Uswahilishaji wa Tanzania kama Hatua ya Ukombozi Kamili: Dhana na Mikakati ya Kimatendo
Transcript of Uswahilishaji wa Tanzania kama Hatua ya Ukombozi Kamili: Dhana na Mikakati ya Kimatendo
Uk. wa 1 kati ya 21
Uswahilishaji wa Tanzania kama Hatua ya Ukombozi Kamili: Dhana na Mikakati ya Kimatendo
Athumani S. Ponera
Mhadhiri, Idara ya Kiswahili
Chuo Kikuu cha Dodoma
Simu: +255 767 95 97 84
Baruapepe: [email protected]
Ikisiri
Lugha ya Kiswahili ni mhimili mkuu wa michakato mbalimbali ya kupatikana kwa uhuru
hapa Tanzania. Ni matarajio ya viongozi na wananchi wote kuwa baada ya kuwa huru
maendeleo yangefululiza katika nyanja mbalimbali za maisha yao. Hata hivyo, hatua ya
kimaendeleo iliyofikiwa haiendani na uhalisi wa matarajio. Kutofikiwa huko kumekuwa
kukizua manung’uniko na malalamiko katika nyanja mbalimbali. Malalamiko haya ni ithibati
ya kutokuwapo kwa ukombozi kamili. Miongoni mwa sababu za kutofikiwa kwa matarajio ya
Watanzania kimaendeleo ni tandabelua iliyopo kuhusu matumizi ya lugha. Katika uga wa
elimu, mathalani, kumekuwapo malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu kuchujuka
kwake kunakoendelea kutokea. Shabaha ya makala hii ni kutalii hali hii kwa jicho mahususi,
huku ikirejelea tafiti, maoni na mapendekezo yaliyowahi kutolewa na viongozi, watafiti, na
wanaisimu mbalimbali. Tiba inayoibuliwa humu kuhusu namna ya kuukomboa mfumo wa
elimu wa Tanzania ni Uswahilishaji, yaani, hali ya kukifanya Kiswahili kitamalaki katika
nyanja zote muhimu za maisha (k.v. elimu, uchumi, sayansi, tiba) kwa watu wanaotumia
lugha ya Kiswahili kama lugha yao ya kwanza au ya pili. Kutamalaki huko, hatimaye,
kutakifanya Kiswahili kiwe bidhaa na zana ya kiukombozi. Makala imeegemea katika elimu
kwa kuamini kuwa iwapo elimu itaswahilishwa, ni wazi kuwa ni rahisi kwa vipengele vingine
vyote vya maisha ya Waswahili kuswahilishwa pia. Dhana hii ya Uswahilishaji imejadiliwa
huku ikijiegemeza katika maswali yafuatayo: a) Uswahilishaji ni nini? b) Vikwazo vya
Tanzania Kuswahilishwa ni vipi? c) Ucheleweshwaji wa Uswahilishaji una athari gani kwa
kizazi cha sasa na baadaye? d) Kizazi cha sasa kifanye nini ili Kuiswahilisha Tanzania?1
Istilahi muhimu: Uswahilishaji, ukombozi kamili, mikakati ya kimatendo.
1 Makala hii ilinenepeshwa na maoni ya washiriki wa mijadala ya semina za kitaaluma za Vyuo Vikuu viwili, Chuo Kikuu
cha Waislamu Morogoro (iliwasilishwa na kujadiliwa Januari 28, 2013) na Chuo Kikuu cha Dodoma (iliwasilishwa na
kujadiliwa Mei 8, 2013).
Uk. wa 2 kati ya 21
1.0 Utangulizi
Lugha ya Kiswahili imekuwa nembo muhimu sana ya kulitambulisha eneo la Afrika Mashariki
duniani kote. Kiswahili, kama lugha ya mawasiliano hutumiwa na watu wa nchi za ukanda wote wa
Afrika Mashariki. Baadhi ya nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. Kwa kigezo cha jumla (cha kiisimujamii), kati ya nchi hizo, Tanzania
inajichomoza kama nchi ya Kiswahili (na kwa hivyo, ni nchi ya Waswahili). Hii ni kutokana na
mazingira ya kiisimujamii ambapo Kiswahili kinatumika katika nchi ya Tanzania kwa shughuli zote.
Nchini Tanzania, Kiswahili ni lugha rasmi; pia ni lugha ya taifa. Kwa jumla, Kiswahili ni zaidi ya lugha
kwa Watanzania; Kiswahili ndiyo maisha yenyewe! Hii ni kwa sababu, hutumiwa na kila mtu katika kila
tukio, kila muktadha, kila mahali, na kila wakati. Shughuli mbalimbali nchini Tanzania kama vile siasa,
utamaduni, utawala, utendaji, elimu, michezo, burudani, na hata mazungumzo hutumia Kiswahili kwa
namna ya moja kwa moja au kwa uficho. Shughuli hizi zinatumia Kiswahili bila kujali kama zinafanywa
na watu wa kada, mazingira wala kiwango fulani cha elimu. Hali hii ilikuwepo toka nyakati za kabla ya
uhuru. Licha ya kutamalaki huko kwa lugha ya Kiswahili katika maisha ya Watanzania, bado eneo nyeti
la elimu linasuasua kutokana na matumizi hafifu ya lugha hii. Wataalam wengi wameshafanya tafiti
mbalimbali kuhusu mgogoro huu wa matumizi ya Kiswahili katika elimu nchini Tanzania.
Baadhi ya tafiti hizo ni ule uliofanywa na Mlama na Matteru (1978) kuhusu „Haja ya Kutumia
Kiswahili Kufundishia katika Elimu ya Juu‟. Hawa, katika ripoti yao, walibainisha jinsi lugha ya
Kiingereza inavyoathiri ujifunzaji katika ngazi za kuanzia sekondari na kuendelea. Na wakapendekeza
kuwa Kiswahili kitumike badala ya Kiingereza; na kwa kufanya hivyo, kitakuzwa na kuwa lugha ya
kitaalamu. Pia, walipendekeza kuwa mbinu za ufundishaji wa lugha za Kiingereza ziboreshwe. Utafiti
mwingine ulifanywa mwaka 1984 na Waingereza, Ciper na Dodd; chini ya ufadhili wao. Hawa
walijikita katika kuchunguza ujuzi wa wanafunzi katika lugha ya Kiingereza. Majawabu ya utafiti wao
yakaonesha kuwa kiwango cha wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari katika lugha ya Kiingereza
Uk. wa 3 kati ya 21
ni kidogo sana. Baada ya utafiti huu, ndipo mnamo mwaka 1986 serikali ya Uingereza ikaanzisha mradi
maalum wa kuimarisha Kiingereza katika shule za sekondari.
Tafiti nyingine zilizofanyika miaka ya hiyo ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 kuhusu
matumizi ya lugha katika elimu nchini Tanzania ni ule wa 1986 wa Campbell na Qorro; pamoja na ule
wa 1991 uliofanywa na Rubagumya. Campbell na Qorro waliutafiti uwezo wa wanafunzi wa shule za
sekondari katika kuelewa vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza. Walibaini na kubainisha
kuwa asilimia 95 ya wanafunzi siyo tu hawawezi kuelewa, bali pia hawawezi kusoma vitabu hivyo.
Rubagumya (1991), kwa upande wake, alichunguza matumizi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza
katika shule za sekondari. Alionyesha kwamba lugha ya Kiingereza inatumika kwa sababu tu ya
kulazimishwa na sera. Matokeo ya kulazimishwa huko ni kwamba sehemu kubwa ya mafundisho
hutolewa na walimu kwa kutumia Kiswahili. Pia, mijadala mingi ya ujifunzaji ifanywayo na wanafunzi
hufanywa kwa Kiswahili. Zaidi, utafiti wa Rubagumya ulibaini kuwa siyo wanafunzi tu, bali, hata
walimu wana uwezo mdogo wa kutumia lugha ya Kiingereza katika ufundishaji. Kwa ujumla, matokeo
ya tafiti hizo zote yameonyesha kuwa jamii ya Watanzania inataabishwa na matumizi ya Kiingereza
katika uga wa elimu.
Nje ya uga huo wa elimu pia kuna matatizo na mataabiko makubwa kuhusu matumizi ya lugha
hizi mbili, yaani Kiswahili na Kiingereza. Hapa ninakusudia nyuga kama vile za utawala, sheria, na
utabibu. Miongozo ya kiserikali inatambua na kuafiki kuwa Kiingereza kitumike kwa mawasiliano
katika nyuga hizo na nyinginezo. Katika baadhi yazo, Kiingereza kinatumika nusunusu (kwa
kuchanganya na Kiswahili) na katika nyinginezo kinatumika, au niseme, kinatakiwa kitumike kwa
asilimia mia. Mathalani, katika mazingira ya elimu ya juu, lugha ya Kiingereza inatakiwa itumike siyo
tu kama lugha ya kufundishia na kujifunzia, bali pia mawasiliano mengine yote. Hata hivyo, uhalisi
unaonyesha kuwa bado Kiswahili ndiyo lugha inayotamalaki katika kuendesha shughuli mbalimbali za
asasi za elimu ya juu kama vile vikao, mikutano, na mijadala. Kwa upande wa mazingira ya kitabibu,
Uk. wa 4 kati ya 21
Kiingereza kinatumika nusunusu. Matabibu huitumia kuwasiliana wao kwa wao (katika hatua
mbalimbali za kutibu—kutoka kwa daktari, kwenda kwa m-maabara, kurudi kwa daktari, na kwenda
kwa mfamasia). Mzunguko huu haumhusu kabisa mgonjwa (ambaye ndiye anaandikiwa nyaraka hizo;
na kwamba, ndiye apaswaye kuzirejelea katika ufuatiliaji wa matibabu yake katika tukio la ugonjwa huo
au kwa siku zitakazofuatia). Mifano hii miwili inatosha kutuleta kwenye hoja muhimu kadhaa. Mosi,
nchi haina utaratibu unaoeleweka na madhubuti kuhusu matumizi ya lugha. Pili, ukosefu huo wa
utaratibu maalum unasababisha madhara mengi kwa jamii. Miongoni mwa madhara hayo ni yale
yaliyotajwa katika ripoti za watafiti waliodondolewa hapo juu.
Katika kujaribu kujibu baadhi ya malalamiko na maoni ya wananchi, wanaisimu, wanataaluma
pamoja na watafiti; wanasiasa au watawala wamewahi kuonyesha juhudi kadhaa. Katika juhudi hizo,
kumewahi kutolewa nyaraka, kuundwa kwa tume kadhaa pamoja na kutolewa kwa miongozo na
matamko kuhusu kuanza kutumia Kiswahili kufundishia elimu zetu zote. Juhudi ya kwanza ilitolewa
mwaka 1969. Hii ilihusu waraka wa wizara iliyokuwa inahusika na masuala ya elimu. Waraka huo
ulitumwa kwa wakuu wa sekondari nchini kote wakielezwa kuwa Kiswahili kingeanza kutumika
kufundishia masomo ya sekondari. Matumizi yenyewe yangefanywa kwa awamu tatu na ndani ya miaka
miaka mitatu (kuanzia mwaka 1969 hadi 1971); kwamba, mwaka 1969 matumizi ya Kiswahili
yangeanza kufundishia somo la siasa. Kisha, mwaka 1970 lingefuatia somo la sayansi kimu; na mpango
ungekamilika mwaka 1971 kwa masomo mengine yaliyosalia. Ninaliita wazo hili juhudi kwa kuwa
angalau tunathamini kuwako kwake kinadharia. Hata hivyo, utekelezaji wake haukufanikiwa hata
kuanza!
Miaka kumi baadaye, wizara hiyohiyo ikafufua wazo lake hili kwa kutangaza kuwa “…siku
moja Kiswahili kitafanywa lugha ya kufundishia” (Mdee, 2007). Tangazo hili likakitaka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam kianze maandalizi ya kiutekelezaji (kuandaa vitabu na nyaraka nyinginezo za
kufundishia). Kabla utekelezaji wa tangazo hili haujaanza, Rais akaunda tume ya elimu. Mapendekezo
Uk. wa 5 kati ya 21
ya tume hii yakafufua hamu ya Waswahili wa Tanzania kuhusu kujikomboa kielimu kwa kuitumia lugha
yao wenyewe katika kufikiri na kuunda mawazo mapya. Tume ilipendekeza kuwa Kiswahili kianze
kutumiwa kufundishia katika elimu ya sekondari kuanzia Januari 1985. Na kianze kutumiwa katika
ngazi ya Chuo Kikuu kuanzia mwaka 1992 (yaani ambao wangeanza nacho mwaka 1985 wangeendelea
nacho hadi Chuo Kikuu). Wazo hili lililotokana na kazi iliyotumia kodi za Watanzania nalo lilipotea
hewani kama moshi wa sigara!
Mwaka 1986 wazo hili la kutumiwa kwa Kiswahili katika elimu ya sekondari lilipigiwa tena
mbiu. Safari hii mbiu ilitoka vinywani mwa jopo la wanaisimu. Hawa nao, kama walivyopendekeza
wengine, kwa msisitizo sana walishauri kuondokana na fikra mgando za kung‟ang‟ania kutumia
Kiingereza katika elimu; badala yake Kiswahili kitumike na Kiingereza kifundishwe kama somo la
lazima katika ngazi zote za elimu. Kwa mara nyingine, mawazo mazuri ya wanataaluma hao yakaishia
kufunikwa na mavumbi katika mashubaka!
Miaka kumi baadaye, yaani mwaka 1996 nchi ikaingia tena katika mjadala, tena safari ukiwa
mzito (pengine ni kwa sababu ya mpanuko wa vyombo vya habari nchini pamoja na imani ya watu
kuwa Rais mpya wa wakati huo — Rais Mkapa alikuwa na vionjo vya kupenda lugha). Wazo
lilifufuliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambao walikwenda ikulu kumpongeza Ndugu
Rais kwa kuchaguliwa kwake. Ndani ya salamu hizo za pongezi wakamwomba aruhusu Kiswahili kipate
hadhi yake ya kutumiwa kwa asilimia 100 katika ufundishaji na ujifunzaji wa ngazi zote za elimu.
Jawabu la Ndugu Rais katika kutatua mvutano wa mawazo ya watu waliogawanyika katika pande mbili
(waliopendelea Kiingereza kiendelee kutumiwa na waliopendelea Kiswahili kianze kutumiwa) lilitaka
kuhusishwa kwa wananchi katika maamuzi haya. Hivyo, ilitakiwa uanzishwe utaratibu wa jinsi ya
kuwahusisha wananchi katika jambo hili adhimu. Kwa bahati mbaya, wazo hili zuri la Rais Mkapa
halikuonekana tena kimatendo!
Uk. wa 6 kati ya 21
Awamu ya nne ya utawala wa Tanzania ilianza kwa nuru ya aina yake kwa wadau wa masuala
ya lugha kufuatia kauli ya Rais wa awamu hii, Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake ya
mwanzo kwa taifa (hotuba ya Disemba 2005) iliyogusia kuuhuisha uzalendo kwa taifa letu. Mwangaza
huo wa furaha ya Waswahili wa Tanzania ulitokana na kuamini kuwa uzalendo huo, pamoja na mambo
mengine, ungehuishwa sana kwa kuheshimu, kuthamini, na kutukuza utamaduni wetu ambapo lugha ya
Kiswahili ni miongoni mwa vielelezo vyake. Huu, kama auitavyo Samala (2003), ni uzalendo wa
kiutamaduni; uzalendo uhusishao lugha, maadili ya taifa pamoja na shauku ya kisanaa. Na kwamba,
Waswahili waliendelea kutumaini kuwa, miongoni mwa matendo ya kuonyesha heshima, thamani, na
utukufu wa lugha ya Kiswahili, kwa ngazi ya kimakuzi iliyofikia kwa sasa ni kuiruhusu itumike rasmi
katika ngazi zote za elimu. Ni takribani miaka nane sasa ndoto hii ya Waswahili bado haijaingia katika
uhalisi!
Kufifishwa kwa maoni hayo ya wataalamu, wanaisimu na wananchi wa kawaida pamoja na
matamko na miongozo ya watawala kuhusu utaratibu mbovu wa kutumia lugha kumeendelea kuiweka
Tanzania katika hali mbaya sana kielimu na kijamii. Wananchi wameendelea kuyumba na
kunung‟unika. Hali ya matumizi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza katika miktadha rasmi nchini
Tanzania ni ya kusikitisha sana. Wananchi wengi wana maarifa shinda kuhusu lugha hizi mbili.
Watanzania hawana uhuru kamili wa kutumia Kiswahili katika miktadha rasmi kama vile ya kisheria na
ya kitabibu. Maendeleo yanatokea kwa kusuasua katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Lawama na
manung‟uniko yanasikika kutoka kila kona ya nchi kuhusu utaratibu wa matumizi ya lugha. Utaratibu
huo ndiyo unatoa mazao ya kielimu ambayo yanalalamikiwa. Wanafunzi wanalalamika! Walimu
wanalalamika! Wahadhiri wanalalamika! Viongozi wa mashirika mbalimbali wanalalamika! Ajabu zaidi
ni kwamba wahusika wa asasi zihusikazo na uratibu wa masomo na utahini nao wanalalamika! Chanzo
kikuu cha malalamiko hayo ni kulazimishwa kwa matumizi ya lugha ya Kiingereza kuanzia katika elimu
Uk. wa 7 kati ya 21
ya sekondari hadi elimu ya juu. Wanafunzi wanahitimu wakiwa na maarifa nusunusu; hawana uwezo wa
kutosha wa kuleta tija katika maendeleo ya taifa.
Je, nani amsaidie mwenzake kutuliza malalamiko yake? Ni kwa nini maoni ya wananchi,
wataalamu na wanaisimu yanapuuzwa bila kupatiwa majibu yenye kukata kiu? Ni taifa gani liwezalo
kupata ustawi bila kuhusisha fikra za wataalamu wake wa sekta mbalimbali? Ni nini kinakwaza
utekelezaji wa maoni na mapendekezo ya kitaalamu kuhusu suala hili? Ni nani anaridhia kuwapo kwa
manung‟uniko na malalaniko haya? Mataabiko haya yana tija ipi kwa taifa? Ni kweli taifa limefikia
ukomo wake wa kujikwamua kuhusu utaratibu wa matumizi ya lugha kulingana na vigezo faafu vya
kiisimujamii? Makala hii inajaribu kutoa suluhu ya kuondokana na mkwamo huu wa kijamii kwa
kutambulisha matumizi na utekelezaji wa dhana ya Uswahilishaji wa Tanzania.
2.0 Dhana ya Uswahilishaji
Katika makala hii Uswahilishaji unachukuliwa kuwa ni hali ya kuifanya lugha ya Kiswahili
itamalaki na itumike katika nyanja zote muhimu za maisha kama vile elimu, uchumi, sayansi, teknolojia,
utabibu, utawala, na sheria kwa watu wanaotumia lugha ya Kiswahili kama lugha yao ya kwanza au ya
pili (na kwa hiyo, wana umilisi mkubwa wa lugha ya Kiswahili). Hivyo, uswahilishaji unalenga
kikifanya Kiswahili kiwe bidhaa na zana yenye tija kwa Waswahili! Jambo hili ni la kisera, hivyo
linahitaji mipango na mikakati madhubuti ili kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inaenea na
kujitokeza bayana katika kila kipengele cha maisha ya Mswahili wa Tanzania. Kupitia dhana ya
Uswahilishaji, Kiswahili kitajitokeza dhahiri katika vipengele mbalimbali vya mawasiliano kama vile
mazungumzo (hili lina unafuu hata sasa), maelezo na maelekezo ya bidhaa, maelezo na maelekezo
huduma, pamoja na nyaraka. Pia, kitajitokeza bayana katika taaluma mbalimbali. Dhana ya
Uswahilishaji hailengi kuzifuta lugha nyinginezo (za makabila wala za kimataifa), bali inalenga
kuichomoza zaidi lugha ya Kiswahili ili kuipa upekee lugha yenyewe na Tanzania kwa ujumla. Hivyo,
dira ya sera hii ya Uswahilishaji yapaswa kutamka bayana kuwa itokeapo mazingira yoyote ya
Uk. wa 8 kati ya 21
kimawasiliano ambayo yatahitaji matumizi ya lugha zaidi ya moja basi Kiswahili kinatakiwa kijitokeze
kwanza na kisha kifuatiwe na lugha hiyo(zo) nyinginezo.
Tanzania, kama ilivyokwisha kudokezwa katika usuli wa makala hii, ni nchi ambayo Kiswahili
ndiyo nembo yake kuu. Uhuru, amani, umoja na mshikamano uliopo katika nchi hii haviwezi kamwe
kutenganishwa na lugha ya Kiswahili. Hata hivyo, mdhihiriko wa nembo hiyo una nguvu zaidi
kinadharia ikilinganishwa na nguvu ya kimatendo. Zaidi ya hilo, mdhihiriko wenyewe una nguvu zaidi
nje ya mipaka ya Tanzania kuliko ndani ya Tanzania. Mbali na Tanzania kujulikana sana na mataifa
mengi ya Afrika na ulimwenguni kwa ujumla kama nchi inayolelewa na kuongozwa na Kiswahili, hali
iko tofauti kabisa ndani ya nchi. Mathalani, ni vigumu sana kwa mgeni yeyote atokaye nje ya nchi ya
Tanzania kuonja ladha ya Kiswahili baada tu ya kutua sehemu yoyote ya Tanzania. Hii ni kwa vile,
sehemu kubwa ya maandishi mbalimbali kama vile matangazo ya biashara, na maelekezo yaliyopo
mitaani, barabarani na katika vyombo vya habari yako katika lugha ya Kiingereza. Vilevile, nembo za
bidhaa mbalimbali zipo katika lugha Kiingereza. Katika nchi ya Tanzania, si ajabu kumkuta mtu
anatumia neno au jina la Kiingereza katika kutambulisha au kutangaza bidhaa au eneo lake la biashara
ilhali hajui hata sababu wala maana halisi ya jina au neno lenyewe. Matangazo kama vile „Ponera
Restaurant’, „Stella Saloon’, au „Rashid Barbering Shop’ ni mengi sana nchini Tanzania. Haya ni
majina yanayobuniwa na wamiliki wa ofisi husika. Ubunaji na matumizi ya majina yenyewe, kwa
kawaida, huwa hauzingatii utashi wa kiisimu, bali mazoea tu. Kadhalika, kuna huduma nyingi zitokazo
katika asasi za kiserikali au zisizo za kiserikali pamoja na makampuni binafsi na kwenda kwa wananchi
wa kawaida huku zikitumia lugha ya Kiingereza. Mathalani, baadhi ya nyaraka za kiserikali, maelekezo
ya sehemu kubwa ya dawa, vipengele mbalimbali vya huduma za simu (kama vile maelezo ya simu
zenyewe, na kadi za muda wa maongezi) hupatikana katika lugha ya Kiingereza.
Hali hii, licha ya kuchukuliwa kuwa ni ya kawaida mbele ya macho ya Watanzania, ni sehemu
kubwa sana ya udhaifu wa nchi katika kupangilia matumizi ya lugha katika mazingira ya uwingi-lugha
kama ya Tanzania. Ni ajabu sana katika nchi ambayo Kiswahili kinatumiwa na zaidi ya asilimia 97,
Uk. wa 9 kati ya 21
kuona maelekezo na matangazo ya biashara yanatumia lugha ya Kiingereza kwa zaidi ya asilimia 83
(chanzo: utafiti mdogo wa kuchunguza matumizi ya lugha katika nembo, maelekezo na matangazo ya
biashara katika mitaa na vyombo vya habari). Jamii nyingi hapa ulimwenguni hujitahidi kutafuta namna
yoyote ya kujipa upekee katika mambo chanya. Hufanya hivyo kwa kutumia vipengele mbalimbali
kulingana na makubaliano na mahitaji yao. Lugha ni miongoni mwa vipengele hivyo. Hata hivyo, ni
nchi chache sana ulimwenguni huweza kufikia maafikiano katika matumizi ya lugha. Hii ni kutokana na
ukweli kwamba jamii au nchi nyingi zimo katika hali ya uwingi-lugha. Chambilecho Buliba na
Wenzake (2006:108) kuwa “Fikra inayotumika kupanga lugha lazima ioane na matakwa na matarajio ya
jamii inayopangiwa lugha”. Hivyo, Tanzania, ikiwa mojawapo ya nchi chache zenye kiwango kidogo
cha mgongano wa lugha (kwamba angalau Kiswahili kinajulikana, kinatumiwa na kukubaliwa na
sehemu kubwa ya wananchi wake), iko katika nafasi nzuri sana ya kujitengenezea upekee na tija kubwa
kupitia lugha ya Kiswahili. Kinyume chake, licha ya wananchi kutangaza matakwa na matarajio yao
kwa lugha ya Kiswahili, bado „fikra sahihi‟ kuhusu jinsi ya kuitumia kutupatia tija zaidi hazijapatikana.
Hivyo basi, kwa kuwa mpaka sasa tayari wananchi wa kawaida, wanaisimu, na wanataaluma wa
taaluma nyinginezo (nje ya isimu) wameonesha kukihitaji Kiswahili katika nyanja muhimu za maisha
yao kama vile elimu, sayansi na tiba, ni vema basi tukaingia kimatendo katika kuiswahilisha nchi yetu.
3.0 Kwa nini Tanzania Haijaswahilishwa Hadi Leo?
Nimekwishagusia hapo juu kuhusu juhudi kadhaa zilizokwisha kufanywa katika kukifanya
Kiswahili, mbali ya kuwa lugha ya mawasiliano kama ilivyo hivi sasa, kiwe lugha ya kitaaluma, pia iwe
taaluma. Hoja na ufafanuzi wa kutosha umetolewa. Swali muhimu hapa ni kwamba tatizo ni nini? Nani
anakwaza kutokea kwa jambo hili? Jambo lililo bayana kuhusu maswali haya ni kwamba hakuna
majawabu bayana yaliyosikika kupinga matumizi ya Kiswahili kuanzia elimu ya sekondari na
kuendelea. Kauli pekee iliyowahi kusikika kuhusu kutotumiwa kwa Kiswahili katika elimu ya juu ni ile
ya Rais wa kwanza, Ndugu Mwalimu Nyerere. Mdee (2006:194) amedai kuwa Mwalimu Nyerere,
Uk. wa 10 kati ya 21
akihutubia wadau wa UKUTA, alisema bayana kuwa Kiswahili kisitumike kufundishia elimu ya juu
kwa hofu ya kuiua lugha ya Kiingereza ambayo aliiita kuwa ni „Kiswahili cha dunia‟. Pengine kauli hii
ndiyo iliyowapofua sana viongozi wa serikali, vyama vya siasa, mashirika, makampuni, asasi za elimu
na taasisi mbalimbali. Kwa maoni yangu, upofu huu ndiyo unawafanya wasiwe tayari hata kupokea
mapendekezo ya wataalamu wala kuruhusu mijadala kuhusu suala hili. Ninaamini kuwa rai hii ya
Mwalimu Nyerere ilitolewa katika miktadha tofauti sana na iliyopo hivi sasa. Miktadha ninayoikusudia
hapa ni ya kiwakati, makuzi ya uelewa, mwamko wa wananchi, kiasi cha uhitaji, pamoja na mtagusano
wa kijamii. Kwa wakati wake, Mwalimu aliweza kueleweka, au niseme, hao wachache waliokuwa na
fursa ya kupata taarifa walimwelewa. Hivi sasa, jamii ya Watanzania ama inahitaji majawabu na
ufafanuzi wa kutowezekana kwa Uswahilishaji wa Tanzania au utendekeji wa dhana ya Uswahilishaji.
Kwa jumla, kwa maoni yangu, hali hii imekwazwa na makundi makubwa mawili ambayo ni
wananchi wa kawaida pamoja na wananchi waliopata fursa ya kuwa wasomi/wanataaluma, wanasiasa na
viongozi. Wananchi wa kawaida, kwa upande wake, limechangia kwa kiasi kidogo kutokana na tabia za
upole na uanakondoo. Kauli hii ninaitoa kutokana na ukweli kuwa viongozi na wanasiasa huwekwa
madarakani na wanachi ili wawatumikie kwa yale yanayopaswa kukubaliwa na wote. Sasa, kwa suala
hili la kutotumiwa kwa Kiswahili katika elimu ya sekondari na ya juu, Watanzania watu wazima
hatuwezi kukwepa kabisa shutuma za watoto wetu na vizazi vijavyo kwa adha mbalimbali zitokeazo
kwalo. Matakwa tunayo, matarajio tunayo, malengo tunayo, uwezo pia tunao; kwa nini tukubali kuishi
pasipo kupatiwa majawabu ya matakwa na matarajio yetu kuhusu matumizi ya Kiswahili kwa asilimia
100 katika maisha yetu hapa nchini?
Upande mwingine, tena huu ni mkubwa zaidi, wapo wasomi wa taaluma mbalimbali, wanasiasa
na watawala. Hawa, kwa maoni yangu, wamechangia kutoswahilishwa kwa Tanzania kwa kwa kiasi
kikubwa. Kuna sababu kadhaa zinazonisukuma kuwatwisha wadau wa kundi hili uzito mkubwa wa hali
hii: Mosi, hawa ndiyo wenye upeo mkubwa wa kuona na kutafakari kuhusu utendekaji wa masuala
Uk. wa 11 kati ya 21
mbalimbali ya kijamii. Kwa hili, pengine wametafakari ila wanapata kigugumizi kisicho na msingi
kudhihirisha athari za tafakuri zao. Pili, kundi hili ndilo lenye watu waliopewa dhamana ya kuliongoza
taifa kuelekea kwenye ustawi wa kimaisha. Hata kama hatua za kiustawi tulizozifikia katika nyanja
mbalimbali ni nzuri, kwa maoni yangu, zingekuwa nzuri zaidi kama nchi hii ingesikiliza matakwa na
matarajio ya wananchi wake kwa lugha ya Kiswahili. Tatu, katika kundi hili ndimo kuna Watanzania
wanaoshangaza sana kwa kuwa wapo katika nafasi nzuri ya kuboresha sera na mipango-lugha katika
elimu, lakini huishia kuungana na walalamikaji! Mathalani, humu ndimo kuna wanaisimu, wahadhiri na
viongozi wa Vyuo Vikuu ambao hawaishi kulalamikia uwezo duni wa wanafunzi na wahitimu wao
katika taaluma pamoja na umilisi duni wa lugha ya Kiingereza. Je, wanafanya nini ili kuliondoa tatizo
hili? Yatosha tu kuishia kufanya utafiti na kutoa matokeo na kisha kuridhia yaishie kugubikwa na vumbi
huko mashubakani? Kwa ujumla, wadau wa kundi hili, kwa makusudi au bila kukusudia, ndiyo kiini cha
mataabiko mengi wayapatayo Watanzania kuhusu kutokuwapo kwa sera, mipango wala mikakati
madhubuti ya lugha ya Kiswahili.
Mbali na mgawanyo huo wa jinsi jamii ilivyoshiriki kukwamisha Uswahilishaji wa Tanzania,
sababu za jumla za tatizo hili zipo katika makundi makubwa mawili, yaani sababu za ndani na za nje.
Sababu za ndani ni zile zitolewazo na wapinzani wa kuswahilishwa kwa Tanzania waliomo ndani ya
nchi (ambapo nyingi hutolewa na kundi lenye wasomi, wanasiasa na viongozi). Sababu za nje ni zile
zinazotokana na kani na sera za mataifa ya nje.
3.1 Sababu za ndani
kundi hili linahusisha sababu zifuatazo:
a) Kuhusu gharama za Uswahilishaji
Kwamba, mchakato wa kuiswahilisha nchi unahitaji gharama kubwa. Washadidiaji wake wanadai kuwa
ni gharama sana kutafsiri maarifa mengi ambayo yapo katika lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili.
Uk. wa 12 kati ya 21
Hapa wanarejelea vitabu vya kiada na ziada vya kuanzia kidato cha kwanza hadi ngazi ya Chuo Kikuu.
Majawabu ya hoja hii yamekwishatolewa vizuri na watetezi wengi waliowahi kuandika kuhusu jambo
hili. Kwa ufupi, washadidiaji wa pingamizi hili wanasahau kuwa kupanga ni kuchagua! Kwamba, iwapo
tutalimakinikia jambo hili, tunahitaji wastani wa bilioni 60 tu kulifanya litokee kimatendo — izingatiwe
hapa kuwa hizi ni pesa zenye uwezo wa kujenga uwanja mmoja tu wa mpira wa miguu kama ule wa
Taifa ulioko Temeke! Zaidi ya hilo, si lazima pesa hizo zitolewe katika bajeti ya mwaka mmoja. Je,
katika maisha yetu hapa Tanzania, kuna mambo mangapi yasiyo na tija kwa umma yanayoteketeza kiasi
cha pesa kama au zaidi ya hicho? Jawabu jema zaidi kuhusu hoja hii ni kwamba tayari juhudi za
kuandaa nyenzo za kufundishia na kujifunzia kama vile vitabu na kamusi zilikwishaanza na zimefikia
katika hatua nzuri. Tayari kuna vitabu vya kufundishia masomo ya kemia, fizikia na bayolojia
vimekwisha kuandaliwa. Baadhi yavyo, kwa mfano, kitabu cha kemia kiitwacho Furahia Kemia
(kilichoandaliwa na kuchapishwa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili) kipo madukani na kinagombewa
sana na walimu na wanafunzi wa somo hilo. Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha zote mbili, yaani
Kiingereza na Kiswahili kwa namna ya tafsiri-mkabala (ukurasa mmoja umeandikwa kwa Kiingereza na
ukurasa unaokabiliana nao yametafsiriwa maarifa hayo). Vilevile, tayari kuna kamusi kadha
zilizokwishaandikwa na tayari zinatumika. Kwa mfano, kuna Kamusi ya Sheria, Kamusi ya Tiba na
Kamusi ya Bayolojia, Kemia na Fizikia. Bila shaka, kwa hoja hizi, madai ya wapinzani yamebakia kuwa
chapwa. Kupanga ni kuchagua! Tuchague kuiswahilisha Tanzania, tupange!
b) Kuhusu kutokujitosheleza kwa lugha ya Kiswahili kimsamiati na istilahi
Hoja hii nayo inashadidiwa sana na wapingaji wa Uswahilishaji. Madai yao yanajikita katika kushindwa
kwa Kiswahili kupata msamiati wa dhana mbalimbali hususan za sayansi na teknolojia. Pia,
wanadhihaki utohoaji na ukopaji wa istilahi kadhaa kama vile „kisoma mbali‟, „kompyuta‟, n.k. Pia
wabezaji hawa huenda mbali zaidi hadi kukifungamanisha Kiswahili na lugha ya Kiarabu, hivyo, kudai
kuwa Kiswahili siyo lugha kamili kwa sababu ya madai kuwa takribani theluthi mbili ya msamiati wake
Uk. wa 13 kati ya 21
una vionjo vya lugha ya Kiarabu. Hawa nao wamepatiwa majawabu ya kutosha sana na watetezi
walionitangulia. Wanasahau kuwa utohoaji na ukopaji wa msamiati na istilahi ni kaida ya lugha yoyote
(ithibati nzuri ni jinsi ambavyo tunakuta msamiati na istilahi nyingi za Kilatini, Kiyunani au Kifaransa
katika lugha ya Kiingereza ambayo inapapatikiwa). Wanasahau kuwa kisu hupata makali kadri
kinavyotumiwa; na kwamba, Kiswahili kitapata msamiati na istilahi zake katika kila kona kadri jamii
itakavyokuwa inaitumia. Makali hayo yatakuwa yanaongezeka kadri jamii hiyo itakavyokuwa inakua na
kuvumbua vitu mbalimbali na kuvitumia katika maisha yao. Kupanga ni kuchagua. Tuchague
kuiswahilisha Tanzania ili Kiswahili kipate makali zaidi ya kimsamiati, kimuundo, kisemantiki, na
kihadhi.
c) Kuhusu madai kuwa Kiingereza ni lugha ya kitaaluma, kisayansi na ki-ajira
Hoja hii imefanikiwa sana kusambazwa akilini mwa Watanzania. Ithibati ya kutamalaki kwake yaweza
kutazamwa kupitia mhamo wa kifikra unaotokea kwa kasi kuhusu usomeshaji. Wazazi wengi wenye
uwezo wa kiuchumi hufikiria kuwasomesha watoto wao (hususan kwa ngazi ya chekechea na elimu ya
msingi) katika shule zinazotumia lugha ya Kiingereza kama lugha ya mawasiliano na ya kufundishia.
Bila hata kufikiria kuhusu kiasi cha maarifa watakachokipata huko, wazazi wanaamini kuwa watoto wao
watapata „ulimi mwepesi‟ katika lugha ya Kiingereza. Na hatimaye, kuajiriwa katika sehemu nzuri. Kwa
jumla, hawa wanaamini kuwa kujua Kiingereza ndiyo kuelimika. Wanasahau kuwa kama Kiingereza
ndiyo elimu, basi kusingekuwa na ulazima wa kuwa na shule katika nchi ambazo Kiingereza ni lugha
yao ya awali ikiwemo Uingereza yenyewe!
d) Woga wa kizandiki wa wasomi na watawala
Uzandiki hapa umetumika kumaanisha hali ya kuaminisha watu waamini kitu au hali isiyokuwepo; ni
upotoshaji au unafiki. Viongozi wengi na watawala, kwa wazi na kwa ufiche, wameendelea
kuwaaminisha watu kuwa iwapo Kiswahili kitatumika kufundishia sekondari na elimu ya juu, hadhi ya
Uk. wa 14 kati ya 21
elimu itashuka. Hoja hii inaungana kiasi na hoja ya hapo juu kwamba Kiingereza ni lugha ya kitaaluma.
Bali tofauti hapa ni woga unaoshindiliwa kuhusu dhana ya kushuka kwa hadhi ya elimu yetu iwapo
itatolewa kwa Kiswahili. Hoja yangu hapa inalenga kuwakumbusha wapinzani wa Uswahilishaji kuwa
pamoja na hicho Kiingereza kutumiwa hadi sasa, bado hali ya umilisi wake iko chini sana. Hivyo, hoja
hapa iwe kuungana na mapendekezo ya wanazuoni na watafiti kuhusu uboreshaji wa ufundishaji wa
lugha ya Kiingereza. Hili halina ulazima wa kuunganishwa na utumiwaji katika kufundishia (kwa
sababu tayari limekwishashindwa).
e) Kuhusu kushindwa kwa Kiswahili katika elimu ya msingi
Hili ni bezo maarufu kuwa hakuna haja ya kukitumia Kiswahili kufundishia ngazi za juu za elimu kwa
kuwa hata katika ngazi hii ya elimu ya msingi ambayo inakitumia kufundishia na kujifunzia, bado hali
ya ufaulu wa mitihani ni hafifu sana. Hoja hii ya kipropaganda ni dhaifu sana ikimakinikiwa kwa jicho
la kiutendaji. Majawabu ya hoja hii ni haya: Kwanza, hakuna mwanasaikolojia au mwanazuoni yeyote
aliyewahi kusema kuwa ni lazima darasa lote lifaulu mtihani. Zaidi ya hilo, kiwango cha ufanisi wa
wahitimu wa elimu ya msingi hakiwezi kutenganishwa na mfumo mbovu wa kuwatafuta na kuwaandaa
walimu wa wanafunzi hao! Wanafunzi hao hufundishwa na walimu walioathirika na mfumo wa elimu
ya kukaririshwa. Baya zaidi, upatikanaji wa walimu na maandalizi yao, kama asemavyo Kamugisha
(2012), ni wa bahati nasibu. Kwamba, walimu wengi wa Tanzania ni wale waliofaulu kwa kupata daraja
la tatu na la nne. Ni ajabu sana kutumaini mavuno mema kwa mfumo hafifu kama huu wa upataji na
maandalizi ya walimu wa wanafunzi wetu. Jibu jingine lipo kwenye ukweli kuwa kuna tofauti kubwa
sana ya ufaulu wa somo la Kiingereza na masomo mengine yatumiayo Kiswahili. Ufaulu wa somo la
Kiingereza ni wa kiwango cha chini sana ukilinganishwa na ule wa masomo mengine wanayotahiniwa
wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi (Sikombe, 2010).
f) Kutokuwa na sera ya lugha
Uk. wa 15 kati ya 21
Hili ni janga la nchi nyingi za bara la Afrika! Nyingi zimerithi sera na mipango-lugha iliyoachwa na
wakoloni wake. Mathalani, Tanzania mpaka sasa haina sera yake ya lugha, bali tunaendesha masuala ya
lugha kupitia Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997. Pamoja na ukweli kuwa lugha ni kijenzi kimojawapo
cha utamaduni, ifahamike hapa kuwa, lugha ndiyo roho ya kuwapo kwa ustawi wa jamii yoyote ile.
Hivyo, kwa mtazamo wangu, kukosekana kwa sera ya lugha inayojitegemea ndiko kumetuleta hapa
tulipo. Kwa kuambatishwa katika Sera ya Utamaduni, matamko yahusuyo lugha yamekosa nguvu ya
kujulikana. Naamini wakati umefika wa kuwa na sera madhubuti ya lugha, na dhana ya Uswahilishaji
iwe ni miongoni mwa mihimili itakayoishikilia sera hiyo.
3.2 Sababu za Nje
Sababu za nje zinahusu kani na mipango ya mataifa ya nje katika kuhakikisha kuwa lugha zao
zinaendelea kuenea na kutumika katika „mataifa madogo‟. Ili kuhakikisha hili linatimia, huweka sera na
mipango kadhaa ili kuyalaghai mataifa haya. Hufanya hivyo huku jicho lao wakilielekeza katika
manufaa ya kiuchumi walengayo kuyapata. Kwa lengo hili, ndipo tunapoona mataifa hayo yakianzisha
mashirika ya lugha zao ili yawe mawakala wa ukuzaji na uenezaji wa lugha hizo. Sera pamoja na
mipango yao hiyo hupata nguvu sana punde kuzukapo vuguvugu la mijadala ya Watanzania kuamshana
kutumia Kiswahili kufundishia katika ngazi zote za elimu. Mathalani, katika mwanzoni mwa miaka ya
1990 kulizuka Operesheni ya kufufua ufundishaji wa Kiingereza inayofadhiliwa na Shirika la
Maendeleo la Uingereza. Ikumbukwe kuwa katika wakati huu nchi ilikuwa katika mjadala na hamu ya
kutaka kuona utekelezaji wa mapendekezo ya ile Tume ya Rais (ya kuanza kutumia Kiswahili kwa
kidato cha kwanza mwaka 1985 na Chuo Kikuu mwaka 1992) pamoja na mjadala wa wanaisimu wa
mwaka 1986. Kwa maoni yangu, hali hii ndiyo iliwasukuma Waingereza kuhuisha mpango wao wa
kufufua Kiingereza ili kufifisha juhudi za Waswahili na hivyo kulifikia lengo lao. Kwa hakika,
nionavyo, ulaghai kama huu ukijumlishwa na vitisho kutoka kwa mataifa haya „makubwa‟ ni sababu
tosha ya kuwasukuma viongozi wetu kupuuza maoni na matakwa ya wanataaluma na wananchi kwa
Uk. wa 16 kati ya 21
jumla. Na hivyo, kuendeleza kasumba ya mataifa ya Afrika ya kuzoea kuishi kikasuku katika masuala
mbalimbali. Wito wangu hapa ni kwa wahusika kujiuliza: Iwapo hayo „mataifa makubwa‟
yanayodhaniwa kuwa lugha zao zina nguvu hayajaridhika na ueneaji wa lugha zao, iweje sisi Waswahili
tuendelee kuzishabikia lugha zao bila kuweka mipango madhubuti ya kuiendeleza lugha yetu? Zaidi ya
swali hilo, napenda kukumbusha hapa kuhusu uhusiano uliopo baina ya ushabiki huu tuufanyao kwenye
lugha ya Kiingereza na utumwa. Chambilecho Gandhi (1965) wakati anajenga hoja ya Wahindi kutumia
Kihindi katika nyanja zote za maisha yao:
… mtumwa hupenda kuiga tabia na mbinu za bwana wake kama vile mavazi, lugha n.k.
Taratibu hupenda tabia za bwana wake na kutupilia mbali mambo yake… Kiingereza
hakiwezi kuwa kuwa lugha yetu ya taifa wala ya kufundishia. Tumezidumaza lugha zetu
kwa kutumia Kiingereza. Tumewapa mzigo mkubwa wanafunzi wetu. Huu utumwa wa
lugha ya kigeni umewanyima mamilioni ya wananchi wetu kupata maarifa mengi muhimu
kwa miaka mingi… [Gadhi (1965:8) kama alivyonukuliwa na Mdee (2007:192-193)].
Maneno haya ya Gandhi yanajitosheleza sana, wala hayahitaji ziada yoyote ili kuleta uelewa na
ushawishi kuhusu hoja hii ya kuiswahilisha Tanzania. Hima, tuiswahilishe Tanzania ili kuachana na
utumwa huu! Katika sehemu ifuatayo nitaeleza hatua tuwezazo kuzifuata ili kuifikia dhana ya
Uswahilishaji kimatendo.
4.0 Mchakato wa Uswahilishaji
Utekelezaji wa dhana ya Uswahilishaji itafikiwa kimatendo iwapo mambo yafuatayo yatazingatiwa:
a) Kutoa tamko la kikatiba kuwa lugha ya Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi ambayo
lazima itumike kwa uhuru na ufasaha katika shughuli na vipengele vyote vya umma nchini
Tanzania. Na kwamba, yatokeapo mazingira yoyote ya kimawasiliano ambayo yatahitaji
matumizi ya lugha zaidi ya moja basi Kiswahili kinatakiwa kijitokeze kwanza na kisha kifuatiwe
na lugha hiyo nyingine;
b) Kuchambua na kuandaa lugha za kigeni zitakazoruhusiwa kufundishwa au kujifunza katika asasi
za elimu Tanzania. Lugha hizo, kwa maoni yangu, ni Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, lugha za
Uk. wa 17 kati ya 21
Mashariki ya Mbali (Kichina, Kijapani, Kirusi na Kikorea). Kila mwanafunzi (katika ngazi zote)
atatakiwa asome angalau somo moja la lugha ya kigeni;
c) Kuandaa mpango maalum wa jinsi ya kuwapata watu wafaao kuwa walimu, mfumo wao wa
mafunzo, pamoja motisha walimu wa masomo ya lugha ya Kiswahili na lugha za kigeni (ambazo
zitakuwa zinafundishwa kama masomo) ili kuboresha umilisi wa wanafunzi. Uboreshaji wa
ufundishaji wa lugha za kigeni uhusishe pia mataifa husika;
d) Kuandaa kamati zitakazojumuisha wataalamu wa tafsiri na ukalimani na wanazuoni wa fani
mbalimbali ili kuendeleza shughuli ya kutafsiri nyaraka za kufundishia na kujifunzia;
e) Kuanzisha programu za masomo ya tafsiri na ukalimani kama masomo ya lazima katika ngazi ya
elimu ya sekondari. Kisha kupanua Shahada za Tafsiri na Ukalimani katika Vyuo Vikuu
vitoavyo Shahada hizi, na;
f) Kuanza utekelezaji wa tamko la Uswahilishaji baada ya mwaka mmoja toka litakapoingizwa
katika katiba. Muda huo utatosha kwa hatua mbalimbali za maandalizi ya „mhamo huo wa
lugha‟ katika elimu, biashara (kubadilisha vitabu, matangazo, bidhaa n.k.).
5.0 Faida za Uswahilishaji
Iwapo Tanzania yote itawahilishwa, ni wazi kuwa itapata tija zifuatazo: Mosi, itaongeza ajira
kwa wananchi wake. Hivi sasa kuna Vyuo Vikuu kadhaa hapa nchini vifundishavyo masomo ya
Shahada za Lugha ya Kiswahili zifundishwazo kwa lugha ya Kiswahili (Shahada za Awali, za Umahiri
na za Uzamivu). Mifano yake ni Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo
Kikuu cha Waislamu Morogoro. Baadhi ya mambo yafundishwayo katika programu hizo ni stadi za
uandishi, tafsiri, ukalimani, utafiti wa lugha, uhariri, na usomaji wa prufu. Wataalamu hawa ndiyo
rasilimali muhimu sana katika kuiswahilisha Tanzania kwani watahitajika sana katika „mhamo huu wa
lugha‟ kwa kushiriki katika michakato kama vile kuandika, kutafsiri, na kuhariri. Matumizi ya
wataalamu hawa hayataishia katika kipindi cha mhamo wa lugha tu, bali pia yatakuwa endelevu
Uk. wa 18 kati ya 21
kutokana na kuwa kuna bidhaa mbalimbali na wageni wengi waingiao nchini kila siku. Kwa kuwa nchi
itakuwa imeswahilishwa — Kiswahili kitakuwa kimetapakaa katika kila eneo, itawalazimu wageni hao
kuhitaji huduma za tafsiri na ukalimani kutoka kwa wenyeji. Hali hii ni tofauti na sasa ambapo hata
majina ya mitaa yameandikwa kwa Kiingereza. Vilevile, huduma muhimu, bidhaa na nyaraka
mbalimbali za kibinadamu zimewekwa kwa Kiingereza. Hali hii huwarahisishia kazi wageni wajao
nchini katika kujipatia huduma. Ajira pia zitaongezeka kwa Watanzania kuhitajika nje ya nchi — katika
mataifa yenye hamu ya kukitumia Kiswahili. Mataifa haya yapo mengi, na yanaendelea kuongezeka.
Nafasi hii ya kutoa huduma ya Kiswahili huko kwa hivi sasa, kwa kiasi kikubwa, imeshikwa na wa-
Kenya ambao, kitaaluma, wameimakinikia lugha ya Kiswahili kuliko Watanzania. Kwa upande
mwingine, hali hiyo ya kuongezeka kwa ajira za ndani na nje ya nchi, mbali na kuongeza pato la
Mtanzania mmojammoja, itakuwa inaongeza pato la taifa. Hivyo, kuongeza ustawi wa Tanzania kwa
ujumla.
Tija nyingine ni kuinua uelewa na uendeshaji wa mambo rasmi kama vile elimu, utabibu,
sayansi, sheria na teknolojia. Kwa kiasi kikubwa, mambo hayo hivi sasa huendeshwa kwa ugumu wa
kukariri na kulazimishwa. Hivyo, kwa namna moja au nyingine, kukwaza mnyiririko wa maendeleo.
Tija ya nne ni kuleta haki na usawa kwa Watanzania wote. Kama ilivyodokezwa hapo juu
mhamo wa kifikra wa Watanzania wengi kuhusu shule zifaazo kuwaelimisha watu wao, watu wasio na
uwezo ndiyo wawapelekao watoto wao katika shule za serikali. Wenye uwezo wengi hupeleka katika
shule zitumiazo lugha ya Kiingereza kama nyenzo ya mawasiliano na ya kufundishia. Wakiongozwa na
fikra za kuamini kuwa Kiingereza ni elimu, wamiliki wa shule hizi huweka mkazo zaidi katika kujua
lugha. Kwa upande wa kiasi cha maarifa, wahitimu wa shule hizi hawana tofauti yoyote na wahitimu wa
shule nyingine za serikali. Fikra za namna hiyohiyo zimewagubika pia waajiri wengi wa Tanzania
ambao wako tayari kumwajiri mtu tu kwa sababu ana uwezo wa kujieleza kwa Kiingereza hata kama
kimaarifa anazidiwa na yule asiye na uwezo wa kujieleza Kiingereza. Ni wazi kuwa, kwa mwenendo
huu, wahitimu wa shule za serikali huwa katika kundi la hasara zaidi kuliko wenzao wale waliohitimu
Uk. wa 19 kati ya 21
katika shule hizi „za Kiingereza‟. Hatimaye, kuweka upogo mkubwa wa ki-ajira baina ya Watanzania.
Hivyo, kama Tanzania itaiswahilishwa, ni wazi kuwa itasaidia hakuwakomboa wachochole ambao
wanaunda sehemu kubwa ya jamii.
6.0 Madhara ya Kutoswahilishwa kwa Tanzania kwa Kizazi cha Sasa na Baadaye
Iwapo nchi itaendelea kuwa katika hali hii ya kutoswahilishwa, Watanzania tutaendelea
kuzipoteza tija zilizobainishwa hapo juu. Yaani, jamii ya wanyonge wa kiuchumi wataendelea
kutengwa; tutaendelea kupoteza fursa ya ajira za ndani na nje kwa Watanzania wengi ambao wana sifa
ila wanakwamishwa na usomakinifu wetu katika Kiswahili. Vilevile, tutaendelea kuwa na kizazi butu
kielimu, kizazi cha kukariri au kama akiitavyo Kiputiputi (2007:107) kuwa ni kizazi cha unataji wa
kielimu; na siyo uchakataji wa kielimu. Kizazi cha kunata elimu ni kile ambacho kinaishi kwa kukariri
bila kuwa na uelewa wa dhati. Na kile cha uchakataji ni kinyume chake, yaani hupata elimu kwa uelewa
wa dhati na huwa na uwezo wa kuzalisha mawazo kutokana na elimu yao kwa uhuru na upevu. Kizazi
cha unataji ni hatari sana kwa ustawi wa taifa kwa sababu uwezo wake wa kutafiti, kuvumbua, na
kubuni ni mdogo sana. Tanzania, ambayo ina kiasi kikubwa sana cha kizazi cha unataji imo katika
hasara kubwa ya ki-ustawi. Hivyo, iwapo itaendelea kuwa katika hali hii ya kutoswahilishwa itazidi
kutumbukia katika giza la ustawi kutokana na kuendelea kudumaza uwezo wa kufikiri pamoja na
teknolojia asilia.
Madhara mengine ni kuporomoka kwa umoja wa kitaifa kutokana na kuwatenganisha
Watanzania kielimu, kiajira na kihadhi kama nilivyodokeza hapo juu. Matokeo yake huweza kuzaa
uwezekano mkubwa wa kuwapo kwa machafuko kutokana na fukuto la muda mrefu la manung‟uniko,
chuki na hasira za kitabaka.
7.0 Hitimisho na Mapendekezo: Kizazi cha sasa kifanye nini ili Kuiswahilisha Tanzania?
Shaaban Robert, ambaye ni miongoni mwa waasisi wa dhana ya kuiswahilisha nchi ya Tanzania, kupitia
kalamu yake, aliwahi kusema hivi:
Uk. wa 20 kati ya 21
“…wasio Waafrika wanadai kuwa Kiingereza kitumike… Waafrika wanadai kuwa
Kiswahili kitumike… katika kila pigano upande mmoja hushinda. Bila shaka,
Kiingereza kitashinda. Bali, yatabiriwa kuwa utakuwa ni ushindi wa kitambo tu…
Haiyumkiniki kuwa wenyeji wa mahali popote katika ulimwengu waweza kuridhika
kuishi katika lugha ngeni milele” (Shaaban Robert, 1948).
Kwa hakika, “kitambo” akisemacho Shaaban kimekwisha kupita sana! Kila kizazi kina dhima
yake ya msingi kinayopaswa kuitimiza. Vizazi vilivyotangulia vilihusika na majukumu mbalimbali
kama vile kutafuta uhuru, kutafuta nyenzo ya mawasiliano ya kitaifa, pamoja na kujenga misingi ya
umoja wa kitaifa. Nimedokeza hapo juu kuhusu hali ya kuulizana maswali yasiyo na majibu
inayoendelea hapa nchini kuhusu matumizi ya Kiingereza na Kiswahili. Nimedokeza pia kuhusu
kunung‟unikiana na kulaumiana kunakoendelea kuhusu ubutu wa kimaarifa na wa lugha ya Kiingereza
kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu. Nimedokeza pia kuhusu kuwepo kwa kasi ya jongoo
katika ufikiwaji wa maendeleo hapa Tanzania. Bila shaka, dhima ya kizazi cha sasa ni kuondoa maswali
yasiyo na majibu, manung‟uniko pamoja na lawama kwa kushiriki kikamilifu katika hatua yoyote
itakayokuja mbele kuhusu kuishamirisha dhana ya Uswahilishaji. Haya, ili kujitofautisha na vizazi
vilivyopita, yanapaswa kufanywa kwa matendo siyo kuishia midomoni wala kuendelea kugugumia
mioyoni. Hii ndiyo mikakati ya kimatendo. Hivyo, ninapendekeza yafuatayo:
a) Kuanzia sasa, wananchi wa kawaida, wanafunzi wa ngazi zote, wafanyakazi na wengine wote
wenye mapenzi mema na nchi ya Tanzania tuhubiri kauli mbiu ya “Tuungane kwa Kiswahili
kwanza, mengine yatafuatia”;
b) Watanzania tuunganishe nguvu na kudai kuwapo na kutendeka kwa jambo hili. Miongoni mwa
mikakati iwezayo kukoleza nguvu ya tafiti zilizotangulia ni kulifanya suala hili kuwa ajenda ya
kitaifa. Aidha, kuhakikisha kuwa suala hili lijitokeze dhahiri katika katiba ya nchi; na
c) Kulifanya jambo hili liwe ndiyo dhima kuu ya kizazi cha sasa kwa taifa letu.
Uk. wa 21 kati ya 21
8.0 Bibliografia
Buliba, A. na Wenzake (2006). Isimujamii. The Jomo Kenyatta Foundation. Nairobi.
Gandhi, M.K. (1965). “Our Language Problem”. A.T. Hingorani (Mhar.). Bombay.
Kamugisha, N. R. (2010). “Implementation of Learner-Centered Approach and Materials in Field
Research for Improving Teaching and Learning of Geography in Advanced Level Secondary Education
in Tanzania: A Case of Morogoro Municipality”. Tasnifu ya Shahada ya Umahiri, Chuo Kikuu cha
Dodoma.
Mlama, P. na Matteru, M.L. (1978). “Haja ya Kutumia Kiswahili Kufundishia katika Elimu ya Juu”.
BAKITA.
Rubagumya, C.M. (Mhar.) (1989). Language in Education in Africa. Clevedon. Philadelphia,
Multilingual Matters Ltd.
Sikombe, Y.Y. (2010). “Lugha ya Kiswahili katika Kufundishi na Kujifunzia Elimu ya Juu”. Tasnifu ya
Shahada ya Umahiri katika Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Simala, I. (2003). “Uzalendo wa Lugha ya Kiswahili katika Enzi ya Utandawazi” katika Kiswahili na
Utandawazi. BAKITA.
Tumbo-Masabo, Z.N. na E.F.K. Chiduo (2007). Kiswahili katika Elimu. Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili, Dar es Salaam.