kutokana na kuwapo kwa mitazamo inayotofautiana miongoni
mwa jamii juu ya dhana hizo. Mjadala wetu umeongozwa na nadharia ya
Udhanaishi.
Hatimaye, utafiti umebaini kuwa mitanziko inayowapata wahusika huwaweka katika
hali ngumu ya kuamua jambo la kufanya. Wahusika hao hujikuta wakiwa katika njia
panda, kwani hukabiliwa na wakati mgumu kuhusu uamuzi wa kuchukua. Hii ni kwa
sababu kila uamuzi wapangao kuuchukua, huwa na madhara kwao. Kutokana na hali
hiyo, mara nyingi husukumwa katika kutafuta njia itakayoonekana ni bora kwao na
inayoweza kuonekana kama njia ya kumaliza matatizo yanayokuwa yanawakabili.
Hivyo, mara nyingi husukumwa katika kuchukua maamuzi ya kujiua.
175
Baada ya mjadala huu unaoonesha sababu za mitanziko ya wahusika katika riwaya
teule za Euphrase Kezilahabi, sehemu inayofuata inatathmini uhusiano uliopo baina
usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya
matukio ya kujiua katika jamii.
4.4 Uhusiano wa Mchakato wa Kujiua katika Fasihi na Uhalisi katika Jamii
Katika sehemu hii, tunafanya tathmini ya uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya
mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi na vichocheo vya
matukio ya kujiua katika jamii. Tathmini hii inafanyika ili kubaini iwapo matukio ya
mchakato wa kujiua yanayosawiriwa katika riwaya teule yanaakisi matukio halisi ya
kujiua katika jamii zetu. Msukumo wa kufanya tathmini hii unatokana na mjadala
tuliofanya katika lengo la kwanza la utafiti hii. Katika lengo hilo, tulibainisha usawiri
wa matukio yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase
Kezilahabi. Hivyo, tathmini hii inafanyika ili kuthibitisha kuwa mwandishi wa kazi
za fasihi ni zao la jamii inayomzaa na kumkuza. Pia, huandika kazi kwa kuakisi
mambo halisi yanayotokea katika jamii yake kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na
kijamii.
Sambamba na hilo, katika utafiti huu matukio ya mchakato wa kujiua
yaliyobainishwa na kujadiliwa katika sehemu ya 4.2 yanawahusu wahusika wakuu
watatu. Nao ni Rosa Mistika katika riwaya ya Rosa Mistika, Kazimoto katika riwaya
ya Kichwamaji na Tumaini katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo. Katika mjadala
huo tulibainisha kuwa changamoto mbalimbali za kimaisha zilizowakumba wahusika
hao, zilichangia na kuwafikisha katika hatima ya maisha yao ya kujiua au
kujisababishia kifo.
Katika sehemu hii, tunatathmini uhusiano wa matukio ya mchakato wa kujiua katika
riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii. Uhusiano huo
tunautathmini kwa namna kuu mbili: Mosi, uhusiano wa sababu za matukio ya kujiua
zinazoibuliwa na mwandishi katika riwaya teule na vichocheo vya kujiua kwa
wahusika katika jamii zetu. Pili, uhusiano wa njia za kujiua zinazojichomoza katika
riwaya teule na katika maisha halisi ya jamii zetu.
176
4.4.1 Uhusiano wa Sababu za Matukio ya Kujiua
Katika kuchunguza uhusiano wa sababu za matukio ya kujiua, tunatathmini kile
kilichoibuliwa na mwandishi katika riwaya teule kwa kuhusianisha na vichocheo vya
kujiua katika maisha halisi ya jamii zetu. Utafiti huu umebaini kuwa, mara nyingi
mtu hufikia uamuzi wa kujiua kutokana na kuathiriwa kisaikolojia kiasi cha kukata
tamaa na kuona kama dunia imemkataa na kwamba hawezi kuishi tena. Imebainika
kwamba mtu huyo huamini kwamba, suluhisho lake ni kujiua. Kulingana na tasinifu
hii, kuathirika kisaikolojia ni kufanya mambo tofauti na tabia au haiba iliyozoeleka
kwa mhusika. Kuathirika huko huweza kusababisha mhusika kujiona hana thamani
tena katika jamii yake. Hali hiyo humkatisha tamaa na husababisha aingiwe na
mawazo ya kujidhuru. Matokeo yanaonesha kwamba mawazo hayo huanza na hisia,
kisha hufuatiwa na kitendo chenyewe cha kujiua. Maelezo haya yanaungwa mkono
na Nsolezi12
anayedai kuwa:
Kujiua huanza na hali ya hisia ambapo mhusika kushindwa
kujizuia kutokana na janga au tatizo analokuwa anakabiliana
nalo. Mtu hufikia hatua ya kujiua kutokana na sababu
zinazotibua hisia au kupatwa na matukio ya kuumiza sana,
kiasi cha kuona kwamba hana sababu ya kuendelea kuishi
tena. Sababu hizo ni kama vile kukataliwa na familia yake,
jamii yake, mpenzi wake na kufiwa na mtu au watu wake wa
karibu. Mvurugiko wa kisaikolojia na mtikisiko wa kihisia,
ndio husababisha mtu kujiua. Hata hivyo, si rahisi sana
kuelewa kiasi cha mtikisiko na mvurugiko huo. Suala lililo
bayana ni kwamba kuna uhusiano mkubwa baina ya kujiua na
masuala ya kisaikolojia.
Kwa upande wake, Kubller-Ross (1991) anadai kuwa mtu hufikia uamuzi wa kujiua
baada ya kushindwa kuipokea hali, tukio au jambo fulani zito linalomsumbua na
kumuumiza. Mtaalamu huyo anafafanua hatua tano apitiazo mtu aliyekumbwa na
tatizo kubwa ambalo huweza kumsababisha achukue uamuzi wa kujiua. Hatua hizo
ni: kukataa au kujikana, kupandwa na hamaki au hasira, kukosa jibu sahihi la tatizo
linalomkumba au linalomkabili, kupatwa na mfadhaiko au sonona, na mwisho ni
12 Mahojiano baina ya mtafiti na Dkt. Florentina Nsolezi yalifanyika katika viunga
vya Chuo Kikuu cha Dodoma Novemba 30, 2019. Dkt. Florentina Nsolezi ni
Mhadhiri wa Saikolojia katika Idara ya Elimu ya Saikolojia na Mafunzo ya Mitaala,
Chuo Kikuu cha Dodoma.
177
kushindwa kukubaliana na hali au tukio lenyewe. Kwa kuzingatia hatua hizo,
imebainika kuwa mtu huamua kujiua kutokana na kukataa au kushindwa kulipokea
na kulikubali tatizo au jambo linalokuwa linamkabili. Hali hiyo humkatisha tamaa na
kuchukulia kwamba kujiua kwake, ndilo suluhisho pekee la tatizo lake. Hoja hii
inaungwa mkono na Kano13
anayedai kuwa:
Suala la kujiua ni la kisaikolojia na linauhusiano mkubwa na
aina ya tabia aliyonayo mhusika. Kimsingi, kuna aina mbili za
watu; yaani wandani (introvert) na wasondani (extrovert).
Mara nyingi wanaofikia hatua ya kujiua ni wandani kwa
sababu wana tabia ya kuyakumbatia mambo kutokana na tabia
ya ukimya wao. Aidha, kutokana na tabia yao ya hushindwa
kuwashirikisha matatizo yao watu wao wa karibu, hubaki
wakinung‘unikia na kuumia mioyoni mwao. Matokeo yake,
huweza kufanya hukumu ndani kwa ndani kwa kuchukua hatua
ya kujiua, kutokana na kupata msongo wa mawazo. Wasondani
ni wa wazi, hupenda kuongea na mara nyingi wanapopatwa na
madhila au matatizo, huwashirikisha watu wao wa karibu
ambao huwasaidia katika kuyatatua au kuwapa ushauri wa
namna ya kukabiliana nayo.
Kwa jumla, utafiti umebaini kuwa kuna uhusiano mkubwa baina ya kujiua na
masuala ya kisaikolojia. Hii ni kwa sababu kabla ya kufikia uamuzi wake, mhusika
hupata mvurugiko wa kisaikolojia, ambao humsukuma kufanya kitendo hicho.
Mvurugiko huo husababisha mhusika kupata mtikisiko wa akili, ambao humsukuma
kufanya kitendo cha kujiua kwa kuamini kwamba, hilo ndilo suluhisho la matatizo
yanayomkabili. Matokeo yanaonesha kuwa mhusika hufikia hatua hiyo kutokana na
kukata tamaa, kujiona mpweke, kuwa na tabia ya kuzungumzia masuala ya kujiua,
kupatwa na sonona pamoja na magonjwa mengine ya akili. Mambo haya pia
yamebainishwa na mwandishi wa riwaya teule katika kazi zake kwa kuwa,
ameandika kazi hizo kwa kuyamulika masuala yaliyomo ndani ya jamii yake. Huu ni
13 Mahojiano baina ya mtafiti na Dkt. Erasto Kano yalifanyika katika viunga vya
Chuo Kikuu cha Dodoma Januari 18, 2020. Dkt. Erasto Kano ni Mhadhiri wa
Saikolojia katika Idara ya Elimu ya Saikolojia na Mafunzo ya Mitaala, Chuo Kikuu
cha Dodoma.
178
uthibitisho kuwa, kuna uhusiano mkubwa baina ya sababu za matukio ya kujiua
yanayosawiriwa katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika
jamii. Matukio hayo yanatokana na athari katika masuala ya mapenzi, magonjwa ya
akili na athari katika malezi. Masuala mengine ni mizozo na migogoro ya kifamilia,
vifo vya wapendwa wao, ukosefu wa kazi na matatizo kazini pamoja na changamoto
mbalimbali za maisha.
4.4.1.1 Kujiua Kunakosababishwa na Athari za Mahusiano ya Kimapenzi
Changamoto mbalimbali zitokanazo na athari za mahusiano ya kimapenzi ni
miongoni mwa vichocheo vinavyosababisha watu wengi kujiua. Baadhi ya
changamoto hizo ni mafarakano baina ya wapenzi hao, kushindwa kutimiziana ahadi
za makubaliano yao, kukataliwa, kuachwa na kutelekezwa, na kusalitiana. Matokeo
yanaonesha kuwa mara nyingi wahusika wanapokumbwa na changamoto hizi,
huweza kuathirika kisaikolojia na hata kufikia hatua ya kukata tamaa kwa kuona
kuwa, hawana thamani tena katika jamii. Kutokana na hilo, huweza hata kuchukua
uamuzi wa kujiua kama suluhisho la matatizo yao. Utafiti umebaini kuwa, matukio
ya kujiua yanayotokana na athari za mahusiano ya kimapenzi yanayosawiriwa katika
riwaya teule yanalandana na vichocheo vya matukio ya namna hiyo yanayojitokeza
katika maisha halisi ya jamii zetu. Hii ni kwa sababu kazi za Fasihi ni zao la maisha
halisi ya jamii.
Kwa mfano, katika riwaya ya Rosa Mistika, mwandishi anabainisha athari
zitokanazo na mahusiano ya kimapenzi zinazoweza kusababisha mtu kujiua, hasa
pale wahusika wanaposhindwa kutimiziana na kufikia makubaliano ya malengo na
mipango yao. Suala hili linasawiriwa kupitia kwa mhusika mkuu Rosa Mistika
anayechukua uamuzi wa kujiua. Hii ni baada ya kukataliwa na kuachwa na mchumba
wake Charles. Ifahamike tu kwamba kabla ya kuchukuliwa kwa uamuzi huo, Rosa
anadharauliwa, anachukiwa na kulaumiwa sana na jamii yake kutokana na tabia na
mwenendo wake mbaya wa kujihusisha na kufanya mapenzi ovyo. Jamii hiyo
inathubutu hata kumpa majina kama vile ―kahaba‖, ―malaya‖, ―lab‖, ―mwasherati‖,
―mzinzi‖, na ―mvunja ndoa za watu.‖ Majina haya siyo tu kwamba yanamfanya
aonekane hafai katika jamii yake, bali yanaathiri pia fikra na mtazamo wake
kuhusiana na suala la maisha. Matokeo yake ni kwamba, anafikia uamuzi wa
kuyaona maisha kama upuuzi, ikizingatiwa kwamba miongoni mwa watu wanaotoa
179
shutuma na lawama hizo ni baba yake mzazi, Zakaria, na mchumba wake, Charles.
Zaidi ya hayo, anasikitishwa sana na kitendo cha Charles kuwa miongoni mwa watu
wanaomsimanga na kumlaumu kwa madai ya kukosa bikra, ilhali yeye mwenyewe ni
miongoni mwa watu wenye tabia za kuwaharibia mabinti bikra zao. Kutokana na
hilo, anapata msukumo wa kujiua ili kuyakomesha maisha yake ya taabu na
misukosuko, huku akimwachia Charles ujumbe ulioandikwa kwa wino wa damu.
Ujumbe huo unasema:
… Charles ninajiua kwa ajili yako. Lakini kwa kuwa
ninakupenda, ninakwambia siri moja kubwa uzingatie. Charles
kuoa bikira ni bahati tu wala si kitu cha kutafuta: ukimwonja
mchumba wako kabla ya ndoa si bikira tena, hata kama
alikuwa (uk. 93).
Kwa hakika, ujumbe huo siyo tu kwamba unasikitisha, bali unaibua simanzi na
masononeko kwa Charles mwenyewe na kwa jamii kwa jumla. Aidha, taswira
inayojitokeza tumfikiriapo Rosa akiwa katika hatua ya kuandika ujumbe huo
tulioudondoa, ni ya mtu mwenye masikitiko, aliyekosa matumaini, na anayeyajutia
maisha yake. Anakata tamaa na kukengeuka misingi ya jamii yake. Kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi, haoni tena faida ya kuishi na anatamani
kifo kimchukue haraka. Kipacha (2019) anaeleza kwamba Rosa aliona hakuna
sababu ya kuendelea kuishi katika hali ya maumivu yaliyogubikwa na mkururo wa
usaliti, uonevu, uongo na ukandamizwaji, tangu ngazi ya familia, ujirani, kwenye
taasisi za kishule na jamii kwa jumla. Anafafanua zaidi kuwa, aliamua kufikia
hitimisho hilo kwa kuona kwamba hakuna sababu ya kuendelea kuishi kwa
kusalitiwa. Hivyo, alichagua kujiua kama njia mojawapo ya suluhisho la matatizo
yake.
Matokeo yanaonesha kwamba kitendo cha Rosa kubakwa na kudhalilishwa na
mchumba wake, Charles, ndicho kinachompa nguvu na msukumo wa kuchukua
uamuzi wa kujiua kwake. Anaamua kufanya hivyo kama njia ya kujikomboa na
kujitoa katika mauvivu makali ya kisaikolojia na kiontolojia, yanayoyagandamiza
maisha yake. Anakufa huku akitabasamu kwa sababu ya ugumu wa maisha yake
unaohusishwa na suala la mahusiano ya kimapenzi. Hivyo, anaamua kukiita kifo
hicho kimjie kwa haraka, huku akikifurahia kwa kusema: ―Asante, kifo njoo upesi‖
(uk. 91). Kauli hii inafanana na maelezo ya Camus (1954) anayedai kuwa,
180
madhumuni ya maisha siyo kuishi kwa furaha, bali kufa ukiwa mwenye furaha.
Suala hili ndilo linalomtokea Rosa Mistika, kwani kama inavyoelezwa katika msingi
wa tatu wa nadharia ya Udhanaishi, anautafuta uhuru wake binafsi kwa kukifurahia
kifo ambacho kwake, ndilo suluhisho la maisha yake.
Katika utafiti huu tumebaini kwamba masuala ya watu kupishana katika mapenzi
kama yanavyosawiriwa katika riwaya teule, yamekuwa yakiripotiwa pia mara kwa
mara katika jamii zetu. Tukio mojawapo la namna hiyo lilitokea huko Bukoba tarehe
17.12.2018 na kuripotiwa katika gazeti la Habari Leo la Desemba 19, 2018. Katika
tukio hilo lenye kichwa cha habari kisemacho: ―Amuua Mpenzi Wake Akidai
Amemsaliti, Naye Ajiua‖ inaelezwa kwamba:
Mwalimu Karoli Domisian alimuua mpenzi wake aitwaye
Regina Temu kwa kumnyonga na tai. Baada ya hapo, naye
aliamua kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya
manila, ambapo kabla ya kujiua kwake aliacha ujumbe
unaobainisha kuwa, alifikia uamuzi huo kutokana na mpenzi
wake huyo kumsaliti katika masuala ya mahusiano ya
kimapenzi (kur. 1 – 2).
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa, hili ni miongoni mwa matukio mengi
yanayohusiana na masuala ya mapenzi yanayozikumba jamii zetu. Matukio kama
haya yamekuwa na athari kubwa na yanasababisha watu kujiua au hata kuwaua
wenzi wao. Daniel Marandu, ambaye ni mtaalamu wa Saikolojia kama
anavyoripotiwa katika gazeti la Mtanzania la Novemba 30, 2019, anathibitisha kuwa
matukio haya ni mengi na yameshamiri katika jamii zetu. Katika ufafanuzi wake,
anabainisha sababu mojawapo ya watu kujiua kuwa ni msongo wa mawazo
unaotokana na mahusiano ya kimapenzi. Anasema:
Hii ―stress‖ (msongo wa mawazo) ni mbaya zaidi bora ya
kufiwa na mzazi, unaweza kulia siku mbili ukasahau, lakini ya
mapenzi ni tofauti. Wengi wao, wanajikatia tamaa na
kujinyonga… Watu wasitafute ―solution‖ (njia au ufumbuzi)
ya kudumu kwa tatizo ambalo ni ―temporary‖ (la muda),
kuachwa katika mapenzi ni safari tu kwa sababu atakuja
mwingine. Hivyo, watu wanapaswa kuwa wavumilivu.
Ukizidiwa tafuta mtu mweleze shida yako kwa sababu
unavyomwelezea mtu unatema zile sumu. Kwa hali ilivyo
sasa, misawajiko ya mahusiano ya kimapenzi imekuwa ni
chachu kubwa ya watu kujinyonga kwa sababu wengi,
wamereplace mapenzi na pesa. Hivyo, mtu mwingine
181
hushindwa kujizuia pale anaposikia kuwa, mpenzi wake ana
mahusiano na mtu mwingine (kur. 1 - 2).
Maelezo haya yanaonesha kuwa watu wengi wana msongo wa mawazo unaotokana
na athari za mahusiano ya kimapenzi. Kutokana na hali hiyo, Marandu anawashauri
watu wanaokumbwa na matukio ya aina hiyo, kutafuta mtu wa karibu au wataalamu
wa masuala ya saikolojia na magonjwa ya akili, wanaoweza kuwapa ushauri juu ya
mambo hayo.
4.4.1.2 Kujiua Kunakosababishwa na Athari katika Malezi na Migogoro ya
Kifamilia
Kutofautiana katika suala la malezi ya watoto baina ya wazazi au walezi pamoja na
migogoro ya kifamilia, ni miongoni mwa sababu zinazochochea watu kufikia
maamuzi ya kujiua. Katika hali ya kawaida, kila mtu bila kujali hali aliyo nayo,
anahitaji na anastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake. Halikadhalika, watoto
nao wana haki zao za msingi wanazohitaji kuzipata kutoka kwa wazazi au walezi
wao. Hata hivyo, wazazi au walezi wanapotumia mamlaka yao kwa kuwanyanyasa,
kuwakandamiza, kuwasema vibaya, kuwapiga na hata kuwabana na kuwanyima sana
uhuru wao, huweza kusababisha watoto hao kukengeuka misingi ya malezi yao. Hii
inatokana na ukweli kwamba malezi ya namna hiyo huwaathiri kisaikolojia na
kuwafanya wajitathmini walivyo. Matokeo yake, baadhi yao hufikia uamuzi wa
kujiona kuwa hawafai na hawastahili kuendelea kuishi. Hivyo, kama inavyoelezwa
katika msingi wa nne wa nadharia ya Udhanaishi, wengine huchukua uamuzi wa
kujiua kama suluhisho la matatizo yanayokuwa yanawakabili.
Suala hili limesawiriwa vyema katika riwaya ya Rosa Mistika. Katika riwaya hii,
mwandishi anamtumia Rosa Mistika kama kipaza sauti chake kwa kulalamika na
kuhoji aina ya malezi yanayopaswa kutolewa kwa watoto. Utafiti umebaini kwamba,
Rosa Mistika anachukizwa na kulalamikia malezi ya ukali, vitisho, ukatili, na
kunyimwa uhuru kutoka kwa baba yake, Zakaria, pamoja na masista wa sekondari ya
Rosary. Hali hiyo inamsukuma mwandishi kujaribu kuudodosa uwezo na nafasi ya
fikra za wazazi na dini kuhusu suala la malezi ya watoto, hususani wa kike.
Anazisuta fikra za kuwalea watoto kwa kuwanyima uhuru wao kama anavyofanyiwa
Rosa Mistika, huku Zakaria akijisifu kwamba anajua kuwalea mabinti zake (uk. 9).
182
Matokeo yanaonesha kwamba uhusiano wa Rosa na baba yake ulibadilika baada ya
kutambua ukweli kuwa, chanzo cha matatizo yake ni malezi kutoka kwa baba yake.
Matatizo hayo yalizusha mgogoro wa kimalezi kama unavyojidhirisha kupitia
majibizano baina yao. Hapo ndipo Rosa anafikia hatua ya kumtamkia baba yake
maneno makali aliyoyatunza moyoni mwake kwa muda mrefu. Anasema: ―Kila
wakati unatuchunga. Unafikiri utatuoa wewe!‖ (uk. 58). Kauli hii inaonesha kwamba
uhusiano wao umevurugika na umegeuka kuwa uadui baina yao.
Kutokana na hilo, utafiti umebaini mkengeuko wa wazi wa kimalezi, kwa kuwa Rosa
hakubaliani tena na aina ya malezi anayoyapata kutoka kwa baba yake. Athari za
kisaikolojia zitokanazo na malezi ya ukali, ya kukandamizwa, kubanwa na
kunyimwa uhuru wa kufanya mambo yake, zinajidhihirisha waziwazi. Haoni tena
umuhimu wa kumsikiliza na kuzingatia malezi ya baba yake, aliyoyavumilia kwa
muda mrefu. Matokeo yake, malezi hayo yanakuwa chanzo cha mgogoro baina yake
na baba yake kiasi cha kujenga chuki na uadui dhidi yake. Hii ni baada ya kubaini
kwamba alinyimwa uhuru wake, na hivyo kulazimika kuutafuta kwa nguvu kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi. Mwandishi anathibitisha hili
anaposema kuwa:
Maisha ya binadamu ni kama mti. Mti unahitaji maji, hewa na
mwanga. Kama mti ukinyimwa mwanga wa kutosha na miti
mingine, utarefuka. Utajaribu kupita miti yote ili upate
mwanga. Zakaria aliwanyima binti zake mwanga wakati ule
walipokuwa wakiuhitaji sana. Aliwapiga; aliwakataza
kuzungumza na mvulana yeyote. Nao kama mti walijaribu
kujirefusha ili wapate mwanga, na walirefuka kweli; kiasi cha
kutoweza kuonywa na mtu yeyote (uk. 47).
Dondoo hili linaonesha sababu za wazi za kuathirika kisaikolojia kwa Rosa. Matokeo
yake anaamua kuutafuta uhuru wake kwa nguvu. Hata hivyo, anautumia uhuru huo
vibaya kwa kujitumbukiza katika bahari ya mapenzi kiasi cha kuparamia wanaume
wengi, bila kuchukua tahadhari. Tabia yake inaanza kubadilika akiwa katika shule ya
sekondari ya Rosary. Hii ni baada ya kutoka katika mikono ya baba yake; na tabia hii
inaota mizizi akiwa katika Chuo cha Ualimu Morogoro. Mabadiliko hayo ya kitabia
yanaendelea hata baada ya kumaliza mafunzo yake ya ualimu. Matokeo yake,
anafikia maamuzi ya kujiua kutokana na kushindwa kuhimili mgogoro wa nafsi na
maumivu makali ya kuachwa na mpenzi wake, Charles (uk. 93).
183
Matokeo yake ni kwamba, tukio hilo linamwibulia kesi na analazimika kutoa sababu
za kujiua kwake. Hata hivyo, badala ya kueleza kuwa sababu za kujiua kwake ni
Charles kama alivyoeleza katika ujumbe wake kabla ya kujiua, anaelekeza lawama
hizo kwa Zakaria. Anamlalamikia kuwa, yeye ndiye chanzo cha kuharibika kwa
maisha yake kutokana na aina ya malezi aliyompa (uk. 98). Hii inatupa picha
kwamba katika jamii zetu, wapo wazazi na walezi wenye tabia kama ya Zakaria.
Hawa huwalea watoto wao kwa mkono wa chuma, huku wakiwabana na
kukandamiza uhuru na haki zao za msingi. Hata hivyo, utafiti huu haukusudii
kusema kuwa watoto wanatakiwa kuachwa na kufanya lolote walitakalo, bali
unaeleza kuwa wazazi na walezi wanatakiwa kutambua kwamba, watoto nao wana
haki zao za msingi. Hivyo, wanatakiwa kupewa nafasi ya kusikilizwa ili kuweza
kubaini hisia, matamanio na matarajio yao ya baadaye. Kitendo cha kuwabana sana
na kuwapa malezi ya ukali na vitisho, huweza kuwaathiri kisaikolojia. Pia,
kuchochea na kusababisha migogoro na mizozo baina yao na wazazi au na walezi
wao. Kulingana na nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi mizozo na migogoro hiyo
husawiriwa ndani ya fasihi ili kuficha mambo anuwai ya kijamii ambayo
hayajasuluhishwa. Kushindwa kusuluhishwa kwa migogoro hiyo ndiko husababisha
wengine hushindwa kuvumilia mateso na manyanyaso wayapitiayo. Hivyo, huamua
kuchukua maamuzi ya kujiua kama ilivyotokea kwa Rosa Mistika.
Jambo lililo dhahiri ni kwamba matukio ya watu kujiua yakihusishwa na masuala ya
malezi, kama ilivyomtokea Rosa Mistika, yapo na yamekuwa yakitokea mara kwa
mara katika jamii zetu. Wakati mwingine kujiua huko kumekuwa kukisababishwa na
malezi ya kikatili kutoka kwa wazazi au na walezi wao au kwa kulelewa na watu
wengine tu pasipo kuwatambua wazazi wao halisi. Kwa mfano, katika gazeti la
Mtanzania la Februari 22, 2019, kuna taarifa inayoeleza kwamba:
Tarehe 19 Februari, 2019, Jasmini Ngoye (miaka 18)
mwanafunzi wa Sekondari ya Lupanga Manispaa ya
Morogoro, alijiua kwa kujipiga risasi, ambapo kabla ya kujiua
kwake aliacha ujumbe unaoeleza kuwa, yeye ni mtoto
asiyewajua wazazi wake na asiyejua mahali alikozaliwa (kur.
1 – 2).
Tukio la namna hii kama inavyosawiriwa katika riwaya ya Rosa Mistika,
linathibitisha kuwa katika jamii zetu kuna matukio mengi ya watu kujiua
184
yanayohusishwa na aina ya malezi wayapatayo kutoka kwa wazazi au walezi wao.
Kitendo cha Jasmini kulalamika kuwa, alikuwa hawajui wazazi wake wala mahali
alikozaliwa, kinaleta picha kwamba hakuridhishwa na aina ya malezi aliyokuwa
anayapata kutoka kwa walezi wake. Hii inaonesha kwamba alitamani kulelewa na
wazazi wake kama wangekuwepo. Hali hiyo ndiyo iliyomwathiri kisaikolojia kiasi
cha kuongelea na kutabiri juu ya kifo chake kabla ya kuchukua uamuzi wa kujiua.
Sambamba na suala la malezi katika riwaya ya Rosa Mistika, utafiti umebaini
kuwapo kwa migogoro na mizozo ya mara kwa mara baina ya Zakaria na Regina.
Migogoro hiyo ijapokuwa haiwahusu watoto wao moja kwa moja, ukweli ni kwamba
kwa kiasi kikubwa wanapoiona na kuishuhudia huwaathiri kisaikolojia. Hii ni kwa
sababu mara nyingi migogoro na mizozo hiyo itokeapo, huwafanya wanafamilia hao
kuwa na woga na hofu. Pia, huwa ni chanzo cha kukosekana kwa amani, utulivu na
maelewano baina yao (uk. 3). Katika sehemu hiyo mwandishi anaonesha namna
Regina anavyoivumilia migogoro na mizozo inayotokea mara kwa mara katika
familia yake.
Kama inavyoelezwa katika msingi wa tatu wa nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi,
mwandishi anaonesha kwamba usuluhishi wa migogoro unaosawiriwa ndani ya
fasihi na namna anavyoyasuka matukio yake, unaficha tu migongano anuwai ya
kijamii ambayo haijasuluhishwa. Anaonesha kuwa si kila mtu anaweza kuwa na
uvumilivu kama huo wa Regina, kwa kuwa wengine huamua kujiua kama njia ya
kuyakwepa matatizo hayo. Hii ni kwa sababu maisha ya namna hiyo, siyo tu kwamba
huwakosesha furaha, bali huwakatisha tamaa ya kuendelea kuishi kama
inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi. Mfano mzuri ni Rosa Mistika ambaye
haoni sababu ya kuendelea kuvumilia maumivu ya kisaikolojia anayoyapata kutoka
kwa baba yake; hivyo, anaamua kujiua. Anachukua uamuzi huo kutokana na
migogoro ya mara kwa mara baina yake na baba yake, na baada ya kushuhudia
migogoro na mizozo ya muda mrefu anayofanyiwa mama yake.
Matokeo yanaonesha kuwa, kuna uhusiano baina ya migogoro na mizozo
inayosawiriwa katika riwaya ya Rosa Mistika na vichocheo vya migogoro ya namna
hiyo, inayotokea katika mazingira halisi ya maisha ya jamii. Migogoro na mizozo
hiyo kwa kiasi kikubwa, ndiyo huchochea watu kujiua hasa pale wanaposhindwa
185
kuvumiliana. Kwa mfano, katika gazeti la Mwananchi la Februari 19, 2018
linaripotiwa tukio la kujiua kwa mwalimu Respicius Kazimbaya (46) wa shule ya
msingi Dutumi, mtaa wa Kambitano, Kata ya Lukobe Mkoani Morogoro. Taarifa
hiyo inaeleza kuwa:
Tukio hilo lilitokea Februari 17, 2018 kutokana na migogoro
na mizozo ya kifamilia na kwamba mwalimu huyo, alichukua
uamuzi wa kumuua mkewe, Scrinda Andrew Magumba (42),
kwa kumkatakata mapanga kichwani na shingoni. Pia,
alimchomachoma sehemu mbalimbali za mwili wake kwa
kutumia kitu chenye ncha kali. Kisha, siku moja baada ya
tukio hilo, mwili wa mwalimu huyo, ulikutwa ukining‘inia
kwenye mti wa mwembe, akiwa amejinyonga kwa kutumia
kitenge. Akithibitisha kutokea kwa tukio hili, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mororogo Ulrich Matei alisema kuwa, taarifa
za awali zilibaini kwamba, ugomvi wao ulitokana na
mwanaume huyo kutaka kuuza nyumba yao, iliyoko Lukobe
Manispaa ya Morogoro. Jambo hilo, lilipingwa vikali na mke
wa mwalimu huyo kiasi cha kuzusha mgogoro, uliosababisha
kutokea kwa vifo hivyo (uk. 4).
Utafiti umebaini kuwa, hili ni tukio mojawapo miongoni mwa matukio mengi
yanayotokana na migogoro na mizozo ya kifamilia, yanayozikumba jamii zetu.
Migogoro na mizozo hiyo inahusiana sana na ile inayosawiriwa katika riwaya ya
Rosa Mistika, kama ilivyokwisha kujadiliwa hapo awali katika kipengele hiki. Kwa
mantiki hiyo, mwandishi anaibua migogoro na mizozo hiyo ili kuipa jamii yake
mwanga wa kuyajadili matatizo halisi, yanayomkumba binadamu huyo. Haya ndiyo
yanayojadiliwa katika nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi kwani huyasawiri mambo
mbalimbali yanayoikumba jamii kulingana na mazingira halisi ya maisha yake.
4.4.1.3 Kujiua Kunakosababishwa na Athari za Magonjwa
Magonjwa sugu au kuugua kwa muda mrefu ni miongoni mwa sababu za matukio ya
watu kujiua. Watu hao hukata tamaa ya kuendelea kuishi kutokana na kuathirika
kisaikolojia kiasi cha kushindwa kuendelea kuvumilia mateso au maumivu
wayapatayo. Wengine huchukua uamuzi wa kujiua kutokana na msongo wa mawazo
usababishwao na vitendo vya unyanyapaa na unyanyasaji wafanyiwavyo na watu
wanaowauguza au kuwahudumia. Pia, kutokana na maradhi yao, wengine hufikia
hatua ya kujihisi kwamba wao ni kero kwa familia au kwa jamii, na kwamba,
hawana umuhimu kutokana na kutohitajika kwao tena.
186
Suala hili linasawiriwa katika riwaya ya Kichwamaji kupitia kwa Kazimoto
anayeamua kujiua baada ya kuugua ugonjwa mbaya wa zinaa ulioathiri kizazi chake.
Mwandishi anaeleza kwamba ugonjwa huo aliupata baada ya kufanya mapenzi na
msichana malaya, aitwaye Pili. Kisha, Kazimoto naye, alimwambukiza mke wake
Sabina, ambapo kutokana na athari za ugonjwa huo, alizaa mtoto mwenye kichwa
kikubwa. Kitendo hicho, kilisababisha Kazimoto kupata msongo wa mawazo na
kufikia hatua ya kujiua ili asiendelee kuzaa kizazi kibaya. Hili linathibitishwa na
yeye mwenyewe anaposema kuwa: ―Nimejiua. Siwezi kuendelea kuzaa kizazi
kibaya‖ (uk. 195). Kauli hii inathibitisha kuwa, magonjwa sugu au kuugua kwa muda
mrefu humwathiri mtu kisaikolojia. Pia, huweza kusababisha akengeuke misingi ya
jamii yake na hata kukata tamaa ya maisha na kujiua kama inavyoelezwa katika
msingi wa nne wa nadharia ya Udhanaishi.
Kama inavyosawiriwa katika riwaya ya Kichwamaji, matukio ya watu kujiua
kutokana na magonjwa sugu au kuugua kwa muda mrefu ni mengi na yamekuwa
yakitokea mara kwa mara katika jamii zetu. Gazeti la Nipashe la Desemba 27, 2018,
lenye kichwa cha habari kisemacho, ―Ajinyonga hadi kufa kwa kuchoka kusumbua
familia‖ ni uthibitisho wa kuwapo kwa matukio haya. Taarifa hiyo inaeleza kuwa,
Awetu Makunula (44), mkazi wa Nakayaya Wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma,
alijinyonga hadi kufa kwa madai ya kuchoka kusumbua familia kutokana na hali ya
familia yake. Inaelezwa kwamba Makunula alikutwa akining‘inia juu ya mti wa
mkorosho, jirani na nyumba ya wazazi wake. Akielezea kuhusiana na maisha ya
mkewe, Salumu Namtikwe anasema:
Tulikuwa tumelala wote lakini ilipofika majira ya saa kumi na
moja alfajiri, aliniaga kuwa anatoka nje kufagia uwanja wa
nyumba kwani anataka kuwahi kwenda shambani. Mimi
nikaendelea kulala. Baada ya muda mfupi kupita, nilipata
taarifa kuwa, mke wangu amejinyonga hadi kufa, baada ya
kujining‘iniza katika mti uliopo jirani na nyumbani kwa
wazazi wake. Baada ya kupata taarifa hizo, nilikwenda eneo la
tukio na kumtambua marehemu. Kwa muda mrefu sasa mke
wangu alikuwa akisumbuliwa mara kwa mara na maradhi
mbalimbali. Jambo hilo, lilimfanya aishi maisha ya unyonge,
ya kukosa amani na matumaini, na ya kukatisha tamaa (kur. 3
- 4).
187
Kutokana na tukio hilo ni dhahiri kwamba kujiua kwa Makunula ni mojawapo ya
matukio mengi yanayotokea katika jamii zetu, yanayosababishwa na athari za
magonjwa mbalimbali. Athari hizo kama zinavyosawiriwa kwa Kazimoto katika
riwaya ya Kichwamaji, ndizo zinazosawiriwa pia, katika jamii zetu kutokana na
matukio mengi ya kujiua yanayoripotiwa mara kwa mara. Hii inaonesha kwamba
kuna kulandana kwa ujitokezaji wa matukio ya kujiua yanayosababishwa na athari za
magonjwa mbalimbali katika riwaya teule na katika jamii zetu. Mwandishi wa
riwaya ya Kichwamaji anapotupa picha ya ugonjwa wa ajabu wa Kazimoto, analenga
kuthibitisha kuwa, Fasihi ni dhihirisho la ujumi na ubunifu wa jamii katika
kupambana na mazingira yake. Kutokana na hilo, kama inavyofafanuliwa katika
msingi wa pili wa nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi, kamwe haiwezi kutengwa na
harakati za binadamu zinazoongoza maisha yake.
Kwa jumla, sababu za matukio ya watu kujiua katika jamii zetu ziko nyingi. Hata
hivyo, kwa kuwa katika sehemu hii tulikusudia kutathmini uhusiano wa matukio ya
kujiua, yanayosawiriwa katika riwaya teule na vichocheo vya matukio hayo katika
jamii, kipengele hiki kimetathmini uhusiano wa sababu za kutokea kwa matukio
hayo. Katika kufanya hivyo tumebaini kwamba kuna sababu kuu tatu za matukio ya
kujiua yanayosawiriwa katika riwaya teule yenye uhusiano na vichocheo vya
matukio ya kujiua katika jamii. Matukio hayo ni: kujiua kunakosababishwa na athari
za mahusiano ya kimapenzi, kujiua kunakosababishwa na athari katika malezi na
migogoro ya kifamilia, na kujiua kunakosababishwa na athari za magonjwa.
4.4.2 Uhusiano wa Njia Zinazotumika katika Kujiua
Katika lengo la kwanza la utafiti tulibainisha kuwa, mara nyingi tukio la mtu kujiua
huwa halimtokei ghafla, bali ni mchakato ambao kwa kawaida huchukua muda
mrefu hadi kukamilika kwake. Katika lengo hilo pia, tulieleza kuwa mtu huamua
kujiua kutokana na sababu fulani, ambayo humfikisha katika kiwango cha juu kabisa
cha ubinafsi wake au upeo wa mwisho wa kufikiri kwake. Kutokana na hilo, mtu
huyo huchukua uamuzi wa kujiua kama suluhisho la matatizo yanayomkabili kwa
wakati huo. Hata hivyo, utafiti umebaini kuwa, mazingira aliyokulia mhusika au
jamii inayomkuza na kumlea, huwa na athari kubwa inayoweza kumfikisha mtu huyo
katika hatima ya maisha yake. Pia, mazingira hayo humpa mhusika msukumo wa
kufikiria na hata kuchagua njia anayoona inafaa katika kutimiza matakwa yake. Hii
188
ni kwa sababu mazingira hayo, ndiyo huwezesha mhusika kubaini njia rahisi ya
upatikanaji wa nyenzo za kumsaidia katika kufikia uamuzi anaokuwa ameuchukua.
Hivyo, matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa njia za kujiua zinazosawiriwa katika
riwaya teule, zina uhusiano na njia zinazotumiwa na wahusika katika mazingira
halisi. Miongoni mwa njia hizo ni kujiua kwa kujinyonga, kujipiga risasi, kujichoma
kisu na kwa kutumia sumu.
4.4.2.1 Kujiua kwa Kujinyonga
Kwa mujibu wa BAKITA (2017), kujinyonga ni kitendo cha kujifunga kamba au kitu
chochote kinachoweza kufunga shingoni, aghalabu kwa lengo la kujitoa uhai. Watu
wengi wamekatisha na kupoteza maisha yao kwa kutumia njia hii. Mwandishi wa
riwaya ya Rosa Mistika anaeleza kuwa, hata Rosa Mistika kabla ya kuamua na
kufikiria njia nyingine ya kuitumia katika kujiua kwake, njia hii ya kujinyonga ndiyo
iliyomjia kwanza akilini mwake. Anaeleza kuwa:
Rosa akiwa chumbani mwake, alisikia makofi yakipigwa.
Moyoni mwake alifikiri kwamba wanafunzi walikuwa
wakishangilia kufukuzwa kwake. Akiwa chumbani mwake
Rosa hakuweza kuona ulimwengu. Alitafuta kamba akakosa.
Alichukua mkanda wa gauni lake, aliona haufai (kur. 65 - 66).
Kutokana na nukuu hii, tunabaini namna mazingira aliyomo mhusika
yanavyochangia na kumsaidia katika kuchagua njia ya kujiua kwake. Mwandishi
anaibua mazingira aliyomo Rosa, na ambayo anayatumia katika kutafuta na kupanga
njia anayoiona kuwa rahisi kwake katika kutekeleza kusudio lake la kujiua. Njia ya
kujinyonga ndiyo inayomjia kwa haraka zaidi na anataja vifaa ambavyo ni rahisi
zaidi kupatikana katika mazingira aliyomo — kamba pamoja na mkanda wa gauni
lake. Hii inadhihirisha kwamba, mazingira kama inavyofafanuliwa katika nadharia
ya Sosholojia ya Kifasihi yana athari kubwa kwa mtu anayepanga kujiua. Hii ni kwa
sababu humpa msukumo wa kuamua ni njia gani aitumie katika kutimiza kusudio
lake.
Hata hivyo, ifahamike tu kwamba kabla ya mhusika kuchukua uamuzi wa kujiua,
huwa katika mahangaiko na mfadhaiko unaotokana na mvurugiko wa kisaikolojia.
Aidha, kutokana na ukubwa na ugumu wa suala lenyewe la kujiua, mhusika hujaribu
kutafuta kila njia ili kurahisisha na kufanikisha tukio hilo. Hili ndilo linalomtokea pia
189
Rosa Mistika, kwani anaposhindwa kufanikisha tukio lake la kujiua kwa kujinyonga,
anatafuta njia nyingine inayompa msukumo zaidi wa kutaka kutekeleza kitendo
hicho (uk. 66). Kama inavyoeleza nadharia ya Udhanaishi, anafanya jitihada zote
hizi ili kutafuta uhuru wake binafsi na uwezo wake wa kujifikiria na kujiamulia
mambo yake mwenyewe. Jitihada hizo zinamfanya akate tamaa ya maisha na
kukengeuka misingi ya jamii yake kwa kufanya tukio la kujiua, ambalo kwa hakika
halikubaliki katika jamii yake.
Kwa hiyo, kutokana na mwandishi kutusawiria mazingira na njia za kujiua kwa
Rosa, utafiti huu ulifanyika katika jamii ya mwandishi ili kubaini kuhusu kuwapo au
kutokuwapo kwa matukio ya kujiua pamoja na njia zitumiwazo na wahusika katika
kujiua kwao. Matokeo yanaonesha kwamba katika jamii hiyo, kuna uhusiano wa
matukio na njia za kujiua zinazotumiwa na wahusika kama zinavyosawiriwa katika
riwaya teule. Hili linathibitishwa na Kalogosi14
anayeeleza kuwa:
Matukio ya watu kujiua katika kisiwa chetu cha Ukerewe
hususani, hapa Namagondo, yamekuwa yakiripotiwa mara
kwa mara. Wengine hujinyonga na wengine hujiua kwa
kujitupa katika ziwa au mito. Kwa mfano, mto Nabili
unaoanzia Kazilankanda ni miongoni mwa mito mikubwa
katika jamii ya Wakerewe, ambapo watu wengi hujiua kwa
kujirusha humo. Hufanya hivyo ili kukwepa aibu itokanayo na
mambo mabaya na ya aibu. Mambo hayo ni kama vile:
kukutwa akifanya mapenzi na mke au mume wa mtu,
kudharauliwa na kushindwa kutimiza majukumu mbalimbali
ya kifamilia. Katika jamii ya Wakerewe, matukio ya kujiua
hutokea zaidi kwa wanaume. Aidha, vijana ndio hujiua zaidi
kutokana na masuala ya mahusiano ya kimapenzi na migogoro
ya kifamilia.
Maelezo ya Kalogosi yanathibitisha na kutupa picha halisi ya mambo yanayotokea
katika jamii ya mwandishi na yale yaliyoandikwa katika riwaya teule. Aidha, njia za
14 Mahojiano baina ya mtafiti na Mch. Charles Bita Kalogosi Desemba 18, 2019.
Yalifanyika katika Kijiji cha Namagondo katika kisiwa cha Ukerewe. Mch. Charles
Bita Kalogosi ni Mchungaji katika Kanisa Jipya la Mitume katika kijiji cha
Namagondo.
190
kujiua kwa wahusika zinazoelezwa na mwandishi katika kazi zake, ndizo
zinazoonekana kutumiwa pia na wahusika wanaochukua uamuzi wa kujiua katika
jamii yake. Kulingana na nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi, kazi yoyote ya fasihi
huzuka kutokana na taswira ya kijiografia, kimazingira na kiutamaduni. Hili
linathibitishwa na Kezilahabi mwenyewe anaposema:
Mimi hupendelea zaidi kutumia mandhari halisi. Ukitazama
kwa uangalifu maandishi ya Kiswahili, waandishi ambao
wamefanikiwa ni wale ambao wameweka wahusika wao chini
ya mazingira wanayoyaelewa na hasa yale ya kabila lao. Mimi
mwenyewe niandikapo riwaya zangu nahakikisha kuwa
wahusika wangu wanakulia na kukomaa Ukerewe Kisiwani na
baada ya hapo ninaweza kuwafanya watembee na kukaa mijini
Tanzania nzima (Kezilahabi, 2003).
Hoja ya Kezilahabi kwamba uandishi wake huzingatia mandhari halisi ya maisha
aliyokulia inatupa picha ya kuona kuwa, ubunifu wake katika kuumba wahusika
wake, na namna anavyosuka matukio yake, anahusianisha na maisha halisi ya jamii
yake. Hii inatokana na ukweli kwamba Fasihi ni dhihirisho la ujumi na ubunifu wa
jamii katika kupambana na mazingira yake kama inavyofafanuliwa katika nadharia
ya Sosholojia ya Kifasihi.
Kwa upande mwingine, Simbe15
anaelezea sababu za matukio mengi ya kujiua
kuwakumba zaidi wanaume tofauti na wanawake. Anasema:
Kinachosababisha waanaume wengi hufikia hatua ya kumaliza
au kujiua kabisa tofauti na wanawake, ambao hujaribu kujiua
pasipo kumaliza ni sababu za kimaumbile. Katika mchakato
wote wa kujiua kwamba atamaliza au hatamaliza,
hutegemeana na hali yake ya akili au historia ya magonjwa ya
akili. Hii ni kwa sababu asilimia 90 ya watu wanaojiua, huwa
na tatizo au magonjwa ya akili.
15 Mahojiano baina ya mtafiti na Dkt. Gema Peter Simbe Novemba 29, 2019.
Yalifanyika katika viunga vya Hospitali ya Magonjwa ya Akili Mirembe. Dkt. Gema
Peter Simbe ni Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili ya Watoto na Vijana
katika hospitali hiyo.
191
Kwa hiyo, utafiti umebaini kuwa mwandishi wa riwaya teule aliamua kuyasawiri
mazingira yenye uhusiano na yale ya jamii yake ili kudhihirisha kuwa, kazi yoyote
ya fasihi ni taswira ya kijografia, kimazingira na kitamaduni ya jamii husika. Pia,
kazi hiyo hufungamana na historia ya jamii husika, kama inavyoelezwa katika
nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi.
Utafiti umebaini kuwa matukio ya watu kujiua kwa kujinyonga, yameshamiri katika
jamii zetu na yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika vyombo mbalimbali
vya habari. Suala hili kama linavyoripotiwa katika gazeti la Habari Leo la Novemba
5, 2018, linathibitishwa na DCP Adriane Magayane ambaye ni Naibu Kamishina wa
Polisi kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, (IGP) Simon Sirro. Katika
taarifa hiyo, Magayane anaeleza kuwa, vitendo vya watu kujiua kwa kujinyonga
vinaongoza nchini, vikifuatiwa na matumizi ya sumu, risasi na kwa kutumia visu.
Anasema:
Watu 262 kati ya 333 waliojiua nchini katika kipindi cha
mwaka 2016 hadi Juni 2018, walijinyonga wakifuatiwa na
watu 67 waliojiua kwa sumu. Aidha, katika kipindi cha Januari
2018 hadi Juni mwaka 2018, mikoa iliyoripoti matukio mengi
ya kujiua ni Mwanza matukio 29, Mbeya 18, Dodoma 11,
Tabora 11 na Shinyanga matukio 8 (kur. 1 – 2).
Aidha, takwimu hizo za kipolisi zinabainisha kwamba katika mwaka 2016 pekee,
watu 131 walijiua. Kati ya hao watu 101 walijiua kwa kujinyonga na watu 30 kwa
kutumia sumu. Mwaka 2017 watu 88 walijiua; kati yao, 71 walijiua kwa kujinyonga,
16 kwa kutumia sumu na mmoja kwa risasi. Pia, katika kipindi cha Januari 2018 hadi
Juni 2018 matukio ya watu kujinyonga yaliongezeka kutoka 71 mwaka 2017 hadi 90
yakifuatiwa na matumizi ya sumu ambayo ni 21. DCP Magayane anaendelea kueleza
kuwa:
Katika kipindi hicho, wanaume waliongoza kwa kujiua kwa
matukio 283 sawa na asilimia 84.98, huku idadi ya wanawake
ikifikia 50 ambayo ni sawa na asilimia 15.02. Taarifa hiyo
inabainisha zaidi kuwa mwaka 2016 wanaume waliojiua
walikuwa 106, sawa na asilimia 80.92, huku wanawake
wakiwa 25, sawa na asilimia 19.08 wakati mwaka uliofuata wa
2017, wanaume waliojiua walikuwa 81, sawa na asilimia
92.05 na wanawake 7, sawa na asilimia 7.95 (uk. 2).
192
Kutokana na taarifa hizi, tunapata picha ya jumla kuwa, tatizo la watu kujiua katika
jamii zetu lipo na ni kubwa. Hivyo, jamii zetu zinatakiwa kuitikia wito wa Shirika la
Afya Duniani, uliotolewa katika vyombo mbalimbali vya habari, likiwemo gazeti la
Mtanzania la tarehe 25 Januari 2018. Wito huo unazitaka jamii zote duniani
kushirikiana katika kulikabili tatizo la watu kujiua. utafiti umebaini kwamba
miongoni mwa njia za kukabiliana na tatizo hili ni kutoa elimu kwa jamii ya namna
ya kuwatambua watu wenye dalili za kutaka kujiua. Aidha, jamii inatakiwa
kuwawahisha hospitalini wale wenye dalili au tatizo la akili. Pia, inatakiwa kuchukua
hatua mbalimbali za kutatua migogoro na matatizo yanayowakumba ili kuwaepusha
na msongo wa mawazo, ambao ni chanzo kikubwa cha watu kujiua.
Akizungumzia sababu za ongezeko la idadi ya watu kujinyonga nchini,
mwanasaikolojia Daniel Marandu kama anavyoripotiwa na gazeti la Mtanzania la
Novemba 30, 2019, anasema kuwa:
Hali hiyo inatokana na mfumo mzima wa maisha kubadilika,
likiwamo suala la upatikanaji wa fedha, ajira na mengineyo.
Unakuta mtu zamani watoto wake walikuwa wanasoma shule
za gharama lakini kutokana na hali ilivyo sasa, anashindwa
kumudu na kukata tamaa. Siku hizi watu wengi wanaachishwa
kazi kwa kupunguzwa katika makampuni mbalimbali pamoja
na wenye vyeti feki na kusababisha watu hao kukata tamaa ya
maisha. Utakuta mtu amefanya kazi miaka 55, lakini leo
anakuja kutumbuliwa kwa cheti feki. Hivyo, anajiona kuwa
hapati hata yale mafao yake ya miaka yote hiyo na mbele
haoni ‗future‘ hivyo anaona bora ajinyonge (uk. 3).
Mtaalamu huyu anatoa picha halisi ya matukio yanayosawiriwa katika jamii, kwani
ni kweli kwamba matukio ya watu kujiua kwa kujinyonga yamekuwa yakiongezeka
siku hadi siku kutokana na mihemko na misukosuko wanayopitia katika maisha yao.
Kujiua huko huchangiwa na mambo mengi, ambayo kwa kiasi kikubwa, huwaelemea
wahusika na kuwasababishia msongo wa mawazo hasa pale wanapokosa majibu
sahihi ya namna ya kukabiliana na changamoto zao za maisha. Tukio mojawapo
linalothibitisha kuwa matukio ya watu kujiua kwa kujinyonga yapo katika jamii,
lilitokea huko Bukoba tarehe 17.12.2018, kama lilivyofafanuliwa katika kipengele
cha 4.4.1.1.
193
Tukio lingine la namna hiyo, lilitokea mnamo tarehe 24.09.2018 katika Kijiji cha
Mwakiligiri kata ya Mhunduru wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza, kama
linavyoripotiwa katika www.ippmedia.com. Taarifa hiyo inaeleza kwamba:
Ndugu Kwilokeje Boniface (35), alimuua mkewe, Shija
Chagula (30), kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni wivu
wa mapenzi. Mwanaume huyo alimpiga mkewe sehemu
mbalimbali za mwili wake na baada ya hapo naye kuamua
kujiua kwa kujinyonga. Kutokea kwa tukio hilo kulitokana na
Boniface kumtuhumu mke wake kuwa, alikuwa akitoka nje
ya ndoa yao. Hivyo, kabla ya tukio hilo Boniface alifagia
uwanja na kuondoka. Baada ya muda mfupi, alirudi
nyumbani na kubaini kuwapo kwa mataili ya baiskeli.
Kutokana na hilo, palizuka ugomvi baina yao na ndipo
alipoamua kumpiga mkewe na kumkaba hadi kufa.
Alipobaini kuwa mke wake alikuwa amefariki, ndipo na yeye
aliamua kujiua kwa kujinyonga.
Zaidi ya hayo, huko Tabora kituo cha Televisheni ya Afrika Mashariki
(https://www.eatv.tv/news/current-affairs/) kinaripoti matukio ya watu wawili
waliojiua kwa kujinyonga mnamo tarehe 31.12.2019. Watu hao ni Basili Stephen
Sungu (38) wa shule ya Ikongolo. Huyu alijinyonga katika dari ya chumba
alichokuwa amelala na mkewe, aitwaye Theresia Jumanne Ally (35). Taarifa hiyo
inaeleza zaidi kuwa, uchunguzi wa awali ulibaini kwamba, wanandoa hao walikuwa
na mizozo ya kifamilia na huenda ndiyo iliyosababisha Basili kuamua kujiua. Tukio
lingine lililotokea katika mtaa wa Juhudi katika Manispaa ya Tabora. Katika tukio
hilo, mjasiriamali ndugu James Albert (22), alikutwa akiwa amejinyonga kwenye
kenchi la sebule ya nyumba yake kwa kutumia mkanda wa begi.
Matokeo yanaonesha kwamba haya ni baadhi tu ya matukio ya watu kujiua kwa
kujinyonga, na yamebainishwa kama ithibati ya kushamiri kwake, yanayotokea katika
jamii zetu siku hadi siku. Aidha, tumebaini kuwa njia za kujiua zinazotumiwa na
wahusika katika riwaya teule zinahusiana na zile zinazotumiwa na wahusika
waliotajwa katika matukio yaliyobainishwa hapo awali katika kipengele hiki. Kwa
mfano, katika riwaya ya Rosa Mistika utafiti umebaini kuwa Rosa anaonekana
akihangaika kutafuta kamba, kisha mkanda wa begi ili aweze kufanikisha azma yake
yake ya kujiua. Vivyo hivyo, wahusika waliotajwa katika matukio yaliyoripotiwa
katika jamii, imebainika kwamba wametumia kamba au mkanda wa begi ili kutimiza
azma zao.
194
4.4.2.2 Kujiua kwa Kujipiga Risasi
Kujipiga risasi ni njia nyingine inayotumiwa na watu katika kuyaondoa maisha yao.
Mara nyingi wahusika huacha ujumbe unaobainisha sababu za kujiua kwao. Utafiti
umebaini kuwa, njia hii kwa namna inavyosawiriwa katika riwaya teule, ina
uhusiano mkubwa na matukio halisi yanayohusishwa na njia hii, yanayotokea katika
jamii. Kwa mfano, katika riwaya ya Kichwamaji mwandishi anabainisha namna
Kazimoto anavyoamua kujiua kwa kujipiga risasi, baada ya kupitia changamoto
mbalimbali za kimaisha. Miongoni mwa changamoto hizo ni vifo vya ndugu zake
ambao ni Rukia, mama yake, mtoto wake, pamoja na Kalia. Kabla ya kufikia uamuzi
huo, mwandishi anamchora Kazimoto akiwa katika kina cha tafakuri kuhusiana na
namna kifo chake kitakavyomjia. Anatafakari njia mbalimbali zinazoweza
kuyaangamiza maisha yake, ikiwamo hiyo ya kujiua (uk. 84).
Katika sehemu hiyo, mwandishi anaitafakarisha hadhira yake juu ya maisha, kifo na
hatima yake. Anamtumia mhusika wake Kazimoto kubainisha hali anayokuwa nayo
mtu mwenye dalili za kujiua. Kinachodhihirika bayana ni kwamba mtu huyo huwa
katika hali na tabia tofauti na ile iliyozoeleka. Huonesha dalili za kuyachukia maisha
na kuwaza mambo yahusianayo na kifo. Aidha, imebainika kwamba mtu huyo
husikia sauti tofauti zikimwita. Sauti hizo humwelekeza na kumpa msukumo wa
kufikiria kifo na namna anavyoweza kujiua. Hii ni kwa sababu, suala la kujiua lina
uhusiano mkubwa na magonjwa ya akili16
kama inavyofafanuliwa katika nukuu
inayosema kuwa:
Kuna uhusiano mkubwa baina ya kujiua na magonjwa ya akili.
Tafiti mbalimbali zinabainisha kwamba kuna baadhi ya
magonjwa ya akili ambapo mgonjwa husikia sauti za watu
wakimwelekeza au wakimhoji na kumlazimisha ajiue. Kwa
hiyo, anaposikia sauti hizo huzifuata na kutekeleza kitendo
hicho. Kwa msingi huo, watu wengi hujiua kwa sababu ya
kusikia sauti, kwani kusikia sauti na kupata msongo wa
mawazo ni sehemu ya magonjwa ya akili. Huwezi kujiua
16 Mahojiano baina ya mtafiti na Dkt. Enock Changarawe Novemba 27, 2019.
Yalifanyika katika viunga vya Hospitali ya Magonjwa ya Akili Mirembe. Dkt. Enock
Changarawe ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya akili katika hospitali hiyo.
195
kama si mgonjwa wa akili. Watu wengi hujiua kutokana na
msongo wa mawazo au mshituko wa jambo fulani, kukata
tamaa ghafla na kadhalika. Mtu mwenye shida ya magonjwa
(msongo wa mawazo) huweza kujiua kwa sababu ya kujiona
kwamba hana thamani duniani na anaona ni bora achukue
maamuzi ya kujiua. Msongo wa mawazo ni chanzo namba
mbili cha vifo vya vijana wenye umri kati ya miaka kumi na
tisa na ishirini na tisa (19 – 29). Kwa mujibu wa takwimu
zilizochapishwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC),
tarehe 30.10.2019, watu milioni mia nne hamsini (M. 450)
duniani wanakabiliwa na tatizo la msongo wa mawazo. Hali
hiyo husababisha wengi wao kupata tatizo la afya ya akili.
Baadhi ya watu hao hupata wakati mgumu wa kutafuta
matibabu kutokana na unyanyapaa unaohusishwa na tatizo la
afya ya akili. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba kuna uhusiano
mkubwa kati ya magonjwa ya akili na kujiua, ingawa wengi
wanaweza kuwa si wangonjwa wa akili wa muda mrefu bali
huweza kupata msongo wa mawazo wa ghafla na kujiua.
Kimsingi, kitendo cha kusikia sauti na kupata msongo wa mawazo, ni dalili
mojawapo ya magonjwa ya akili. Hii ina maana kwamba suala la mtu kujiua kama
lilivyoelezwa hapo awali, lina uhusiano mkubwa na masuala ya magonjwa ya akili.
Suala hili linaungwa mkono na Ng‘ambi17
anayesema kuwa:
Kuna baadhi ya magonjwa ya akili ambapo mgonjwa husikia
sauti za watu wakimhoji na kumtaka ajiue kabla watu wengine
hawajamuua. Mara nyingi mtu huyo hupata msukumo wa
kuzisikiliza na kuzifuata sauti hizo. Inajulikana kwamba
asilimia tisini ya watu wanaojiua huwa na matatizo ya akili na
asilimia chache zinazosalia hutokana na matatizo mengine.
Hata hivyo, ukiwaza vizuri utagundua kwamba mtu yeyote
anayejiua kwa wakati ule tendo hilo linapofanyika, hali yake ya
akili huwa si sawa. Ifahamike kwamba ugonjwa wowote ule ni
mkusanyiko wa dalili. Hivyo, kila mtu ana tatizo la akili,
ingawa viwango vinatofautiana. Magonjwa ya akili
yanayohusiana na sonona na msongo wa mawazo, huweza
kusababisha mtu kujiua.
17 Mahojiano baina ya mtafiti na Bw. Paschal John Ng‘ambi Novemba 29, 2019.
Yalifanyika katika viunga vya Hospitali ya Magonjwa ya Akili Mirembe. Bw.
Paschal John Ng‘ambi ni Muuguzi Kiongozi katika hospitali hiyo.
196
Maelezo haya yanaleta picha kuwa, binadamu au kiumbe kingine chochote kile
kinaweza kuumwa kiungo fulani katika mwili wake. Kuna watu wanaumwa moyo au
tumbo la uzazi au la kawaida. Hivyo, imebainika kuwa akili nayo inaweza kuumwa
kama ilivyo kwa kiungo kingine chochote. Akili ikiumwa ndipo mgonjwa huanza
kusikia sauti kama vile mtu anamwita na anajiona ni bora afe kwa sababu amepoteza
imani ya kuishi au kujisikia kutokuwa na amani ya kuishi. Hali hiyo ndiyo
iliyomkumba Kazimoto, kwani inaelezwa kuwa kabla ya kuchukua uamuzi wake wa
kujiua, alisikia sauti zikimwita pasipo kujua sauti hizo zinamaanisha nini na zinatoka
wapi. Anasema:
―Nilisimama pale dirishani kwa muda mrefu nikifikiri.
Nilifikiri furaha ilikuwa imetawaliwa sana na huzuni. Salima
ambaye siku moja alitwambia kwamba kwa jambo lile alikuwa
haoni tofauti yetu na ng‘ombe, yeye mwenyewe hana raha
sasa. Wakati nilipokuwa nikifikiri juu ya maisha nilisikia kitu
fulani kama sauti ikiniita‖ ―Kazimoto!‖ Sauti ilisikika
polepole. ―Naam,‖ nilijibu kimoyomoyo. Nilikwenda ndani ya
chumba cha kulala. Sabina alikuwa amejifunika shuka akilia
kwa kwikwi. Nilichukua kitu fulani. Nilikuwa sifahamu jambo
nililokuwa ninafanya, isipokuwa nguvu fulani zilikuwa
zikiniongoza – sauti! Sauti!‖ (uk. 195).
Kwa kuzingatia nukuu hii, matokeo yanaonesha kwamba tukio la mtu kujiua,
huambatana na mvurugiko wa akili yake. Ndiyo maana mwandishi anaeleza kuwa,
Kazimoto akiwa katika mchakato huo wa kujiua anashindwa kutambua kila
kinachomtokea katika maisha yake kwa wakati huo, bali anasukumwa na nguvu isiyo
ya kawaida inayomtaka atimize kusudio lake. Hivyo, ni dhahiri kuwa watu wengi
hujiua kwa kufuata na kusikiliza sauti, ambazo huwaelekeza kufanya tukio la kujiua.
Mwandishi anaonesha kuwa, hata Kazimoto kabla ya kuchukua uamuzi wake wa
kujiua, anatokewa na hali ya namna hiyo na anasikia sauti zikimpa msukumo wa
kufanya tendo hilo. Msukumo huo unamfikisha katika tukio halisi la kujiua kwa
kujipiga risasi huku akiacha ujumbe juu ya meza ukielezea sababu za kujiua kwake
(uk. 195).
Kujiua basi, ni jambo linaloelekeana sana na matendo na ni mchakato unaoambatana
na viashiria na tabia fulani anazoonesha mhusika, kabla ya kitendo chenyewe cha
kujiua. Kwa hiyo, kujiua ni matokeo ya tabia na vitendo hivyo. Mtu mwenye
ugonjwa wa akili huonesha hisia, fikra na tabia zisizokuwa za kawaida. Vilevile,
197
huweza kufanya matendo yasiyokuwa ya kawaida, ijapokuwa mwenyewe huwa
hatambui hali hiyo. Matokeo yanaonesha kuwa magonjwa mengi ya akili
husababishwa na vinasaba vya urithi, sababu za kisaikolojia pamoja na vichocheo
vingine vya kimazingira. Vichocheo hivyo ni kama vile matumizi ya madawa ya
kulevya, maisha magumu, kuzidisha mambo kama vile kusoma sana, mrundikano wa
mambo au matatizo ya kimaisha, pamoja na ulevi. Hata hivyo, imebainika kuwa
binadamu yeyote ana uwezekano wa kupata ugonjwa wa akili wakati wowote bila
kujali kama ni kijana au mzee.
Kwa jumla, utafiti umebaini kuwa matukio ya watu kujiua kwa kujipiga risasi,
yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara na vyombo vya habari katika jamii zetu.
Matukio haya yamekuwa yakihusishwa na masuala mbalimbali kama vile kusalitiana
katika mapenzi baina ya wapenzi au wanandoa pamoja na visasi mbalimbali. Hili
linathibitishwa katika gazeti la Habari Leo la Septemba 11, 2019. Taarifa hiyo inadai
kuwa: ―Watanzania 666 wamejiua kwa kipindi cha miaka minne kinachoanzia 2016
hadi 2019, ambapo kati ya hao, watu 5 wamejiua kwa kujipiga risasi.‖ (uk. 8).
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime anathibitisha hili katika mazungumzo
yake na waandishi wa habari kwenye maandhimisho ya Siku ya Kupinga na Kuzuia
Kujiua, ambayo hufanyika kila mwaka Septemba 10.
Tukio lingine la kujiua kwa risasi lilitokea katika Mkoa wa Mwanza, Mei 25, 2018.
Taarifa ya tukio hilo, ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Ahmed Msangi.
Alielezea tukio hilo kuwa:
Ndugu Maxmilliani Ngedere Tula (miaka 40), alimpiga risasi
mke wake aitwaye Teddy Patrick (miaka 38) kwa kutumia
bastola yenye namba BJ. 30666 yenye usajili 00103129, kisha
naye kujiua kwa kujipiga risasi. Anafafanua zaidi kuwa wote
wawili walikuwa wafanya biashara wa samaki. Anaongeza
kuwa tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya wanandoa hao
kurudi nyumbani wakitokea kwenye shughuli yao ya biashara.
Anaendelea kueleza kuwa, wanandoa hao wakati wakiwa
chumbani kwao, walisikika kama wanagombana ambapo
muda mfupi baadaye, ilisikika milio ya risasi kadhaa huko
chumbani kwao (Global Habari Tv on line Mei 26,2018).
Kutokea kwa tukio hili ni uthibitisho kwamba matukio ya kujiua kwa kutumia njia
mbalimbali yapo katika jamii zetu. Matukio haya kama ilivyoelezwa hapo awali,
198
huchangiwa sana na masuala mbalimbali ya kijamii, yanayofungamana na maisha ya
jamii husika. Hivyo, ni wazi kuwa kuna uhusiano wa njia za kujiua kwa wahusika,
zinazosawiriwa katika riwaya teule na zile zinazotumiwa na wahusika katika maisha
halisi ya jamii.
4.4.2.3 Kujiua kwa Kujichoma Kisu
Hii ni njia nyingine ya kujiua inayosawiriwa katika riwaya teule na katika jamii.
Utafiti umebaini kuwa, kuna uhusiano wa namna njia hii inavyosawiriwa na
wahusika katika riwaya teule na hali halisi ya watu kujiua katika jamii. Kwa mfano,
katika riwaya ya Rosa Mistika mwandishi anamwonesha Rosa Mistika akiwa katika
harakati za kujiua kwa kujichoma kisu, mara tu baada ya kupewa barua ya
kufukuzwa Chuo cha Ualimu Morogoro. Inaelezwa kwamba baada ya kupokea barua
hiyo, anaamua kulala kitandani akilia na kutokwa na machozi mengi, kiasi cha
kuweza kujaza kikombe cha chai, huku kichwa chake kikimwanga. Kilio hicho
kinasababisha amlalamikie na kumlaumu Mungu kwa madai kwamba, ndiye chanzo
cha mateso na mahangaiko yake (uk. 45). Matokea yake anaamua kukata tamaa
kwani haoni sababu ya kuendelea kuishi kama inavyoelezwa katika nadharia ya
Udhanaishi. Mwandishi analithibitisha hili anaposema:
… Mwishowe alikumbuka kwamba alikuwa na kisu kidogo
sandukuni. Alifungua sanduku upesiupesi ili akomeshe taabu
zake na hasira yake kushuka. Alikitoa. Alikikunjua. Rosa
alipasua gauni lake tumboni apate mahali pa kupitishia kisu.
Alifumba macho aliposikia kisu kinagusa tumbo lake. Rosa
alianza kukisukuma polepole ili kiingie tumboni mwake.
Ngozi ya juu ilikuwa imekwisha kwaruzwa aliposikia mkono
wake unashikwa. Rosa alikuwa mikononi mwa Albert (uk.
66).
Dondoo hili linamwonesha Rosa Mistika akiwa katika hali ya mahangaiko, mateso
na maumivu makali, yanayomkatisha tamaa ya maisha yake. Hali hiyo ndiyo
inayompa msukumo wa kufanya maamuzi ya kutaka kujiua kwa kisu pale
anapolazimishwa kuacha chuo na kurudi nyumbani bila ya cheti cha ualimu.
Kutokana na hilo, anaona kuwa maana ya maisha ni upuuzi mtupu. Hivyo, anaamua
kukengeuka misingi ya jamii yake kwa kutaka kufanya kitendo cha kujiua, ambacho
hakikubaliki na ni kinyume na maadili ya jamii yake.
199
Kwa jumla, katika kipengele hiki tumebaini kuwa kuna uhusiano wa njia hii ya watu
kujiua kwa kutumia visu kama inavyosawiriwa katika riwaya ya Rosa Mistika, na
matukio halisi ya kujiua katika jamii. Taarifa kuhusiana na suala hili, inathibitishwa
na gazeti la Habari Leo la Septemba 11, 2019. Inataja watu 219 waliojiua kwa
kujichoma visu kwa kipindi cha miaka minne kinachoanzia 2016 hadi 2019 na
kwamba idadi hiyo inafuatia, baada ya wale waliojiua kwa kujinyonga, ambao ni
367. Zaidi ya hilo, inabainisha wingi wa matukio ya watu kujichoma visu kwa
kipindi hicho cha miaka minne, ambapo kwa mwaka 2016 pekee, matukio hayo ni
131 (uk. 8). Hii ni idadi kubwa ikilinganishwa na miaka mingine.
4.4.2.4 Kujiua kwa Kutumia Sumu
Kujiua kwa kutumia sumu ni njia nyingine inayotumiwa na watu wengi katika
kuyakatisha na kuyafupisha maisha yao. Katika riwaya ya Kichwamaji suala hili
linajitokeza kupitia kwa Kazimoto anayetafakari njia inayoweza kuyaondoa maisha
yake. Miongoni mwa njia hizo ni sumu. Anasema:
―Usiku nilianza kufikiri juu ya kifo. Nilifikiri jinsi kifo changu
kitakavyonijia – kwa ugonjwa, kwa ajali au kwa
kukatwakatwa na wezi? Labda kwa uzee au kwa sumu! ….‖
(uk. 84).
Katika dondoo hili, mwandishi anabainisha njia kadhaa za kujiua, zinazomjia
Kazimoto akilini mwake, ikiwamo ya kutumia sumu. Kwa kufanya hivyo, anatupa
picha na kuthibitisha kuwa tendo la kujiua, huwa halimtokei mtu kwa ghafla bali
huwa ni mchakato wa muda mrefu au mfupi kutegemeana na sababu husika. Tafakuri
inayofanywa na Kazimoto inaonesha kuwa, mchakato wa kujiua kwake unachukua
muda mrefu, ndiyo maana anafikiria hata njia inayoweza kutumika katika kuyaondoa
maisha yake. Hii inatokana na ukweli kwamba kujiua huanza na sababu
inayohusishwa na tukio katika muktadha fulani, ambapo tukio lingine huweza
kutokea ghafla na kufanya mchakato huo, kuwa mfupi na wakati mwingine kuwa
mrefu. Hili linafafanuliwa na Ng‘ambi (keshatajwa) anaposema kuwa:
Kwa hakika, mpaka mtu anafikia tendo lenyewe la kujiua,
huwa anapitia hatua kadhaa. Hatua hizo ni kama vile,
matamanio ya kufa (death wish), mawazo ya kujiua (suicidal
ideas or thoughts), kujirudiarudia kwa viwango vya kufikiria
kujiua na kupanga kujiua pamoja na kuamua njia
atakayoitumia kufikia azma hiyo.
200
Hili ndilo linajitokeza pia kwa Kazimoto, kwani tukio la kujiua kwake halimtokei
ghafla, bali linachukua muda mrefu. Anafikia hatua ya kufikiria njia ya kuitumia
katika kujiua kwake kutokana na kukata tamaa ya maisha.
Kwa upande wa riwaya ya Rosa Mistika, kuna tukio moja tu la msichana mmoja
kumwekea Rosa sumu kwenye maji kwa lengo la kumdhuru. Tukio hilo linamtokea
Rosa akiwa katika shule ya Msingi Nyakabungo, Mkoani Mwanza, ambapo baada ya
kuchemsha maji hayo, yanabadilika rangi. Aidha, maji hayo yanapo mwagwa nje,
kesho yake, sehemu hiyo inageuka na kuwa kichuguu kikubwa (uk.72-73). Hii ina
maana kuwa sumu hiyo iliwekwa kwa makusudi katika maji hayo kwa lengo la
kuyaangamiza maisha ya Rosa Mistika. Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kuwa sumu ni
njia mojawapo inayotumiwa na watu katika kuyaondoa maisha yao au kuyaondoa na
kuyakatisha maisha ya watu wengine.
Nje ya fasihi, utafiti umebaini kuwapo kwa matukio ya watu kujiua kwa kutumia
sumu katika jamii. Gazeti la Habari Leo la Septemba 11, 2019, linabainisha matukio
ya watu waliojiua kwa kutumia sumu kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi 2019 kuwa
ni watu 75. Matukio hayo ni kama ifuatavyo: ―Mwaka 2019 watu 8, mwaka 2018
watu 21, mwaka 2017 watu 16 na mwaka 2016 watu 30‖ (uk. 8). Taarifa hiyo
inabainisha sababu za watu hao kujiua kuwa, ni pamoja na masuala ya mahusiano ya
kimapenzi, ugomvi wa kifamilia, matatizo kazini na ugumu wa maisha. Inaongeza
kuwa msongo wa mawazo, ndio unaowasukuma zaidi watu kujiua kutokana na
kukosa watu wa kuwapa ushauri wa namna ya kukabiliana na vyanzo vyake.
Kutokana na hilo, imebainika kuwa matukio mengi ya watu kujiua kwa njia
mbalimbali ikiwamo ya kutumia sumu, yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara.
Aidha, tukio lingine la mtu kujiua kwa kutumia sumu liliripotiwa na kituo cha
televisheni cha Azam tarehe 30.4.2018. Taarifa hiyo inaeleza kuwa Maganiko Nunda
(42) mkazi wa Geita, aliamua kujiua kwa kunywa sumu tarehe 29.4.2018. Sababu ya
kujiua kwake inatajwa kuwa ni mgogoro baina yake na mkewe, Salome Josefu.
Akisimulia kuhusiana na mgogoro huo, Frank Maganiko, ambaye ni mtoto wa
marehemu, anadai kuwa kwa muda mrefu baba yake alikuwa ametofautiana na
mama yake. Kutokana na hilo, mama yake aliamua kuondoka hapo nyumbani siku
nne kabla ya tukio hilo kutokea. Frank anafafanua zaidi kuwa, mara kwa mara baba
201
yake alikuwa akitishia kwamba atajiua au kuua mmojawapo wa wanafamilia.
Hatimaye, azma yake ikatimia huku akiacha ujumbe unaobainisha sababu za
kuchukua uamuzi huo. Ujumbe huo unasema:
Mimi Maganiko C. Nunda,
Ndugu zangu, na jamii inayonizunguka, nawaomba nimechoka
na manyanyaso ninayoifanyia hii familia yangu, mke pamoja
na watoto mpaka sasa mama watoto wa familia hayupo.
Ukweli hapa mimi ni kikwazo cha kuisumbua familia, sana
sana mke wangu ninachomfanyia imefikia sehemu sasa hata
mimi mwenyewe kimeniumiza na sioni tena umuhimu wa
kuishi popote pale duniani.
Taarifa zaidi kuhusiana na tukio hilo inadai kuwa, kabla ya tukio hilo marehemu
alionekana akinywa pombe nyingi tofauti na hali yake ya kawaida. Kitendo hicho
kiliwashangaza watu wengi. Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa, kulikuwa na
msuguano wa kutoelewana baina yake na mkewe. Kutokana na hilo, ndipo Maganiko
alipoamua kujiua. Hata hivyo, taarifa hiyo ilifafanua kuwa uchunguzi zaidi wa tukio
hilo, ulikuwa bado unaendelea ili kubaini hasa chanzo chake, ikiwa ni pamoja na
kubaini aina ya sumu aliyoitumia.
Kinachojitokeza kupitia tukio hilo ni kwamba jamii haina elimu ya kutosha
kuhusiana na dalili za mtu anayepanga kujiua. Hii inatokana na ukweli kwamba
mhusika alishaanza kuonesha dalili hizo kwa kuongelea masuala ya kujiua au kuua
mmojawapo wa wanafamilia, lakini hakuna aliyeshtuka na kuchukua hatua za
kumsaidia. Pia, kitendo cha mhusika kunywa pombe nyingi tofauti na hali yake ya
mazoea kilitosha kubaini kuwa, hakuwa katika hali yake ya kawaida. Matokeo yake
hata mke wake aliamua kujitenga naye kwa kumwacha peke yake, hadi alipokutwa
na mtoto wake akiwa amejiua. Alifikia hatua hiyo kutokana na kukosa msaada. Hali
hiyo ilisababisha akate tamaa kama inavyoelezwa katika nadharia ya Udhanaishi kwa
kuona kwamba maisha yake hayana maana tena na hana mahali pengine pa kuishi.
Kwa jumla, sehemu hii ilikusudia kufanya tathmini ya uhusiano baina ya usawiri wa
matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya
kujiua katika jamii. Uhusiano huo umechunguzwa kwa namna mbili. Mosi, uhusiano
wa sababu za matukio ya kujiua zinazosawiriwa katika riwaya teule na vichocheo
vya kujiua katika jamii. Pili, uhusiano wa njia za kujiua zinazosawiriwa katika
202
riwaya teule na katika mazingira halisi ya jamii. Tathmini hiyo inaonesha kuwa,
kuna uhusiano mkubwa baina ya sababu za matukio ya kujiua zinazosawiriwa katika
riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii kwa jumla. Hata
hivyo, licha ya kuwapo kwa uhusiano huo, utafiti umebaini kwamba matukio ya
kujiua katika riwaya teule, ni usawiri wa kisanaa wa mwandishi. Hii ina maana kuwa
mwandishi ameamua kuyasawiri matukio hayo kama nyenzo ya kupenyezea na
kupitishia falsafa yake ya Udhanaishi kama kipengele kimojawapo cha kifasihi.
Aidha, tumebaini kuwa kuna uhusiano baina ya njia za kujiua zinazosawiriwa katika
riwaya teule na zile zinazotumiwa na wahusika katika mazingira halisi ya jamii.
Hivyo, kwa kuwa dhima mojawapo ya fasihi ni kuimulika jamii na kusawiri kuhusu
kuwapo au kutokuwapo kwa jambo fulani, utafiti umebaini kwamba suala la kujiua
lipo katika jamii kama linavyosawiriwa katika riwaya teule.
Sambamba na hilo, tumebaini kuwa mwandishi haishii katika kulisawiri tu suala la
kujiua, bali anaihakiki jamii yake kwa kuchunguza mfumo wa maisha pamoja na
mchakato mzima wa mtu hadi kufikia hatua ya kujiua. Vilevile, tumeona kuwa kuna
uhusiano mkubwa kati ya kujiua na masuala ya magonjwa ya akili pamoja na athari
za kisaikolojia. Hii ina maana kwamba mtu hufikia hatua ya kujiua baada ya
kuathiriwa kiakili na kisaikolojia. Pamoja na hayo yote, tasinifu imebainisha kuwa
watu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu dalili za mtu kujiua, licha ya kuwapo
kwa matukio mengi ya watu kujiua katika jamii. Kwa mantiki hiyo, mtafiti anaona
kuwa kama hazitachukuliwa jitihada za kutosha za kuielimisha jamii kuhusiana na
suala la watu kujiua, basi tatizo hili litaendelea kuzikumba na kuziathiri jamii zetu
siku hadi siku.
4.5 Muhtasari wa Sura ya Nne
Kwa jumla, sura hii ilijikita katika kujadili matukio ya mchakato wa kujiua
yanavyosawiriwa katika riwaya ya Rosa Mistika (1971), Kichwamaji (1974), na
Dunia Uwanja wa Fujo (1975). Pia, ilijadili sababu mbalimbali za mitanziko ya
wahusika kama zinavyosawiriwa katika riwaya hizo. Hatimaye, imehitimishwa kwa
kutathmini uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika
riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii.
203
Katika uchunguzi wetu tulibaini kwamba hizi ni riwaya za mwanzo kabisa za
kiuhalisia za Euphrase Kezilahabi. Nazo, zinajikita katika kushughulikia matatizo
halisi yanayozikumba jamii katika mazingira halisi, hususani mazingira ya
mwandishi. Vilevile, tulibaini kwamba riwaya hizi ni za kiuhalisia kwa sababu
zinaakisi hali halisi ya maisha ya jamii husika. Aidha, wahusika wake ni wa kawaida
kwani wanapatikana katika mazingira ya kawaida na wanasawiri tajiriba za maisha
ya jamii husika.
Sura inayofuata inawasilisha muhtasari wa matokeo ya tasinifu hii, mahitimisho
pamoja na mapendekezo ya maeneo yanayohitaji kutafitiwa zaidi.
204
SURA YA TANO
MUHTASARI, HITIMISHO NA MAPENDEKEZO
5.1 Utangulizi
Sura hii inawasilisha muhtasari wa matokeo ya utafiti, hitimisho, na mapendekezo ya
maeneo yanayohitaji utafiti zaidi.
5.2 Muhtasari wa Tasinifu Hii
Tasinifu hii ina jumla ya sura tano. Sura ya kwanza inajenga msingi wa utafiti kwa
kuanza na ufafanuzi wa dhana muhimu zilizotumika katika utafiti huu, usuli wa
tatizo la utafiti, tamko la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, manufaa ya
matokeo ya utafiti, pamoja na mawanda ya utafiti. Lengo kuu la utafiti lilikuwa ni
kuchunguza usawiri wa mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase
Kezilahabi na kuona kama kujiua huko ni mwangwi wa mtanziko wa kijamii au la.
Ili kufikiwa kwa lengo hili kuu, utafiti ulikuwa na malengo mahususi matatu: Mosi,
kubainisha usawiri wa matukio yanayounda mchakato wa kujiua katika riwaya teule
za Euphrase Kezilahabi; pili, kuchunguza sababu za mitanziko ya wahusika
zinazosawiriwa katika riwaya teule; na tatu, kutathmini uhusiano baina ya usawiri wa
matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya
kujiua katika jamii.
Sura ya pili inahusu mapitio ya maandiko na viunzi vya nadharia zilizotumika katika
utafiti huu. Misingi ya nadharia ya Udhanaishi na ile ya Sosholojia ya Kifasihi ndiyo
iliyomwongoza mtafiti, na hatimaye, kufikiwa kwa lengo kuu pamoja na malengo
mahususi. Maandiko yaliyopitiwa yaligawanywa kama ifuatavyo: Mosi, mapitio ya
maandiko kuhusu kazi za Euphrase Kezilahabi kwa jumla; pili, mapitio kuhusu
mchakato wa kujiua katika riwaya teule za Euphrase Kezilahabi; na tatu, mapitio
kuhusu dhana ya kujiua kwa mitazamo ya nje ya Fasihi. Baada ya kupitia maandiko
hayo, mianya mbalimbali ya kiutafiti ilibainishwa. Mianya hiyo ni pamoja na: tafiti
zilizotangulia kushindwa kubainisha kwa kina matukio ya mchakato wa kujiua,
sababu za mitanziko ya wahusika, na kutotathminiwa kwa uhusiano wa usawiri wa
matukio ya kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya kujiua katika jamii. Pia,
tulibaini kwamba tafiti nyingi zimefanywa kwa mwegamo wa nadharia moja tu ya
Udhanaishi pasipo kuhusisha na nadharia nyingine, ikiwamo ya Sosholojia ya
Kifasihi, ili kubaini uhusiano wa matukio ya kujiua katika riwaya na miktadha ya
205
maisha ya jamii. Vilevile, tafiti hizo zilifanywa kipwekepweke kwa jicho la
kisosholojia, kisaikolojia, na kiafya pasipo kuhusishwa na fasihi. Hali kadhalika,
utafiti huu umebaini kwamba tafiti nyingi za kifasihi zilizotangulia, zilishughulikia
tatizo la kujiua kwa kujikita katika matini pekee pasipo kuchunguza hali halisi katika
jamii.
Sura ya tatu imefafanua kwa kina namna utafiti huu ulivyofanyika. Vipengele
muhimu vilivyoshughulikiwa ni usanifu wa utafiti, mkabala wa utafiti, eneo la
utafiti, walengwa wa utafiti, na njia za ukusanyaji wa data. Vipengele vingine ni
mchakato wa ukusanyaji wa data, mbinu za uchambuzi wa data, maadili na itikeli za
utafiti, pamoja na uhalali na uthabiti wa data. Kwa jumla, data zilikusanywa kwa
kutumia mbinu kuu mbili, ambazo ni: usomaji na uchambuzi makini wa matini teule
pamoja na mahojiano na watafitiwa uwandani. Usanifu wa utafiti huu ni wa
kifenomenolojia, na mkabala wa uchanganuzi wa data ni wa kitaamuli. Mbinu
iliyotumika katika uchambuzi wa data ilikitwa katika mwegamo wa kimaudhui.
Mbinu hii ilimwezesha mtafiti kuunganisha, kuainisha, kulinganisha na kufafanua
data zilizopatikana maktabani na zile za uwandani, hivyo, kuwezesha upatikanaji wa
matokeo bora.
Sura ya nne ilihusu uwasilishaji wa data na mjadala wa matokeo ya utafiti. Sehemu
ya kwanza ilihusu ubainishaji wa usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika
riwaya teule za Euphrase Kezilahabi. Utafiti umebaini kwamba matukio ya mchakato
wa kujiua yameshamiri katika riwaya teule zote tatu. Katika riwaya ya Rosa Mistika,
matukio yaliyobainishwa yanamhusu mhusika mkuu, Rosa Mistika, ambayo ni:
kupigwa na baba yake, kuwachongea wasichana wenzake, kuota ndoto, na
kusimamishwa shule, kufumaniwa na kufukuzwa chuo. Matukio mengine ni kutoa
mimba, kujitenga na kutengwa na jamii yake, na kuachwa na mchumba wake,
Charles. Katika riwaya ya Kichwamaji, matukio yaliyobainishwa yanamhusu
mhusika mkuu, Kazimoto. Nayo ni: kunyimwa kazi, Rukia kutiwa mimba, vifo vya
Rukia na mama yake, na kifo cha Kalia. Matukio mengine ni kifo cha mtoto wake,
kuugua ugonjwa wa ajabu, na kujitenga kijamii. Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa
Fujo, matukio ya mchakato wa kujiua yaliyobainishwa ni: matukio ya aibu na
fedheha, na tukio la Tumaini kumuua Mkuu wa Wilaya. Kwa jumla, matokeo ya
utafiti yanaonesha kuwa matukio yanayosawiriwa katika riwaya hizo, ndiyo
206
yaliyounda mchakato wa kujiua kwa wahusika. Vilevile, utafiti umebaini kwamba
wahusika hao kabla ya kuchukua uamuzi wa kujiua, walipitia changamoto nyingi
maishani mwao. Hatimaye, walikosa uvumilivu ambapo, walikata tamaa na
kuchukua uamuzi wa kujiua.
Sehemu ya pili, imejadili sababu za mitanziko ya wahusika zinazosawiriwa katika
riwaya teule za Euphrase Kezilahabi. Utafiti umebaini kwamba sababu mbalimbali
za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, na kifalsafa, kwa kiasi kikubwa, huchangia watu
kupata mitanziko ya kimaisha. Sababu za kijamii zilizobainishwa ni: mfumo wa
malezi na mahusiano ya kimapenzi. Kuhusiana na mfumo wa malezi, tumebaini
kwamba ili kujenga misingi bora na imara ya maisha ya watoto, jamii inatakiwa
kushikamana na kushirikiana katika jukumu zima la malezi. Kwa upande wa
mapenzi, tumebaini kwamba mahusiano ya kimapenzi ni janga linalosababisha
mifarakano na mitanziko katika jamii. Sababu za kiutamaduni zilizobainishwa ni:
urithi wa mali, mila na desturi, pamoja na masuala ya dini na elimu. Vilevile, utafiti
umebaini kwamba masuala haya yanatakiwa kufanyika kwa tahadhari kubwa ili
yasiwe chanzo cha mitanziko katika jamii. Kuhusiana na sababu za kiuchumi,
tumebaini kwamba, hizi huweza kusababisha mtu kukosa mwelekeo wa maisha na
hata kukata tamaa. Sababu zilizojadiliwa ni umaskini na hali ngumu ya maisha na
tatizo la ukosefu wa kazi. Pia, tasinifu inabainisha sababu za kifalsafa ambazo pia,
huweza kuwa chanzo cha mtu kupata mitanziko. Sababu hizo zimegawanywa katika
makundi matatu, ambayo ni: mtanziko kuhusu dhana ya maisha, dhana ya kifo, na
dhana kuhusu Mungu. Utafiti umebaini kwamba dhana ya maisha ni ngumu
kueleweka kutokana na kuwapo kwa mitazamo mbalimbali isiyofanana miongoni
mwa watu. Kuhusiana na suala la kifo na maisha baada ya kifo, nalo pia lina
mitazamo mbalimbali. Kwa upande mwingine, suala la kuwapo au kutokuwapo kwa
Mungu limezua mjadala mkubwa miongoni mwa watu. Mkanganyiko huo, ndio
husababisha mitanziko kwa wahusika.
Katika sehemu yetu ya tatu, tulifanya tathmini ya uhusiano baina ya usawiri wa
matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na vichocheo vya kujiua katika
jamii. Utafiti umebaini kwamba kuna uhusiano mkubwa baina ya matukio ya kujiua
yaliyomo katika riwaya teule na vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii kwa
jumla. Hata hivyo, utafiti umebaini kwamba kwa namna fulani mwandishi wa riwaya
207
teule, aliamua kuyasawiri matukio hayo katika riwaya zake kama mbinu ya kisanaa
ya kuipenyeza na kuipitisha falsafa yake ya Udhanaishi kama kipengele kimojawapo
cha kifasihi.
Hatimaye, sura ya tano imetoa muhtasari, hitimisho na mapendekezo kuhusu tafiti
zijazo. Imeanza na utangulizi wa mambo yaliyoelezwa katika sura hii na kufuatiwa
na muhtasari wa matokeo ya utafiti kwa jumla. Kisha, imetoa hitimisho la utafiti
linalojumuisha vipengele vitatu, ambavyo ni: utoshelevu wa nadharia zilizotumika,
mchango mpya wa utafiti huu, na mapendekezo kuhusu tafiti zijazo.
5.3 Hitimisho la Tasinifu Hii
Sehemu hii inalenga kutoa ufafanuzi wa maeneo makuu matatu, mbayo ni:
utoshelevu wa nadharia zilizotumika, mchango mpya unaotokana na utafiti, na
mapendekezo kuhusu tafiti zijazo.
5.3.1 Utoshelevu wa Nadharia Zilizotumika
Utafiti umetumia nadharia mbili, ambazo ni: Nadharia ya Udhanaishi na nadharia ya
Sosholojia ya Kifasihi. Misingi au mihimili ya nadharia hizi imemsaidia na
kumwongoza mtafiti katika mjadala wa utafiti wake. Nadharia ya Udhanaishi
ilimwongoza katika mjadala wa matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule
na sababu za mitanziko ya wahusika zinazosawiriwa katika riwaya teule za Euphrase
Kezilahabi. Nadharia hii ilikuwa mwafaka katika malengo hayo kwa sababu matukio
ya kujiua na sababu za mitanziko hutokana na mhusika kukata tamaa, kama
inavyobainishwa katika misingi ya nadharia hii. Mjadala wa lengo la tatu ulihusisha
misingi ya nadharia zote mbili. Hii ni kwa sababu lengo hili lilikusudia kutathmini
uhusiano baina ya usawiri wa matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na
vichocheo vya matukio ya kujiua katika jamii. Hivyo, misingi ya nadharia hizi
ilikamilishana, kwani tukio la mtu kukata tamaa na kujiua linahusishwa na misingi
ya nadharia ya Udhanaishi, na vichocheo vya kujiua huchangiwa na mazingira ya
kijamii kama inavyoelezwa katika nadharia ya Sosholojia ya Kifasihi.
Hivyo, mtafiti anaamini kwamba, kwa kuwa nadharia hizo mbili zimejengana na
kukamilishana, matokeo ya utafiti huu yamekidhi haja na kutosheleza ubora na
uthabiti wa kile kilicholengwa. Hii ni kwa sababu matokeo yake yamekidhi kusudio
la mtafiti na anaamini kwamba matokeo haya yatakidhi hata haja na kiu za wasomaji
208
na jamii kwa jumla katika mambo mengi, ambayo hayakufahamika awali kabla ya
kufanyika kwa utafiti huu.
5.3.2 Mchango Mpya wa Matokeo ya Utafiti Huu
Utafiti una mchango mkubwa kwa jamii na taifa kwa jumla kama ifuatavyo:
5.3.2.1 Mchango wa Kijamii
Utafiti una mchango kwa jamii kwa sababu unaipa mwanga wa kutambua kuwa
matukio ya kujiua huwa hayamtokei ghafla, bali ni mchakato kwa anayejiua. Kama
ilivyofafanuliwa katika tasinifu hii, tofauti na tafiti mbalimbali zilizotangulia, kujiua
kulitazamwa kama tukio tu, hivyo kulifanya suala hilo kueleweka kwa mawanda
finyu. Utafiti huu umebaini kwamba kujiua husababishwa na mambo mengi ambayo
humzonga mhusika kabla ya kufikia kitendo chenyewe. Hivyo, matokeo ya utafiti
yataisaidia jamii kuyafahamu baadhi ya matukio ya mchakato wa kujiua, sababu za
mitanziko ya wahusika, na athari za miktadha mbalimbali anayopitia mhusika katika
maisha yake, ambayo huweza kusababisha kufikia maamuzi ya kujiua.
5.3.2.2 Mchango wa Kitaaluma
Mosi, utafiti unaleta mtagusano wa kitaaluma kwa kuzishikamanisha nyuga
mbalimbali zikiwamo za Afya, Saikolojia, Sosholojia, na Fasihi. Kutokana na
mwingiliano huo wa kitaaluma, jamii itaongeza na kupanua welewa zaidi kwamba
suala la kujiua ni mtambuka na linaweza kushughulikiwa na nyuga mbalimbali,
ikiwamo Fasihi.
Pili, ni mchango wa kinadharia na kiuchambuzi. Hii inatokana na ukweli kwamba
watafiti wengi waliozitafiti kazi za Euphrase Kezilahabi walijiegemeza zaidi katika
nadharia ya Udhanaishi. Hivyo, utafiti huu licha ya kuendeleza nadharia hiyo ya
Udhanaishi, pia umetumia nadharia nyingine ambayo ni Sosholojia ya Kifasihi.
Tumefanya hivyo ili kuonesha kuwa kuna nadharia nyingine zinazoweza ama
kusimama peke yake kushughulikia kazi za kidhanaishi au kwa kushirikiana na
nadharia yenyewe ya Udhanaishi katika kuhakiki kazi za Euphrase Kezilahabi.
Tatu, matokeo ya utafiti huu ni chanzo kimojawapo muhimu cha taarifa kwa watafiti
na wasomaji wengine wanaochunguza na kutafiti kazi za Fasihi zenye mwelekeo wa
kujiua. Aidha, kwa kuwa utafiti huu una mawanda ya kisaikolojia, kisosholojia na
209
kiafya, una mchango pia, kwa watafiti wa nyuga hizo, na siyo kwa uga wa Fasihi
peke yake.
5.3.2.3 Mchango wa Kisera
Matokeo ya utafiti huu yanaweza kutumiwa na watunga sera, pamoja na wakuuzaji
mitalaa ya elimu kulipatia uzito suala la kujiua na kuchukua hatua madhubuti za
kuielimisha jamii kuhusu namna ya kujiepusha nalo. Elimu hiyo ni pamoja na
kuzielewa dalili za mtu anayekusudia kuchukua uamuzi wa kujiua, namna ya
kuwasaidia watu wenye dalili hizo na kuepuka unyanyapaa. Kutekelezwa kwa jambo
hili kutaiepusha na kuikinga jamii na balaa hili.
5.3.3 Mapendekezo Kuhusu Tafiti Zijazo
Sehemu hii inatoa mapendekezo yanayotokana na mada ya utafiti uliofanyika kwa
ajili ya tafiti zijazo. Maeneo yanayopendekezwa hayakuwa sehemu ya malengo ya
utafiti wetu. Hata hivyo, kwa kuwa yanahitaji zaidi majibu ya kiutafiti, tunadhani
kwamba ipo haja ya kumakinikiwa na tafiti zijazo.
Pendekezo la kwanza linahusu haja ya kufanyika kwa utafiti kuhusu mchakato wa
kujiua katika jamii nyingine za Tanzania ili kubaini zaidi ukubwa wa tatizo hili
katika jamii kwa upana wake. Hii inatokana na ukweli kwamba kutokana na suala la
muda na rasilimali, utafiti huu haukuweza kuchunguza matukio ya mchakato wa
kujiua katika jamii zote za Tanzania, bali kwa kiasi kikubwa uliilenga jamii ya
mwandishi wa riwaya teule. Hata hivyo, mifano ya jamii nyingine imetolewa kama
ithibati tu ya kile kilichobainika katika jamii ya mwandishi. Hivyo, kwa kuwa
imethibitika kwamba matukio ya mchakato wa kujiua bado yapo katika jamii zetu,
kuna haja ya kufanya utafiti zaidi katika jamii nyingine za Tanzania. Hii itasaidia
kubaini iwapo matukio ya mchakato wa kujiua yaliyobainishwa katika utafiti huu,
yanafanana na kujiua kwa wahusika katika jamii nyingine za Tanzania.
Pendekezo la pili ni wito wa tafiti nyingi zaidi kufanyika katika tanzu nyingine za
Fasihi kama vile Ushairi, tamthiliya, na Fasihi Simulizi. Hii ni kwa sababu matokeo
ya tafiti hizo, yatazisaidia jamii zetu kuelewa mambo mbalimbali yanayozikumba,
likiwemo suala la kujiua. Pia, kueleweka kwa mambo hayo kutayapa uzito zaidi
matokeo ya utafiti huu kuhusu kuwapo kwa matukio ya kujiua pamoja na mazingira
na michakato ya mtu kujiua.
210
Pendekezo la tatu ni kwamba, kwa kuwa utafiti huu umelishughulikia suala la kujiua
kwa kuhusisha masuala ya kisaikolojia, kiafya, na kisosholojia; kuna haja ya suala
hili kutafitiwa pia, kwa kulihusisha na masuala ya Kiikolojia na Kijaala au Ujaala.
Katika mtazamo wa jumla, Ujaala ni hali ya kunasibisha kuwapo kwa viumbe
waliomo duniani, pamoja na hali au matukio yote yawakumbayo, na uwezo wa
Mungu. Hii ina maana kwamba hata uwezo wa kisanii pamoja na mambo
yamtokeayo binadamu, ya ustawi wake na anguko lake, hutokana na kani ya Mungu,
ambayo iko juu ya uwezo wake, huyo binadamu. Hivyo, matukio ya mchakato wa
kujiua yachunguzwe kwamba, hutokea kwa kuhusishwa na mipango ya Mungu,
yaani kwamba kujiua kwa mtu kuchunguzwe kama ni mpango wa Mungu.
Kwa upande wa Kiikolojia, utafiti ufanyike kwa kuhusisha mchakato wa kufa na
kujiua kama sehemu ya kutengeneza uwiano katika jamii kwa manufaa ya viumbe
wote na vizazi vyote. Hii ni kwa kuwa uhakiki wa Kiikolojia huchunguza uhusiano
uliopo kati ya fasihi na mazingira. Hivyo, kufanyika kwa utafiti wenye mwegamo
huo, kutasaidia kutetea na kupigania mazingira na kuinusuru dunia isiangamizwe na
uharibifu wa matendo ya mwanadamu. Aidha, kufanyika kwa utafiti kwa mtazamo
wa Kiikolojia, kutawezesha kuusaili mtazamo unaomwona binadamu kuwa kiini cha
ulimwengu, mlengwa wa kila jambo, mmiliki na mnufaika halali wa mazingira, na
maumbile yote. Kwa kufanya hivyo, utasaidia kumbainisha binadamu kama kiumbe
na zao mojawapo tu la maumbile; na kwamba hana haki kuwazidi viumbe wengine.
211
MAREJELEO
Adolf, G. (2019, Novemba 30). Ajinyonga Baada ya Kuamka na Kumkosa Mkewe
Kitandani. Mtanzania (uk. 3).
Allan, R. (2003). Senior Biology 2. New Zealand: Bio Zone International Ltd.
Awolalu, J. O. (1976). ―What is African Traditional Religion?‖ Studies in
Comparaetive Religion. 10 (2), (1 – 10).
Babbie, E. (1999). The Basics of Social Research. Belmont: Wadsworth Publishing
Company.
BAKITA, (2017). Kamusi Kuu ya Kiswahili ya BAKITA. Dar es Salaam: Longhorn
Publishers Ltd.
BAKIZA, (2010). Kamusi la Kiswahili Fasaha. Kenya: Oxford University Press,
East Africa Ltd.
Balisidya, M. L .Y. (1973). Fasihi ya Kiswahili. Mulika, (2: 12 – 17).
BBCswahili.com. (2018). Dira ya Dunia. Taarifa ya Habari za Dunia. Siku ya
Jumanne, tarehe 25.9.2018, Saa Tatu Usiku.
Brentano, F. (1995). Psychology from an Empirical Standpoint. London: Routledge.
Bryman, A. (2004). Social Research Methods. New York: Oxford University Press.
Camus, A. (1954). The Stranger. New York: Vintage Books.
Camus, A. (1984). The Myth of Sisyphus, and Other Essays. London: Penguin.
Chuachua, R. (2016). Falsafa ya Riwaya za Saaban Robert na Euphrase Kezilahabi
katika Muktadha wa Epistemolojia ya Kibantu. Tasinifu ya Shahada ya
Uzamivu katika Fasihi ya Kiswahili (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha
Dodoma.
212
Cohen, L. na Lawrence, M. (2000). Research Methods in Education. London:
Routledge.
Coser, L. (1963). Sociology through Literature: An Introductory Reader. Prentice
Hall, Englewood Cliffs.
Cruswell, J. W. (2009). Research Design: Qualitative, Quantitative and Mixed
Method Approaches, (toleo la 3). London: Sage Publications.
Densin, N. K. na Lincoln, Y. S. (Wah.), (2000). Handbook of Qualitative Reseach.
London: Sage Publications.
Diegner, L. (2002). Allegories in Euphrase Kezilahabi‘s Early Novels. Swahili
Forum, (ix: 43 – 74).
Diegner, L. (2005). Intertextuality in the Contemporary Swahili Novel: Euphrase
Kezilahabi‘s Nagona and William Mkufya‘s Ziraili Na Zirani. Paper Presented
at 17th
Swahili Collequim in Bayreuty, Mei 21 - 23, 2004. AAP 51: 117 - 125
http://www.ifeas.uni-mainz.de/SwaFo/SF12Diegner.pdf, 10/12/2017, saa 5
Asubuhi.
Durkheim, E. (1979). Suicide: A Study in Sociology (Translated by J. A. Spaulding &
G. Simpson). New York: The Free Press. (Original Work Published in 1897).
Drake, P. and Linda, H. (2011). Practitioner Research at Doctoral Level:
Develioping Coherent Research Methodologies. New York: Routledge and
Taylor & Francis Group.
Enon, J. C. (1998). Education Research, Statistics and Measurement. Kampala
Uganda: Makerere University.
Ezra, F. (2019, Septemba 27). Watu 200 Hujiua Tanzania. Tanzania Daima (uk. 3).
Famila ya Maamkio Mapanda (1997). Biblia Takatifu. Jimbo la Bologna Italia:
Mediagraf, Noventa Padovana PD.
213
Faustine, S. (2017). Falsafa ya Waafrika na Ujenzi wa Mtindo wa Uhalisiajabu
katika Riwaya za Kiswahili. Tasinifu ya Shahada ya Uzamivu katika Fasihi ya
Kiswahili (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dodoma.
Faustine, S. (2019). Falsafa ya Waafrika kama Kijenzi cha Mtindo na Uhalisiajabu
katika Riwaya za Kiswahili. Koja la Taaluma za Insia, Wah. Ponera, A. S na
Z. A. Badru. Dar es Salaam: Karljamer Publishers Limited. Kur. 378 – 401.
Flavian, L. (2012). Usimulizi katika Riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo. Tasinifu ya
Digrii ya Uzamili (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam..
Freeman, E. (1971). The Theatre of Albert Camus (A Critical Study). London:
Methuen and Co. Uk. 5.
Freud, S. (1900). The Interpretation of Dreams. The Complete and Definitive Text,
Translated and Edited by James Strachey (2010). Basic Book Group. New
York: The Hogarth Press, Ltd.
Friedman, M. (1973). Burried Alive: The Biography of Janis Joplin. New York:
Morrow.
Fuluge, A. (2013). Dhana ya Kujiua katika Kazi za Kezilahabi. Tasinifu ya
Kukamilisha Mahitaji ya Masomo ya Umahiri katika Kiswahili
(Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dodoma.
Gay, L. R. (1987). Educational Research: Competence for Analysisi and Application.
Ohio: Merril Publishing Company.
Glucksman, M. L na Kramer, M. (2017). Manifest Dream Content as Predictor of
Suicidality. Psychodynamic Psychiatry, 54(2), (175 – 185).
Hegel, G. W. F. (1956). The Philosophy of History (Tafsiri ya J. Sibree). New York:
Dover Publications Inc.
Hountondji, P. J. (1983). African Philosophy: Myth and Reality. London: Hutchinson
University Library for Africa.
214
Jimbo Kuu Katoliki la Songea (1998). Katekisimu Ndogo ya Kanisa Katoliki.
Peramiho: Peramiho Printing Press.
Karerega, B. D. & Shenk, D. W. (1980). Islam and Christianity. Nairobi: Uzima
Press.
Katare, E. R. (2007). Julius Kambarage Nyerere: Falsafa Zake na Dhana ya
Utakatifu. Dar es Salaam: Creative Prints Limited.
Kaufmann, W. (1976). Existentialism, Religion and Death. New York: Meridian.
Kezilahabi, E. (1971). Rosa Mistika. Dar es Salaam: East Africa Literature Bureau.
Kezilahabi, E. (1973). Dunia Uwanja wa Fujo. Dar es Salaam: East Africa Literature
Bureau.
Kezilahabi, E. (1974). Kichwamaji. DSM: EAPH.
Kezilahabi, E. (1979). Gamba la Nyoka. Arusha – Dar es Salaam: EAP.
Kezilahabi, E. (1985). Cha Mnyonge Utakitapika Hadharani: (Mzalendo, 7 Aprili
1992), Misingi ya Hadithi Fupi, (107 – 113).
Kezilahabi, E. (1985). African Philosophy and the Problem of Literary Interpretation.
Tasinifu ya Shahada ya Uzamivu (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha
Wisconsin Madison.
Kezilahabi, E. (1990). Nagona. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Kezilahabi, E. (2011). Mzingile. Nairobi: Vide – Muwa Publishers Limited.
Kezilahabi, E. (2003). Utunzi wa Riwaya na Hadithi Fupi, katika Makala za Semina
ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III Fasihi. Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (203 – 231).
215
Kipacha, A. (2019). Kifo au Maisha ya Maumivu: Usomaji wa Rosa Mistika ya
Euphrase Kezilahabi kwa Jicho la Kikanushi. Katika Ponera, A. S & Badru, Z.
A. (Wah.), Koja la Taaluma za Insia: Kwa heshima ya Prof. Madumulla (422 -
434). Dar es Salaam: Karljamer Publishers Ltd.
Kitereza, A. (1980). Bwana Muyombokere na Bi. Bugonoka, Ntulanalwo na
Bulihwali, Juzuu ya I na II. Dar es Salaam: Tanzania Printing House.
Kitomari, S. (2018, Desemba 27). Ajinyonga hadi Kufa kwa Kuchoka Kusumbua
Familia. Nipashe (uk. 3).
Kombo, D. K. na Tromp, D. L. (2006). Proposal and Thesis Writing and
Introduction. Nairobi: Pauliness Publications.
Kothari, C. R. (2004). Research Methodology: Methods and Techniques. New Delhi:
New Age International Publishers.
Kothari, C. R. (2009). Research and Methodology: Methods and Techniques. New
Delhi: New Age International Publishing Ltd.
Lyimo, J. (2019, Februari 24). Watoto Wawili Marafiki Wajinyonga. Mwananchi
(uk. 4).
Kubler-Ross, E. (1991). On Death and Dying. New York: Macmillan Publishing Co.
Madumulla, J. S. (1993). Mwandishi wa Riwaya ya Kiswahili na Suala la Ukweli wa
Maisha. Fasihi, Uandishi na Uchapaji, ed by Mulokozi, M. M. & C. G.
Mung‘ong‘o. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press, (141 – 153).
Madumulla, J. S. (2009). Riwaya ya Kiswahili: Nadharia, Historia, na Misingi ya
Uchambuzi. Dar es Salaam: Mture Educational Publishers Limited.
Magesa, L. (1977). African Religion: The Moral Traditionals of Abundant Life.
Nairobi: Pauline Publications Africa.
Magesa, N. J. (1999). Mbinu za Ndoa Visiwani Ukerewe. Dar es Salaam: Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
216
Maltsberger, J. T. (1993). Dream and Suicide. Suicide and Life - Threatening
Behavior. Vol. 23 (1), The American Association of Suidology. New York:
Plenum.
Mason, M. (2011). The Sample Size and Saturation in PhD Studies Using Qualitative
Interviews. Forum: Qualitative Social Reseach, 11(3), (45 – 52).
Mbatiah, M. (1998). Mienendo Mipya katika Uandishi Mpya wa Kezilahabi: Nagona
na Mzingile. Mulika, (24: 1 – 11).
Mbiti, J. S. (1969). African Religions and Philosophy. London: Heinemann.
Mbiti, J. S. (1970). The Concept of God in Africa. London: S.P.C.K.
Mbiti, J. S. (2010). Introduction to African Religion. Kampala: East African
Educational Publishers Ltd.
Mbiti, J. S. (2011). African Religions and Philosophy. Kampala: East African
Educational Publishers Ltd.
Menkiti, I. (1984). Person and Community in African Traditional Thought. Katika R.
Wright (mhariri). African Philosophy, An Introduction of Lanham. MD:
University Press of America.
Merriam, S. B. & Tisdell, E. J. (2016). Qualitative Research: A Guide to Design and
Implementation. 4th
Edition. San Francisco. Jossey-Bass.
Mlaga, W. (2019). Euphrase Kezilahabi kama Mwanafalsafa Kamili: Mifano Kutoka
Riwaya ya Mzingile. Mulika Na. 37, Dar es Salaam: TUKI.
Mlacha, S. A. K. (1985). Wahusika katika Riwaya ya Kiswahili Tanzania. Mulika,
Na.17.
Mlacha, S. A. K. (1991). Point of View as Stylistic Device in Kiswahili Novels.
Kiswahili: Jarida la Uchunguzi wa Kiswahili, (58: 54 – 61).
217
Mlacha, S. A. K na Madumulla, J. S. (1991). Riwaya ya Kiswahili. Dar es Salaam:
Dar es Salaam University Press.
Mnenuka, A. J. (2011). Falsafa ya Maisha katika Ushairi wa Mugyabuso Mulokozi
na Shaaban Robert. Kioo cha Lugha, (9: 104 – 121).
Moustakas, C. (1994). Phenomenological Research Methods, Thousand Oaks, CA:
Sage.
Mpalanzi, L. E. (2019). Makutano kati ya Dini ya Jadi na za Kigeni: Mifano kutoka
Riwaya Teule za Kiswahili. Kioo cha Lugha, (17: 114 – 131).
Mphahlele, E. (1976). A Guide to Creative Writing. Nairobi: EALB.
Msangi, S. E. (2012). Taswira katika Riwaya za Euphrase Kezilahabi: Aina na
Sababu za Kutumiwa kwake katika Rosa Mistika, Nagona na Mzingile.
Tasinifu ya Kukamilisha Mahitaji ya Digrii ya Kwanza katika Sanaa na
Elimu (Haijachapishwa). Chuo cha Waislamu Morogoro.
Msokile, M. (1992). Misingi ya Hadithi Fupi. Dar es Salaam: Dar es Salaam
University Press.
Muhando, P. na Balisidya, N. (1976). Fasihi na Sanaa za Maonesho. Dar es Salaam:
TPH.
Muller, R. W. (1964). The Testament of Samuel Beckett. London: Faber and Faber.
Mulokozi, M. M. (1983). Dunia Uwanja wa Fujo (Mapitio ya Kitabu). Kiswahili:
Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, 50(1), (1 – 12).
Mulokozi, M. M . (2010). ―A Survey of Kiswahili Literature: 1970 - 1980‖, Current
Research Interest: Kiswahili Language and Literature, Writing and Publishing.
University of Dar es Salaam. www.gap.urgent.be/Africafocus 18/11/2018 saa
9.20 usiku.
Mulokozi, M. M. (2017). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam:
KAUTTU.
218
Mungah, C. I. (1999). Dhana ya Maisha katika Novela Mbili za Euphrase
Kezilahabi: Nagona na Mzingile. Tasinifu ya Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji
ya Shahada ya ―Masters of Arts‖ (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Nairobi.
Mung‘ong‘o, C. G. (1977). Mirathi ya Hatari. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota
Publishers Ltd.
Musau, P. M. (1985). Euphrase Kezilahabi: Mwandishi Aliyekata Tamaa. Tasinifu
ya MA (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Nairobi.
Musau, P. M. (1995). Kezilahabi na Thomas Hardy Sarafu ya Pili? Kioo cha Lugha,
(1. Na. 2.
Mwandishi Wetu. (2017, Januari 25). Tanzania ya 27 Afrika Matukio ya Watu
Kujinyonga – WHO. Mtanzania (uk. 4).
Mwandishi Wetu. (2019, Septemba 11). Watanzania 666 Wajiua kwa Visu, Sumu,
Kujinyonga. Habari Leo (kur. 1: 8).
Mwaniki, J. M. & Geoffrey, G. G. (2009). Fundamental of Biology. Dar es Salaam:
Educational Publishers.
Narizvi, S. (1982). The Sociology of Literature of Politics. Australia: Edamund
Burke.
Neubeck, K. (1986). Social Problems: A Critical Perspective. New York: Random
House.
Ndosi, N. K, Mbonde, M. P, na Lyamuya, E. (2004). ―Profile of Suicide in Dar es
Salaam.‖ Dar es Salaam, East African Medical Journal, Vol. 81 No. 4, uk. 207
- 211.
Njogu, K. na Chimerah, R. (2008). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu.
Nairobi: Jommo Kenyatta Foundation.
219
Oriedo, H. E. (2000). Fani katika Riwaya za Shaaban Robert: Kusadikika, Utubora
Mkulima na Siku ya Watenzi Wote. Tasinifu ya Shahada ya Uzamivu
(Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Moi.
Patton, M. Q, na Michael, C. (2002). Qualitative Research Methodology: A Guide to
Using Medicine. London: Sans Frontieres.
Practorius, R. T. (2006). ―Suicide and Community Traumatic Events: Is there a
Connection?‖ Ph.D Thesis, The School of Human Resource Education and
Workforce Development, Texas University.
Ponera, A. S. (2014). Ufutuhi katika Nathari ya Kiswahili: Ulinganisho wa Nathari
za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi. Tasinifu ya Shahada ya Uzamivu
ya Sayansi Jamii katika Fasihi ya Kiswahili (Haijachapishwa). Chuo Kikuu
cha Dodoma.
Ponera, A. S. (2016). Suala la Matumizi ya Nadharia kama Kiunzi cha Tafiti za
Kitaamuli: Mfano wa Matumizi ya Nadharia ya Ukanivali. Journal of
Humanities, 3 (116 – 129).
Ponera, A. S. (2019). Misingi ya Utafiti wa Kitaamuli na Uandishi wa Tasinifu.
Dodoma: Central Tanganyika Press.
Reed, E. (1975). Women’s Revolution: From Matriarchat Clan to Patriarchal
Family. New York: Path Finder Press, Inc.
Robert, S. (2013). Kufikirika. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers.
Sabinus, J. (2018, Novemba 5). Wanaojinyonga Nchini Idadi Yao Inatisha. Habari
Leo (kur. 1 - 2).
Sakkos, T. (2008). ―Existentialism and Feminism in Kezilahabi‘s Novel
Kichwamaji.‖Swahili Forum, (15: 51 – 61).
Selden, R. na Wenzake (2005). A Reader Guide to Contemporary Theory. London:
Pearson Education Ltd.
220
Sengo, T. (2009). Utafiti wa Utani Ukwereni. Dar es Salaam: AERA Kiswahili
Researched Product.
Senkoro, F. E. M. K. (1977). Riwaya ya Kiswahili na Maendeleo ya Umma. Tasinifu
ya Uzamili (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Senkoro, F. E. M. K. (1995). Euphrase Kezilahabi: Shaaban Robert wa Pili. Kioo cha
Lugha, Juzuu 1.
Senkoro, F. E. M. K. (1996/7). Nadharia ya Fasihi na Fasihi ya Kiswahili ya
Majaribio. Kioo cha Lugha 2.
Senkoro, F. E. M. K. (2006). Fasihi ya Kiswahili ya Majaribio: Makutano ya Fasihi
Andishi na Simulizi. Kioo cha Lugha, (4: 22 – 38).
Senkoro, F. E. M. K. (2007). Uhalisiamazingaombwe katika Fasihi ya Kiswahili:
Istilahi Mpya, Mtindo Mkongwe. Kioo cha Lugha, (5: 1 – 12).
Senkoro, F. E. M. K. (2011). Fasihi. Dar es Salaam: KAUTTU.
Schram, T. H. (2003). Conceptualizing Qualitative Inquiry. Upper Sanddle River,
NJ: Merrill Prentice Hall.
Sletteboe, W. (1997). Dilemma: A Concept Analysis, in Journal of Advanced
Nursing 26 (3), (449 – 454).
Sletteboe, W. (1987). Celebrities & Suicide: A Taxonomy and Analysis (1948 -
1983), American Sociological Review, 52(3), (401 – 412).
Taylor, D. J na wenzake. (1997). Biological Science. New York: Cambridge
University Press.
Temples, P. (1959). Bantu Philosophy. Paris: Presence Africaine.
Tiwari, P. & Ruhela, S. (2012). ―Social Isolation & Depression among Adolescent: A
Comparative Perspective‖, 2nd International Conference on Social Science
and Humanity IPEDR vol. 31, IACSIT Press, Amity University, Singapore.
221
TUKI. (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: Oxford University Press.
TUKI. (2014). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: Oxford University Press.
Van Manen, M. (2014). Phenomenology of Practice: Meaning–giving Methods in
Phenomenological Research and Writing. Wulnut Creek, CA: Left Coast
Press.
Vasques, A. S. (1973). Art and Society. New York: Monthly Review Press.
Wafula, R. M na Njogu, K. (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: The
Jomo Kenyatta Foundation.
Wellek, R. na Warren, A. (1949). Theory of Literature. London: Penguin Books Ltd.
Wamitila, K. W. (1997). What‘s in a Name: Towards Literary Onomastics in
Kiswahili Literature AAP 60: Swahili Forum VI, pp. 35 – 44.
Wamitila, K. W. (2002). Uhakiki wa Fasihi, Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi:
Phoenix Publishers Limited.
Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus
Books Publications Limited.
Wamitila, K. W. (2006). Uhakiki wa Fasihi, Misingi, na Vipengele Vyake. Nairobi:
Phoenix Publishers Ltd.
Wamitila, K. W. (2008). Kanzi ya Fasihi: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi.
Nairobi: Vide Muwa Publishers Ltd.
Wanjala, F. S. (2013). Kitovu cha Fasihi Simulizi kwa Shule na Vyuo. Mwanza:
Serengeti Publishers Ltd.
Williams, R. M. (1970). American Society: A Sociological Interpretation. New York:
Random House.
222
Wiredu, K. (1980). Philosophy and African Culture. London: Cambridge University
Press.
Wizara ya Elimu na Utamaduni. (1992). Historia ya Falsafa ya Elimu. Dar es
salaam: National Printing Company.
WHO. (2018). Tanzania ya 27 Afrika Matukio ya Watu Kujinyonga: (Mtanzania, 25
Januari, 2018; uk. 4).
229
B. Miongozo ya Ukusanyaji wa Data
B.1 Mwongozo wa Usomaji na Uchambuzi makini wa Matini
Vyanzo vya Kusomwa Vipengele Sababu
Riwaya teule na vyanzo
mbalimbali vya taarifa
kama vile magazeti,
redio, na televisheni.
Matukio ya mchakato wa
kujiua na sababu za
mtanziko wa wahusika
katika riwaya teule
Kubainisha ujitokezaji
wa matukio ya mchakato
wa kujiua na kubaini
sababu za mitanziko ya
wahusika katika riwaya
teule.
Miktadha ya utokeaji wa
matukio ya mchakato wa
kujiua.
Kubainisha uhusiano wa
sababu za matukio ya
kujiua na njia za
wahusika kujiua.
B.2 Mwongozo wa Mahojiano
B.2.1 Mahojiano kwa Viongozi wa Dini
Jina langu ni Adria Fuluge, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Fasihi ya
Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma. Mada ya utafiti ni: ―Usawiri wa Mchakato wa
Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase Kezilahabi: Ni Mwangwi wa
Mtanziko wa Kijamii?” Lengo la utafiti huu ni kuchunguza na kubaini matukio ya
mchakato wa kujiua katika riwaya teule, pamoja na miktadha ya utokeaji wake katika
jamii ya mwandishi. Kabla ya kuanza mahojiano haya, naomba kukujulisha kuwa
taarifa utakazotoa zitakuwa ni siri baina ya mtafiti na wewe, na zitatumika tu kwa
lengo la utafiti huu. Tafadhali, naomba ushirikiano wako katika mahojiano haya.
1. Tafadhali, unaweza kututajia jina lako na kutupa maelezo mafupi kuhusu
huduma za kiroho unazofanya katika jamii yako.
2. Kwa mtazamo wako, mchakato wa kujiua ni nini?
3. Kwa maoni yako na unavyofahamu, ni matukio gani husababisha watu
kujiua? Je, ni miktadha ya namna gani husababisha mtu kuchukua uamuzi wa
kujiua?
4. Katika vitabu vitakatifu na mafundisho ya dini yako, kujiua kunatazamwaje
na ni adhabu gani humpata anayejiua? Je, unadhani fikra za watu wanaojiua
kuhusu Mungu na maisha yao kwa jumla zikoje?
5. Kwa maoni yako, unafikiri kuna uhusiano gani baina ya matukio
yanayosababisha mhusika kujiua na miktadha (mazingira) ya jamii husika?
230
B.2.2 Mwongozo wa Mahojiano kwa Wananchi wa Ukerewe
Jina langu ni Adria Fuluge, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Fasihi ya
Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma. Mada ya utafiti ni: ―Usawiri wa Mchakato wa
Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase Kezilahabi: Ni Mwangwi wa
Mtanziko wa Kijamii?” Lengo la utafiti huu ni kuchunguza na kubaini matukio ya
mchakato wa kujiua katika riwaya teule, pamoja na miktadha ya utokeaji wake katika
jamii ya mwandishi. Kabla ya kuanza mahojiano haya, naomba kukujulisha kuwa
taarifa utakazotoa zitakuwa ni siri baina ya mtafiti na wewe, na zitatumika tu kwa
lengo la utafiti huu. Tafadhali, naomba ushirikiano wako katika mahojiano haya.
1. Tafadhali unaweza kututajia jina na umri wako?
2. Unamfahamu Euphrase Kezilahabi? Kama ndiyo, elezea ni kwa vipi na kwa
namna gani?
3. Kuna madai kuwa jamii ya watu wanaoishi katika Mkoa wa Mwanza,
hususani katika kisiwa cha Ukerewe, ina tabia ya kujiua. Je, madai hayo yana
ukweli kiasi gani? Na kama ni kweli, ni watu wa rika na jinsia gani zaidi
wanaofanya mambo hayo?
4. Kama madai ya swali la tatu hapo juu ni ya kweli, je, ni miktadha/mazingira
gani husababisha kutokea kwa mambo hayo? Je, nini husababisha watu hao
kujiua? Na, je, kabla ya kujiua kwao, huonesha dalili gani au zipi?
5. Kama madai ya swali la nne hapo juu ni kweli, je, matukio hayo ya mchakato
wa kujiua hutokea wakati gani na katika miktadha au mazingira gani?
Hutumia mbinu gani katika kutimiza azma hiyo?
B.2.3 Mwongozo wa Mahojiano kwa Viongozi wa Serikali
Jina langu ni Adria Fuluge, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Fasihi ya
Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma. Mada ya utafiti ni: ―Usawiri wa Mchakato wa
Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase Kezilahabi: Ni Mwangwi wa
Mtanziko wa Kijamii?” Lengo la utafiti huu ni kuchunguza na kubaini matukio ya
mchakato wa kujiua katika riwaya teule, pamoja na miktadha ya utokeaji wake katika
jamii ya mwandishi. Kabla ya kuanza mahojiano haya, naomba kukujulisha kuwa
taarifa utakazotoa zitakuwa ni siri baina ya mtafiti na wewe, na zitatumika tu kwa
lengo la utafiti huu. Tafadhali, naomba ushirikiano wako katika mahojiano haya.
231
1. Matukio ya watu kujiua yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika
vyombo vya habari hapa nchini. Je, hali ikoje katika Mkoa huu wa Mwanza?
2. Kulingana na unavyofahamu, ni kundi la rika na umri gani limekuwa
likihusishwa na mchakato wa kujiua mara kwa mara?
3. Kama tatizo hili lipo katika Mkoa huu wa Mwanza, je, wanaojiua zaidi ni
wale wanaotoka mjini au vijijini? Kiwango chao cha elimu kikoje?
4. Matukio ya mchakato wa kujiua hutokea zaidi wakati gani na katika miktadha
ya namna gani? Na, je, wanaojiua huacha ujumbe au taarifa yoyote
inayohusiana na tukio la mchakato huo wa kujiua?
5. Kwa nafasi yako ya uongozi serikalini, kuna jitihada gani katika kumaliza au
kutatua na kukabiliana na tatizo hili?
6. Ni miktadha ya namna gani ya kijamii ambayo huweza kusababisha mhusika
kujiua? Je, Serikali hukabiliana vipi na miktadha hiyo ili kupunguza au
kutokomeza matukio haya ya kujiua?
B.2.4 Mwongozo wa Mahojiano kwa Wataalamu wa Saikolojia na Magonjwa ya
Akili
Jina langu ni Adria Fuluge, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Fasihi ya
Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma. Mada ya utafiti ni: ―Usawiri wa Mchakato wa
Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase Kezilahabi: Ni Mwangwi wa
Mtanziko wa Kijamii?” Lengo la utafiti huu ni kuchunguza na kubaini matukio ya
mchakato wa kujiua katika riwaya teule, pamoja na miktadha ya utokeaji wake katika
jamii ya mwandishi. Kabla ya kuanza mahojiano haya, naomba kukujulisha kuwa
taarifa utakazotoa zitakuwa ni siri baina ya mtafiti na wewe, na zitatumika tu kwa
lengo la utafiti huu. Tafadhali, naomba ushirikiano wako katika mahojiano haya.
1. Tafadhali, unaweza kututajia jina lako na kutupa maelezo mafupi kuhusu
huduma za kiafya unazofanya katika jamii yako.
2. Kwa mtazamo wako, kujiua ni nini na mchakato wa kujiua ni nini? Je, kuna
aina ngapi za kujiua?
3. Wewe ni mtaalamu wa saikolojia/magonjwa ya akili. Unadhani kuna
uhusiano gani baina ya masuala ya kisaikolojia/kiakili na mchakato wa
matukio ya kujiua?
4. Je, ni sababu na matukio ya namna gani husababisha mtu kujiua? Je, mtu
anayetaka kujiua huwa na tabia au dalili zipi?
232
5. Tafiti mbalimbali za kisaikolojia, kishosholojia na kiafya zimefanyika
kuhusiana na watu kujiua, lakini bado tatizo hili lipo katika jamii. Nini maoni
yako juu ya hili?
6. Kuna uhusiano gani baina ya magonjwa ya akili na mtu kujiua? Je, anayejiua
ni lazima awe na matatizo au magonjwa ya akili?
B.2.5 Mwongozo wa Mahojiano kwa Wataalamu na Wahakiki wa Kazi za
Fasihi
Jina langu ni Adria Fuluge, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Fasihi ya
Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma. Mada ya utafiti ni: ―Usawiri wa Mchakato wa
Kujiua katika Riwaya Teule za Euphrase Kezilahabi: Ni Mwangwi wa
Mtanziko wa Kijamii?” Lengo la utafiti huu ni kuchunguza na kubaini matukio ya
mchakato wa kujiua katika riwaya teule, pamoja na miktadha ya utokeaji wake katika
jamii ya mwandishi. Kabla ya kuanza mahojiano haya, naomba kukujulisha kuwa
taarifa utakazotoa zitakuwa ni siri baina ya mtafiti na wewe, na zitatumika tu kwa
lengo la utafiti huu. Tafadhali, naomba ushirikiano wako katika mahojiano haya.
1. Kwa namna unavyomfahamu Kezilahabi kwa kupitia kazi zake au kwa
kuonana naye ana kwa ana, unaweza kumwelezeaje kitabia na maisha yake
kwa jumla?
2. Ni tukio au matukio gani ya kujiua yaliyomo katika kazi teule (Rosa Mistika,
Kichwamaji, na Dunia Uwanja wa Fujo) za Euphrase Kezilahabi
unayoyakumbuka? Je, matukio hayo yana maana gani katika mchakato wa
kujiua?
3. Kwa maoni yako, unaweza kuelezeaje kuhusu kuwapo au kutokuwapo kwa
uhusiano baina ya matukio ya mchakato wa kujiua katika riwaya teule na
miktadha ya jamii ya mwandishi?
4. Suala la kujiua linajitokeza sana katika muktadha wa kisosholojia, kiafya na
kisaikolojia, na tafiti nyingi zimefanywa kwa mwegamo huo. Je, Fasihi ina
nafasi gani katika mchakato wa kujiua?
5. Pamoja na tafiti mbalimbali kufanyika kuhusiana na tatizo la watu kujiua
katika jamii, bado tatizo hili lipo na linazikumba jamii nyingi duniani kote,
ikiwa ni pamoja na Tanzania kwa umahususi. Unadhani tatizo hili
linachangiwa na nini, na nini kifanyike?
233
C. Taarifa za Watafitiwa
Na Jina Shughuli
Afanyayo
Mahali pa
Mahojiano
Tarehe ya
Mahojiano
1 Dkt. Athumani
Salumu Ponera
Mhadhiri
Mwandamizi
Chuo cha
Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere
17/2/2020
2 Dkt. Stella Faustine Mhadhiri Chuo Kikuu cha
Dodoma
9/11/2019
3 Dkt. Erasto Kano Mhadhiri Chuo Kikuu cha
Dodoma
18/1/2020
4 Dkt. Florentina
Nsolezi
Mhadhiri Chuo Kikuu cha
Dodoma
30/11/2019
5 Dkt. Rashid
Chuachua
Mh. Mbunge
Jimbo la Masasi
Jijini Dodoma 10/11/2019
6 Dkt. Enock
Changarawe
Daktari Bingwa
wa Magonjwa
ya Akili
Hospitali ya
Mirembe Dodoma
27/11/2019
7 Dkt. Gema Peter
Simbe
Daktari Bingwa
wa Magonjwa
ya Akili
Hospitali ya
Mirembe
29/11/2019
8 Dkt. Ramadhan
Thomas Kadala
Mhadhiri Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam
1/10/2019
9 Dkt. Angelus
Mnenuka
Mhadhiri Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam
1/10/2019
10 Pd. Ibrahim Ngassa Padre Viunga vya
Seminari ya
Mtakatifu Maria
Nyegezi Mwanza
17/12/2019
11 Bw. Flavian Ilomo Mhadhiri
Msaidizi
Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam
2/10/2019
12 Bw. Selestino
Helman Msigala
Mhadhiri
Msaidizi
Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam
30/9/2019
13 Bw. Paschal John
Ng‘ambi
Muuguzi
Kiongozi
Hospitali ya
Mirembe
29/11/2019
14 Bw. Edmund
Makaranga Tangi
Mkulima Namagondo,
Ukerewe
17/12/2019
15 Bw. Pantaleo Vicent
Tilibuzya Nagane
Mkulima Namagondo,
Ukerewe
17/12/2019
16 Bw. Angelo Msusa Mkulima Murutunguru,
Ukerewe
17/12/2019
17 Bi. Veneranda
Pantaleo
Muuguzi
Mstaafu
Namagondo,
Ukerewe
18/12/2019
234
18 Bi. Muyango
Mkokolo Mkama
Mkulima Namagondo,
Ukerewe
18/12/2019
19 Bi. Rozina Mugabe
Bununja
Mwalimu Namagondo,
Ukerewe
17/12/2019
20 Bi. Mungere
Mtesigwa
Mwalimu Namagondo,
Ukerewe
19/12/2019
21 Mch. Charles Bita
Kalogosi
Mchungaji Namagondo,
Ukerewe
8/12/2019
22 Bi. Regina Tanu Mwalimu S/M Nakasahenge,
Namagondo
18/12/2019
23 Bi. Aneth Benedicto Mkulima Namagondo,
Ukerewe
18/12/2019